STRAIKA WA MWANASPOTI : Uhondo wa EPL umeanza tutarajie nini?
Muktasari:
Bahati nzuri ni kwamba ligi imeanza wakati dirisha la usajili likiendelea kuwa wazi na kutarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
HATIMAYE Ligi Kuu ya England (EPL) imeng’oa nanga na kuwapa fursa mashabiki kote duniani kurejea kwenye runinga zao ili kuifuatilia. Ligi hii inawafuasi wengi duniani kote, na hata ilipoanza mwishoni mwa wiki ni wengi walioifuatilia kujua kilichojiri katika mechi za awali.
Bahati nzuri ni kwamba ligi imeanza wakati dirisha la usajili likiendelea kuwa wazi na kutarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu. Ligi hiyo imeanza kwa mbwembwe zake za kawaida, timu ndogo zikizishangaza wababe. Mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, Manchester Utd walianza na Tottenham uwanjani Old Trafford. Ilikuwa ni ushindi wa bao 1-0 lililotiwa kimiani na beki wa Spurs Kyle Walker, aliyejifunga. Walker alijaribu kumpokonya straika Wayne Rooney aliyekuwa akijitayarisha kuuweka kimiani na kujifunga na ushindi huo ulikuwa ni zawadi maalum kwa Kocha Louis Van Gaal aliyekuwa akisherehekea miaka 64 za kuzaliwa kwake. Katika hiyo mechi japo United ilishinda lakini haikuonyesha makeke yalizooleka kama wababe wa EPL. Tunaweza kusema kuwa labda bado wachezaji waliosajiliwa bado hawajatulia kwenye klabu hiyo, jambo ambalo linaweza kuchukua muda kiasi kutulia. Hata hivyo mlinda lango Sergio Romeo aliyeanza mechi hiyo badala ya David De Gea alionyesha ukomavu mkubwa sana na nampigia upato kuwa mmoja wa nyota wa United watakaofanya vema msimu huu.
Hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote na alistahimili mashambulizi makali ambayo Spurs iliyafanya dakika za mwisho kabla ya mechi hiyo kumalizika. Mashabiki wa Man United wanangojea kuona ni yapi mazuri yataonekana msimu huu. Lakini cha msingi ni kuwa United lazima iimarishe safu yake ya ulinzi kwani kulionekana udhaifu fulani, udhaifu ambao kama hautarekebishwa itakuwa ngumu kushinda taji hilo msimu huu.
Ni msimu wa tatu sasa umeingia bila wao kutwaa taji lolote lile. Watetezi wa taji hilo Chelsea ‘The Blues’ ilifungua ukurasa kwa kutoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Swansea City nyumbani kwao Stamford Bridge. Matokeo ambayo Kocha Jose Mourinho hakuyafurahia. Lakini ikumbukwe kuwa kama kuna timu ambayo huangaisha miamba wa soka EPL huwa ni Swansea. Kumbuka msimu uliopita iliifunga Man Utd na Arsenal nyumbani kwao na ugenini. Kiungo Oscar aliiweka Chelsea kifua mbele kupitia mkwaju mkali kabla mchezaji Kwame Ayew, mtoto wa Abedi Pele wa Ghana kusawazisha dakika chache baakaye. Ilikuwa ni mechi yake ya kwanza katika EPL baada ya kusajiliwa kutoka Olympique Mersaille msimu huu. Ayew kwa kweli alionyesha ukomavu wake na tayari kulingana na mechi hiyo alivyoicheza tayari ameonekana kutulia. Dakika Chache baadaye Federico Fernandez aliweza kujifunga na kuweka Chelsea kifua mbele kabla ya Bafetimbi Gomis kusawazisha kupitia mkwajo wa penalti baada ya kuangushwa kwenye eneo la hatari na mlinda lango wa Chelsea Thibaut Courtois ambaye alionyeshwa kadi nyekundu. Swansea na hicho kiwango walionyesha Stramford Bridge itabakia moja ya timu ndogo ambazo kwa kweli zitahaingaisha msimu huu. Mchezaji wao Montero alikuwa mwiba mkubwa sana katika safu ya ushambulizi na usumbufu wake ndio uliompa Mourinho kutotulia katika benchi lake.
Siku ya Jumapili wapiga mitutu Arsenal, vijana wa Emirates walijitosa uwanjani kumenyana na klabu ya West Ham United. Matokeo hayakuwa mazuri kwa wafuasi wa Arsenal kwani dakika chache kabla mechi hiyo kukamilika tulishuhudia wafuasi hao wakiondoka uwanjani shingo upande baada ya kunyukwa mabao 2-0 nyumbani. Arsene Wenger amekuwa na tabia ya kutosajili wachezaji wa kimataifa, jambo ambalo limekuwa likimponza kila wakati. Klabu nyingine zimenunua wachezaji, lakini Wenger mchezaji mkubwa ambaye alisajiliwa alikuwa Petr Cech pekee kutoka Chelsesa. Kumekuwa na tetesi za hapa na pale za kutaka kumsajili Karim Benzema kutoka Real Madrid, na nina uhakika ya kwamba atafanya usajili huo iwapo anatarajia kugombea taji hilo msimu huu. Kumbuka kwa sasa ana mshambuliaji mmoja tu, Olivier Giroud ambaye Jumapili aliendelea na mtindo wake wa kawaida wa kupoteza nafasi za wazi. Iwapo Arsene Wenger anataka taji hilo itabidi aingie sokoni. Ni miaka 11 sasa tangu Arsenal ilitwa taji la EPL mara ya mwisho. Na tulichokishuhudia cha kufungwa nyumbani na West Ham kupitia mabao ya Kouyate na Zarate itabakia kuwa wimbo ule ule siku nenda siku rudi. Nina uhakika kupoteza hiyo mechi inampa Wenger usingizi wa mang’amng’amu, hatalala. Nawahakikishia ndani ya siku 21 zijazo kabla ya dirisha la usajili kufungwa atakuwa amesajili wachezaji wasiopungua wawili hivi akiwemo Karim Benzema.
Hayo yakitendeka a Liverpool, miamba wa soka waliosahaulika ilianza kampeni yao msimu huu kwa kuinyuka Stoke City bao 1-0, bao lililofungwa kwa njia ya ustadi sana na Mbrazili Courtinho. Liverpool kwa mda mrefu imekuwa ikianza ligi kwa kusuasua lakini msimu huu ikiwa ugenini ilifurahisha mashabiki wao kwa ushindi huo mkubwa. Itabakia kutazama ikiwa itaendelea na mziki huo hadi mwisho wa msimu. Mbali na miamba wa soka Chelsea, Man Utd na Arsenalikuanza ligi kwa hatihati kulikuwa na mechi nyingine za kusisimua. Leceister iliibomoa Sunderland kwa kipigo cha mabao 4-2, Bournemouth wageni katika ligi kuu msimu huu ililambishwa 1-0 nyumbani kwao na Aston Villa, Everton ikaponea chupuchupu kwa sare ya 2-2 dhidi ya Watford, huku Newcastle ilitoka sare ya 2-2 na klabu ya Mkenya Victor Wanyama, Southampton. Wakati huo huo Klabu ya Norwich ilikubali kupokea kichapo cha mabao 3-1 nyumbani kwao dhidi ya Crystal Palace na jana usiku tulikuwa tukisubiri kushuhudia wababe Manchester City kujitupa nyumbani kukata utepe wa EPL msimu huu.
Kwa kifupi ni kwamba vumbi la EPL limeanza na tutashuhudia uhondo kwa miezi 10 ijayo kabla ya kupatikana mshindi. Ni mapema kuanza kutabiri, muhimu tusubiri tuone itakavyokuwa.