SPOTI DOKTA: Tatizo la afya ya akili kwa wanasoka lipo hivi!

Muktasari:
- Siku hii inatambuliwa pia na Shirika la Afya Duniani (WHO) na mwaka huu maadhimisho yake yalipambwa na kauli mbiu isemayo; ‘Ni wakati wa kuipa kipaumbele afya ya akili mahali pa kazi’.
OKTOBA 10 ya kila mwaka imetengwa kama Siku ya Kimataifa ya Afya ya Akili Duniani.
Siku hii inatambuliwa pia na Shirika la Afya Duniani (WHO) na mwaka huu maadhimisho yake yalipambwa na kauli mbiu isemayo; ‘Ni wakati wa kuipa kipaumbele afya ya akili mahali pa kazi’.
Inaelezwa kauli hiyo ililenga kuboresha ujuzi, kuongeza ufahamu na kuendesha vitendo vinavyostawisha na kukuza na kulinda afya ya akili ya kila mtu ikiwa ni hali ya msingi ya kibanadamu.
Katika kona hii ya Spoti Dokta, inatupia jicho la tatu kwa wanasoka wanaocheza kwenye viwanja kuanzia vya kufanyia mazoezi pamoja na kambi wanazoishi ikiwa ni eneo la kazi.
Pamoja ya kwamba michezo ni burudani na vile vile moja ya nyenzo muhimu katika kukabiliana na Afya ya akili, lakini wachezaji wa soka wanajikuta ni wahanga wa tatizo hilo la afya ya akili.
Takwimu za afya ya akili Duniani zinaonyesha katika kila watu nane, mmoja anaishi na tatizo la afya ya akili. Ingawa ni kweli, kiwango na makali ya matatizo hayo yanatofautiana mtu na mtu.

Afya ya akili ni haki ya msingi kwa watu wote, yeyote yule na popote pale alipo, anayo haki ya kufikia kiwango kikubwa zaidi cha afya ya akili kwani ni muhimu kwa ustawi wake na jamii.
Wanasoka kama ilivyo kwa wanadamu wengine na wao wanakabiliwa pia na mtetereko wa afya ya akili ikiwamo kupata matatizo ya afya ya akili ikiwamo shinikizo la akili, sonona (depression), hofu kali au woga na matatizo ya akili yanayotakana na matumizi ya vilevi.
Uwepo wa matatizo ya afya ya akili ni moja ya vitu vinavyoweza kumfanya mchezaji kucheza chini ya kiwango au kukosa umakini wakati anacheza ikiwamo kufanya makosa yanayoepuka.
Matatizo ya Afya ya akili yanaweza kuwa ya wastani, kati na yale makali zaidi ambayo ndio yanaharibu utu na ubora wa maisha ya mchezaji katika eneo lake la kazi.
Leo katika kuunga mkono siku hii, tutapata ufahamu wa matukio yanayoweza kumfanya mchezaji wa soka kupata matatizo ya Afya ya akili.
MAJERAHA NA AFYA YA AKILI
Majeraha wanayopata wachezaji ni moja ya matatizo ya kiafya yanayochangia kutokea kwa matatizo ya akili ikiwamo kupata tatizo la sonona kwa kiingereza depression.
Mfano kwa sasa, staa mkubwa wa Manchester City, Rodri atakuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima kutokana na kupata majeraha ya goti yuko katika hatari kupata tatizo la akili.
Kipindi hiki mchezaji aliyepata jeraha baya huwa katika msongo wa mawazo anapowazia hatima yake kisoka. Wengi hupatwa na hali ya hofu ya kushindwa kurudi tena katika soka akiwa timamu.

Uwepo wa benchi bora la ufundi na uwepo wa wataalam wa sailkolojia kwa wanasoka ndiyo nyenzo muhimu katika kuwakinga au kuwatibu wale wanaopata mtetereko wa akili.
WOGA WA MABADILIKO
Mara nyingi katika soka huwa ni kawaida kabisa kwa wachezaji kupatwa na tatizo la akili la woga hasa anapobadilishiwa kocha, benchi la ufundi au klabu.
Hapa hulazimika kwa viongozi, wataalam wa afya na wanasaikolojia kuzungumza vyema na wachezaji hasa pale panapotokea mabadiliko kama hayo ambayo yanaweza kuwapa hofu.
MIKATABA NA SHINIKIZO LA AKILI
Wachezaji wanaweza kuhamishwa katika klabu bila kikomo katika nyakati tofauti katika kipindi chote chao cha kazi na mchakato wa mkataba mipya unaweza kuwa kuwa tofauti na maslahi yake.
Mchezaji anaweza kuhama au kuuzwa na kutoka katika klabu kubwa na kwenda ndogo au kutoka ligi kubwa kwenda ligi ndogo.
Mfano mikataba mifupi ni ya kawaida kwa wachezaji wa kulipwa huwa na masilahi madogo kwa baadhi ya timu. Hali hii huwafanya wanasoka kuwa katika hali ya shinikizo la akili.
Hali inaweza kumfanya mchezaji kughadhibika kirahisi anapokuwa katika majukumu yake ya uwanjani.
Uwepo wa benchi bora la ufundi kunasaidia kubaini hali za wachezaji hatimaye kuchukua hatua za kumkinga mchezaji wa aina hii asipate hali ya shinikizo la akili.
UTENDAJI NA WASIWASI
Utendaji wa mchezaji unaweza kuambatana na hali ya wasiwasi hasa pale mchezaji anaposhinikizwa kufanya majukumu fulani ambayo kwake yanaweza kuwa magumu kufanya uwanjani.
Kufanya kazi chini shinikizo kubwa kutoka kwa walimu wake, viongozi au washabiki inaweza kumfanya mchezaji utendaji wake uwanjani kuwa na wasiwasi hasa anapoona matakwa ni makubwa kuliko uwezo.

Uwepo wa viongozi bora ikiwamo kocha na nahodha bora inaweza kusaidia kumpa hamasa na ari mchezaji hivyo kuweza kuondokana na hali hiyo.
KUSTAAFU NA HASIRA
Ikumbukwe wanasoka wengi wa kulipwa wamekuwa wakicheza tangu utoto, undani wa maisha ya huwa ni vigumu kujulikana na watu wengi.
Baadhi ya wachezaji mwisho wa kazi yao ya kucheza inaweza kuwa ya kutisha na kuhuzunisha, hasa inapotokea kulazimika kustaafu soka kutokana na majeraha au changamoto za kiafya kama magonjwa ya moyo.
Uzoefu unaonyesha baadhi ya wachezaji wa soka wanakumbwa na tatizo la afya ya akili ikiwamo la mabadiliko hasi ya hisia yaani kuwa na hasira isiyo ya kawaida.
Itakumbukwa mchezaji wa soka wa Nigeria, Jay Jay Okocha ni balozi maalumu wa afya ya akili kwa wachezaji waliostaafu.
Hii ilitokana na ukweli kuna ongezeko la visa vingi vya wanasoka waliostaafu kupata matatizo ya akili mbalimbali ikiwamo sonona, shinikizo la akili na mabadiliko ya kitabia kama vile ulevi.
Habari nzuri ni kuwa tatizo la afya ya akili kwa wanasoka bado halijawa mzigo katika medani ya soka, hii ni kutokana na uwepo wa wataalam wa afya katika klabu wanatoa elimu na kufuatilia afya za wachezaji, ikiwamo upimaji afya kabla ya kununuliwa.