SIO ZENGWE: Pre-Season ni kutapanya fedha au maandalizi?

TUNAFIKIA ukingoni mwa msimu ambao ni mwanzo wa kipindi cha usajili na maandalizi ya timu kwa ajili ya msimu ujao.

Hiki si kipindi kinachokuja ghafla, la hasha! Ni kipindi ambacho hujulikana hata kabla ya msimu uliopita kuanza, hivyo ni kipindi ambacho maandalizi ya kukifanikisha yanaweza kufanyika hata miezi 12 kabla.

Kwa klabu kubwa duniani, tayari mipango yote ilishakamilika kwa ajili ya kipindi hiki, na kile cha maandalizi ya msimu (pre-season). Na maandalizi hayo huhusu kila idara.

Kwa wale wachezaji ambao wanatakiwa kupewa mkono wa kwaheri, benchi la ufundi linakuwa limeshandaa orodha yao na kuiwasilisha kwa uongozi, wakiwemo wale ambao mikataba yao bado haijaisha na hivyo kuachana nao huhitaji mazungumzo na mipango ya kuwapeleka sehemu nyingine kwa mkopo kumalizia kipindi kilichobaki kwenye mkataba au kukubaliana kuachana.

Pia hapa ndipo kuna hekaheka za usajili. Kwa wenzetu, si kipindi cha kuanza kutafuta wachezaji wa kuwasajili, bali kukimbia kukamilisha usajili wa wachezaji ambao wamekuwa wakifuatiliwa kwa muda mrefu kwa ajili ya kuziba mapengo kwenye timu au kuongeza ushindani katika baadhi ya nafasi.

Na kwa sababu ya ubora wa mchezaji huyo, basi ushindani dhidi ya klabu nyingine kuwania saini yake huwa mkubwa. Lakini ushindani huu haumaanishi kwamba klabu hizo zimeanza ghafla kumuwania mchezaji kama huyo.

Maandalizi pia huhusisha mechi ambazo timu hutakiwa kucheza kwa malengo ya kibiashara, kujaribu wacheaji vijana wanaofuzu kutoka shule za soka za klabu hizo wanaotarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza.

Kwetu, hiki ni kipindi cha kuhaha kokote kule viongozi wanakosikia kuna mchezaji mzuri au anawaniwa na moja ya klabu za hapa nchini. Ni kipindi ambacho kimetafsiriwa kuwa cha ufisadi wa fedha za usajili kwa tuhuma kuwa wale wanaopewa dhamana ya kufuatilia wachezaji, hutafuta wale wa bei rahisi na kudai wametumia fedha nyingi, huku wakijikatia sehemu ya hizo fedha walizozitoa.

Siamini sana katika hilo kutokana na jinsi mifumo inavyoboreshwa katika klabu zetu. Lakini nachoamini ni kutokuwa na maandalizi ya kutosha ya kufuatilia kwa muda mrefu wachezaji watakaofaa kwenye timu.

Matokeo yake huwa ni kutopata wachezaji sahihi na hivyo kuonekana kama wamedanganya kwa ajili ya kujipatia chochote. Lakini hilo linaweza kuwepo kwa kiwango kidogo.

Zipo klabu ambazo hutumia kipindi hiki kusubiri makombo tu. Yaani kusubiri Yanga, Simba na Azam zitaacha wachezaji gani ai zinataka kuwatoa kwa mkopo wachezaji fulani ili ziwadake kirahisi.

Hata ile Mtibwa Sugar ambayo ilikuwa na utamaduni wote wa klabu ndogo za barani Ulaya, sasa imebadilika. Badala ya kuwa kiwanda cha kuzalisha nyota vijana na kuwatambulisha katika jukwaa kubwa, imeingia katika mtindo wa kusubiri makombo.

Katika kipindi hiki ambacho kanuni za ligi zinaruhusu wachezaji 12 wa kigeni kusajiliwa huku 11 wakiruhusiwa kuanza, ni vigumu kuwa na timu bora ya taifa kama hata viwanda vya kuzalisha nyota wazawa vinaanza kubadili sera zake za kukuza vijana.

Wengi watakwambia eti mahitaji ya Ligi Kuu ndivyo yanavyotaka. Kweli? Kwa hiyo hakuna haja ya kukuza vijana wetu. Hatuoni ufahari kwa vijana kama Dickson Job, Nickson Kibabage, Kibwana Shomari na Denis Nkane kuwa sehemu ya timu bora Ligi Kuu wakiwa ni mazao ya programu za vijana za klabu?

Na mechi hizo huchezwa kwa maeneo ya kimkakati kibiashara na si eti kutafuta timu kali kutoka mataifa mengine. Manchester United inaweza kucheza na Chelsea mechi ya maandalizi nchini Marekani. Huko timu zote hazitalazimika kutumia vikosi vya kwanza, isitoshe nyota wengine wanakuwa na mapumziko marefu zaidi iwapo wanakuwa kwenye majukumu ya kitaifa ya nchi zao.

Kwanini Marekani? Ni kwa sababu za kibiashara. Soko la Marekani kisoka bado ni dogo wakati idadi ya watu ni kubwa na hivyo kunahitajika sana kuitangaza soka Marekani au China au sehemu nyingine zenye fursa kwa ajili ya kupata mashabiki na kupoanua wigo wa soka.

Hapa, timu zetu eti utasikia zinaenda Uturuki, au Morocco au Dubai wakati jazina mkakati wowote wa kibiashara kwenye nchi hizo zaidi ya kutapanya fedha. Hakuna soko ambalo Simba, Yanga, Azam au labda Singida United imelilenga Morocco, Uturuki au Dubai. Kwa hiyo inakuwa ni kupoteza muda na fedha.

Kocha wa Simba alilalamika baada ya timu kupoteza mechi mbili akisema kuwa tangu afike, imekuwa ni mechi tu na hakuwa amepata muda wa kutosha kuiandaa timu. Mechi hizo ni zile za mashindano na za kirafiki dhidi ya timu ya Russia.

Mwaka juzi, Yanga ilienda Morocco kimafungu na kurudi kimafungu. Huko walikutana na janga la Covid-19 lililowavuruga na kusababisha timu ipoteza kipindi muhimu cha pre-season ambacho huanza na mazoezi ya kurudisha miili katika utimamu na kuishia kwa kuanza kucheza mechi zisizo ngumu kabla ya msimu kufunguliwa.

Cha ajabu, kila ambacho hufanywa na klabu zetu kubwa hutafsiriwa vizuri sana na vyombo vyetu vya habari. Unaweza kusikia eti mchambuzi au mwandishi anamsifu kiongozi wa klabu fulani kutokana na timu kwenda kwa mfano Ufaransa kwa ajili ya maandalizi, akisema hilo linawezekana kwa sababu ya uwekezaji tu. Lakini haangalizi faida na umuhimu kimpira na kibiashara wa kuipeleka timu Ufaransa kwa wiki mbili.

Kwa hiyo mara nyingi, viongozi wa klabu huona ufahari kupeleka timu nje ya nchi badala ya kuangalia faida za kimpira na kibiashara. Kwa mfano, ingekuwa busara kwa Yanga kwenda kucheza mechi DRC kutangaza zaidi jina lake kwa kutumia nyota kutoka nchi hiyo na hivyo kutengeneza soko kubwa zaidi la bidhaa zake.

Hali kadhalika Simba ambayo kwa kipindi cha miaka mine imejitangaza sana barani Afrika, ilitakiwa iwe imechungulia wapi panahitaji kuongeza nguvu ili kukuza jina lake na hivyo kukuza soko.

Bila kufanya hivyo itakuwa ni kutapanya fedha na kusubiri chawa wasifu halafu mwishoni mwa siku ni kutofaidika na kipindi muhimu cha usajili na maandalizi ya msimu mpya.

Tunahitaji akili mpya katika matumizi ya kipindi cha usajili na maandalizi kwa ajili ya msimu ujao.