SPOTI DOKTA: Sababu nchi za Afrika Mashariki na Kati kutawala riadha

Muktasari:
- Kwa miongo kadhaa, wakimbiaji wa Afrika Mashariki wametawala katika mchezo wa riadha duniani katika ukimbiaji wa umbali kutoka mita 3,000 kwenda juu.
WAKATI wa Olimpiki mwaka 2008, 2012 na 2016, wanariadha kutoka Afrika Mashariki kutoka Kenya na Ethiopia, walishinda theluthi mbili ya medali zote za dhahabu katika mashindano ya masafa ya kati na marefu.
Kwa miongo kadhaa, wakimbiaji wa Afrika Mashariki wametawala katika mchezo wa riadha duniani katika ukimbiaji wa umbali kutoka mita 3,000 kwenda juu.
Ingawa katika mbio ndefu Tanzania nayo haiko nyuma, kwani miaka umewahi kutoa wanariadha bora kabisa duniani ikiwamo John Akhwari mwaka 1968 na Filbert Bayi ambaye aliweka rekodi ya dunia katika mita 1500 mwaka 1974.
Kuanzia miaka ya 2015 kuna Alphonce Simbu na Gabriel Geay ambao amekuwa na rekodi nzuri katika mbio ndefu za Olimpiki na mashindano ya riadha dunia IAAF.
Hata kwa hapa Tanzania wanariadha wengi wanatokea maeneo ya kaskazini mkoani Manyara katika maeneo ya mwinuko kama ilivyo kwa Kenya na Ethiopia.

Ethiopia na Kenya ndio wamekuwa vinara karibu katika kila mashindano makubwa ya kimataifa ya riadha katika mbio ndefu, wakitoa idadi kubwa ya washindi wa medali za dhahabu.
Waamekuwa wakishinda mbio kubwa za marathoni tangu mashindano ya Olimpiki ya 1968, wanaume na wanawake kutoka Kenya na Ethiopia wametawala mashindano ya maili 26.2.
Mwaka 1991 mshindi wa wanaume katika mbio za Boston Marathon alikuwa ni Mkenya au Muethiopia mara 26 kati ya 29.
Katika Olimpiki Paris 2024 iliyofanyika mwezi Agosti kati ya medali 13 za dhahabu zilizoshinda nchi za Afrika, 8 zilikuja katika riadha, huku wakimbiaji wa Afrika Mashariki wakitawala mbio ndefu.

Wanariadha wa Kenya waliongoza mbio hizo, huku Beatrice Chebet akipata medali mbili za dhahabu katika mashindano ya Wanawake ya mita 5000 na 10000.
Emmanuel Wanyonyi alipata medali ya dhahabu katika mbio za 800m za Wanaume. Historia inaonyesha kuwa wanaume Wakenya wametawala mbio za mita 800 tangu 2008.
Huku Faith Kipyegon alipata medali ya dhahabu katika mbio za mita 1500 za Wanawake.
Tamirat Tola wa Ethiopia aliendeleza mafanikio ya Afrika Mashariki kwa kushinda dhahabu katika mbio za marathon za Wanaume.
Berihu Aregawi wa Ethiopia na Tsige Duguma walishinda medali za fedha katika mbio za mita 10000 kwa Wanaume na 800 za Wanawake mtawali.
Joshua Cheptegei wa Uganda ilitwaa medali ya dhahabu ya katika mbio za mita 10,000 za Wanaume, na hivyo kuimarisha ngome ya Afrika Mashariki kwenye mashindano ya masafa marefu.
Mafanikio haya kwa nchi za Afrika mashariki imesababisha tafiti kadhaa kufanyika nchini Ethiopia na Kenya ili kupata majibu sababu zinazochangia kushinda mbio ndefu duniani.
SABABU HIZI HAPA
Wataalam wanaelekeza kwenye mchanganyiko wa mambo yafuatayo yanachangia kutawala kwao katika mbio za masafa marefu.
1. Mazoezi na kuishi katika uwanda wa juu
Jambo moja kuu linalotajwa mara nyingi ni mazingira ya mwinuko wa juu ambapo wengi wa wanariadha wanaishi, hukulia na kufanya mazoezi.
Bonde ufa la Kenya, kwa mfano, liko kwenye mwinuko wa wastani wa mita 1,500 (futi 4,921) juu ya usawa wa bahari. Nyanda za kati za Ethiopia ziko juu zaidi, kutoka futi 4,200 hadi 9,800.
Kufanya mazoezi katika miinuko kama hiyo huongeza uwezo wa mapafu na idadi ya seli nyekundu za damu zenye ufanisi wa kunyaka hewa ya oksijeni katika uwanda wa juu kwenye ufinyu wa hewa hiyo.
Hii ndio inawapa faida kubwa wakati wa kushindana katika miinuko ya chini katika maeneo mbalimbali duniani.
Kitabibu inaitwa adaptation, yaani mwili unanyumbulika kutokana na kuwepo katika mazingira yenye ugumu wa hewa, hivyo wakienda katika uwanda wa chini miili inakuwa tayari ina ustahimilivu wa juu.
2. Lishe ya kiafrika
Lishe ya kawaida ya wakimbiaji wa Kenya na Ethiopia ina wanga nyingi na mafuta kidogo, ambayo hutoa mafuta bora kwa shughuli zenye uhitaji wa uvumilivu.
Chakula kikuu kama ugali au uji mgumu uliotengenezwa kwa unga wa mahindi au mtama, mboga za majani, na protini zisizo na mafuta hutengeneza uti wa mgongo wenye ulalo rafiki katika ukimbiaji.

3. Maumbile na tabia zake
Wakimbiaji wengi waliofaulu wa Afrika Mashariki wana aina ya mwili iliyokonda, yenye ufanisi na wepesi kwa kukimbia umbali mrefu.
Utafiti umeonyesha kuwa miguu ya wastani ya mwanariadha wakenya ni takriban gramu 400 ambayo ni myepesi kuliko ile ya wenzao wa Ulaya.
Aina hiyo huwa faida ya ukimbiaji kwani nyayo za namna hiyo husababisha kuokoa nishati kwa karibu asilimia 8% kwa umbali mrefu.
Tafiti moja iliyofanyika ilibaini Waethiopia wamerithi aina fulani ya chembe za urithi zinazokifanya kituo kikuu cha kuchakata nguvu ya mwili kufanya kwa ufanisi wa juu kutokana na faida ya kimaumbile.
Chembe hizo kwa kawaida zinarithiwa kutoka kwa wazazi kwenda kwa watoto. Hivyo kuifanya jamii hiyo kuwa na aina hiyo ya chembe zenye kuwapa uwezo wa kipekee ndani ya seli zao.
Vile vile seli za mfumo wa fahamu zimeonekana kuwa na uwezo mkubwa katika kufanya kazi kwa ufanisi hata katika eneo lenye hewa ndogo ya oksijeni katika maeneo yenye miinuko.
4. Tamaduni
Mambo ya kitamaduni na kijamii na kiuchumi wanayoishi jamii za Afrika Mashariki ikiwamo kenya na Ethiopia, kutokana na historia nzuri kimataifa imeonekana riadha ni njia rahisi kuondokana na umaskini.
Hadithi za mafanikio za wanariadha ambao wameinua vijiji vyao kuondokana na kadhia katika huduma za kijamii ikiwamo kujenga shule na vituo bora vya afya imeleta hamasa kubwa kwa wakimbiaji wachanga.
5. Ratiba ya maisha ya kila siku
Ratiba ya mafunzo ya wakimbiaji wa Afrika Mashariki mara nyingi ina sifa ya kuwa rahisi. Katika maisha ya Wanariadha wengi hukua wakikimbia umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, wakati mwingine bila viatu, jambo ambalo baadhi ya watafiti wanaamini kuwa huchangia utimamu wa kipekee hatimaye kukimbia kwa ufanisi zaidi.
Adharanand Finn, mwandishi wa “Running with the Kenyans,” alitumia muda kuishi na kufanya mafunzo katika Bonde la Ufa la Kenya. Baadaye alibaini kwamba katika miji kama Iten, kukimbia ni sehemu ya maisha kwa wanajamii wengi.
Wakimbiaji wa muda wote wakiwemo mabingwa wa Olimpiki duniani wanakimbia pamoja na jamii zao, hivyo kukuza utamaduni hatimaye kuleta msukumo kila kona katika maeneo hayo.