Prime
SIO ZENGWE: Kama hatuwezi kusimamia kanuni hii, tuige Wamisri

Muktasari:
- Lakini kiburi kilitajka kuanza kujitokeza tena wakati huo Ligi Kuu ndio kwanza ilikuwa imewekwa chini ya Kamati ya Mashindano ambayo ilitakiwa iongoze hadi kufanikisha uchaguzi ambao uliunda Bodi ya Ligi (TPLB).
Mwaka 2013 kulitokea mzozo wa kukiuka kanuni ambayo ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya elfu mbili kukomesha mtindo uliokuwa ukikomaa wa timu kusababisha mechi kuvunjika au kugomea mchezo na hivyo kupoteza pointi tatu.
Kanuni hiyo ilisaidia sana kuzizuia klabu kugomea mchezo au kusababisha mchezo kuvunjika na hivyo zikawa zinafanya kila jitihada kuhakikisha mechi zao zinaisha au kama zina madai zinafanya jitihada kuhakikisha yanashughulikiwa nje ya uwanja na michezo kuendelea kama ilivyokuwa imepangwa.
Lakini kiburi kilitajka kuanza kujitokeza tena wakati huo Ligi Kuu ndio kwanza ilikuwa imewekwa chini ya Kamati ya Mashindano ambayo ilitakiwa iongoze hadi kufanikisha uchaguzi ambao uliunda Bodi ya Ligi (TPLB).
Mwaka huo, Mtibwa Sugar iligomea penati ya Azam katika mechi ya mzunguko wa pili. Kutokana na kanuni hiyo, ilibidi Mtibwa Sugar ishushwe daraja.

Lakini suala hilo lilisumbua sana wajumbe wa Kamati ya Mashindano maana kuishusha Mtibwa Sugar daraja wakati ligi ikielekea ukingoni, ingemaanisha kuwa matokeo ya mechi zake zote yaondolewe. Hivyo ni timu ambazo zilifungwa na Mtibwa tu ndizo zingefurahia au zisingetetereshwa na uamuzi huo.
Lakini kazi kubwa ilikuwa kwa timu ambazo zilipata ushindi dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara.
Na hasa timu ambazo ama zilikuwa bado zinaona zinaweza kutwaa ubingwa ama zinaweza kuepuka kushuka daraja na hivyo kupoteza pointi sita au nne au tatu, kungeathiri nafasi yao kwenye msimamo wa ligi.
Na mojawapo ya klabu hizo ilikuwa ni Simba ambayo iliishinda Mtibwa katika mechi zote mbili na hivyo ingepoteza pointi sita, hali ambayo ingeipa mwanya Azam kutwaa ubingwa. Wajumbe walibishana na baadaye kufikia muafaka kuwa mechi hiyo irudiwe. Yaani uamuzi ulikuwa wa kuinyang’anya Azam ubingwa iliostahili.

Yamekuwepo matukio mengi ya aina hiyo na sababu hutolewa za ajabuajabu kuhalalisha uovu huo huku timu zinazoonekana kuwa ni ndogo zikiathirika na maamuzi hayo, ambayo yanaelezewa kuw aya kutumia busara badala ya kutumia busara zilizowekwa kwenye kanuni.
Tukirudi kwenye matukio ya hivi karibuni, miaka mitatu iliyopita TPLB ilisogeza muda wa mechi kutoka saa 11:00 jioni hadi saa 1:00 jioni bila ya maelezo yoyote ya maana na bila kufuata kanuni ambayo inataka mabadiliko hayo yafanyika kabla ya saa 24 ya muda wa awali wa kuanza mchezo.
Yanga ilienda uwanjani muda huo, ikisema kuwa mabadiliko hayakufuata kanuni lakini Simba ikaenda uwanjani saa 1:00 lakini muda mfupi kabla ya mchezo kuanza TPLB ikatangaza kuahirisha mechi hiyo.

Ni busara tu zilitumika kuishauri Yanga ikubali kucheza mechi ambayo ilipangwa kufanyika siku nyingine na iliwezekana.
Kwa maelezo ya mwenyekiti wa TPLB, Steven Mguto, hali ilikuwa mbaya eti kwa sababu Simba iliwasili muda ambao ulibadilishwa na waamuzi walikuwepo uwanjani, hivyo wangeamua kufuata kanuni (ambazo hawakuziheshimu wakati wanabadili muda), Yanga ingeshushwa daraja.
Kwa kudhani kuwa TPLB ilifanya uamuzi wa busara na wa kishujaa, Mguto anahoji “we fikiria Simba au Yanga ishushwe daraja itakuwaje?” Yaani haiwezekani. Na kama haiwezekani kwa kanuni, basi haitawezekana hata kwa matokeo ya uwanjani.

Msimu uliopita, Simba iliomba mechi yake na Kagera Sugar iliyokuwa ifanyike Uwanja wa Kaitaba iahirishwe kwa hoja kwamba baadhi ya wachezaji wake waliugua mafua. Bila ya kutafuta ushahidi wowote wa hoja hiyo, TPLB ikatangaza asubuhi kuwa mechi itafanyika kama ilivyiopangwa.
Lakini wakati Kagera Sugar wanajiandaa kwa mchezo huo. TPLB ikatangaza saa mbili kabla ya muda wa mchezo huo kuanza, kuwa mchezo huo umeahirishwa. Kagera Sugar wakajikuta uwanjani peke yao.
Sijui kama tukio hilo liliwapa fundisho la kurekebisha kanuni ili inapotokea timu ina wachezaji waliougua, hasa wakati kunapotokea magonjwa ya mlipuko kama ilivyokuwa Covid, nini kifanyike kuhalalisha kuahirisha mechi. Wenzetu wanataka wachezaji waliougua wawe kuanzia kumi, akiwemo kipa. Idadi hiyo hutoka kwenye orodha ya kikosi cha wachezaji 25 ambacho timu hutakiwa kukitangaza siku tatu kabla ya mchezo.
Na tukio la mwezi uliopita ndio limeibua mzozo zaidi na kuipa onyo TPLB kuwa watu wanafuatilia kwa makini maamuzi yao yote na kuyahusisha na upendeleo ambao hutokana na hofu ya timu kipenzi kushuka au njama za kuiwezesha timu kipenzi kutwaa ubingwa.

Katika matukio yote hapo juu kinaonekana kitu kimoja. Kushindwa kusimamia hiyo kanuni iliyowekwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 kukomesha mtindo wa kugomea mechi au kusababisha mechi kuvunjika.
Ushahidi wote na kauli za Mguto zinaonyesha kuwa kanuni hiyo haiwezi kufuatwa kwa klabu kubwa au hata klabu ndogo kwa kuwa hofu ya timu zilizo katika kiwango kizuri katika mbio za ubingwa zinaweza kuathiriwa sana iwapo zitapoteza pointi zilizopata kwa timu iliyo hatarini kushushwa daraja kikanuni.
Wenzetu wa Misri hilo haliwasumbui. Tuhuma za uamuzi wa upendeleo umesababisha kila mara klabu za Al Ahly, Zamalek n ahata El Masry kuingia kwenye mzozo. Na mara kadhaa Al Ahly imekuwa ikipendekeza mechi dhidi ya vigogo hao zichezeshwe na waamuzi kutoka nje.
Lakini wasimamizi wa Ligi Kuu ya Misri wamekuwa wakisita kutekeleza pendekezo hilo. Kwa hiyo imekuwa kawaida kwa mechi baina yao kutochezwa kutokana na timu moja kugomea kwa sababu tofauti.
Safari hii Al Ahly iligomea mechi dhidi ya Zamalek kwa sababu hizohizo na wapinzani wao walienda uwanjani na taratibu zikafuatwa kuipa ushindi Zamalek. Sababu huwa tofauti kwa El Masry, Ahly na Ismaily.
Lakini inaonekana kama suala hilo halizitingishi klabu hizo kwa sababu zinapoamua kugomea mechi zinakuwa zinajua hali yao kwenye msimamo wa ligi sio mbaya na hivyo zinaweza kutwaa ubingwa hata zikipoteza mchezo huo bikla ya kuingia uwanjani.
Kanuni zao ni kupoteza mchezo na timu iliyoenda uwanjani kupewa ushindi wa pointi tatu na magoli. Kanuni hiyo imeundwa kutokana na utamaduni wa watu wan chi hiyo ya mkaskazini mwa Afrika ambako hata timu zao za taifa huweza kufanya vituko vinavyosababisha mechi isichezwe.
Kama nilivyosema awali, kama hatuwezi kukuna vichwa kutafuta kanuni itakayoadhibu kwa ufanisi timu inayogomea mchezo, basi tuige hiyo kanuni ya Misri ambayo inaipa ushindi timu iliyoenda uwanja.
Lakini ni muhimu kanuni hiyo ikajengewa mazingira ya udhibiti ili anayesababisha mzozo unaogomewa na klabu, asilewe madaraka na kuanza kufanya maamuzi ya hovyo kwa lengo la kuinufaisha timu moja na hivyo bingwa kupatikana kikanuni na si uwanjani.