Slogan za Manara zinavyoishi

KWENYE soka kuna kitu kinaitwa ‘mind game’. Hii ni silaha ambayo imekuwa ikitumiwa kwa lengo la kumnyong’onyesha mpinzani na mtaalamu wa hiyo michezo ni Jose Mourinho, kocha wa AS Roma aliyejua kumvuruga Arsene Wenger wakati akiwa England.
Mourinho aliyekuwa Chelsea alikuwa akiutumia mdomo wake kumvuruga Wenger ambaye alikuwa kocha wa Arsenal na kuna wakati wawili hao waliwahi kuingia kwenye mzozo wa hadi mmoja kumkunja mwenzake wakati mchezo ukiendelea.
Huko ni Ulaya, lakini kwa Tanzania wapo ambao wamekuwa wakitumia midomo yao akiwemo msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire na Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru kuwavuruga wapinzani wao kwenye soka na kuwa silaha muhimu kwao kama sehemu ya kujipa tumaini jipya na kuwafanya mashabiki kuona kuwa inawezekana.
Hilo ndilo ambalo liliwafanya Yanga kuamini kwamba kuna haja ya kumjumuisha kundini aliyekuwa msemaji wa Simba, Haji Manara kutokana na kile ambacho alikifanya akiwa na Wekundu wa Msimbazi.
Manara aliwavuruga wapinzani wa Simba msimu uliopita kuanzia kwenye ligi na hapa Yanga ndio waliokuwa waathiriwa wakubwa kwani alitumia mtandao wake kuwaponda na vyombo vya habari kutoa kauli ambazo zilikuwa na matokeo chanya kwa timu yake ya zamani kwenye michuano ya kimataifa.
Zilikuwepo kauli mbiu ambazo Manara alitamba nazo akiwa Simba. Hizi hapa ni nyingine ambazo alizitumia kubamba kwenye michezo na kuamsha matumaini.
THIS IS SIMBA
Baada ya Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18 kwa mara ya kwanza kufuatia kukaa misimu mitano bila taji ndipo Manara alipoibuka na kaulimbinu ya This is Simba ikiwa na maana ya kujivunia kile ambacho walikifanya.
Kauli mbiu hiyo ilitokea kupendwa na mashabiki wa Simba na tangu hapo mambo yaliendelea kuwanyookea kwani walijikuta wakitwaa ubingwa wa ligi kwa misimu minne mfululizo kama ilivyokuwa miaka ya 1976, 1977, 1978 na 1979.
NEXT LEVEL
Kama kawaida yake mzee wa kuwanyong’onyesha wapinzani kwa maneno ya kukera, Manara, anayejiita Bugatti mara De La Boss alikuja na kaulimbiu ya Next Level baada ya Simba kuanza kufanya vizuri michuano ya kimataifa ikicheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mashabiki wa Simba walikiona kikosi chao sio cha kutesa tu Ligi Kuu Bara, bali wao ni Afrika na ndio maana kila ambapo walikuwa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika walikuwa wakijitokeza kwa wingi kuisapoti timu, na kwenye hilo walifanikiwa.
Hata hivyo, kila wapinzani wa Simba waliokuwa wakienda kwa Mkapa walikuwa wakiondoka na cha kusimulia, kwani ni nadra sana kwa Afrika umati wa watu kujitokeza - tena kwenye michezo ya kuwania nafasi ya kuingia makundi na hata makundi yenyewe.
WAR IN DAR
Miamba ya soka la Afrika, Al Ahly walishtushwa na kaulimbiu hii, lakini baadaye walielewa pengine walidhani kungetokea machafuko jijini Dar maana ujumbe uliobebwa ulikuwa na maana ya vita, lakini hilo halikuwafanya kuepuka kipigo kwa Mkapa.
Mchezo huo ulikuwa wa pili kwa Simba msimu uliopita katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifunga AS Vita tena ikiwa ugenini huko DR Congo. Al Ahly wakiwa na Pitso Mosimane hawakuamini kilichotokea kwa Mkapa kwani walijikuta wakikumbana na kipigo chao cha kwanza msimu uliopita.
Hapo Al Ahly walikuwa wamoto kwani walitoka kushiriki michuno mikubwa zaidi duniani ngazi ya klabu (Klabu Bingwa ya Dunia) ambako waliambulia kushika nafasi ya tatu baada ya kufungwa kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani.
THE RETURN OF CHAMPION
Alipotua tu Yanga, Bugatti na kufanyiwa utambulisho inawezekana kuwa alijifungia ndani kuumiza kichwa ni kauli gani mbiu ambayo anaweza kuibuka nayo na kuiingia vichwani mwa mashabiki wa timu ya Wananchi na kutembea vifua mbele.
Ndipo alipoibuka na kaulimbiu hii ambayo imebeba maana ya kuwa mabingwa wamerejea. Ni imani yake pamoja na Wanayanga kuwa utawala wao unarejea Ligi Kuu Bara baada ya misimu minne iliyopita kuambuliwa patupu. Yanga ndio wanashikilia rekodi ya kutwaa mara nyingi zaidi ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni mara 27 wakiwafuatiwa na Simba 21.
THE POINT OF NO RETURN
Yanga walikuwa miongoni mwa wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa msimu huu, lakini bahati mbaya ni kwamba wamejikuta wakitolewa kwenye Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 2-0. Walianza kupigwa Dar kwa bao 1-0 na hata kwenye mchezo wa marudiano huko Port Harcourt, Nigeria.
Kabla ya Yanga kwenda Nigeria, Bugatti ambaye amekuwa akiwapiga dongo waajiri wake wa zamani, aliamini Yanga inaweza kupindua meza na kuja na kaulimbiu hiyo ambayo ilikuwa na maana kuwa hakuna sababu ya kurudi nyuma kama askari vile wawapo vitani, lakini ndio kama ilivyotokea walikumbana na kipigo kingine.
WASIKIE HAWA
Beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anasema kaulimbiu ni chachu kwao kama wachezaji kupambana kufikia malengo ya klabu na matamanio ya mashabiki ambao siku zote wamekuwa nyuma yao kuwapa nguvu.
“Kwetu wachezaji kauli mbiu kama hizo zimekuwa zikitupa moyo ni sehemu tu ya hamasa na kutufanya tufanye zaidi,” anasema.
Aliyekuwa kocha msaidizi wa Gwambina, Athuman Bilali ‘Bilo’ anasema kazi yoyote inahitaji ubunifu ili kuwa na mvuto, “Amejiunga na Yanga kutokana na ubunifu wake, anastahili kupongezwa kwa kile anachokifanya kwa manufaa ya klabu.”