Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Grealish? England ni sayari nyingine ile

Muktasari:

  • Ni kama mama na mwanawe hata kama ni mwizi, mchokozi bado ataendelea kumlinda na kumsemea mazuri haijalishi majirani wanamuonaje. Kirahisi namna hiyo, bei za wachezaji wa soka raia wa England zimekuwa kubwa. Ni jambo la kushangaza kuamini Jack Grealish alinunuliwa kwa Pauni 100 milioni na Manchester City kutokea Aston Villa, ndio. Hadi sasa ndiye mchezaji wa pili kununuliwa kwa pesa nyingi zaidi pale England tangu kuumbwa kwa misingi ya nchi hiyo.

NENDA Google andika chochote unachotaka kujua kuhusu wachezaji wa England utapata majibu yake hata kama kilifanyika kabla ya Tanzania kupata Uhuru. Siyo kwamba wao wameendelea sana katika teknelojia tangu miaka hiyo, hapana. Lakini, wanaishi sayari yao na walichagua tu kusemea vya kwao haijalishi wewe unavionaje.

Ni kama mama na mwanawe hata kama ni mwizi, mchokozi bado ataendelea kumlinda na kumsemea mazuri haijalishi majirani wanamuonaje. Kirahisi namna hiyo, bei za wachezaji wa soka raia wa England zimekuwa kubwa. Ni jambo la kushangaza kuamini Jack Grealish alinunuliwa kwa Pauni 100 milioni na Manchester City kutokea Aston Villa, ndio. Hadi sasa ndiye mchezaji wa pili kununuliwa kwa pesa nyingi zaidi pale England tangu kuumbwa kwa misingi ya nchi hiyo.

Kirahisi sana ilifikia hatua ya Jesse Lingard kufananishwa na Lionel Messi, Aaron Rasmdale akatajwa kama mmoja wa makipa bora duniani. Phil Foden akapigiwa debe kushinda tuzo ya Ballon D’or.

Wakati mwingine unawaza tu. Ingekuwaje kama Lamine Yamal, staa wa Barcelona angekuwa raia wa England? Ingekuwaje Pedri angekuwa raia wa England. Ndio wako hivyo.

Hata wakati Dunia inawaimba Cristiano Ronaldo na Lionel Messi pale La Liga, England walikuwa wakiimba EPL yao haijalishi ina wachezaji wa aina gani. Haijalishi wengine wamefanyaje. Wao kwao ni kuzuri hata kama unakuona kubaya. Kwao ile sio ligi tu, ni ligi yenye levo ya kuvuka dunia.

Namna hii ndoa nyingi sana za hasara zimefungwa. Waulize Manchester United na Harry Maguire wao. Waulize Man City kuhusu Grealish wao, mtoto wa Kiingereza halisi. Tulimfahamu sana wakati Mbwana Samatta anaichezea Aston Villa. Lakini ndoa ya Grealish imekuwa na mbilinge nyingi za nje ya uwanja kuliko ndani ya uwanja. Tovuti za takwimu zinaonyesha kuwa msimu uliopita alicheza mechi 20 tu akifunga mabao matatu na kutoa asisti tano.

Muda mwingi ungeona picha zake akiwa anatoka klabu asubuhi akiwa hajiwezi kwa kilevi, muda mwingine ungemuona anatamka hadharani anapaswa kuitwa timu ya taifa licha ya kutokuwa na kiwango bora na ungeona wachambuzi wakimsapoti. Hiyo ndio England. Ni rahisi kukuaminisha mchezaji wa kawaida kuwa anafaa kushinda hata tuzo ya mchezo bora wa sayari zote.

Mapema wiki hii kocha Pep Guardiola na Man City wamemuonyesha mlango wa kutokea Grealish. Hawataki tena kuendelea kuwa naye. Inawezekana ni uamuzi sahihi, lakini huenda walihitaji kuufanya muda mrefu.

Pengine hawakuhitaji hata kumsajili wakati ule, lakini ile ni sayari nyingine. Yanayotokea pale ni ngumu kuyaona sehemu nyingine. Huwezi kuwalaumu Man City kwa hilo.

Grealish anakunja mshahara wa Pauni 300,000 kwa wiki - kiasi kinachomfanya kuwa mmoja kati ya wachezaji wanaovuna pesa nyingi zaidi EPL. Achana na pesa za mshahara ukijumlisha na zile walizolipa kama pesa za usajili kwa jumla Man City imepoteza zaidi ya Pauni 150 milioni hadi sasa tangu 2021 ilipomsajili.

Ajabu wakati Chelsea inataka kumsajili Victor Osimhen mwaka jana haikuwa tayari kumpa hata karibu ya mshahara huo na dili liliripotiwa kufa kwa sababu hiyo. Osimhen ni bora kuliko Grealish? Hapana. Ni vile tu amezaliwa na kukulia katika ‘sayari nyingine’.

Wakati huu ambao Man City imemuonyesha mlango wa kutokea Grealish usishangae ukaona kampeni za kumhusisha na timu kubwa za nje ya England.

 Usishangae kuona anakwenda kupokea mshahara mkubwa kuliko atakaoupokea Lamine kwenye mkataba mpya. Hilo lisikutishe.

Kwao, EPL ni ligi ambayo haijawahi kushuka kwa ubora. Haitawahi na haitakaa itokee.

Hii ndiyo sababu waliwasema sana baadhi ya mastaa wa England walioondoka kwenda kucheza Ligi Kuu Saudi Arabia kina Ivan Toney na Jordan Henderson.

Ndiyo maana haikuchukua muda mrefu Henderson kuishi Al-Ettifaq na badala yake akaamua kurudi Ulaya.

Siyo kwa sababu alichoka kucheza huko, bali alifahamu Waingereza wasingemsamehe kwa namna yoyote ikiwa angeendelea kubaki huko.

Achana na hadithi za hawa kina Grealish, Maguire na hata Mason Mount tegemea kuona idadi kubwa ya wachezaji wa kawaida wakipata shavu kubwa na kununuliwa kwa bei mbaya kwa sababu wale hawaishi katika hii sayari yetu, kila kitu ni tofauti kwao.

England ndiyo mahala timu inayoshuka daraja inapata pesa nyingi kuliko bingwa wa Ligue 1.

Ndiyo hapo kampuni hulipa pesa nyingi kwa ajili ya kununua haki za matangazo ya televisheni kuliko sehemu nyingine yoyote duniani.

Usishangae sana, ile ni sayari nyingine.