Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SIO ZENGWE: Tutajipimaje kuwa wachezaji 12 wamesaidia soka letu?

DESEMBA mwaka jana Chama cha Soka England (FA), Ligi Kuu (EPL) na Ligi ya Soka Uingereza (RFL) vilifikia makubaliano ya vigezo vinavyotakiwa kuangaliwa kwa wachezaji kutoka nje baada ya taifa hilo kujiondoa Umoja wa Ulaya (EU), hatua iliyopachikwa jina la Brexit.

Mapendekezo yaliyotolewa na chombo kinachosimamia upitishaji kanuni za soka, GBE, yaliwasilisha serikalini na FA na sasa yameshapitishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Vigezo hivyo vimeunda utaratibu unaotumiwa na Ligi Kuu na EFL, inayoandaa Kombe la Carabao, kusajili wachezaji wa kigeni baada ya Uingereza kukamilisha kujitoa Umoja wa Ulaya Desemba 31, 2020.

Chini ya kanuni mpya zitakazotumiwa kutoa kibali cha kazi, klabu hazitaruhusiwa kusajili mchezaji aliye chini ya miaka 18, wakati walio na umri chini ya miaka 21 wataruhusiwa watatu tu.

Yaani ingekuwa wakati huo, Arsenal wasingemsajili Cesc Fabregas kutoka Barcelona, wala Manchester United isingemchukua Paul Pogba kutoka Le Havre, Ufaransa.

Wachezaji kutoka EU hawatasajiliwa bure kama ilivyokuwa awali wakati walipokuwa wakinufaika na soko huru la ajira kwa nchi wanachama.

Kibali cha kazi kitatolewa kwa mfumo wa pointi. Yaani pointi zitakusanywa kwa kuangalia klabu ambazo nchi anayotoka iko katika kumi bora ya ubora wa Fifa, idadi ya mechi alizochezea nchi yake iwe angalau asilimia 50 ndani ya miaka miwili, idadi ya mechi alizochezea klabu anayotoka na ubora wa klabu na ligi anayotoka.

Pia idadi ya wachezaji wa kigeni inapunguzwa kutoka wachezaji 17 hadi 13. Hii inamaanisha klabu zitajikita zaidi kuangalia wachezaji wa ndani na hivyo kukuza soka la ndani. Thamani ya wachezaji wa ndani pia itaongezeka, wakati vigezo hivyo vitaihakikishia Uingereza kupata wachezaji bora kutoka nje na hivyo kulinda thamani ya ligi hiyo maarufu duniani. Nimetoa mfano huo kwa kuwa najua wengi wanazungumzia kirahisi sana uamuzi wa Shirikisho la Soka (TFF) wa kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka 10 hadi 12, lakini ikiweka masharti kwa wachezaji wanaotumika kuwa wanane tu.

Ni rahisi kutoka mifano ya nchi za Ulaya, lakini idadi inayoonekana kuwa kubwa kwa klabu za barani humo inatokana na sheria za kazi za EU zinazoruhusu mtu mkazi wa nchi hizo kufanya kazi popote bila masharti.

Kwa hiyo, Chelsea inaweza kupanga wageni kikosi kizima, lakini wageni wanaweza kuwa wawili tu, yaani wale wanaotoka Afrika au nchi ambazo si za EU.

Pia, wachezaji kutoka nchi kama za Amerika Kusini mara nyingi huchukua uraia pacha, hivyo kuwa raia wa Ulaya. Ndio maana klabu inapofikia idadi inayotakiwa ya wachezaji wa kigeni, humshauri moja ambaye nchi yake inaruhusu uraia pacha, achukue uraia na hivyo kuachia nafasi kwa mgeni mwingine.

Kwa hiyo ni tofauti na tunapoangalia huku ambako hata mchezaji kutoka Kenya au Uganda ni mgeni.

Lakini tumeona pia jinsi kanuni zinavyotaka mchezaji awe bora, awe amecheza idadi gani ya mechi kwenye klabu yake na timu yake ya taifa na nafasi ya nchi yake katika orodha ya ubora duniani.

Lakini pia tumeona jinsi suala la wachezaji vijana lilivyoangaliwa. Maana yake kama klabu ina kikosi cha vijana, haitaruhusiwa kuwa nao lukuki, bali watatu tu tena wenye umri chini ya miaka 21.

Ni kwa jinsi gani sisi tumezingatia hayo yote hadi tukaamua kuongeza idadi kutoka 10 hadi 12? Tumeweka sheria gani ambazo zitalazimisha klabu kukuza vijana? Ni kwa kiasi gani tumeshirikiana na serikali kuweka kanuni zinazohusu sheria ya kazi? Kama wachezaji watano wa kigeni hawakuweza kukuza vijana wetu, na baadaye wachezaji saba, kisha 10, tumeweka vipimo gani kuhakikisha hawa 12 watatusaidia na ni baada ya muda gani.

Kumbuka, msimu huu walioondoka ni Tuisila Kisinda, Clatous Chama na Luis Miquissone, wote wageni huku timu yetu ya taifa ikiendelea kutofanya vizuri. Pia tukumbuke Tanzania bado ni taifa dogo kisoka duniani na hivyo linahitaji sheria na kanuni zinazosaili mazingira haya na si kuiga tu.