SPOTI DOKTA: Hii ndio siri ya ulaji protini kwa wanamichezo

Hii ndio siri ya ulaji protini kwa wanamichezo

WIKI iliyopita ligi mbalimbali zilisimana kupisha michezo ya kimataifa ya kuwania tiketi za kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia hapo mwakani itakayofanyika nchini Qatar.

Wachezaji wengi walioitwa katika timu zao za taifa ndiyo hao hao keshokutwa wanarudi tena uwanjani katika ngazi ya klabu ya katika mechi za ligi.

Mechi nyingi zilikuwa ngumu zenye upinzani kila mchezaji akitaka kuhakikisha inaisaidia timu yake ya taifa kupata tiketi ya kwenda Qatar.

Hata timu ambazo zilikuwa zinakamalisha ratiba nazo zilikuwa zina upinzani mkali, mfano mzuri ni mechi ya timu ya Taifa ya Tanzania na Madagascar.

Pamoja ya kwamba walikuwa wanakamalisha ratiba lakini kulikuwa na upinzani mkubwa, kiasi cha kutokea tukio la wanajeshi kuvamia katika hoteli waliyofikia timu ya taifa na kuwachukua baadhi ya wachezaji wakidai wamekutwa na maambukizi ya corona.

Kitendo hicho kilipigiwa kelele kutokana na utaratibu uliotumika kuwa sio wa kawaida na ulikuwa wa vitisho. Hali hii ilisababisha kukosekana nahodha wa timu ya taifa Mbwana Samatta.

Ukiacha hayo, jicho la kitabibu linatazama hali wanayoipata wachezaji ambao wanatumika katika timu ya taifa mara kwa mara na huku pia wakiwa na majukumu ya timu zao ngazi ya klabu.

Ni kawaida wachezaji wa kulipwa wanaoshiriki mashindano kama haya kuwakuta wakiwa katika hali ya maumivu ya kimwili kutokana kutumika katika ngazi zote.

Maumivu ya mwili huwa ni kawaida kutokea kwa wachezaji ambao wanatumika sana ikiwamo mashindano kama haya ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia.

Moja ya njia ambazo madaktari wa timu za klabu au timu za taifa zenye uwezo hufanya ni kuwapa wachezaji wao virutubisho vya ziada hasa protini mara tu wanapomaliza mechi.

Wengi huwa hawajui ni kwanini wachezaji hao wanapewa vitu hivyo ambavyo viko kama poda poda au katika hali ya kimiminika.

Kitabibu nyongeza ya virutubisho vya protini ni muhimu kiafya hasa kwa wachezaji ambao wanakumbana na majukumu mengi bila kupumzika.

Protini tunayoipata katika vyakula au katika virutubisho vilivyotengezwa kisayansi ni muhimu sana kwani ndiyo inayojenga mwili.

Kiujumla mwanadamu yoyote anayefanya mazoezi au kufanya kazi ngumu ulaji wa vyakula vya wanga na mafuta ndio chanzo kikubwa cha nishati wakati wa mazoezi.

Lakini ukiacha vyakula hivyo vyakula vyenye protini ni mlo muhimu hasa kwa mwanamichezo ambaye kila siku anashiriki michezo au mazoezi.

Tayari kuna tafiti nyingi zinazothibitisha kuwa protini inatumika wakati wa kufanya mazoezi ya kimwili kama ilivyo kwa wanga na mafuta.

Na hii ndio sababu kubwa wanasoka wa kimataifa wa kulipwa hupewa virutubisho vyenye protini kabla na baada kushiriki mechi au mazoezi.


Siri ya kula protini kwa wingi ni hii

Protini ni kama vile tofali la mwili kwani ujenzi wa mwili hutegemea kirutubisho hiki chenye kitu kinachojulikana kama amino acids, karibia vitu vingi vya mwilini vimetengenezwa na amino acids ikiwamo vichochezi (hormons), vimeng”enya (enzymes) na visaidizi vya kazi za mwilini.

Ili misuli ya mwili iweze kujikunja na kujikunjua inawezeshwa na uwepo wa protini, hapo ndipo misuli ya mwili huwezesha kufanyika kwa mambo mbalimbali ikiwamo kutembea, kukimbia na kuruka

Wakati wa mazoezi makali ndani ya misuli hutokea vijeraha vidogo vya ndani kwa ndani, protini ndio inatupa amino acids inayosaidia ujenzi wa misuli iliyojeruhiwa.

Hii ndio sababu wanamichezo wa kimataifa hupewa kirutubisho chenye protini baada tu ya kutoka katika mechi ngumu ili kuusaidia mwili kurudi katika hali yake ya kawaida na kujijenga pale palipojeruhiwa.

Protini ndio inayoifanya misuli iwe imara na kuweza kudumu kwa kasi yake ile ile kwa kipindi kirefu na huku ikiwa na ufanisi wa hali ya juu.

Vile vile huifanya misuli yetu ya mwili kufanya kazi yake kiufanisi hivyo kumwezesha mwanamichezo kucheza kwa kiwango cha juu.

Wataalam lishe wanashauri kuwa angalau mwanamichezo apate mlo wa protini gramu 2 kwa kila kilo moja ya mwili kwa siku.

Kwa mfano mwanamichezo wa kilo 72 anatakiwa kula gramu 2 zidisha mara 72 jumla unapata gramu 144 za protini anazotakiwa kula kwa siku.

Kwa mazingira yetu ya Tanzania vyakula tunavyoweza kupata protini kwa uraisi na kwa gharama nafuu ni pamoja na maharage ya soya, samaki, maziwa, nyama na mayai.

Samaki ndio wana kiasi kikubwa cha protini ndio maana kwa klabu za kulipwa mlo wanaowapa wachezaji wao huwa hapakosi samaki hii ni kutokana na kujua umuhimu wake.

Aina ya mchezo kama wa soka ni moja ya michezo ambayo huambatana na vijeraha vya ndani kwa ndani au kupata mkazo wa misuli kutokana na kufanya kazi sana.

Hali kama hii ndiyo huleta maumivu ya misuli, hali hii huweza kutoweka kirahisi na haraka kutokana na ulaji wa protini ya kutosha.

Hivi sasa dunia ni kijiji, vyakula vya aina hii vipo kila kona na hata zile protini maalumu kwa wanamichezo zinapatikana. Vile vile viywaji vya wanamichezo vyenye nyongeza ya protini vinapatikana.

Tafiti mbalimbali za kitabibu zinathibitisha kuwa mchezaji mwenye kutumia protini kwa wingi anapona majeraha kwa wakati na pia wako katika hatari ndogo ya kupata majeraha yatokanayo na michezo.

Vizuri wanamichezo kuzingatia ulaji wa vyakula vyenye protini kwa wingi kwa ajili ya kuwa na mwili imara na wenye kuhimili majukumu ya michezo.

Klabu zenye uwezo zijiongeze kwa kuwanununulia vinywaji vya virutubisho vya protini za wanamichezo za kutumia kabla na baada ya mechi.