Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SPOTI DOKTA:Talaka ilivyomuumiza kihisia Pep Guardiola

Muktasari:

  • Hali hiyo imetishia kuwa ngumu zaidi kwa kocha Pep Guardiola mara baada ya wiki iliyopita kutalikiana na mkewe Christina Serra ambaye wamedumu kwa miaka 30.

MANCHESTER City msimu huu imekuwa ikipitia wakati mgumu kutokana kufanya vibaya katika mechi za awali za Ligi Kuu England (EPL) na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hali hiyo imetishia kuwa ngumu zaidi kwa kocha Pep Guardiola mara baada ya wiki iliyopita kutalikiana na mkewe Christina Serra ambaye wamedumu kwa miaka 30.

Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 52 ambaye ni mwanamitindo aliyejaliwa kuzaa na Pep watoto wa wawili wa kike aliamua kuvunja ndoa pasipo sababu za maana.

Kuvunjika kwa ndoa hiyo kulikoamuliwa na mahakama kulisababisha Pep kumwaga machozi ambayo yaliashiria kuumizwa kihisia na tukio hilo ambalo limewastua wengi ikiwamo familia na jamaa wa karibu.

Talaka hiyo imeumiza hisia za kocha huyo ambaye ametoka kusaini mkataba mpya hivi karibuni na Manchester City ambayo kwa sasa inashika nafasi ya tano katika Ligi Kuu England.

Ingawa matatizo ya wanandoa hao yalikuwa ni siri hakuna taarifa zaidi kuhusu chanzo kikuu cha talaka. Itakumbukwa miaka mitano iliyopita mwanamke huyo aliamua kuondoka jijini London na kwenda kuishi jijini Barcelona.

Wakati hayo yanajiri klabu hiyo ilionekana kumpoza kocha huyo Jumapili iliyopita katika mchezo wa EPL ilioshinda mabao 6-1 dhidi ya Ipswich Town.

Lakini, bado inaonekana Pep anapita katika kipindi kigumu kwani mara baada ya tukio hilo alionekana kumwaga machozi ya huzuni wakati akitoka nje ya uwanja.

Mojawapo ya mambo yanayoweza kuteteresha afya ya akili kwa binadamu ni kitendo cha kuumizwa kihisia kutokana na kuvunjika kwa ndoa au uhusiano wa mapenzi.

Matatizo makubwa ya kiafya yanayotokana na ndoa kuvunjika ni pamoja na woga au wasiwasi, msongo wa mawazo ama shinikizo la akili, sonona, kukosa usingizi na kutumia kilevi au dawa za kulevya.

Vilevile mtu hujitenga, kuwa na huzuni, kujitenga na jamii, kutojiamini, hasira kali bila sababu, kukonda na matatizo ya moyo.

Hali kama hiyo inaweza kuathiri akili kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu ya kila siku. Hii ni kwa sababu maumivu hayo ni kawaida kuendana na huzuni kali au msongo mkali wa mawazo.

Hali kama hiyo inapodumu inaweza kumfanya mhusika kushindwa kuweka mkazo wa akili katika majukumu yake ikiwamo uamuzi sahihi au umakini katika utendaji kazi.

Mbaya zaidi hali kama hiyo ya kuumizwa kihisia inaweza kumfanya mhusika kupata mfadhaiko wa akili kiasi cha kuwa mtu mwenye hasira isivyo kawaida.

Vipo viashiria vya hapa na pale ambavyo vilimwonyesha kocha huyo akiwa mkali isivyo kawaida pale wachezaji wake walipokosea au timu kufanya vibaya.

Itakumbukwa kwamba hata katika mechi Jumapili ambayo alionekana kumwaga machozi akiwa na huzuni kali. Hali hiyo ilionyesha kocha huyo anapitia katika nyakati ngumu.

Kiashiria hicho cha kuumia kihisia ni tukio ambalo liliwahi kuandikwa kupitia kona hii pale kocha huyo alipojijeruhi kichwani kwa kujikwangua na kucha kutokana na hasira za kufungwa mechi kadhaa mfululizo.

Hali kama hiyo inaweza kuwa tishio katika utendaji kazi wa kimwili na hatimaye kushusha uwezo wa kusimamia majukumu ya timu.

Kupitia nyakati ngumu kwa Manchester City hivi sasa kumehusishwa na hali ngumu anayopitia kocha wake. Inaelezwa kuwa huenda kulikuwa na mgogoro wa muda mrefu, lakini Pep alikuwa akificha jambo hilo. Inasemekana kuwa sababu ya talaka hiyo imetokana na kocha huyo kujikita zaidi katika majukumu ya klabu yake kuliko masuala ya kifamilia.

Habari nzuri ni kuwa klabu kama za nchi za Ulaya zina huduma bora ya kukabiliana na matatizo ya afya ya akili. Hivyo inaaminika kuwa Pep atapona na atendelea kuwa imara.


AFYA YA AKILI IKO HIVI

Kwa kawaida binadamu anapoumizwa kihisia hali hiyo huambatana na mabadiliko ya ndani ya mwili ambayo yanasababisha kupata matatizo ya akili.

Kutalikiana sio jambo dogo, mlolongo mzima  wa kisheria mpaka kufikia hatua ya ndoa kuvunjika huambatana na mambo yanayoleta shinikizo la akili au sonona ikiwamo gharama za mahakama, kupoteza mali, kubadili makazi au kuanza maisha mapya.

Kwa kawaida mtu ambaye ameumizwa kihisia anaweza kujikuta akijitenga na jamii au kujikataa na kujiona ni mtu mkosaji au asiye na bahati.

Kuwa na hali ya woga au wasiwasi pale mtu anapovunja uhusiano huwa na hali ya hofu ya kuumizwa tena endapo ataingia katika uhusiano mpya.

Kubadili mwenendo wa maisha na kuanza maisha mengine bila mwenza wa zamani kwa binadamu kunawaweka katika hatari ya tatizo la hofu kali na wasiwasi mkubwa.

Mtu anaweza kukosa hamu ya kula kiasi cha kushindwa kula vizuri na hatimaye afya yake inaweza kudorora ikiwamo kupoteza uzito mwingi, huku pia akikosa lishe kunakochochea matatizo ya akili.

Vilevile huanza kuonyesha dalili za kukasirika kirahisi na kutaka kushambulia wengine pale anapoudhika. Kuwa mwepesi kukasirika na kupigana bila hata ulazima.

Pia kuna hali ya kukosa usingizi au kupata usingizi. Hii inasababishwa na kuwa na msongo wa mawazo yasiyopata suluhisho.

Mtu anayekosa usingizi au asiyelala vyema akili yake haiwezi kufanya uamuzi sahihi au kukosa umakini katika kuamua mambo mbalimbali.

Kadri mtu anavyozidiwa na msongo wa mawazo ndivyo pia huambatana na mabadiliko ya mapigo ya moyo. Hii ni kwa sababu mtu anapoumizwa mwili huzalisha kichochezi kinachosababisha mapigo ya moyo kuongezeka kasi.

Kadri akili inavyozidi kufikiri kulikokithiri husababisha hali ya kuchanganyikiwa endapo hatua za mapema za kitabibu hazitachukuliwa.

Hali ya kuyumba kiakili isipodhibitiwa inaweza kuleta madhara makubwa zaidi ikiwamo kupata tatizo kubwa la kiakili kama sonana kubwa au kuchanganyikiwa kabisa.

Vilevile mtu aliyeumizwa kihisia anaweza kuangukia katika ulevi au utumiaji dawa uliopindukia. Hali hiyo huwa ni tatizo la afya ya akili ambayo inaweza kuharibu utu.

Pia mtu aliyepata hali hizo anakuwa katika hatari ya kuelemewa na msongo wa mawazo na hatimaye kumfanya kutaka kujiua au kuwa na mawazo ya kujiua hasa anapokosa msaada wa maana kutoka kwa jamii inayomzunguka.