SIO ZENGWE: Hamasa ya Stars imepotea na thamani yake

Muktasari:
- Kabla ya hapo, timu ya taifa haikuwa ikifuatiliwa kwa karibu sana na kuna wakati wananchi walilazimika kutoa msaada wa hadi jezi, hivyo rangi zake kuendana na utashi wa mtoa msaada. Haikuwa ajabu kwa kipa mmoja wa timu ya taifa kuvalia jezi yenye nembo ya timu ya taifa ya England akiwa langoni mwa Taifa Stars jijini Mwanza.
WAKATI Mbrazili Marcio Maximo akiwa kocha wa Tanzania, kulikuwa na hamasa kubwa kutoka kwa wananchi kwa timu yao ya taifa ya soka baada ya miaka mingi ya kutothaminiwa.
Kabla ya hapo, timu ya taifa haikuwa ikifuatiliwa kwa karibu sana na kuna wakati wananchi walilazimika kutoa msaada wa hadi jezi, hivyo rangi zake kuendana na utashi wa mtoa msaada. Haikuwa ajabu kwa kipa mmoja wa timu ya taifa kuvalia jezi yenye nembo ya timu ya taifa ya England akiwa langoni mwa Taifa Stars jijini Mwanza.
Lakini ujio wa Maximo na mambo mengine mengi yaliyoambatana nayo, kama uongozi wa Rais Jakaya Kikwete kama shabiki na raia namba moja wa Tanzania, uongozi wa Shirikisho la Soka (TFF), upatikanaji wa mechi kubwa za kirafiki na kupatikana kwa udhamini mnono, kulibadilisha mtazamo wa mashabiki kwa timu yao ya taifa.
Watu, si tu wakaanza kujazana uwanjani, bali pia kununua jezi za timu ya taifa na kuzivaa kila wakati timu hiyo ilipokuwa na mechi na hivyo mara kadhaa uwanja kujazana watu kuiona timu yao pendwa.

Pamoja na mambo hayo mengine yaliyochangia hamasa kupanda, Maximo mwenyewe aliibeba Taifa Stars mabegani mwake, akichukua jukumu la kuhamasisha mashabiki kila wakati alipopata muda wa kuizungumzia timu yake kuhusu mchezo uliokuwa unatarajiwa kufanyika.
“Nataka uwanja wote uwe wa bluu,” alisema Maximo kila mara alipohamasisha mashabiki kufika viwanjani kuishangilia timu yao.
Hakuishia kuzungumza na waandishi wa habari tu, kila mara kabla na baada ya mazoezi alikubali kusimama na kuzungumza na mashabiki, japo kwa maneno ya kuokotaokota huku akijaribu kutafuta mtu anayejua Kiingereza amtafsirie aweze kuelewana na aliyekuwa akiongea naye.
Haikuwa ajabu kumuona Maximo akijaribu kumuita mtu ambaye hamfahamu jina lakini ameona amevalia barakashia kwa kumuita “salama aleikhum” ili angalau ageuke na kusalimiana naye.

Kwa kufanya hivyo, mashabiki wakawa sehemu ya timu ya Taifa na ni sehemu ya Mbrazili huyo. Taifa Stars ikawa na mvuto na mechi zake zikajaa. Mashabiki wakaifuatilia hata ilipokwenda kucheza mechi nje ya nchi, ingawa walikuwa ni wachache—ila hawakuwa wale wanaolipiwa na TFF kama ilivyo kwa wengi hivi sasa.
Maximo hakuwa na matokeo mazuri sana wala mabaya sana uwanjani, lakini alionekana anaijenga timu ambayo ingekuwa tishio baadaye kwa kuwa watu waliona maendeleo. Matokeo ya mechi ngumu za mashindano na kirafiki dhidi ya timu kama Senegal, Afrika Kusini, Cameroon, Ivory Coast na Brazil hayakuwa mazuri lakini hayakuchukiwa wala kubezwa kwa kuwa timu ilionekana.
Jumamosi nilikuwa nazungumza na baadhi ya mashabiki wa soka na mmoja akauliza: “Hivi Stars itacheza lini?” Nikasikitika sana kwamba hajui timu ya taifa lake itacheza lini pamoja na taarifa zote zilizochapishwa na vyombo vya habari.

Lakini nikagundua kuwa hata kuwe na taarifa zinazojaza vyombo vyote vya habari, kama hakuna hamu kwa timu, watu kama hao wa kujiuliza kama Stars inacheza au siku ambayo itacheza, watakuwepo wengi tu.
Hapa si kutimiza wajibu wa kutoa taarifa kuhusu timu, bali kuwepo na hamasa kwa Taifa Stars, kitu ambacho kinajengwa kwa ushirikiano wa wadau wote, yaani uongozi wa serikali, uongozi wa shirikisho, benchi la ufundi na sekretarieti ya shirikisho.
Rais Samia Suluhu Hassan anaweka hamasa yake kwa kuahidi fedha za motisha kwa wachezaji na hata kununua tiketi kwa ajili ya mashabiki, lakini pengine kuna udhaifu katika shirikisho, benchi la ufundi na sekretarieti ambayo ndio iko na timu kila inapokuwa kambini.
Hatuoni mechi za kirafiki kubwa ambazo zingevuta mashabiki kwenda uwanjani kuona jinsi wachezaji wetu wanavyopambana na wachezaji nyota duniani kama ilivyokuwa wakati Stars ilipocheza na Afrika Kusini, Cameroon na Brazil. Hata mechi za mashindano hazijawa dhidi ya wale vigogo kama Nigeria, Senegal, Ghana, Morocco (hawa tumekutana nao kidogo) na Afrika Kusini.

Mechi za mashindano zimekuwa za kawaida sana dhidi ya timu kama Guinea (labda kidogo) Algeria, Burundi, Congo DR, Zambia ambazo hazichangii kuongeza hamasa. Hata hivyo, hatuna mamlaka kuamua nani tupangiwe, lakini zile za kirafiki zinawezekana kabisa. Na si tu zitachangia kuongeza hamasa, bali zitakuwa kipimo kizuri kwa vijana wetu na nyenzo nzuri ya kuongeza ubora na hatimaye hamasa.
Hii ni kazi ambayo inatakiwa kufanywa na sekretarieti.
Suala la Rais Samia kujitolea kununua tiketi kwa ajili ya mashabiki, pia haliko chini ya mamlaka ya sekretarieti wala shirikisho, ni utashi wa mkuu wa nchi.
Lakini kwanini Rais anafikia uamuzi wa kununulia mashabiki tiketi. Pengine ni baada ya kuona hamasa hakuna na hivyo aweke mkono wake. Mara nyingine tiketi zikishatangazwa kuwa ni za bure, zinazuia watu wengine hata kwenda uwanjani kwa kuwa wanakuwa wanajua kuwa hali uwanjani haitakuwa nzuri kwa kuwa wengi wanapenda kuchangamkia vya bure. Maana yake ni nini? Shirikisho na sekretarieti hawana budi kutengeneza mkakati wa nini wanataka kifanyike katika mchango huo wa rais ili kuendeleza thamani ya Stars na kutowarudisha nyuma wale ambao wamezoea kwenda uwanjani kwa kujigharamia bila ya kusumbuka au kugombania tiketi zilizofadhiliwa.
Hata hamasa ya kutoa tiketi kwa kushindanisha mashabiki haifanyiki. Kazi ya sekretarieti imekuwa ni kutangaza kiingilio na muda wa mechi.

Hata uteuzi wa waandishi wanaofuatana na timu katika safari zake unafaa uangaliwe. Ukichukua wahariri, utajihakikishia habari kwenye kurasa au muda hewani, lakini si ripoti za kina ambazo zinatafutwa hadi kwenye vyumba vya kuvalia ambako si rahisi kwa wahariri kufika.
Benchi la ufundi pia lina mchango mkubwa katika kuongeza hamasa kwa mashabiki. Kwanza benchi ndilo linahitaji msaada mkubwa wa nguvu ya mashabiki, lakini pia ndilo linaloweza kutengeneza hiyo hamasa kwa kutoa taarifa nzuri kuhusu timu na kuomba huo msaada.
Kwa kocha ambaye anazungumza mambo ya jumla jumla kuhusu timu, na wala haonyeshi kwamba mashabiki ni sehemu ya timu, huyo atasubiriwa akosee ndipo akosolewe na si watu kuungana naye uwanjani kuisukuma timu ifanye vizuri.
Kocha Hemed Morocco haonekani kuwajibika kwa mashabiki kama ilivyokuwa kwa Maximo. Na humsikii akizungumzia mashabiki kuwa ndio tegemeo lake katika kusaidia ufundi wake ufanikiwe uwanjani.
Anazungumza kikawaida, kana kwamba ameambiwa ni lazima uzungumze na akimaliza, ndio imetoka.
Kwa hiyo, ili hamasa kwa timu yetu ya taifa irudi, hakuna budi kila mdau ashike nafasi yake ipasavyo na aongeze ubunifu ili Taifa Stars irejee kwenye thamani yake na watu wasiichukulie kuwa ni timu ya kawaida au yatima bali ni timu ambayo ina kila kitu kinachostahili kutafutwa kwa bei yoyote.
Ni muhimu hamasa ya Taifa Stars irejeshwe ili thamani yake pia irejee.