Prime
KOMBE LA SHIRIKISHO (FA): Fainali ya rekodi, heshima

MWISHO wa ubishi. Ndiyo, ngoja tuone itakuwaje katika fainali ya msimu huu ya Kombe la Shirikisho (FA) inayopigwa Jumapili.
Mechi hiyo ya kufungia msimu wa 2024-2025 inazikutanisha Yanga inayotetea taji kwa msimu wa nne na Singida Black Stars kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja,visiwani Zanzibar. Hii ni fainali ya pili ya michuano hiyo kupigwa Zanzibar.
Yanga inayoshikilia taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo, itashuka New Amaan, ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa fainali zilizopita dhidi ya Azam FC, lakini ni siku chache kwao tangu iifumue Dodoma Jiji kwa mabao 5-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Ni fainali ngumu kutabirika kwa rekodi za timu hizo, Yanga ikisaka taji la nne mfululizo la michuano hiyo, huku Singida ikilisaka la kwanza, kwani haijawahi kufika hatua kubwa kama hiyo tangu enzi ikiifahamika kama Ihefu kabla ya kubadilisha jina hilo msimu huu.
Hii ni fainali ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika michuano hiyo, huku rekodi zikiibeba zaidi Yanga, japo dakika 90 za fainali hiyo ndizo zitakazoamua kwa kuzingatia Singida sio wepesi kwani msimu uliopita ilifika pia nusu fainali na kung’olewa na Yanga.
Hapo chini ni uchambuzi wa namna fainali hiyo itakavyokuwa kwa kuzingatia rekodi baina ya timu hizo katika michuano hiyo, lakini hata aina ya vikosi vya timu hizo zilizoweza kupenya kuanzia hatua ya 64 Bora hadi kufika hapo zilipo. Endelea...!

YANGA WABABE
Kama hujui, hii ni fainali ya tano mfululizo kwa Yanga katika michuano hiyo, ya kwanza ilipoteza mbele ya Simba mechi hiyo iliyopigwa Julai 25, 2021 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma.
Katika mechi hiyo ilishuhudia kiungo mkabaji wa Yanga, Mukoko Tonombe akilimwa kadi nyekundu sekunde chache kabla ya mapumziko kwa kumchezea vibaya, nahodha wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’.
Kadi hiyo ni kama iliigharimu Yanga kwani ililala kwa bao pekee lililowekwa kimiani na kiungo mkabaji raia wa Uganda, Taddeo Lwanga ‘Injinia’ dakika ya 80 kwa kichwa akimalizia mpira wa kona iliyochongwa vyema na winga, Luis Miquissone.
Tangu ilipopoteza pambano hilo la Lake Tanganyika, Kigoma hadi sasa unaposoma makala haya, Yanga haijapoteza tena mchezo wowote wa michuano ya Kombe la Shirikisho ikiweka rekodi ya kucheza mechi 23 na zote ikishinda hadi kutinga fainali hizi.
Awali, Simba ndiyo iliyokuwa ikishikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi (17) mfululizo bila kupoteza kuanzia msimu ya 2019-2020, 2020-2021 na 2021-2022 ilipotolewa nusu fainali na Yanga kwa kulazwa bao 1-0 lililotokana na shuti kali la mbali la kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’, aliyepo Azam FC kwa sasa.
Mechi hiyo iliyoitibulia Simba ilipigwa Mei 28, 2022 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na kuivusha Yanga hadi fainali na kubeba ubingwa wa kwanza kati ya mitatu iliyotwaa hadi sasa mfululizo kwa msimu huo wa 2021-2022 kwa kuichapa Coastal Union kwa penalti 4-1.
Mchezo huo wa fainali uliopigwa Julai 2, 2022 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha ulishuhudiwa ukimaliza dakika 90 kwa sare ya 2-2 na kuongezwa dakika 30 na kila timu iliongeza bao moja na kufanya matokeo ya dakika 120 kuwa sare ya 3-3.
Yanga ikipata mabao yake kupitia kwa Feisal Salum Dk 57, Heritier Makambo 82’ na Denis Nkane dk 113, wakati Abdul Suleiman ‘Sopu’ akipiga hat trick kwa kuwafungia Wagosi mabao yote matatu dakika za 10, 87 na 98’.

SAFARI ILIVYOANZA
Katika msimu huo ambao Yanga iliinyang’anya taji Simba kwa kuing’oa nusu fainali, safari ya ubingwa kwa Vijana wa Jangwani ilianza kwa kuitoa Ihefu kwa mabao 4-0 katika pambano lililopigwa Desemba 15, 2021 na kutinga 32 Bora ilipokutana na Mbao FC na kuichapa kwa bao 1-0 siku ya Januari 29, 2022.
Katika hatua ya 16 Bora, wababe hao wa soka nchini, walikutana na Biashara United na kuifunga mabao 2-1 mechi ikipigwa Februari 15, 2022 na kufuzu hatua ya robo fainali ambapo huko ilivaana na Geita Gold na kumaliza dakika 90 kwa sare ya 1-1 kabla ya kuvuka kwenda nusu fainali kwa ushindi wa penalti 7-6 mechi iliyopigwa Aprili 10, 2022.
Ndipo katika nusu fainali bao la kombora la mbali la Fei Toto likaizamisha Simba na kuitemesha taji na kwenda kuvaana na Coastal katika fainali kali iliyopigwa jijini Arusha na Yanga kubeba taji kwa msimu huo ambao pia ilimaliza pia kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa rekodi ya bila ya kupoteza.

MOTO WA 2022-2023
Katika msimu huu, Yanga ilianza michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho kwa kupangwa kukutana na Kurugenzi FC ya Kagera katika hatua ya 64 Bora na kushindwa kwa kishindo kwa mabao 8-0, mchezo ukipigwa Desemba 10, 2022 jijini Dar es Salaam.
Yanga iliendeleza kugawa dozi nene katika michuano hiyo hatua ya 32 Bora baada ya kuifumua Rhino Rangers ya Tabora kwa mabao 7-0, mechi ikipigwa Januari 29, 2023 na kufuzu hatua ya 16 Bora na ilipangwa kuvaana na Tanzania Prisons ya Mbeya,
Katika mchezo huo wa 16 Bora uliopigwa Machi 3, 2023, Yanga ilishinda kwa mabao 4-1 na kukata tiketi ya robo fainali na ilipangwa kukutana na Geita Gold mchezo uliopigwa Aprili 8, 2023 na kushinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Fiston Mayele.
Yanga ilikutana na Singida Big Stars (sasa Fountain) katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa Mei 21, 2023 mjini Singida na kushinda kwa bao 1-0 na kufuzu kwenda fainali na ilikutana na Azam FC, mechi ikipigwa Juni 12, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Bao pekee lililoizamisha Azam liliwekwa kimiani kwa kichwa na Mzambia, Kennedy Musonda dakika ya 13 akimalizia mpira wa krosi ya beki Djuma Shaban ambaye awali alipiga kona fupi kwa Tuisila Kisinda na kunyunyiza mpira uliotendewa haki na mshambuliaji huyo aliyekuwa ametu kikosi katika dirisha dogo katika msimu huo.
Bao hilo lilidumu na kuifanya Yanga kutetea taji kwa msimu wa pili mfululizo ikifikisha jumla ya mechi 12 bila kupoteza katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho.

MSIMU WA 2023-2024
Yanga iliuanza msimu huu kibabe kwa kugawa dozi katika safari ya kutetea taji ikianza hatua ya 64 Bora kwa kuifumua Hausing ya Njombe kwa mabao 5-1 katika mechi iliyopigwa Januari 30, 2024 na kutinga hatua ya 32 Bora,
Katika hatua hiyo ya 32 Bora, watetezi hao walikutana na maafande wa Polisi Tanzania, Februari 20, 2024 na kuwafumua kwa mabao 5-0 na kuvuka salama kwenda 16 Bora na huko ikakutana na Dodoma Jiji siku ya Aprili 10, 2024 kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma na kushinda kwa mabao 2-0.
Hatua ya robo fainali, Yanga ilikutana na Tabora United katika mchezo uliopigwa Mei Mosi, 2024 na kushinda kwa mabao 3-0 na kuvuka kwenda nusu fainali na ilikutana na Ihefu (sasa Singida BS) kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Mechi hii ilikuwa dume kwelikweli, kwani ilishuhudiwa zikipigwa dakika 120 na Yanga kushinda bao 1-0 lililopatikana katika dakika za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu na kufuzu kwenda fainali kukutana na Azam FC.
Mchezo huu wa fainali ulipelekwa mjini Unguja kwene Uwanja wa New Amaan Complex na Yanga kushinda kwa penalti 6-5 baada ya dakika 120 kushindwa kutoa mshindi kwani timu hizo hazikufungana.
Mechi hiyo iliyowapa Yanga ubingwa wa tatu mfululizo wa michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho ilipigwa Juni 2, 2024, ikifikisha jumla ya michezo 18 bila kupoteza.

MSIMU HUU SASA
Katika msimu huu wa 2024-2025, Yanga ilianza kutetea taji kwa kupangwa kuumana na Copco FC ya Mwanza inayoshiriki First League na watetezi hao waliibuka na ushindi wa mabao 5-0.
Ushindi huo ulipatikana katika pambano hilo la hatua ya 64 Bora lililopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Jan 25 mwaka huu , 2025 na Shekhan Ibrahim alifungua pazia kwa kufunga bao dakika ya 35’.
Prince Dube alifunga bao la pili dakika ya 57 kaabla ya Maxi Nzengeli kufunga kwa penalti dakika ya 68 huku Dube Abuya na Mudathir Yahya kufunga mengine mawili ya mwisho na kuivusha Yanga kwenda hatua ya 32 Bora.
Katika hatua ya 32 Bora, Yanga ilipangwa kuvaana na Coastal Union mchezo uliopigwa pia kwenye Uwanja wa KMC Complex siku ya Machi 12 na watetezi hao kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 yaliyofungwa na Maxi Nzengeli aliyetupia mawili dk 2 na 15, kisha Mfungaji Bora wa michuano hiyo kwa msimu uliopita, Clement Mzize alifunga la tatu dk ya 21 muda mchache baada ya Miraj Abdallah kuifungia bao Coastal dk ya 18.
Yanga ikavuka salama hadi hatua ya 18 Bora na kama kawaida, watetezi wakatoka na ushindi kwenye Uwanja wa KMC Complex dhidi ya Songea United iliyopo Ligi ya Championship.
Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 na kuifanya ifikishe mechi ya 21 mfululizo katika Kombe la Shirikisho bila kupoteza kwa mabao ya Duke Abuya dakika ya 22 na jingine la Jonathan Ikangalombo ‘Ikanda Speed’ aliyefunga dakika ya 54.
Katika robo fainali, Yanga ilipangwa na Stand United iliyopo Ligi ya Championship na iliyotinga play-off ya mwisho ya kuwania kupanda Ligi Kuu kuzifuata Mtibwa Sugar na Mbeya City zilizotangulia mapema.
Katika mechi hiyo, Yanga ilifanya kweli kwa kuifumua Chama la Wana kwa mabao 8-1, yaliyofungwa na Stephane Aziz KI aliyetupia manne dakika za 16, 51, 60 na 64, Clatous Chama dk 32 na 41, Nickson Kibabage dk 20 na Kennedy Musonda dk 86, huku la kufutia machozi la Stand likifungwa na; Msenda Senga dk 49.
Katika nusu fainali, Yanga ilikutana na JKT Tanzania na kuwachapa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga kupitia mabao na Prince Dube dk 41 na Mudathir Yahya liefunga sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho na kuipeleka timu hiyo fainali.

SINGIDA SASA
Ukiachana na nusu fainali iliyoicheza msimu uliopita ikitumia jina la Ihefu, timu hiyo kwa sasa ikifahamika Singida BS haijawahi kucheza hatua kubwa kama hii ya fainali.
Singida iliyomaliza msimu wa Ligi Kuu ikishika nafasi ya nne na kukata tiketi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, haikufika hapo kirahisi kwani njia zake zilikuwa ngumu, lakini ilikaza buti na kupasua anga hadi kukutana na Yanga.
Safari ya Singida kuitafuta fainali ilianzia hatua ya 64 Bora kwa kukutana na Magnet inayoshiriki Ligi ya Mabingwa wa Mkoa na kuifumua mabao 2-0 aliyowekwa kimiani na Maarouf Tchakei na Emmanuel Keyekeh na kufuzu 32 Bora.
Katika hatua hiyo ya 32 Bora, Singida ilipangwa tena na timu ya Mabingwa wa Mkoa (RSL) Leo Tena iliyoiduwaza Dodoma Jiji katika hatua ya 64 na Walima Alizeti hao hawakutaka kuremba kwani waliwafumua kwa mabao 4-0, kupitia Tchakei, Josephat Bada, Elvis Rupia, Hernest Malonga liyefunga kwa penalti.
Katika hatua ya 16 Bora safari hii Singida ilipangwa na timu ya Ligi Kuu, KMC na kuifunga kwa bao 1-0 la dakika ya 35 lililotokana na beki wa Wana Kinondoni, Abdallah Said ‘Lanso’ kujifunga katika harakati za kuokoa na kuivusha Singida kwenda robo fainali.
Kama ilivyokuwa 16 Bora, Singida katika robo fainali ilipewa timu ya Ligi Kuu, Kagera Sugar iliyoshuka daraja baada ya misimu zaidi ya 20 na kuwafumua kwa mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani na Victorien Adebayor dakika ya 11 na Jonathan Sowah dk 66’.
Katika nusu fainali Singida ilipangwa kuvaana na Wekundu wa Msimbazi, Simba na bila kutarajiwa, vijana hao wa Singida waliibuka na ushindi wa mabao 3-1, ikiwa ni siku chache tangu ilipotoka kulala 1-0 kwenye mechi ya kiporo cha Ligi Kuu iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo ya nusu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo mjini Karatu mkoani Manyara, Singida ilipata ushindi kwa mabao ya Jonathan Sowah dakika ya 17 na Emmanuel Keyekeh akafunga mawili dakika ya 35 na 48’, kabla ya Jean Charles Ahoua kuifungia Simba bao la kufutia machozi kwa friikikii ya dakika ya 67.
NAMBA HAZIONGOPI
Licha ya kwamba hii ni fainali ya kwanza kwa timu hizo kukutana, ila rekodi zinaibeba Yanga, kwani imekuwa ikiiburuza Singida katika michuano hiyo tangu ikiifahamika kama Ihefu na hata kwenye Ligi Kuu, bado watetezi hao wanaonekana ni wababe.
Katika michuano ya Shirikisho timu hizo zinakutana kwa mara ya nne, lakini katika mechi tatu za nyuma, Yanga imeibuka kidedea zote, ikianza hatua ya 64 Bora kwa msimu wa 2017-2018 zilipokutana mara ya kwanza na Yanga kushinda kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.
Mara ya pili zilikutana msimu wa 2020-2021 Ihefu ikiwa imepanda Ligi Kuu kisha kushuka msimu huo huo na ilipoteza kwa mabao 4-0 katika hatua ya 32 Bora na msimu uliopita ilipigwa tena 1-0 katika nusu fainali kwa bao la dakika ya 101 la Stephane Aziz Ki, aliyeuzwa Wydad Casablanca ya Morocco.
Safari hii ikitumia jina la Singida BS inakutana tena na Yanga kwa mara ya nne ikiwa ni fainali yao ya kwanza na itakuwa na kazi ya kutaka kulipa kisasi mbele ya watetezi hao.
Katika mechi za Ligi Kuu, timu hizo zimekutana mara nane, huku sita kati ya hizo Yanga ikiibuka wababe, ilihali Singida enzi ikitumia jina la Ihefu imeshinda mara mbili tu tena zote zikiwa nyumbani na hakuna mechi iliyoisha kwa sare baina ya timu h1zo.
Yanga imevuna jumla ya mabao 16 katika mechi hizo nane za Ligi Kuu, huku Singida/Ihefu, ikivuna mabao matatu, likiwamo moja ililopata msimu huu ilipolala 2-1.
Hivyo fainali hii ya msimu huu, Yanga itakuwa ikisaka heshima na kulinda rekodi kwa wapinzani wao, ilihali Singida ikisaka taji la kwanza na kumaliza unyonge kwa Yanga.
Nani atakayeibuka kidedea katika fainali hiyo ya aina yake? Ni suala la kusubiri na kuona!