SPOTI DOKTA: Utimamu wa Arajiga, Kayoko unapatikana hivi

Muktasari:
- Ili kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi ni lazima mwamuzi na waamuzi wasaidizi wawe timamu kimwili.
MWAMUZI wa soka anahitaji kuwa na mwili mkakamavu ambao unamwezesha kwenda na mwendokasi wa mchezo huo ambao unahitajika kuwa na kasi, nguvu na kutumia akili kuamua.
Ili kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi ni lazima mwamuzi na waamuzi wasaidizi wawe timamu kimwili.
Lakini pia anahitaji kuwa na mwili mkakamavu wenye ustahimilivu kwani ni kawaida mwamuzi wa uwanjani kukimbia umbali wa kilomita 11 wakati wa mechi moja yenye ushindani mkali.
Na huku waamuzi wasaidizi nao kwa hukimbia wastani wa kilomita 7 kwa kila mechi yenye ushindani pia ikiwa na kasi kubwa.
Vikundi vyote viwili vinaonyesha ushahidi wa kuweza kupata uchovu hasa wakati wa kuelekea mwisho wa mchezo. Kumbuka uchovu ni moja ya matatizo yanayochangia kufanya uamuzi mbovu.
Mwamuzi wa mpira wa miguu ndiye anayepewa jukumu la kutekeleza burudani inayotazamwa na maelfu ya watu ambao wana kiu ya kuona unafanyika uamuzi wa haki na sahihi.
Marefa huchezesha mechi hizo wakipata shinikizo au kupingwa na wachezaji wa nje na ndani ya dimba hivyo huwa katika wakati mgumu hasa pale anapokuwa na udhaifu katika kusimamia sheria za mchezo.
Kuna wakati mchezo unakuwa mkali na kasi kubwa, refa huhitaji kufanya uamuzi katika matukio mawili hadi matatu yanayoonekana kwa dakika nzima huku akiwa ametoka katika kasi fupi akihema na kutweta.
Mwendokasi wa mchezo na marudio ya uamuzi muhimu mara nyingi huongezeka wakati mchezo umefikia dakika za mwishoni akiwa ameisha kimbia kimbia umbali mrefu.
Tunapata picha kuwa waamuzi wana mahitaji makubwa kwa mifumo ya mwili kutumia aerobic yaani kupata nguvu kutegemea oksijeni wakati akikimbia kasi ya wastani na kutumia anaerobic kupata nguvu bila kutegemea oksijeni pale anapokimbia mbio fupi kwa kasi.
Hivyo waamuzi pamoja na wasaidizi wao huhitaji kufanyiwa uchunguzi wa afya kabla ya kupewa majukumu ya uchezeshaji soka katika ligi kubwa au mechi za kimataifa.
Wanavyopimwa afya kabla ya kuajiriwa
Kama ilivyo kwa wachezaji ambao hupimwa afya kabla ya kununuliwa kutoka klabu nyingine ndivyo pia marefa wa soka na wao hupimwa afya zao.
Ingawa ni kweli marefa wengi huwa na umri wa miaka 35 kuendelea lakini na wao huhitajika kupimwa afya ikiwamo uchunguzi wa jumla wa kiafya.
Huchunguzwa matatizo ya kimaumbile ikiwamo nyayo bapa, majaribio ya uwezo wa utendaji wa viungo vya kimwili, vipimo vya damu kuangalia maambukizi mbalimbali na picha za uchunguzi.
Vile vile hufanyiwa uchunguzi wa kina wa afya ya moyo kuangalia dosari ya kimaumbile ya kuzaliwa, magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu na mwenendo wa moyo.
Kuchunguzwa afya ya akili ili kuweza kubaini endapo ana matatizo yoyote ikiwamo sonona, hofu, shinikizo la akili au mabadiliko ya kihisia.
Itakumbukwa kuwa mwamuzi wa soka anahitaji kuwa na afya bora kiakili ili aweze kutoa uamuzi sahihi au kuhukumu kwa umakini, huhitaji kuona na kukumbuka sheria zinazoendesha mchezo huo.
Kukidhi vigezo vya afya kwa mwamuzi ndivyo kunawapa nafasi kuweza kuchezesha mechi za kimataifa zilizo chini ya FIFA ambazo zimefanyika wiki hii maeneo mbalimbali duniani.
Namna wanavyojijenga na kulinda utimamu wa mwili.
1.Mafunzo ya uvumilivu
Kama ilivyo kwa wachezaji ambao huwa na mazoezi ya pamoja katika klabu na vivyo hivyo waamuzi nao mara baada ya kuanza majukumu ya uchezeshaji hujiandaa kwa mazoezi.
Mazoezi hayo huwa yanajumuisha ya viungo na ya kukimbia kasi fupi na ndefu.
Mafunzo haya ni ya ustahimilivu yanaweza kufanywa kwa kiwango cha chini, wastani na cha juu. Ili kuunda msingi mzuri wa mazoezi yao, wanahitaji mazoezi hayo kwa muda mrefu.
Kasi na nguvu huongezeka polepole kwani mwili huhitaji kuzoea hali ngumu kidogo kidogo na hatimaye kujibadili na kujiimarisha na kuwa na mwili imara wenye ustahimilivu.
2.Mazoezi ya kujenga misuli na nguvu
Nguvu lazima iwe kubwa kwa marefa ili aweze kutoka kasi kwa pumzi kali pasipo kuishiwa nguvu. Marefa nao hufanya mazoezi mepesi ikiwamo kukimbia kidogo kidogo kujenga ustahimilivu.
Na pia hufanya mazoezi magumu ikiwamo kasi fupi na huku wakichanganya mazoezi ya “gym” ikiwamo ya kubeba vitu vizito vya wastani ili kujenga na kuimarisha misuli ya mwili. Hula lishe maalumu ya kujenga mwili na kuwapa nguvu.
3.Mafunzo ya kasi na wepesi
Ni kawaida refa ambaye anachezesha mechi ngumu kukimbia kilomita 11 kufanya mazoezi ya kukimbia kilomita 22. Lengo ni kuwa na kasi na wepesi katika kuchezesha mchezo wa soka.
Hitaji kuwa wepesi na kunyumbulika kirahisi wakati anachezesha. Hufanya mazoezi ya kupasha mwili moto, mazoezi ya viungo kabla na baada ya mechi na pia wakati wakiwa mapumziko.
Ni bora kufanya mbio chache, nzuri kuliko kufanya mbio nyingi zenye viwango duni.
4.Mazoezi kwenye uwanja wa mpira
Kuna mazoezi mengi mazuri ambayo yanaweza kufanywa kwenye uwanja wa mpira. Mfano FIFA na UEFA imeunda muongozo mazoezi ambayo waamuzi wanawekewa katika apps ili kuyafanya.
Kwa kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mpira, ambapo mienendo mingi inafanana na mechi, mazoezi yatakuwa na tija zaidi kwani yatakuwa yanahusiana na kile wanachotakiwa kufanya.
5.Mbinu na mazoezi ya kuzuia majeraha
Mazoezi ya kupasha mwili moto ikiwamo mazoezi ya viungo, kasi fupi na ndefu kabla na baada ya mchezo ni moja ya njia za kujikinga na majeraha yatokanayo na michezo.
Mazoezi ya kujenga wepesi, ya nguvu na yale ya kuimarisha misuli ya miguu pamoja na mbinu za uchezeshaji uwanjani zinawasaidia kuepuka kujijeruhi au kujeruhiwa kwa kugongana na wachezaji.
6.Lishe bora na kupumzika
Ili kuwa na utimamu bora kiafya na kuulinda katika kazi yake huzingatia lishe bora, kuburudisha akili, kupumzika na kulala kwa saa 8-10 kwa usiku mmoja.
Hatari ya Uamuzi mbovu iko hivi
Refa aliye katika hatari ya kuchezesha vibaya na kufanya uamuzi mbovu ni yule ambaye hayuko timamu yaani kuwa mgonjwa, anayetumia dawa za matibabu, mwenye shinikizo la akili, kutumia kilevi au dawa ya kulevya, uchovu na mvurugiko hisia ikiwamo hasira.
Uchovu ni moja ya mambo yanayoharibu utendaji kazi wa mifumo ya mwili ikiwamo mfumo wa fahamu na misuli ambayo ni muhimu katika kazi ya urefa.
Uchovu unaweza kusababishishwa na vijeraha vya ndani ya misuli, mlundikano wa takamwili katika misuli baada ya kufanya kazi ngumu, kutopumzika na kutokulala vizuri.