Prime
Siri imefichuka... Yanga ilikwama hapa, Aziz KI atajwa

Muktasari:
- Matokeo ya jana usiku yameendeleza maumivu makali kwa mabingwa wa soka wa Tanzania iliyokuwa ikipiga hesabu za kutaka kucheza tena robo fainali ya michuano hiyo kama ilivyofanya msimu uliopita na kuzuiwa kwenda robo fainali na Mamelodi Sundowns kwa penalti baada ya suluhu ya mechi mbili mfululizo.
YANGA imepoteza mechi ya pili mfululizo ya Kundi A katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kucharazwa mabao 2-0 na MC Alger ya Algeria katika mechi iliyopigwa ugenini, ikiwa ni wiki moja tu tangu ilipopasuka nyumbani mbele ya Al Hilal ya Sudan.
Matokeo ya jana usiku yameendeleza maumivu makali kwa mabingwa wa soka wa Tanzania iliyokuwa ikipiga hesabu za kutaka kucheza tena robo fainali ya michuano hiyo kama ilivyofanya msimu uliopita na kuzuiwa kwenda robo fainali na Mamelodi Sundowns kwa penalti baada ya suluhu ya mechi mbili mfululizo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kupoteza mechi mbili mfululizo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa iliyowahi kuicheza pia mwaka 1998 na msimu uliopita, lakini ikirejea ilichowahi kukutana nacho mwaka 2016 katika hatua kama hiyo ya makundi ila ni kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Mabingwa hao wa soka wa Tanzania, walipoteza pia mechi mbili mfululizo za makundi katika michuano hiyo ya Shirikisho kwa kulazwa 1-0 na MO Bejaia ya Algeria pamoja na TP Mazembe ya DR Congo ambao wanatarajiwa kukutana nao kwenye mchezo ujao wa Kundi A ikiwa pia ugenini.
Mwanaspoti liliufuatilia mchezo wa jana usiku na kubaini mambo kadhaa yaliyoiangusha Yanga inayonolewa na Kocha mpya, Sead Ramovic na hapa chini imeyaanisha na kama watayafanyia kazi huenda ikarejea njia kuu kwenye michezo minne iliyosalia katika kundi hilo na kufufua matumaini ya kutinga robo fainali.
ISHU YA KUJIAMINI
Yanga mchezo wa jana sio kwamba haikucheza vizuri kabisa, vipo vipindi ilionyesha utulivu mkubwa wa kuwabana MC Alger hasa kipindi cha kwanza kilichomalizika bila timu hizo kufungana na kipindi cha pili kabla na baada ya kuruhusu bao la kwanza.
Hata hivyo, shida kubwa ya Yanga ilikuwa ni wachezaji wake kupoteza kujiamini kupanga sawasawa mashambulizi yao ya kushtukiza, kila hesabu zao zilipokuwa zinapangwa ziliishia kwa wapinzani kirahisi.

KUPOTEZA PASI
Angalia pasi ambazo zilikuwa zinapigwa na viungo wa Yanga ambao walikuwa wakianzisha mashambulizi Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Stephanie Aziz KI na hata Mudathir Yahya kwa wakati flani.
Yanga ilipoteza pasi nyingi sana ambazo ziliwapunguzia ubora wa kukamilisha mashambulizi yao ya haraka, kwa soka la mashambulizi ya kushtukiza ili ufanikiwe unatakiwa kuhakikisha pasi zako zinakuwa za uhakika kuhakikisha mashambulizi yako yanafanikiwa kitu ambacho wageni walikikosa.
Wachezaji tegemeo kama Pacome Zouzoua, Duke Abuya, Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli hawakuwa katika ubora uliozoeleka kiasi kilimfanya Kennedy Musonda kuwa na kibarua cha kushuka chini kutafuta mipira, ilihali safu ya ulinzi iliyokuwa chini ya nahodha Bakar Mwamnyeto kufanya makosa mengi ya wazi.
KUSHOTO KUNAVUJA
Yanga itaendelea kukumbuka uwepo wa beki wake wa kushoto Chadrack Boka ambaye ndio anapambana kurudi akitokea majeruhi na hili linakuwa rahisi kutokana na mbadala wake Nickson Kibabage kushindwa kufanya mambo makubwa.
Kibabage ameshindwa kuonyesha akili yake imekomaa kufunika kukosekana kwa Boka baada ya kucheza vibaya mechi mbili mfululizo za mashindano hayo makubwa ya klabu Afrika.
MC Alger walitumia eneo hilo kupitisha mashambulizi yao mengi kwenye mchezo huo na kufanikiwa kutengeneza ushindi wao wa kwanza katika mechi mbili ilizocheza.
AZIZ KI AMEPOTEA
Kila timu ina injini yake ya kutengeneza mashambulizi, ukaingalia msimu uliopita Yanga ilikuwa inategemea ubunifu mkubwa wa Aziz KI kufanya mambo makubwa lakini msimu huu kiungo huyo ameendelea kucheza kwa kiwango cha chini.
Aziz KI ameshuka na hata uso wake unaonyesha kuwa ni mchezaji anayehitaji muda kurudisha kiwango chake cha msimu uliopita badala yake angalau unaona ubunifu wa Pacome au hata Chama wakiingia lakini sio kwa raia huyo wa Burkina faso.
MAJERAHI
Yanga bado inateswa na majeruhi walionao kwenye kikosi chao ambao wameondoa ubora wa timu hiyo kucheza kwa kiwango kikubwa, mechi hizi mbili imewakosa Khalid Aucho, Boka, Dickson Job huku kipa Djigui Diarra akicheza mchezo wa jana akiwa na majeraha, hii itaiathiri Yanga katika mechi inazoendelea kuzicheza.

UMALIZIAJI MBAYA
Kule mbele nako Yanga bado haina utulivu mkubwa wa kumalizia nafasi inazotengeneza, jana ilianza na mshambuliaji Kennedy Musonda licha ya kuongeza kitu, lakini bado kushuka kwake chini sana kuliifanya timu hiyo kuwapa utulivu mkubwa mabeki na hata kipa wa MC Alger kuyadhibiti mashambulizi yao hasa kutokana na kupotea kwa Aziz KI.
Hata alipoingia Clatous Chama na Prince Dube, bado hali ilikuwa ngumu kwa safu hiyo ya ushambuliaji ya Yanga na kuwafanya wenyeji watoke na ushindi huo murua wa mabao ya Ayoub Abdellaoui aliyefunga bao la kwanza dakika ya 64 kabla ya Soufiane Bayazid kutupia lingine dakika za majeruhi.

MSIKIE RAMOVIC
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic akizungumzia mchezo wa jana alisema hayakuwa matokeo ambayo waliyatarajia hasa baada ya kuruhusu mabao ambayo yalitokana na makosa yao kwa kupoteza umakini kwenye matukio mawili tofauti.
“Inawezekana haikuwa siku nzuri kwetu, ukitazama tulivyoanza mchezo na matokeo tuliyoyapata ni vitu viwili tofauti, tulifanya makosa mawili ya kupoteza umakini na yakatugharimu, hizi ni mechi ambazo unatakiwa kucheza ukiwa timamu kwa muda wote wa mchezo,” alisema Ramovic aliyeiongoza Yanga katika mechi tatu tofauti ikiwamo moja ya Ligi Kuu ikishinda dhidi ya Namungo na ile ya CAF iliyolala mbele ya Al Hilal.
Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea nchini ili kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho kabla ya kuifuata TP Mazembe wikiendi ijayo katika mchezo wa raundi ya tatu wa Kundi A kwa Ligi ya Mabingwa Afrika.