AHMED FARAS: Mkali wa mabao aliyeweka heshima Morocco

Muktasari:
- Lakini hali ni tofauti kwa Morocco ambako utawaona wanamichezo waliowika wakati wa ujana wao wanatambulika na kuwekwa karibu na wanamichezo chipukizi na ndio washauri wa wanamichezo wa nchi hiyo katika michezo ya kimataifa.
KATIKA nchi nyingi za Afrika, wanamichezo waliozijengea heshima nchi zao husahaulika na kuwa kama hawapo mara tu wanapostaafu. Ni kawaida kuwakuta baadhi yao wakiwa katika hali ngumu za maisha.
Lakini hali ni tofauti kwa Morocco ambako utawaona wanamichezo waliowika wakati wa ujana wao wanatambulika na kuwekwa karibu na wanamichezo chipukizi na ndio washauri wa wanamichezo wa nchi hiyo katika michezo ya kimataifa.
Kwa mfano, ni kawaida kuona wachezaji wanne wa zamani wa nchi hiyo wakitembelea kambi na kufuatana na timu ya taifa au klabu zinapotoka nje ya nchi kwa mechi za Shirikisho la Kandanda la Afrika.
Vilevile, Morocco mara kwa mara huwa na matamasha ya kuwakumbuka wanamichezo mahiri waliostaafu na mara nyingine ndio huwa wageni wa heshima katika mechi za ligi ya nchi hiyo.

Hata timu ya RS Berkane iliyokuja nchini kucheza dhidi ya Simba katika mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF, huenda ilikuwa na wachezaji wastaafu wa nchi hiyo.
Miongoni mwa wachezaji kandanda wastaafu wanaoheshimika sana Morocco ni Ahmed Faras ambaye aliwika alipokuwa akiichezea Barcelona ya Hispania, ambayo mara mbili ilifanya ziara ya Morocco katika miaka ya hvi karibuni kama kuonyesha heshima kwa Faras na wenzake waliowahi kuitumikia klabu hiyo.
Faras alikuwamo katika kikosi cha Morocco katika fainali za Kombe la Dunia kule Mexico ambako Morocco iliminywa na muamuzi na kufungwa 2-1 na Ujerumani Magharibi.
Mwamba huyu wa Morocco wa miaka ya 1960 na 1970 aliyesifika kama mmoja wa wachezaji bora wa Afrika wakati ule, ambaye sasa ana miaka 79, amekuwa hakosekani katika misafara ya timu za Morocco na klabu za nchi hiyo zinapokwenda kucheza nje ya nchi.

Kwa miaka mitano, kutoka 1972 hadi 1976, alisifika kama mshambuliaji makini na miongoni mwa wachezaji walioteuliwa mara nne kugombea tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika. Mara mbili alitokea wa pili, mara moja wa tatu na hatimaye aliibuka mshindi wa mwaka 1976.
Faras aling'ara kwa mchezo maridadi na wa kuvutia na zaidi kwa alivyokuwa hakati tamaa hadi muamuzi alipopuliza filimbi ya mwisho. Siku moja Morocco ikiwa imefungwa 1-0 alimuendea muamuzi na kumuuliza zimebakia dakika ngapi. Alipoambiwa nne alisema: "Hizo zinatosha sana kunisaidia kuleta furaha kwa nchi yangu".
Baada ya dakika tatu Faras alisawazisha na katika dakika ya mwisho ya majeruhi alibandika goli la ushindi.
Faras anatambulika kama mchezaji aliyeiwezesha Morocco kuiwakilisha vizuri Afrika katika fainali za Kombe la Dunia za Mexico 1970.
Hii ilikuwa miaka 36 baada ya Misri kuwa nchi ya kwanza na pekee kutoka Afrika kucheza fainali hizo zilizofanyika Italia 1934 ambapo utawala wa dikteta Alberto Mussolini uliwahonga na kuwatisha waamuzi na kubeba kombe.

Morocco ilicheza vizuri ilipopambana na Ujerumani Magharibi, lakini bahati haikuwa yao na mizengwe ndio iliyosababisha ifungwe.
Morocco iliuona mlango wa Ujerumani kupitia Jarir Houmane aliyefunga bao katika dakika ya 21 baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Faras.
Ujerumani ilisawazisha kupitia Uwe Seeler katika dakika ya 56 na Gerd Muller aliipatia Ujerumani ushindi wa 2-1 katika dakika ya 80, bao lililokuwa na shaka kuwa ni la kuotea.
Baada ya mchezo Faras, huku akilia, alisema: "Siamini hata kidogo. Tuliwazidi Wajerumani kwa kila hali na labda kutojiamini kwa baadhi yetu na siri iliyojificha ya muamuzi ndio iliyofanya tufungwe".
Alizitaka nchi za Afrika zisitishike na sifa zinazopewa nchi za Ulaya kwa soka.
Katika mchezo wa pili wa kundi lao Morocco ilifungwa 3-0 na Peru na ilitoka sare ya 1-1 katika mchezo wa mwisho dhidi ya Bulgaria.

Ahmed Faras alizaliwa Morocco 1946 na tokea alipoanza kucheza daraja la juu alikuwa muda wote mpaka alipostaafu na klabu ya karibu na nyumbani alipozaliwa, Chabab Mohammédia. Aliichezea Morocco kwa miaka 14, kutoka 1965 hadi 1979 na kuwa nahodha wa kikosi hicho kwa miaka minane mfululizo tokea 1971.
Baada ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za 1970, Faras alikuwamo katika kikosi cha Morocco cha michezo ya Olimpiki iliyofanyika Munich, Ujerumani, 1972. Baadaye aliingoza Morocco katika fainali za 1976 za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika Ethiopia kwa mtindo wa ligi na kuiwezesha kubeba kombe, Guinea ikishika nafasi ya pili.
Morocco ilitoka sare ya 2-2 na Sudan, ikaifunga Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) 1-0, na katika mchezo wa mwisho wa kundi lake iliifunga Nigeria 3-1.
Kwa Faras kuifunga Zaire kulimpa furaha kutokana na Zaire kuifunga mwaka 1973 na kuwapokonya tiketi ya kuiwakilisha Afrika katika fainali za Kombe la Dunia za 1974.
Faras alisema: "Waliichukua tiketi ya fainali za Kombe la Dunia mikononi mwetu na sisi tunataka kulichukua Kombe la Afrika mikononi mwao. Kulipiza kisasi katika michezo sio jambo baya".

Baada ya mchezo ule Faras alikuwa hakamatiki hadi walipobeba kombe. Kwa ujumla Faras aliifungia Morocco mabao 42 na klabu yake kuwa mabingwa wa Morocco. Alistaafu 1982 baada ya kuichezea Morocco kwa miaka 14 na klabu yake kwa miaka 17.
Katika mwaka 2006 alichaguliwa na Shirikisho la Kandanda la Afrika kuwa mmoja wa wachezaji 200 bora wa Afrika katika nusu karne iliyopita.
Viongozi na mashabiki wengi wa soka walimtaka Faras alipostaafu kuchukua mafunzo ya kufundisha mpira.
Lakini alikataa na kusema: "Nimekuwa nahodha wa timu kwa miaka minane. Ninajua mzigo mzito aliokuwa nao kocha wakati nikiwa mchezaji. Sina haja ya kutafuta balaa".
Alisema kama ni kuwa mwalimu angeifanya kazi hiyo kwa kuwafunza watoto wake adabu njema na kucheza kandanda, lakini sio kuwa kocha wa klabu au timu ya taifa.
Mpaka sasa anaendelea kuwa mmoja wa washauri wa timu ya taifa na mipango ya kuendeleza soka ya Shirikisho la Kandanda la Morocco.
Yeye na wachezaji mashuhuri wengi wa Morocco, kama Aziz Bouderbala na Mohamed Timouni, walitumika kuifanyia kampeni Morocco kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 ambazo hatimaye iliamuliwa kufanyika Afrika Kusini.
Mara nyingi huandamana na wachezaji wa zamani pale Morocco inapocheza nje ya nchi na alikuwapo Cairo katika fainali za AFCON.
Miaka michache iliyopita, Shirikisho la Kandanda la Afrika lilimchagua kuwa mmoja wa wachezaji 10-Bora wa Afrika kwa karne iliyopita.
Faras alikuwa wa 9 akiwa na pointi 35. Aliyeongoza orodha alikuwa George Weah wa Liberia (95) na kufuatiwa na Roger Milla wa Cameroon (77), Abedi Pele wa Ghana (72) na Lakhdar Belloumi wa Algeria (56).
Mchango wa Faras kwa klabu ya Chabab Mohammedia, Morocco na Afrika, hasa Morocco ilipocheza na Ujerumani kule Mexico hautasahaulika.