Stars kufuzu Afcon 2025 ni vita ya pointi 10
Muktasari:
- Stars na Ethiopia ambazo zinakutana kwa mara ya kwanza tangu Novemba 2015, zimepangwa katika Kundi H pamoja na Guinea ambao walishika nafasi ya pili katika Afcon ya 1976 na mabingwa mara mbili Congo DR.
TAIFA Stars, usiku wa leo inaanza vita ya pointi 10. Ni kampeni ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2025 nchini Morocco.
Itacheza na Ethiopia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa saa 1:00 usiku.
Kimahesabu ni kwamba kwa namna yoyote ile ili Stars ifuzu fainali inahitaji kupata si chini ya pointi 10 kwenye kundi hilo.
Kwa lugha nyingine ni kwamba lazima kwa namna yoyote ipate pointi 9 za nyumbani kwa kuanzia na mechi ya leo na zingine mbili kisha ipate walau sare moja ugenini.
Zikizidi siyo mbaya watanufaika na mkwanja wa Mama kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Stars na Ethiopia ambazo zinakutana kwa mara ya kwanza tangu Novemba 2015, zimepangwa katika Kundi H pamoja na Guinea ambao walishika nafasi ya pili katika Afcon ya 1976 na mabingwa mara mbili Congo DR.
Ni nafasi tena kwa Tanzania kwenda Afcon baada ya kushiriki fainali tatu za 1980, 2015 na msimu uliopita 2023 kule Ivory Coast.
Stars ambao walikuwa wakicheza Afcon kwa mara ya tatu, walipoteza kwa magoli 3-0 dhidi ya Morocco katika mechi yao ya kwanza ya Kundi F Januari 17 kabla ya kutoka sare mbili mfululizo dhidi ya Zambia na Congo DR, na kumaliza nafasi ya mwisho kwenye msimamo wakiwa na pointi mbili.
Baada ya matokeo hayo nchini Ivory Coast, Tanzania imepata matokeo mazuri kwa kushinda mechi tatu na kutoka sare moja kati ya sita walizocheza huku wakifunga magoli sita na wakicheza bila ya kuruhusu bao katika michezo minne. Wamepoteza mechi mbili ambazo ni dhidi ya Bulgaria (1-0) na Sudan (2-1).
Kikosi cha Kaimu kocha mkuu kwa Stars, Hemed Suleiman kitaingia kwenye mchezo wa leo, kikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa kuvutia wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa wa Afrika wa mwaka 2012 Zambia katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia Juni 11, kwa goli la Waziri Junior katika dakika ya tano.
Baada ya ushindi dhidi ya Zambia, Tanzania sasa imepata pointi sita kutoka mechi zao tatu za kwanza katika Kundi E na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo huku wakilenga kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Wakati Tanzania wakitafuta kuendeleza kutoka walipoishia Juni na kuanza kampeni yao ya kufuzu Afcon kwa ushindi, watakutana na timu pinzani ambayo haijapoteza dhidi yao katika mechi 17 kati ya 23 zilizopita, ikishinda mara 10 na kutoka sare mara saba tangu Februari 1969.
Akizunguzia maandalizi ya kikosi chake na utayari wa wachezaji wake katika mchezo huo, Hemed amesema; “Kwanza kabisa nitoe wito kwa Watanzania wote kujitokeza uwanjani kwa ajili ya kutusapoti, mimi kama kocha na wasaidizi wangu tumemaliza kazi yetu ya kuandaa timu na vijana wapo tayari kwa mchezo,”
“Tumepata nafasi ya kuwaona na kuwasoma wapinzani wetu hivyo tunajua ni kwa namna gani tutakabiliana nao, uzuri tulifanya uchaguzi wa kikosi chenye wachezaji ambao wapo fiti hivyo tulikuwa na kazi moja tu ya kuingiza mbinu zetu kwao kwa ajili ya mchezo husika maana muda ulikuwa mchache.”
Kwa upande mwingine, Ethiopia haikuanza vizuri katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia kwani walilazimika kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Djibouti katika Uwanja wa Stade El Abdi Juni 9.
Gabriel Dadzie alifunga bao katika dakika ya 29 na kuiweka Djibouti mbele lakini wageni walijibu mapigo dakika mbili baadaye kupitia Menyelu Wondimu kabla ya kujihami kipindi cha pili ili kuhakikisha sare hiyo.
Kwa matokeo hayo, Ethiopia sasa imeshindwa kushinda mechi yoyote kati ya nne za Kundi A za kufuzu Kombe la Dunia, wakipata sare tatu na kupoteza moja, na kukusanya pointi tatu kati ya 12 na kushika nafasi ya tano.
Kocha wao, Gebremedhin Haile amewahimiza wachezaji kuendeleza mazuri waliyoyafanya katika mchezo dhidi ya Djibouti huku wakiboresha mapungufu yao wakati wanapoanza kampeni yao ya kufuzu Afcon.
“Tanzania wamekuwa na muendelezo mzuri kwa sasa lakini sisi tumekuja hapa kwa ajili ya kupigania matokeo na kuanza vizuri safari ya kwenda Afcon,” alisema.
Ethiopia inaingia katika mechi ya leo bila ushindi katika mechi zao 11 za mashindano, wakipoteza sita na kutoka sare tano tangu waliposhinda 1-0 dhidi ya Rwanda katika mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani mwezi Septemba 2022.
UKUTA CHUMA
Uwepo wa mabeki watatu wa kati wa Yanga, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Bakari Mwamnyeto unatazamwa kama uti wa mgongo wa ukuta wa Taifa Stars kutokana na nyota hao kucheza kwao pamoja kwa zaidi ya miaka mitatu wakiwa Jangwani.
Mabeki hao wamekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Yanga ndani ya msimu mitatu wakitwaa mataji ya ndani na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika misimu miwili iliyopita huku uliopita wakicheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nyota hao walikuwa kizuizi kwa vigogo wengi wa soka la Afrika ikiwemo Mamelodi Sundowns ambayo haikupata bao dhidi ya Yanga ndani ya dakika 180 za michezo yote miwili ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa Afrika.
Bado mabeki hao wanaweza kuendelea kuwa msaada kwa Tanzania katika mchezo wa leo na hata ijayo katika safari ya kupigania tiketi ya kwenda Afcon.
MZIZE, WAZIR JR
Kufanya vizuri kwa mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize kwa sasa inaweza kuwa karata muhimu kwa Hemed katika mchezo wa leo, ikumbukwe pia nyota huyo alifanya vizuri pia hata katika mchezo wa mwisho kwa Stars dhidi ya Zambia.
Mzize na Wazir ambaye kwa sasa anaichezea Dodoma Jiji walitumika kwa pamoja katika mchezo ule, mmoja alishambulia akitokea pembeni hivyo kwa pamoja waliwafanya Zambia kuwa na wakati mgumu.
Huenda katika mchezo huu, Hemed akaanza na washambuliaji wote wawili kama ilivyokuwa dhidi ya Zambia na hata kama ataanza na mmoja bado Stars inaweza kuwa na makali katika safu yake ya ushambuliaji kutokana na ubora wa washambuliaji hao, Wazir ndiye mshambuliaji wa kati halisi aliyemaliza msimu uliopita akiwa na mabao mengi zaidi (12).
KIKOSI ETHIOPIA
Kwa upande wa Ethiopia, Abel Dele, Mesfen Tafese mwenye umri wa miaka 22 na mshambuliaji wa Mamelodi Sundowns Abubeker Nasir, ambaye ana magoli matano katika mechi 22 za timu ya taifa, wameachwa nje kutokana na majeraha.
Wachezaji ambao wametua Tanzania kwa mchezo wa leo ni pamoja na nyota wa Ethiopia Commercial Bank, kipa Firew Getahun, beki Suleiman Hamid na Fetuddin Jemal wameitwa, huku beki Fraser Kass akikosa mechi ya leo kutokana na matatizo ya pasipoti yake.
Canaan Markneh, Gatoch Panom na Binyam Belay walianza mechi dhidi ya Djibouti na wanatarajiwa kuendelea katika nafasi zao katikati ya uwanja.