Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SPOTI DOKTA: Wanasoka kujifua ufukweni iko hivi

Dokta Pict

Muktasari:

  • Watani wao, Yanga walishinda 1-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa huko Mauritania, hivyo kuweka matumaini ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

JIONI na usiku wa Jumapili mambo yalikuwa mazuri sana kwa wadau wa soka ndani na nje ya Tanzania. Timu ya Simba ilipata sare ya 1-1 katika mechi yake dhidi ya Bravos Do Maquis na kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).

Watani wao, Yanga walishinda 1-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa huko Mauritania, hivyo kuweka matumaini ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

Nje ya Tanzania ulishuhudiwa mtanange wa Kombe la FA kati ya Manchester United na Arsenal na kule Saudi Arabia kulikuwa na mechi kali ya El Clasico kati ya mahasimu wa Hispania, Real Madrid na Barcelona katika fainali ya Super Cup.

Katika michezo hii tulishuhudia kandanda la kuvutia lililojaa ufundi mwingi na huku wachezajo wakionekana kuwa timamu kimwili kutokana na unyumbulikaji na kucheza kwa ustahimilivu wa juu.

Katika utimamu wa wachezaji wengi wa kulipwa katika soka huwa hawategemei pekee katika mazoezi ya utimamu wanayopewa na benchi la ufundi bali pia wanajiongeza ikiwamo kujifua ufukweni wakati wa majira ya kiangazi.

Kujiongeza kwa wachezaji si jambo geni kwani hata mastaa kama Kylian Mbappe, Lamine Yamal, Vinicius Junior, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, wamekuwa na tabia ya kujifua ufukweni kutengeneza utimamu.

Siri kubwa ya kujifua ufukweni kwa wanasoka ni kutokana na mazoezi hayo kuchoma zaidi kiasi kikubwa cha mafuta yaliyorundikana mwilini.

Tumeona pia juzi timu ya Taifa ya Zanzibar ikitwaa Kombe la Mapinduzi 2025. Mtakumbuka wachezaji wanaotoka kanda ya pwani huwa na kawaida kujifua ufukweni.

Ufukweni huwa na eneo kubwa, mchanga mwingi, hewa ya kutosha na utulivu mwingi.

Wanamichezo wengi wa maeneo ya Pwani wamekuwa wakifanya hivyo katika muda wao wa ziada ikiwamo siku ambazo hawana mazoezi ya klabu au wakati ambao hawana mechi yoyote.

Si hapa Bongo tu, hata katika nchi kama Brazil ni moja ya nchi ambazo wanasoka wengi hutumia utamaduni wao wa kucheza soka la ufukweni kama njia ya kujenga utimamu wa mwili.

Uchanganyaji wa mazoezi ya kukimbia ufukweni pamoja na kuogelea baharini yana faida kubwa kwa mchezaji kwani anapata utimamu bora wa mwili na hatimaye kulinda pia kiwango chake.

Kujifua ufukweni ni moja ya mbinu ambazo inatumiwa sana kwa miaka mingi na wanasoka wengi wa maeneo ya pwani kama utamaduni kwa ajili kujiburudisha na kutengeneza utimamu wa mwili.

Leo nitawapa ufahamu wa faida na hasara za kujifua fukweni kwa wanasoka.


FAIDA HIZI HAPA

Zoezi hili humfanya mchezaji kuchoma kiasi kikubwa cha sukari (mafuta) ya mwilini kutokana na wakati anakimbia au kucheza soka misuli ya miguu hutumia nguvu nyingi kukimbia na kucheza.

Ufukweni kuna mchanga mwingi sana, wakati wa kukimbia miguu huzama katika rundo la mchanga hivyo kuipunguza kasi na kuhitaji kutumia nguvu kuinyanyua tena ile kupiga hatua na kikimbia.

Hali hii ndiyo inayochangia mwili kutumia nguvu nyingi sana ili kuweza kucheza na kukimbia na hivyo kumfanya mchezaji kupunguza uzito na hatimaye kuwa mwepesi.

Vile vile mchezaji anapokuja kwenye uwanja wa kawaida huwa na wepesi na kuweza kujiamini na kutohisi kuchoka kutokana na mazoea ya mwili na akili kutumia nguvu katika mchanga wa ufukweni.

Faida ya pili ni kuimarisha na kujenga misuli ya miguu. Mchezaji soka yeyote uimara wa miguu yake ndiyo kila kitu kwani ndiyo huitumia kucheza soka.

Zoezi la ufukweni huifanya misuli ya mwili ya miguuni kutumia kiasi kikubwa cha sukari ili kukunjuka na kuweza kuutembeza mwili wakati wa kukimbia na hatimaye huifanya kuwa mikakamavu na kujengeka.

Hali hii pia husaidia kuifanya misuli ya miguu kuwa imara na kuweza kuhimili majeraha yatokanayo na michezo huku pale inapopata majeraha huweza kupona haraka na kwa wakati.

Kutokana na kukaa sana bila mazoezi, misuli na maungio huweza kuwa na uchovu hivyo kushindwa kuwajibika kwa ufanisi wakati wa kucheza. Unapofanya mazoezi haya husaidia kulainisha viungo na kuwa vyepesi.

Kutokana na upana wa eneo la ufukweni na kuwa wazi huku likisindikizwa na upepo mwanana uliosheheni hewa safi yenye oksijeni humfanya mchezaji anayefanya mazoezi kupata hewa ya kutosha.

Hii huwa na faida kwa moyo na mzunguko wa damu na mwili kuweza kupata hewa ya oksijeni kwa wingi.

Hali ya ufukweni huweza kumpa burudani mchezaji na kusahau mambo yanayompa msongo wa mawazo ikiwamo hofu ya yeye binafsi, ndugu, jamaa au wazazi kuugua.

Ufukwe ni eneo la burudani na hata wanasaikolojia wanashauri kwa mtu mwenye shinikizo la akili au msongo wa mawazo kwenda ufukweni kwani wanaamini mazingira hayo husaidia kupeperusha hasira, huzuni, msongo wa mawazo na shinikizo la akili.

Baadaye mwanasoka anapomaliza mazoezi ufukweni na kuamua kuogelea ndipo huzidi kupata utimamu na wepesi kwenye maeneo mengine ya mwili.

Hii ni kwasababu ya zoezi la kuogelea linashika namba moja kuimarisha kujenga maeneo mengi ya mwili kutokana na zoezi hili kuhusisha misuli mingi ya mwili.

Hivyo mchezaji hupata kasi na wepesi na misuli huwa imara na yenye nguvu anapochanganya mazoezi ya ufukweni na kuogelea.


HASARA ZAKE

Mchezaji anayecheza peku peku maeneo hayo anaweza kupata vijeraha vya nyayoni kutokana na uwepo wa vitu vyenye ncha kali ikiwamo nyumba za konokono au mazao mengine ya baharini na miba ya samaki na vitu kama chupa zilizotupwa kiholela.

Kutokana na uwapo wa mchanga mwingi unaozamisha eneo la chini la miguuni mchezaji anaweza kupata majeraha ya kifundo cha mguu na magoti.

Kwakuwa mazoezi haya huupa ugumu mwingi sana mwili wakati wa kujifua pale atakapoyafanya mazoezi kupita kiasi bila kujipa mapumziko anaweza kujipa uchovu na majeraha.

Upepo mkali unaweza kuwa chanzo kupata mafua ya muda na vile vile mchanga unaorushwa machoni unaweza kukereketa machoni.