Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SURE BOY: Simba, Yanga washindwe wenyewe

Muktasari:

UKIBAHATIKA kupiga stori na kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kuna mambo kibao ya maana utayapata tofauti na kumtazama kwa mbali unaweza kumuona ni nunda.

UKIBAHATIKA kupiga stori na kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kuna mambo kibao ya maana utayapata tofauti na kumtazama kwa mbali unaweza kumuona ni nunda.

Katika mahojiano na Mwanaspoti supastaa huyo aameonyesha ni namna gani alivyo mchezaji mwenye nidhamu, malengo na shukrani kwa waliokipaisha kipaji chake.

Anasema soka bila nidhamu na kujituma inakuwa ni vigumu wachezaji wengi watashindwa kuwatendea haki mashabiki kuona burudani kutoka miguuni mwao.

“Hadi nilipofika nimepitia mikononi mwa watu wengi, ila sitaacha kumtaja Heri Mzozo. Ana mchango mkubwa soka la Tanzania. Anastahili kuenziwa na wachezaji wengi. Asilimia kubwa ya maisha aliyatoa kwetu kuhakikisha tunaviendeleza vipaji vyetu,” anasema.

Anasema kipindi anachipukia alipata mafunzo kutoka kwa mastaa waliokuwa na vipaji vya juu waliomsaidia kuwa na mwendelezo mzuri. “Maisha ya soka yana raha na maumivu makali. Kama mchezaji anakosa uvumilivu ni ngumu kuishi ndoto zake. Wengi wanajua sipendi kucheza nje, ila leo niwaambie nimewahi kupata ofa nyingi zilizoshindikana kutokana na vitu vilivyo nje ya uwezo wangu.”

Hata hivyo, hajakata tamaa endapo ikitokea bahati kwenda kuuonyesha ulimwengu alichonacho mguuni kwake atakubaliana na ofa hiyo.


MASTAA ALIOWAPA SALUTI

Sure Boy anawataja Haruna Moshi ‘Boban’, Athuman Idd ‘Chuji’, Shaban Kisiga na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwamba licha ya kuwa na vipaji vikubwa, hawakuwahi kulewa sifa zaidi ya kuwajibika uwanjani.

“Kwa namna walivyocheza soka kubwa, wakati mwingine nawaza wangekuwa ndio chipukizi wa sasa wangelewa sifa na kuondoka kwenye mstari. Hawa jamaa hawakuwa na papara zaidi ya kuwajibika na kazi dimbani.”

Anamtolea mfano Boban alivyo na akili nyingi na hapendi mambo ya kupinda.

“Boban anapenda unyoofu wa mambo, wengi wanamshindwa hapo. Anashauri maisha, akili yake ni kubwa ukibahatika kukaa naye utaelewa ni mtu wa aina gani. Hapendi kuona kipaji cha mtu kinaishia njiani,” anasema.


MZOZO NI BABA

Sure Boy anasema kwa maisha ya soka Mzozo anamchukulia kama baba kwa sababu ni chanzo cha kucheza Ligi Kuu Bara baada ya kukilea kipaji chake. “Kabla ya kukutana na Mzozo nilikuwa kwenye kituo cha soka cha Wakati Ujao kipo Mikocheni. Huko nilikuwa na Dommy ambaye aliniambia ili kipaji changu kikue nikacheze Friends Rangers,” anasema Sure Boy.

“Baada ya kufika Friends Rangers akanikabidhi kwa Mzozo. Kama bahati kulikuwa na mechi kanipanga winga nilicheza vizuri sana. Tangu hapo akawa ananipanga mechi zote hata wakija mastaa waliokuwa wanatamba Ligi Kuu hakuacha kunipanga.”

Anasema Friends Rangers ilimkutanisha na mastaa mbalimbali baadhi yao anawataja kuwa ni Boniface Pawasa, Athuman Machupa, Credo Mwaipopo na wengineo wengi, jambo lililokuwa linamrahisishia kazi uwanjani.

“Kaka zangu hao walifanya nipende zaidi mpira. Hata wakati wa mechi nikienda kucheza iwe na Yanga, Simba, Moro United sikuwa napata kazi kwani nilikuwa nakutana nao. Hivyo walisaidia kulea zaidi kipaji changu,” anasema Sure Boy.

Anasema Mzozo alikuwa anamchezesha nafasi mbili - beki namba mbili na winga na alimtunga jina la ‘Kistuli’ kutokana na ufupi aliokuwa nao.

“Ukiachana na Mzozo kocha wa Habibu Kondo (KMC) ndiye aliyenibadilisha kutoka kucheza namba mbili hadi kiungo ninayocheza,” anasema.


CITY WALIMLAZA NA VIATU

Anasimulia kwamba ilikuwa Juni 17, 2013, Taifa Stars ilicheza dhidi ya Ivory Coast, Uwanja wa Mkapa kwamba alikutana na mastaa kama Yaya Touré na Didier Drogba ambao walimpongeza baada ya mechi. “Ninachojivunia katika mechi hiyo ni kufuatwa na Toure kuniambia nimecheza vizuri na anakubali kipaji changu. Hiyo ni faraja kubwa katika maisha yangu ya soka,” anasema.

Ukiachana na hilo, anasema hataisahau mechi ya Mbeya City ile ya moto waliyocheza nayo Uwanja wa Azam Complex na kutoka sare ya mabao 3-3. “Kipindi hicho Peter Mwalyanzi na Deus Kaseke walikuwa tishio. Ile mechi ilipigwa ilikuwa ya kulala na viatu, hiyo kwangu ni bora na ilikuwa ngumu,”anasema.


CHIPUKIZI WA KUFIKA MBALI

Su-re Boy anawataja Feisal Salum ‘Fei Toto’ (Yanga), Kenny Ally Mwambungu (KMC), Awadhi Salum (Mtibwa Sugar) kwamba wakiongeza juhudi watafika mbali.

“Ni wachezaji ambao wanacheza nafasi yangu ninawaona mbali sana. Wakisaidiwa kukuzwa vipaji vyao na wao wenyewe kujitunza na kujituma,” anasema.

Anasema shida ya wachezaji wa sasa hawachukulii soka kama kazi na hawajitambui hilo ndilo linalowaondoa kwenye mstari.

“Ukiachana na hilo, vipaji kwa sasa vinapungua Ligi Kuu tofauti na zamani maskauti walifanya kazi ya kufuatilia vipaji kuanzia chini. Kipindi tunaachiwa vijiti na kaka zetu kina Chuji kulikuwa na ushindani mkali sana wa vipaji ndio maana soka lilikuwa la burudani,” anasema.

Mbali na hilo anamzungumzia aliyekuwa kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi kwamba ni kati ya mafundi aliowahi kufurahia kazi zao baada ya kukutana uwanjani. “Kuna wachezaji wengi ambao wamechangia kuwa hapa wakiwemo niliowajata hapo juu, maana nilikuwa nawakuta Friends Rangers. Hivyo walikuwa wanasema dogo kazana utafika mbali.”


MAISHA AZAM FC

Sure Boy anasema huu ni mwaka wa 13 Ligi Kuu, hivyo amejifunza mambo mengi.

“Jumla ya miaka niliyokaa 16 kwa sababu nilijiunga nayo (Azam) tangu ikiwa Ligi Daraja la Kwanza. Hivyo kuna furaha kubwa na changamoto zake nilizopitia, ila yote ni maisha ya kazi yoyote duniani,” anasema.

Anasema pamoja na kuwa na kila kitu kwenye timu yao, yapo mambo ambayo yanasababisha wakwame kwenye harakati za kupigania ubingwa kama ratiba, timuatimua ya makocha na waamuzi viwanjani.

“Kila kocha anapokuja anakuwa na mfumo wake ambao mchezaji lazima uufuate. Pia kuna wakati waamuzi wanakosa sababu kutokana na wakati mwingine kutokuwa sawa,” anasema.

Ukiachana na hilo, anasema msimu walioondoka John Bocco, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na Aishi Manula kwa pamoja ulichangia timu kuyumba.

“Wachezaji hao kuondoka kwa pamoja wakati walikuwa ni muhimili wa timu kuliyumbisha timu, maana waliokuwa wanakuja katika nafasi zao walishindwa kufikia viwango vyao.”


KUSIMAMISHWA, BOCCO

Sure Boy anasema hayupo tayari kulizungumzia suala la kushimamishw akwao na waajiri wake kwa kuwa wameshatoa adhabu inatosha. “Kwa namna nilivyoitumikia Azam kwa miaka 16 siyo vyema kubishana na mabosi wangu. Hao ni kama wazazi. Nimepokea nimenyamaza, ninachojua nimeitumikia timu hiyo kwa moyo na jasho,” anasema.

Sure Boy anamtaja straika anayemkubali tangu aanze kucheza soka la ushindani kuwa ni Bocco ambaye anapambana kuweka heshima ya mabao.

“Bocco anastahili heshima kwa kizazi chetu. Anaonyesha nidhamu ya kazi na matunda yake yanaonekana. Hayo yameanzia Azam, Simba na Taifa Stars.” Lakini kwa upande wa Agrey Morris, anasema ana heshima kwa kucheza soka la nidhamu kuanzia Azam hadi taifa Stars alikoagwa kwa heshima.


SOKA LAMPA MKE

sure Boy anasema kupitia soka pesa yake ya kwanza aliyosajiliwa Azam FC, alioa mke ambaye amezaa naye watoto watatu - Abubakar, Apsa na Lukuman ambao hataki hata mmoja acheze soka.

“Usajili wangu wa kwanza ndio nilipata pesa ya kwenda kutoa mahari. Ukiachana na mke hadi nilipofika soka silidai na wala halinidai, hivyo tu siwezi kufafanua sana,” anasema.

Anapoulizwa kama jina la baba’ke limekubeba? Sure Boy anasema licha ya baba yake kuwa staa kwa sababu alicheza zamani Yanga, jina lake halijambeba bali ameliendeleza baada ya kupambana kivyake. “Baba yangu kuwa na jina kubwa kwenye soka haviingiliani na kile ninachotakiwa kukifanya uwanjani. Yeye kabakia kama mshauri wa kunielekeza nini nifanye.”

Pamoja na baba’ke kuichezea Yanga, anasema hajawahi kumshauri achezee timu hiyo zaidi ya kuacha aamue mwenyewe wapi panapomlipa. “Ni kweli Yanga wamenifuata mara nyingi, lakini wanakuja wakati ambao nina mkataba. Labda ije itokee ukiisha huu ambao nimebakiza mwaka mmoja, ila kazi yangu ni kucheza ikinihitaji Simba, Kagera Sugar popote nacheza,” anasema.

Mbali na hilo, anafafanua namna anavyokumbana na shutuma kila anapocheza mechi dhidi ya Yanga kuonekana hajitumi kisa baba’ke kacheza huko.“Kama kuna timu nimeifunga basi ni Yanga na nimetoa asisti nyingi za mabao. Simba sijawahi kuifunga. Huwa nanyamaza tu mashabiki wanaponishambulia, akili yangu imekomaa kupokea magumu hayo.”


VITUKO VYA NDONDO

Asilimia kubwa ya wachezaji Kiafrika, wamecheza soka la mtaani (chandimu), kama ilivyo kwa Sure Boy anayesimulia vimbwanga alivyokutana navyo.

Anasema kabla ya kusainiwa Azam FC alikuwa anaichezea Nyuki FC ya mtaani kwao na anakumbuka walicheza mechi ya kirafiki Kigogo katika Uwanja wa Kimtiku ila kilichotokea nusura asitishe ndoto yake ya soka.

“Ni muda mrefu sana na sikumbuki tulicheza na timu gani, ile mechi tulishinda, tukaanza kukimbizwa na wahuni wa Kigogo huku na kule nikapigwa mtama na baunsa mmoja nikaangukia shimoni. Baadaye nikajikongoja kutoka humo na kukimbia.

“Baada ya kutoka pale niliazimia kwamba sitaki tena soka. Nilipolisahau tukio hilo nikarejea tena kufanya kazi hiyo,” anasema.

Tukio lingine ni wakati yupo Nyuki FC walicheza na Agle, Uwanja wa Barafu yalikuwa ni mashindano ya Kombe la Ng’ombe kilichotokea hatakisahau maishani mwake.

“Nakumbuka nilichelewa kufika na mwenzangu Ally Bwabwa, sasa tulipofika tu kipindi cha kwanza kilimalizika ndio kilikuwa kinaanza cha pili, kocha akawa anatufanyia mabadiliko.

“Bwabwa kaniambia nianze kuingia, ila kwa kuwa nilikuwa nafunga kamba ya viatu nikamwambia aingie yeye, ile tu kuingia akapofuka macho. akaanza mwenzenu sioni jamani analia, waliokuwa pembeni wakaanza kucheka wanamwambia aache utani ni wakati wa kazi, kumbe mwenzetu alishikika kweli.

“Eneo la tukio mganga wa timu pinzani alikuwepo pale, akaanza kutuambia msichanganyikiwe mwenzenu ataona na mtego ule ulikuwa wangu mimi. Nilipoona hilo nikavua jezi na mpira ukaishia hapo. Tukaenda kwa Shekh akamsomea dua akaja akaona saa 8:00 za usiku,” anasema.


WASIKIE WAKONGWE

Winga wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel anasema anatamani kumuona Sure Boy anamalizia soka lake nje, baada ya kufanya kazi kubwa nchini.

“Tayari ametuonyesha uwezo wake. Huu ni wakati wa Sure Boy kwenda kucheza nje ya nchi, kwangu mimi ni kati ya viungo bora kabisa katika ligi yetu na amekuwa na mwendelezo wa kiwango chake,” anasema.

Boniface Pawasa, beki wa zamani wa Simba naungana na Gabriel kuhusu Sure Boy akisema: “Wakala anayemsimamia anapaswa kumtafutia timu nje, ili kipaji chake kikaonekane huko. Naamini kabisa atakwenda kufanya vitu vikubwa zaidi.”