Dokta Tanzania Prisons: Hii ndio hatari ya dawa za kuongeza nguvu kwa mastaa

Muktasari:
- Katika mahojiano na Mwanaspoti, Dk Chinyele anasema kuna haja ya kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wachezaji ili kufahamu kuhusu afya zao na pia kujua kukabiliana na majeraha ya aina tofauti.
TABIBU wa timu ya Tanzania Prisons, Dk Damas Chinyele ametoa elimu kwa wachezaji namna wanavyotakiwa kuzingatia baadhi ya mambo kwa usalama wa afya wakati wa kutimiza majukumu uwanjani.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Dk Chinyele anasema kuna haja ya kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wachezaji ili kufahamu kuhusu afya zao na pia kujua kukabiliana na majeraha ya aina tofauti.
“Kuna majeraha makubwa na ya kawaida. Makubwa ni yale daktari hawezi kuyamudu kutibu hadi vifanyike vipimo sahihi kama X-Ray, CT-Scan na MRI ili kujua shida ni nini - kugundua hayo itatokana na maelezo ya mchezaji mwenyewe au nishuhudie pindi anaumia uwanjani,” anasema.
“Nitafanya uchunguzi (physical examination) nikigundua hali isiyo ya kawaida nitatafuta msaada kwa wataalamu wengine kwa uchunguzi zaidi na wao pia huhitaji X-Ray, CT SCAN na MRI ili kuthibitisha kile tunachokihisi, mfano majeraha ya magoti (knee injury ) na sehemu ya kiungo cha chini ya miguu (ankle), kuchanika au kukatika kwa msuli unaoshikilia paja na mguu wa chini (Anterior Cruciate Ligament tear), kukatika kwa msuli unaolala kati ya mfupa wa paja (femur) na mguu (tibia).”
Anaendelea kusema: “Majeraha madogo ni kama kuvutika kwa misuli ya nyuma ya paja (hamstring) na thigh contusion ambayo hutokea hasa kwenye msuli wa mbele ya paja pale mchezaji anapogongwa mguu na mchezaji mwenzake.” Anasema alishawahi kukutana na tatizo gumu la mchezaji, jambo la kwanza alihakikisha anampa huduma ya kwanza ya kuhakikisha anapumua vizuri, kisha akawahishwa hospitali kwa uangalizi zaidi.
“Nahifadhi jina la mchezaji. Kilichotokea alikanyagwa na mguu eneo la ubavu na mchezaji wa timu pinzani wakati wa kugombania mpira eneo la goli, hivyo alidondoka chini akaanza kukata pumzi, akapewa huduma ya kwanza ili kuyaokoa maisha yake. Ndiyo maana unasisitizwa upendo michezoni na kuepuka kuchezeana rafu ambazo hazina ulazima,” anasema Dk Chenyele na kuongeza:
“Ukiacha wachezaji nimetibia wagonjwa wengi ambao wana kesi ngumu, hiyo ni kazi yetu kuhakikisha tunaokoa maisha ya watu na tunaifanya kwa moyo mmoja.”
WACHEZAJI NA AFYA ZAO
Daktari huyo anasema kwa asilimia kubwa ya wachezaji wanauelewa mkubwa na wengine ni wadadisi kufahamu kuhusiana na magonjwa ambukizi kama yatokanayo na zinaa.
“Wengine wanauliza kuhusiana na magonjwa yanayoambukiza kama Ukimwi ila kuhusu TB bado sijakutana na swali hilo, na sina hakika kama wanauelewa nalo na ni jambo muhimu wanapaswa kulijua,” anasema.
Anafafanua jambo lingine kuwa mchezaji asipopumzika vya kutosha kwa maana ya kulala usingizi kwa muda unaotakiwa, anaweza akapata changamoto ya kukosa nguvu uwanjani, mwili unakuwa haujapata kinachotakiwa, hivyo ikitokea akakutana na mwenzake anayetumia nguvu ni rahisi kupata majeraha au kucheza chini ya kiwango.
“Pia sio sahihi kwa mchezaji aliyetumia kilevi kuingia mazoezini hadi pombe imuishe katika mwili wake, kwani pombe hufanya mzunguko wa damu mwilini kuwa juu, hivyo anapoongeza na mazoezi damu inakuwa juu mara mbili yake na huenda athari zikatokea papo hapo - kupata kizunguzungu, kuzimia. Kwa kifupi mengi yanaweza yakatokea kuhatarisha afya ama uhai wake,” anasema.
Jambo lingine alilozungumzia ni dawa za kuongeza nguvu kwa wachezaji jinsi zinavyoweza kuwaweka katika hatari za kiafya miongoni mwa changamoto wanayoweza kupata ni matatizo ya moyo kusimama (cardiac arrest), moyo kutanuka (cardiomegaly), kuwa na hofu na mashaka ambayo hajui yanatoka wapi (anxiety), ukorofi na kutotulia (aggression), uraibu wa kushindwa kuishi bila kutumia kitu fulani (addiction and dependence).
“Mchezaji anapaswa kuangalia na kesho yake, mfano anayechoma sindano ya ganzi anaweza akainufaisha timu ama mwenyewe kujisikia vizuri kwa muda mchache, ila madhara yake ni kuongeza ukubwa wa tatizo (over uses),” anasema.
WALE VYAKULA HIVI
Dk Chinyele anasema mchezaji wa mpira wa miguu anahitaji kula vyakula vya kuupa mwili nguvu kabla ya kwenda mazoezini au mechi na pia kunywa kinywaji cha kumuongezea sukari ambayo wakati wa mazoezi hutumika sana huku akinywa maji ya kutosha.
“Kabla ya mechi ama mazoezi mchezaji anatakiwa kula vyakula vya wanga kama wali, ugali na vyakula vya kujenga mwili vya protini kama samaki, nyama, karanga vipo vingi,” anasema na kuongeza:
“Ninachosisitiza ni maji kama hapati maji ya kutosha anaweza akapata changamoto ya kukamatwa au kukakamaa kwa misuli (musle tear).”
ELIMU YAKE
Dk Chinyele ana Stashahada ya Udaktari wa Tiba aliyosomea katika Chuo Kikuu cha Kampala; Stashahada ya Sayansi ya Saikolojia aliyoipata Chuo cha St Augustine, Morogoro na mwanadiplomasia aliyosomea Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam.