SIO ZENGWE: Kitenge, Kamwe, Priva watoa somo kwa waandishi

SIO ZENGWE: Kitenge, Kamwe, Priva watoa somo kwa waandishi

MMWAMUZI msaidizi wa Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2006, Ole Hermann Borgan aliyekuwa anajiandaa kwenda Paris kuchezesha mechi baina ya Barcelona na Arsenal, alichukuliwa picha na baadaye kuchapishwa katika gazeti la Drammens Tidende la Norway na kuzua tafrani. Alivaa jezi ya Barcelona.

Alishangaza watu kupiga picha akiwa amevaa jezi ya moja ya timu ambazo angehusika kuchezesha siku inayofuata.

Refa mkongwe wa Norway, Rune Pedersen aliliambia gazeti lililochapisha picha hiyo kuwa “ni sheria ambayo haijaandikwa kuwa waamuzi hawatakiwi wafanye chochote ambacho kinaweza kusababisha kuibuka shaka dhidi yao la kuegemea upande mmoja”.

“Picha hii inaweza kutumiwa kabla ya mechi na hata baada ya mechi kama kutakuwa na uamuzi wowote wa ajabu,” alisema kiongozi huyo na kushauri Chama cha Soka Ulaya (Uefa) kumbadilisha.

Mwamuzi huyo alibadilishwa mara moja na nafasi yake kupewa mwamuzi mwingine wa Norway.

Imekuwa ni kawaida yetu kutetea vitu vinavyoonekana kuwa ni vibaya kwa kuwa tu; “hakuna sheria” inayokataza. Mantiki inaweza kuwepo, lakini ukakuta watu wameshupalia udhaifu wa sheria.

Wiki iliyopita tulishuhudia tukio kama hilo ambalo linaweza kutetewa kwa kutokuwa na sheria au kanuni inayozuia. Waandishi watatu walihusika katika matukio mawili yaliyoihusu Yanga na baadaye matendo yao ya nyuma yakaibuka kuwasakama.

Mtangazaji wa Efm, Maulid Kitenge alikabidhiwa kadi ya uanachama wa Yanga katika mkutano na waandishi wa habari. Hilo halikuzungumziwa sana kwa kuwa lilionekana la kawaida machoni pa wengi.

Baadaye jioni, Ali Kamwe na Privaldinho walitangazwa kuajiriwa katika nafasi za mawasiliano za klabu hiyo, ambayo ajira za chini zinalazimisha waombaji wawe ni wanachama wa Yanga.

Si dhambi na wala si kosa la jinai kwa waandishi na watangazaji kuwa wanachama wa klabu au chama chochote cha siasa, lakini kimaadili kutangazwa au kujitangaza hadharani husababisha kuibuka kwa shaka kwa wasomaji magazeti, watazamaji wa televisheni au wasikilizaji wa redio, na siku hizi wafuatiliaji wa habari mitandaoni.

Lakini matendo yao ya nyuma ndiyo yameibuka hoja.

Kwa kitenge suala liko wazi kwamba hata kama anaipenda Yanga vipi, kimaadili haikuwa sawa kukabidhiwa kadi hadharani tena katika hafla rasmi. Ni vigumu kukubalika kesho iwapo atazungumzia Simba vibaya hata kama kweli imekosea.

Kamwe alifanya kazi kubwa msimu uliopita kuchangisha fedha kwa ajili ya kumzawadia mshambuliaji ambaye angeibuka na mabao mengi kuliko wengine. Alijitetea kuwa alianza kampeni hiyo hata kabla ya George Mpole kupambana vikali na Fiston Mayele ambaye ni Mcongo.

Haijulikani ni kwa nini haikuwa kipa bora mzawa, kiungo bora mzawa au beki bora mzawa! Na haijulikani iliishia wapi, lakini baadhi ya waandishi wakongwe walijaribu kumueleza ubaya wa kampeni yake, hasa kama mwandishi na mchambuzi; ingekuwa vigumu kwake kumkosoa Mayele, hata kama anakosea.

Leo, Kamwe ana kazi kubwa ya kuonyesha kuwa Mayele ndiye bora hata kama haibuki mfungaji bora. Na kuna mbinu nyingi za kumgeuza Mayele kuwa mfungaji bora hata kama atazidiwa kwa idadi ya mabao na wazawa. Kazi yake haikumruhusu afanye mambo hayo.

Privaldinho alikuwa na kazi kubwa ya kutafuta kiungo bora mwanzoni mwa msimu. Alidiriki hata kupiga picha na Clatous Chama na kuandika chini yake kuwa “huyu ndiye kiungo bora kwangu”. Hakukuwa na sababu ya kupiga naye picha na kuiweka Instagram kuonyesha watu msimamo wake katika mjadala ambao haukuwa wa maana wa kutafuta nani bora kati ya Chama na Aziz Ki. Kalamu na hoja zake kwenye kipindi zingetosha kuonyesha kuwa Chama ni bora, hivyo kuipa thamani kazi yake. Kutoka nje ya kipindi na kuingia mitandaoni, kuchapisha picha uliyopiga na Chama kunaonyesha nguvu ya chombo chako cha habari haijatosha kuonyesha ubora wa mchezaji unayemuamini.

Na katika matukio ambayo hayazuiwi na sheria wala kanuni, ni zile tabia za waandishi kujivalia jezi za klabu za ndani na nje ya nchi bila ya kujua kufanya hivyo kunamaanisha nini kikazi. Picha za Privadinho akiwa amevalia jezi za Simba, zilisambaa mara baada ya kutangazwa kuwa muajiriwa wa Yanga kitengo cha mtandao.

Ametetewa kuwa alikuwa akivalia hata jezi za Yanga kwa kuwa alikuwa akitangaza duka la vifaa vya michezo. Ningeelewa kama alivalia jukwaani kama model katika hafla maalum na kwamba anafanya kwa malipo na si kuzunguka nazo mitaani.

Kwa kampuni za habari zilizojengwa vizuri, zina sera inayozuia waajiriwa kuvaa nguo za rangi au nembo zinazoonyesha mahaba kwa klabu au chama cha siasa kwa kuwa kufanya hivyo hupunguza kuaminika kwa kampuni hizo katika kutenda haki kwa pande zote.

Privadinho, Kitenge na Kamwe ni mifano tu ya waandishi ambao wamekuwa wakifanya mambo kama hayo, hasa uvaaji wa jezi za klabu na kujitambulisha mahaba yao, bila ya kujiuliza mara mbili kwamba vitendo hivyo vinamaanisha nini kwa taaluma. Ni dhahiri kwamba watatu hao si waandishi wa kwanza kushabikia au kuwa wanachama wa moja ya klabu za hapa nchini na nje. Wapo ambao walifikia kuteuliwa kushika nafasi za uongozi, lakini hawakujitangaza hadharani kwanza, ukiachilia Masoud ambaye alikuwa mtangazaji Radio Tanzania na kiongozi Yanga au Asha Muhaji aliyekuwa ofisa habari Simba. Hakuna kosa linalohalalisha kosa jingine, bali kosa huwa somo.

Hata kama sheria, kanuni na sera za kampuni zetu hazikatazi kuonyesha mahaba kwa klabu au chama, lakini kwa kuwa kazi ya uandishi inataka kuhudumia wateja wote kwa haki bila ya hofu wala upendeleo, ni muhimu kuwa makini katika matendo yetu.

Ni kweli kwamba gazeti la The Sun lilitangaza kumuunga mkono Tony Blair kabla ya uchaguzi. Lakini ni tukio la kipekee katika tasnia na ambalo ni vigumu kurudiwa.

Kuonyesha wazi kuwa uko upande fulani ni kufanya walaji wa kazi za habari kuanza kutia shaka katika kile wanachopewa kama hakijatengenezwa kwa hofu au upendeleo. Ni dhahiri kuwa na mahaba ya wazi kunaweza kukujengea hofu ya kuripoti kibaya kwa unachopenda au kuripoti kizuri kwa usichopenda na ukiwa jasiri, basi kutakuwa na shaka kwa wale unaowapa ripoti.

Hata kama jamii yetu inaona mambo haya ni ya kawaida, ni muhimu tujenge imani na kuaminika kwa wale tunaowahudumia.