SPOTI DOKTA: Haya ndio madhara ya vitasa kwa mabondia

JUMAMOSI iliyopita ulikuwa ni ‘Usiku wa Vitasa’ uliohusisha mapambano kadhaa ya ngumi yaliyochezwa katika Ukumbi wa Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Katika usiku huo wilayani Temeke pambano kubwa lilikuwa ni kati ya Mtanzania Abdallah Shabani Pazi maarufu kama ‘Dula Mbabe’ na Tshimanga Katompa kutokea DR Congo.

Katika pambano hilo, Mbabe alipoteza pambano hilo baada ya kupigwa kwa pointi. Ni kawaida kwa mchezo wa ngumu kushinda, kushindwa au kufungana pointi. Baadaye kwa wale wapenda vitasa wakakesha kulisubiri pambano la uzito wa juu duniani kati ya Tyson Fury na Deontay Wilder lililopigwa jijini Las Vegas katika uwanja wa T-Mobile Arena.

Katika pambano hilo ambao hapa Bongo lilionekana alfajiri kupitia runinga, Fury alimchapa Wilder katika raundi ya 11 kwa knock out. Pambano la Las Vegas lililokuwa na upinzani mkali lilimaliza ubishi kuwa mbabe ni nani.

Miamba hiyo ilikuwa inakutana kwa mara ya tatu ikiwa mara ya kwanza walitoka sare na ile ya pili Fury alishinda. Mapambano yote haya yalikuwa na mvuto wa kipekee kwa wapenda ngumi - mchezo ambao hivi sasa umepata umaarufu nchini kwa kujulikana kama vitasa.

Mchezo wa ngumi kama michezo mingine huwa na burudani hasa pale unapoona unayemshabikia anavyomtupia makonde mpinzani, huku wengi wakipenda kuona ushindi wa knock out.

Lakini hakuna mchezo rahisi, wacheza vitasa nao hukutana na kadhia kadhaa kutokana na kukutana na vitasa vizito ambavyo vinatua maeneo mbalimbali hasa eneo la kichwa na usoni.

Kwa aliyeona pambano la uzito wa juu ilikuwa ni hatari sana. Pamoja na kwamba Furry alishinda kwa knock out, lakini kila bondia alionja makonde yaliyotua kichwani na kumpeleka chini. Katika raundi ya 11 la pambano hilo Fury alimtupia makonde mawili mazito Wilder ambaye tayari alionekana kuwa hoi upande wa kushoto na kumpeleka chini na kupoteza fahamu.

Alipoteza fahamu kwa dakika chache, lakini baadaye alizinduka. Hali ile ilitisha kumuona bondia amelala chini akiwa amepoteza fahamu. Kama vile haitoshi ukimtazama kila bondia wa pambano lile alikuwa amevimba maeneo ya uso na midomo pamoja na kona za macho zikiwa zimechanika na kuwa na michubuko.

Msemo maarufu wa Kiingereza unasema ‘no pain no gain’ yaani lazima uumie ndiyo upate. Mabondia hao wameumia kwelikweli, lakini malipo wanayolipwa yanawafanya kuwa matajiri hasa mabondia wa uzito wa juu.

Katika kupitia pitia mitandaoni kulikuwa na watoa maoni kadhaa juu ya mchezo wa ngumi, yaani vitasa katika kurasa za mitandao ya kijamii za mabondia wote wa wawili.

Mmoja wa wakosoaji alisema hizo ngumu zinazotua vichwani mpaka kuwafanya wazimie zinawaacha salama kiafya hapo baadaye? Wengine walikuwa wanataka kujua vipi hali ya hapo baadaye ya Wilder ambaye kulikuwa na kila ishara kuwa anahitajika kupelekwa katika huduma za afya?

Wakosoaji wengine walihoji kuhusu glovu zinazotumika pengine ziongezwe sponji na vitambaa zaidi ili kuwakinga mabondia hao wasikumbane na vitasa vyenye makali wanapopigwa. Tofauti na michezo ya ngumi ya radhaa wao huvaa vikinga vichwa, lakini wale wa kulipwa hawavai kitu. Ingawa makundi haya yote wanavaa vikinga meno.

Kupitia matukio haya nimeonelea leo nije na ufahamu kuhusu madhara ya muda mfupi na baadaye ambao anayapata bondia anayeshiriki mara kwa mara masumbwi kwa muda mrefu.


MADHARA YENYEWE

Pamoja na kwamba mchezo wa vitasa ni hatari, lakini baadaye huwa ni hatari kiasi cha kupigwa marufuku duniani. Kwa ujumla mchezo wa ngumi umeonyesha kuhatarisha majeraha ya kichwa, mfumo wa mifupa, misuli na moyo.

Madhara ya muda mfupi ya kiafya ni pamoja na maumivu ya kichwa, kizunguzungu, michubuko usoni na maeneo mengine ikiwamo yale ya misuli ya usoni, mikono na mbavu. Vilevile ni kawaida kupata majeraha ya puani, mdomoni na masikioni ikiwamo maaeneo haya kuvuja damu.

Vilevile ni kawaida pia kwa mabondia wengi kupata tatizo la kupoteza fahamu kwa sekunde kadhaa - hii ni kutokana na vitasa hivyo kutua katika maeneo ya kichwa na kutikisa ubongo. Hali hii baadaye huweza kumfanya pia kupata maumivu sugu ya kichwa, kutosikia vyema, kichefuchefu, kukosa balansi na tatizo la kusahau.

Mtikisiko wa ubongo ndiyo huitwa kitabibu kama ‘concussion’. Ni tatizo la muda ambalo baadaye huweza kupona na kurudi katika hali ya kawaida. Mara chache imewahi kutokea duniani katika mchezo wa ngumi kwa bondia kutupiwa vitasa kiasi cha kupata tatizo la damu kuvuja katika ubongo na kufariki dunia. Ukiacha madhara ya muda mfupi, baadhi ya mabondia wastaafu wameonekana kupata hali ya kuwa na viashiria vya kuathirika kwa mfumo wa fahamu. Viashiria hivyo huwa ni hali kutetemeka mikono na mwili, viungo vya mwili kuwa dhaifu, kupoteza kumbukumbu na pia kuonyesha matatizo ya akili ikiwamo huzuni kali.

Tafiti mojawapo iliyowahi kuchapishwa na jarida la Science Daily uliofanywa na Chuo Kikuu cha Munich cha Ujerumani na Dk Hans Forstl ulionyesha kuwa asilimia 20 ya mabondia waliowahi kucheza wamepata tatizo la kuathirika mfumo wa fahamu na akili.


IMEANDIKWA NA DK SHITA SAMWEL