Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Happy birthday Lionel Messi katika pensheni yenye raha

MESSI Pict

JUA linazama. Ametimiza miaka 38 Jumanne hii iliyopita. Lionel Andres Messi. Tumesafiri naye kwa muda mrefu katika maisha yake ya mpira na mengineyo. Tangu mwaka ule akiwa na umri wa miaka 13 wakati Barcelona walipomtoa Rosario kumpeleka Catalunya kumchoma sindano ili akue vizuri.


Na sasa yupo katika pensheni yake nzuri tu. Katika umri wa miaka 38 anashiriki katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu akiwa na Inter Miami. Majuzi alifunga bao maridhawa dhidi ya Porto. Kuna watangazaji na mashabiki walijiuliza kama Messi anaweza kwisha. Ukweli ni kwamba tayari umri umeshamsaliti Messi.


Yeye wa miaka 38 umri umemsaliti kama ambavyo hasimu wake Cristiano Ronaldo umri umemsaliti katika umri wa miaka 40. Messi halisi asingekuwa Marekani sasa hivi kama ambavyo Ronaldo halisi asingekuwa Saudi Arabia wakati huu. Miguu imewasaliti na hauwezi kuwalaumu. Uzuri ni kwamba nahisi Messi anastaafu akiwa ana tabasamu zaidi. Ana pensheni nzuri zaidi.

Katika michuano hii Messi hawezi kuambulia chochote kwa sababu Inter Miami haina ubavu mbele ya kina Real Madrid, PSG, Manchester City na wengineo ambao wapo katika michuano hii. Hata hivyo Messi hawezi kujali sana. Hii sio michuano maarufu ambayo inaweza kumpa nafasi ya kutwaa mwanasoka bora wa dunia au kumshusha.

MES 01

Messi anacheza katika michuano hii kama bonanza. Haishangazi kuona Lamine Yamal yupo na kaka yake Neymar akipiga danadana pale Brazil katika likizo yake. Barcelona haipo na yeye hayupo. Hajali sana. Sio michuano maarufu. Labda baadaye inaweza kuwa michuano maarufu kiasi cha kumnyima mchezaji tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.

Michuano ambayo inaweza kumnyima hadhi mchezaji ni ligi yake kubwa ya ndani, Ligi ya Mabingwa, Kombe la Dunia na michuano ya Euro. Kwa sasa wanasoka mahiri hawana presha sana katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu ambayo Messi inamkutanisha Aziz ki pamoja. Fifa wanahitaji muda kuipa umaarufu na ndio maana Messi anazeeka vizuri na pensheni yake.

Sana sana kwa sasa Messi ameipa hadhi michuano yenyewe. Na namna ambavyo Messi anazeeka vizuri ni wazi kwamba anaingiza kiasi kikubwa cha pesa kwa Inter Miami na yeye mwenyewe kwa kushiriki michuano hii. Messi ni sura maarufu zaidi katika michuano hii ingawa miguu na umri vinamsaliti. Kuna pesa yake imeingia kwa yeye kushiriki katika michuano hii. Hii ni namna ya kustaafu vema.

MES 02

Kitu kizuri kwake zaidi ni kwamba Messi ameshinda kila kitu. Na mwakani kutakuwa na kombe la dunia ambalo itafanyika pale pale Marekani wakishirikiana na majirani zao Mexico na Canada. Atakwenda katika michuano hii akicheza kama anavyocheza michuano hii. Kisa? Ameshatwaa Kombe la Dunia kama ambavyo wanadamu walikuwa wanahitaji atwae.

Iliwahi kusemwa kwamba ili Messi awekwe katika ngazi moja na Pele, Maradona na wengineo lazima atwae kombe la dunia. Alitwaa pale Doha Desemba 2022. Na ndio maana hana presha. Hata wakati huu anaposubiri michuano hii hapo mwakani atakuwa hana presha. Atacheza michuano hiyo akiwa na miaka 39.

Nani atamuita kucheza Argentina? Hilo ni swali rahisi. Hasimu wake Ronaldo ana wakati mgumu kidogo. Ukweli ni kwamba analazimisha. Miguu imemsaliti na yupo katika kizazi cha dhahabu cha Wareno. Tatizo Ronaldo bado anataka kuwa kila kitu pale Ureno. Akina Rafael Leao wanakaa nje wakiwa na nguvu zao kwa ajili ya kumpisha Ronaldo.

MES 03

Uzuri wa pensheni ya Messi ni kwamba anacheza katika taifa ambalo kwa sasa limeshindwa kuzalisha vipaji maridadi vya kumtupa nje Messi katika kikosi cha timu ya taifa. Zama zile Messi wa leo watu wangeanza kumng’ong’a. Wakati ule Argentina ikiwa na akina na Gabriel Millito, Sergio Aguero, Angel Di Maria na wengineo.

Leo Argentina haina staa mkubwa Manchester United, Arsenal, Real Madrid, Barcelona, Bayern Munich na kwingineko. Ni tofauti na zama zile za kina Aguero achilia mbali akina Di Maria. Messi atakwenda katika Kombe la Dunia akishiriki bila ya presha kwa sababu alikuwepo Doha na alitwaa kombe lenyewe.

Rafiki yangu Ronaldo hana presha katika michuano hii ya Kombe la Dunia la Klabu kwa sababu hashiriki na haiwezi kumnyima hadhi yake. Tatizo ni mwakani. Atahitaji kina Leao wamsaidie kufikia hadhi ya Messi, Maradona na Pele akiwa ba umri wa miaka 41. Ndiyo, ni Februari mwakani tu Ronaldo atatimiza miaka hiyo. Atakwenda Marekani, Canada na Mexico akiwa na umri huo.

MES 04

Kitu kingine ambacho kitamfanya Messi astaafu vema na pensheni yake ni ukweli kwamba bado kampuni zinamuhitaji awepo katika michuano hii na hiyo ijayo ya mwakani. Adidas na wengineo wanamhitaji hata akiwa na umri wa miaka 38. Adidas wanamhitaji Messi kwa ajili ya kutengeneza pesa kwa sababu Ronaldo atakuwa na Nike.

Achana na kina Lamine Yamal, Kylian Mbappe, Bukayo Saka na wengjneo,  hawa kina Messi na Ronaldo bado ni ‘brand’ kubwa kuliko wengineo. Ukienda huko Instagram utajua ni namna gani Nike wanamhitaji Ronaldo na namna gani Adidas wanamhitaji Messi. Hapa ndipo ambapo Messi anazeeka vyema na pensheni yake vizuri baada ya kutimiza miaka 38 Jumanne.

Kuna wale wadhamini wa timu ya taifa ya Argentina. Hawawezi kukubali timu yao iende Marekani bila ya Messi. Na hapo Messi huwa ana hela yake kwa mujibu wa mkataba wake na Shirikisho la Soka la Argentina. Wachezaji wakubwa huwa wanaingia mikataba hii ndio maana Mbappe kuna wakati aligombana na Shirikisho la Soka la Ufaransa.

MES 05

Messi anastaafu na utamu wake. Ndani na nje ya uwanja. Hana deni lolote. Kwangu ni mchezaji bora  wa muda wote. Siwezi kubishana na zama lakini niliwatazama akina Pele na Maradona katika mikanda wakati huo. Naamini Messi anasimama juu yao. Uzuri ni kwamba anastaafu vizuri.

Tumesafiri naye kwa miaka mingi. Tangu miaka 13 mpaka sasa ana miaka 38 lakini naamini kwamba anastaafu vema kuliko wanasoka wengi mahiri walivyowahi kustaafu. Ana mataji na ameshinda kila kitu. Kwa sasa anacheza bonanza tu. Michuano hii kwake ni bonanza na hata kombe la dunia kwake mwakani itakuwa bonanza nyingine. Ana bahati.