SPOTI MIKIKI: Mwaka wa medali, machozi na Jasho

Muktasari:
- Wanamichezo wa ngumi na kriketi wanaufunga vizuri mwaka baada ya kufuzu na kufanya vizuri kimataifa na utabaki kuwa mwaka wao wa medali.
Tunajiandaa kuanza mwaka mpya wa 2025, familia ya michezo ya ‘non soccer ‘ itaendelea kuuukumbuka mwaka 2024 unaoelekea ukingoni, katika maeneo matatu ya medali, machozi na jasho.
Wanamichezo wa ngumi na kriketi wanaufunga vizuri mwaka baada ya kufuzu na kufanya vizuri kimataifa na utabaki kuwa mwaka wao wa medali.
Kriketi ndiyo walifungua dimba kwenye mafanikio hayo mapema Aprili baada ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia.
Timu hiyo ilifuzu baada ya kutinga fainali kwenye mashindano ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 19.
Iliifunga Rwanda kwa mikimbio 59 katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika kwenye Viwanja vya Dar Gymkhana, Dar es Salaam.
Kwa kuingia fainali, Tanzania ilijihakikishia moja kwa moja nafasi ya kupanda daraja kutoka Divisheni ya Pili hadi ya Kwanza kwa mujibu wa Sheria za Chama cha Kriketi cha Dunia (ICC), timu nyingine iliyokula shavu ni Sierra Leone iliyoifunga Nigeria katika mchezo mwingine wa nusu fainali.
Tanzania ndio ilikuwa mwenyeji wa michuano ya kufuzu iliyoshirikisha mataifa manane ya Afrika, ikishinda mechi zake zote nne kwa kishindo dhidi ya Nigeria, Ghana, Msumbiji kabla ya kuitoa Rwanda.
Ndondi wavuna medali
Machi 22, ilikiwa ‘tamu’ kwa Watanzania na wapenzi wa ngumi za ridhaa baada ya kuvuna medali tatu kwenye michezo ya Afrika (All African Games).
Mabondia wa timu ya taifa, Ezra Paul, Yusuph Changarawe na Mussa Maregesi walivuna medali hizo za shaba kila mmoja kwenye michezo hiyo iliyofanyika mjini Accra, Ghana.
Olimpiki ya jasho
Julai ilikuwa ya jasho kwa Watanzania saba walioiwakilisha nchi kwenye michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, iliyofanyika nchini Ufaransa.
Mcheza judo, Andrew Thomas Mlugu ndiye alikuwa Mtanzani wa kwanza kuondoshwa mashindanoni baada ya kupoteza pambano lake la raundi ya pili.
Waogeleaji, Collins Saliboko na Sofia Latiff nao walishindwa kupenya raundi inayofuata kwenye michezo hiyo.
Tegemeo pekee likasalia kwa wanariadha, Alphonce Simbu, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu ambao walikimbia Agosti 10 na 11.
Wote kwa pamoja hawakushinda medali huku mwanariadha mwingine,
Gabriel Geay akishindwa kuchuana kutokana na majeraha kwenye kifundo cha mguu wa kulia.
Mwaka wa machozi
Ulikuwa ni mwaka mgumu wa machozi kwenye tasnia ya ngumi na riadha ambazo ziliwapoteza wapendwa wao.
Miongoni mwa matukio ya kuhuzunisha ni lile la Novemba 30, bondia wa ngumi za kulipwa, Abassi Mselemu alipoteza maisha baada ya kudondoka kwenye pambano la ‘Usiku Wa Left Hook Ya Baba Mwinyi’ kwenye Ukumbi wa Zanzibar Golf Club.
Bondia huyo alipigwa ulingoni na kupoteza fahamu kisha kufariki Desemba 1, 2024 visiwani Zanzibar na mwili wake kuzikwa Dar es Salaam.
Mselemu alicheza pambano la utangulizi la raundi 6 dhidi ya bondia Bakari Bakari, ilipofika raundi ya mwisho alianguka na mwamuzi kumaliza pambano.
Aliwahishwa Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Unguja kutokana na afya yake kutokuwa sawa ambapo umauti ulimkuta akiwa anasubiri kufanyiwa upasuaji.
Isangula afariki
Ni mwaka ambao, bondia mkongwe wa timu ya taifa, Willy Isangula alipoteza maisha.
Bingwa huyo wa Afrika kwenye michezo ya 1987 alifariki baada ya kuugua kwa zaidi ya miaka minane.
“Alipooza kwa muda mrefu, ikasababisha akawa hatembei kabisa, aliendelea na matibabu lakini hivi karibuni alizidiwa tukampeleka hospitali hadi alipofariki akiwa anapatiwa matibabu Hospitali ya Muhimbili,” ilikuwa ni kauli ya simanzi ya mtoto wa marehemu, Joseph Isangula.
Gidabuday agongwa na gari
Septemba 10,2024 pia itabaki kwenye kumbukumbu ya wadau wa riadha nchini waliompoteza aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday.
Gidabuday alifariki saa 7 usiku wa kuamkia Jumanne ya Septemba 10, 2024, baada ya kugongwa na gari eneo la Maji ya Chai, mkoani Arusha na kufia hapo hapo.
Aligongwa kwenye eneo hilo akiwa ameshuka kwenye gari akielekea nyumbani kwake.
Wapenzi wapoteza maisha
Nchini Kenya, mwanariadha wa Olimpiki wa Uganda Rebecca Cheptegei na mpenzi wake Dickson Marangach walifariki dunia.
Wapenzi hao walifariki nyakati tofauti wakiwa Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) Hospitali ya Rufaa ya Moi, wakati wakipatiwa matibabu ya moto wa petroli walioungua.
Cheptegei ndiye alianza kupoteza maisha, siku kadhaa baadaye Marangach naye akafariki.
Cheptegei alifariki dunia Septemba 5, 2024 wakati akipatiwa matibabu ya majeraha aliyoyapata baada ya kumwagiwa petroli kisha kuchomwa moto na mpenzi wake huyo huku sababu ikitajwa ni ugomvi uliosababishwa na mgogoro wa kiwanja pamoja na nyumba.