Prime
Hamdi hatukumuelewa vizuri, lakini hana deni

MILOUD Hamdi ni wale watoto wa wahamiaji wa Algeria waliozamia Ufaransa. Kiufupi ni kama Zinedine Zidane. Wazazi walikwenda Ufaransa zamani wakitokea Algeria. Yeye alizaliwa Saint-Ettiene pale Ufaransa.
Hamdi amekuja na ameondoka. Amefundisha Yanga miezi sita tu. Amewapa mataji matatu kisha ametimkia zake Ismailia ya Misri. Leo Yanga wametwaa ubingwa baada ya kuibamiza Simba katika dabi halafu keshokutwa akatangazwa kuwa kocha mpya wa klabu maarufu nchini Misri Ismailia.
Wengi hawakumuelewa nami ni mmojawapo. Kuna sababu nyingi za kutomuelewa. Kwanza ni namna alivyoingia zake Yanga. Aliletwa kuwa kocha mpya wa Singida Black Stars, lakini Yanga walipoondokewa na Saed Ramovic ghafla akatua zake Jangwani. Ni katika kile ambacho kinaonekana urafiki wa karibu wa Yanga na Singida. Wote tunaelewa.
Hapa nilimuelewa kwamba alikuja nchini kutafuta pesa. Urafiki wa Yanga na Singida Black Stars ulikuwa haumhusu. Kama alihamia Yanga kwa mshahara ule ule au uliongezeka basi kwake ilikuwa poa tu. Ili mradi awe kazini. Lakini nafahamu kwamba alichopenda ilikuwa kufundisha timu kubwa zaidi nchini kuliko Singida. Lazima aliambiwa kwamba Tanzania kuna timu kubwa mbili tu. Yanga na Simba. Kwanini asuse kwenda Yanga au Simba kwa sababu ameletwa na Singida?
Baada ya kuingia Yanga hapo ndio Miloud alituchanganya na ametuacha ametuchanganya. Yanga iliendelea kuwa ile ile tu. Iliendelea kuwa timu kali. Ni kwa sababu na yeye ni kocha mkali au ni kwa sababu timu ilikuwa ina wachezaji wakali ambao aliwakuta na hakuhusika kuwasajili. Labda Jonathan Ikangalombo na Israel Mwenda ndio wachezaji alioingia nao pamoja klabuni.

Yanga iliendelea kuwa ile ile. Clatous Chama naye akaendelea kusugua benchi katika kikosi cha Yanga. Alikuwa anatokea katika benchi ingawa chini ya Miloud alikuwa anapata dakika nyingi zaidi. Vyovyote ilivyo Yanga waliendelea kuwa wakali na ndio umekuwa utaratibu wao tangu Nasreddine Nabi alipowasili kufundisha Yanga.
Nabi aliifanya Yanga kuwa kali huku Yanga yenyewe ikiongeza makali ya kuchukua wachezaji wazuri kila uchao. Yanga ikawa kali kila kukicha. Baada ya Nabi kudengua Yanga kisha akapewa mkono wa ‘Thank You’ alikuja kocha anayeitwa, Miguel Gamondi. Yanga ikazidi kuwa kali zaidi na zaidi. Usisahau kwamba iliongeza wachezaji mahiri kikosini shukrani kwa tajiri yao GSM.
Baada ya muda mrefu wa kutamba, mwanzoni mwa msimu ulioisha Yanga wakaanza kusuasua. Waliishia makundi. Wakafungwa na Tabora United. Wakayumba kidogo na Gamondi akaondolewa. Wakati ule ilitajwa kwamba kocha na wachezaji wake waliendekeza sana starehe na ndio maana kiwango cha timu kikaanza kushuka.

Baada ya hapo akaletwa Ramovic ambaye hakudumu muda mrefu kwa sababu alipokea ofa nono kwingineko. Inatajwa kwamba samaki mkubwa huwa anamla samaki mdogo. Sisi ni samaki wadogo mbele ya wale jamaa wa Afrika Kaskazini. Ndipo akaja Hamdi. Muda wote huu Yanga ilikuwa ile ile isipokuwa katika kile kipindi kifupi kibovu cha Gamondi.
Hapo ndipo ambapo wengi wanashindwa kumuelewa Hamdi. Alikuwa kocha wa uhakika au alitembelea upepo wa kikosi kikali cha Yanga kilichoundwa kuanzia kwa Nabi hadi sasa. Maana kama ushindi mnono wa mabao matano na yeye ameupata. Yanga walikuwa wakali zaidi baada ya ligi kusimama. Walirudi kama nyuki.
Na katika mwendelezo wa hiki hiki ni kwamba watani wao Simba wamejikuta wakiambulia makali ya Yanga ya Hamdi. Baada ya pambano la watani kurushwa hapa na pale hatimaye walikutana pale Kwa Mkapa na Yanga walionekana kuwa bora katika idara zote kuliko Simba. Ni kwa sababu ya msingi wa Nabi, au makali ya Gamondi, au kilichoachwa na Ramovic? Mashabiki wanaweza kujiuliza.

Binafsi nasimama upande wa Hamdi ingawa sina uhakika sana na kitu ambacho ninakisema lakini nasimama upande wake. Ni kwa sababu naamini kwamba aliiweka Yanga katika nafasi yake ile ile ambayo ilikuwapo awali. Na inawezekana aliipandisha zaidi. Watu walikuwa wanasubiri Yanga iyumbe ili kocha aonekane hana jipya.
Kila kocha anayepita Yanga anaonekana kusubiriwa kutibua kazi ambayo mwenzake amefanya lakini haiwi hivyo. Hamdi naye ameukwepa mtego huo. Wakati mwingine inaacha swali nililouliza hapo juu kama kocha ni mzuri au anatembelea nyota ya mastaa waliopo klabuni. Ukweli ni kwamba kama kocha anaibakiza timu pale pale basi ujue ana jambo.
Licha ya mkataba wa miezi sita nilikuwa najiuliza kwanini Yanga walikuwa wanahusishwa na makocha wapya wakati Hamdi yupo. Siri hii nitawatafuta watu wa Yanga wanieleze kwa kina. Kwamba alikuwa kocha wa kawaida? Kwamba alitembelea nyota ya kikosi kile? Labda wao wana siri nzito katika kifua chao lakini mimi nasimama upande wa Hamdi.
Lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba Hamdi alikuwa anajua mwelekeo wake kabla hata mkataba wake na Yanga haujaisha. Na kuna asilimia nyingi kwamba Yanga walikuwa wanajua na wamekaa mezani na Hamdi na kukubaliana na ndio maana wakaanza kusaka kocha mpya. Nataka kuamini katika hilo.
Nataka kuamini kwamba walitamani kuendelea na Hamdi lakini ofa aliyopata kwa Ismailia ilikuwa kubwa kuliko ya kwao na ndio maana wakaanza mipango mipya. Nataka kuamini pia kwamba Miloud ni bonge la kocha na Ismailia walianza kumfuatilia kabla hajafika nchini na walipogundua kuwa ana mkataba wa miezi sita tu wakaamua kumnyakuwa mapema.

Na sasa deni kubwa linaenda kwa kocha ajaye wa Yanga. Hamdi hajaacha deni. Kuanzia Nabi mpaka sasa hakuna kocha ambaye ameacha deni, labda Gamondi ameacha deni kwa Yanga kutolewa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa. Hata hivyo, kiwango cha Yanga kwa kiasi kikubwa kimeendelea kuwa kile kile tu.
Kinachosubiriwa kwa sasa ni uteuzi wa kocha mpya wa Yanga. Hamdi hajaacha deni lakini kocha mpya anaweza kuwa na deni kama tu atashindwa kuipeleka Yanga mbali katika michuano ya kimataifa. Kuna watu wa Yanga wataanza kumkumbuka Hamdi. Wataamini kwamba labda angewapeleka mbali zaidi.
Wakakumbuka namna ambavyo aliumaliza msimu vema kwa kumchapa mtani katika pambano la machozi, jasho na damu. Watamkumbuka pia jinsi ambavyo aliwachapa kina Jonathan Sowah pale Unguja katika pambano la fainali ya Shirikisho. Ndivyo maisha yalivyo wakati mwingine.