MUKASA: Kuna Mpanzu, halafu Pacome... Kuhusu wimbo wa Mimina ilikuwa hivi

Muktasari:
- Mwanaspoti limefanya mahojiano na Mukasa baada ya kuibuka mtunzi bora wa mwaka 2024 wa nyimbo za dini, anasema kiufundi lazima kujua machaguo sahihi ya ufunguzi, kiitikio kuilazimisha hadhara kuimba wimbo, aina ya mdundo uendane na kile kinachoimbwa, hivyo ni baadhi.
MTUNZI mbobevu wa nyimbo za dini na taasisi mbalimbali nchini, Bernard Mukasa amezungumzia muziki kwa jumla ili uweze kupokelewa katika jamii vipo vitu vingi vya kuzingatia.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na Mukasa baada ya kuibuka mtunzi bora wa mwaka 2024 wa nyimbo za dini, anasema kiufundi lazima kujua machaguo sahihi ya ufunguzi, kiitikio kuilazimisha hadhara kuimba wimbo, aina ya mdundo uendane na kile kinachoimbwa, hivyo ni baadhi.

Mshindi huyo wa tuzo mbili za nyimbo za dini, mbali na kubobea kwenye muziki huo, pia ni mfuatiliaji mkubwa wa soka na amekitaja kikosi chake kwa msimu huu wa 2024-2025 akiwajumuisha mawinga, Ellie Mpanzu na Pacome Zouzoua, huku akifichua jinsi Fiston Mayela na Haruna Niyonzima walivyomvuruga enzi wakiwa Yanga. Kivipi? Endelea naye...!
MSHINDI WA TUZO
"Nimechukua tuzo mbili ya mtunzi bora wa nyimbo za dini Tanzania kwa mwaka 2024, kupitia wimbo wa Mshauri wa Ajabu ila kwa jumla nyimbo nilizoziandika ni nne, zinazoimbwa na kwaya tofauti zote ziliingia fainali, kama 'Usiogope Nenda', 'Kaburi Wazi na Amani' na Salama," anasema na kuongeza;
"Tuzo ya pili kama mwanakwaya wa kwaya ya Mtakatifu Kizito Makuburi, tumechukua tuzo ya kwaya bora kwa muziki wa dini wa nyota ya mwaka 2024."

Anasema Mwaka 2005 alichukua tuzo ya Kilimanjaro Music Awards ya mtunzi bora wa jumla wa nyimbo za kidunia na dini, washindani wake walikuwa Tx Moshi William (marehemu), muimbaji wa taarabu, Mzee Yusuph, muimbaji wa nyimbo za dini, Bahati Bukuku na msanii wa Bongo Fleva, Ferooz.
MIMINA NEEMA
Kwa mara ya kwanza Mukasa analiambia Mwanaspoti namna alivyopata wazo la wimbo wa Mimina Neema lilitokana na maji akiwa maeneo anapata kinywaji.
"Wazo la wimbo wa Mimina Neema niliuandika wakati tunaandaa albamu yetu ya 11 ya kwaya ya Mtakatifu Kizito, ulitakiwa wimbo mfupi wa kubeba albamu hiyo, hivyo tukapewa kazi mimi na mwalimu mwenzangu," anasema na kuongeza;
"Siku moja nikiwa na mke wangu tulienda Maua Social Hall kupata kinywaji na kitafunwa, mezani nilikuwa na karatasi na kalamu, wakati naona watu wanamimina vinywaji katika glasi na mimi nikawa na chupa ya maji na glasi, wakati tunaendelea kutumia vinywaji hivyo ndipo wazo la wimbo wa Mimina Neema liliponijia.
"Nilichokizingatia ili jamii iupokee wimbo huo, nilitafuta neno moja tu ama mawili ambayo yatakuwa yanajirudiarudia mara kwa mara ndipo nikapata Mimina Neema na nikaanza kuandika Kiitikio 'Chorus' baadaye nikaumaliza wimbo mzima kwa muda mfupi, tulipoenda katika vikao vya kamati ukapokelewa na umekuwa maarufu hadi leo, umetimiza miaka 10."
WASANII WA KIDUNIA
"Japokuwa sichangamani na wasanii wa muziki wa kidunia, ila baadhi yao nimewahi kushauriana nao jinsi ya kufanya muziki mzuri kama Bushoke, Mwinjuma Muumini. Tulijadili namna nyimbo zake zinatakiwa kuishi, uchaguzi wa ufunguo sahihi, namkubali ana kipaji kikubwa na anahitaji vitu vichache vya kwendana na muziki wa kisasa, msanii mwingine ni Saida Karoli," anasema na kuongeza;
"Nimetunga nyimbo nyingi za tasisi mbalimbali kama bima ya afya, Tamisemi, shule, wimbo wa Afcon ya vijana iliyofanyika hapa Tanzania na mchezaji mmojawapo aliyekuwepo kikosi cha Serengeti Boys ni Kelvin John ila ilishika nafasi ya pili, kwa hiyo haikupigwa siku ya tukio ila ipo siku nitauachia, naamini utapokelewa vizuri. Pia nina oda ya kuandika wimbo kuhusu hospitali ya Taifa ya Muhimbili."
FAMILIA YA MUZIKI
"Familia yangu ni ya muziki kwa maana ya mke wangu anaandika na kuimba nyimbo zake maarufu zaidi ni 'Tuepushiwe Ubinafsi', 'Mji Ule', watoto wangu pia wanaimba na kutunga, hivyo kama familia tuna albamu tatu na ya nne tunatarajia kuiachia Julai," anasema Mukasa ambaye kitaaluma ni mtalaamu wa masoko.
Anasema kwa makadirio ya nyuma alikuwa na nyimbo zisizopungua 3000: "Nitarudi kuzihesabu tena kujua zimefika nyimbo ngapi maana zingine naziachia katika mitandao ya kijamii na zina wafuasi wengi."
UMAARUFU
"Changamoto ya umaarufu ni matarajio kutoka kwa jamii inayomchukulia mtu wa aina hiyo ni tajiri wakati siyo hali halisi wakikutegemea kwa sapoti za maendeleo ya kiwango ambacho huwezi kumudu pia kuna aina ya maisha lazima kuachana nayo. Mfano siwezi kwenda baadhi ya sehemu ambayo nikipigwa picha sitakuwa na neno la kujitetea, unalazimika kuishi katika picha waliyokuchorea," anasema na kuongeza;
"Zamani nilikuwa nikisafiri nilikuwa sichagui nyumba za wageni za kufikia ila siyo kwa sasa, kuna siku nilienda Mahenge tukafika saa 7:00 usiku, tukashikwa na njaa na sehemu iliyokuwa wazi ni baa, nilimwomba dereva ashuke akaangalie chakula, akawa ananilazimishe niende naye kwani hakuna wa kunifuatilia muda huo, aliposhuka mwenyewe kukazuka ugomvi wakaanza kupigana na chupa na akaponea chupuchupu, aliporudi nikamwambia mfano ningepigwa ningejieleza kitu gani kwa tukio hilo."
MAYELE, NIYONZIMA
Anasema mashabiki kuomba kupiga picha ni jambo la kawaida kwake na mkewe, ila iliwahi kutokea akajikuta anaona wivu kwa mbali baada ya mwenza wake kuomba kupigwa picha na mastaa wa zamani wa Yanga.
"Nakumbuka tulienda Mlimani City na mke wangu akamuona Fiston Mayele akiwa Yanga, akamuomba kupiga naye picha kwa Kifaransa, akakubali, alikuwa na furaha iliyopita kiasi, kuna namna nilijihisi vibaya ingawa mwishowe nikakubaliana na hali kwa sababu mimi naye ni mashabiki wa Yanga," anasema na kuongeza;
"Mchezaji mwingine akiwa katika kiwango kikubwa sana Yanga ni Haruna Niyonzima pia alikuwa na furaha sana hadi nikawa najiuliza inakuaje, sijawahi kumwambia hilo kama niliona wivu, ataona kupitia mahojiano yenu, pamoja na hayo yote nilimsafishia picha zake na kuzitunza."

KIMATAIFA SIMBA, YANGA
"Simba na Yanga kimataifa kwa sasa zipo vizuri, isipokuwa ziboresha katika uwekezaji wa usajili, watofautishe wachezaji wa kuwapeleka katika michuano hiyo na ambao watacheza michuano hiyo. Mfano kilichoikosesha Yanga taji ni Khalid Aucho kupata kadi akakosekana mbadala wa kufiti nafasi yake, kwa Simba wamekosa ubingwa kwa kadi aliyopewa Yusuph Kagoma kwani hawakutetereka ila alikosekana mtu wa kutuliza mipira," anasema.
KIKOSI CHAKE BORA 2024/25
Mukasa amekianika kikosi bora kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara 2024-2025 na amewajumuisha Djigui Diarra, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Dickson Job, Ibrahim Hamad 'Bacca', Adolf Bitegeko, Maxi Nzengeli, Elie Mpanzu, Prince Dube, Pacôme Zouzoua na Gibril Sillah, huku kocha wa kikosi hicho ni David Fadlu.
"Mfano kocha Fadlu angekuwa Yanga ingechukua ubingwa wa CAF msimu huu. Kocha wa kiwango cha aina yake kwa miaka ya hivi karibuni Simba ni Patrick Aussems 'Uchebe', kwa Yanga ni Nasreddine Nabi na Miguel Gamondi. Walileta ladha katika ligi ya Tanzania kwani aina ya upangaji wao wa timu haukuwahi kuzoeleka," anasema Mukasa.