2025 ndani ya ngozi ya 2004

Muktasari:
- Hivi ndivyo ulivyo mwaka 2025...kwa nje unaonekana kama mwaka mwingine tu wa kawaida, lakini kwa ndani uko tofauti kabisa kwa upande wa michezo.
HUU ni sawa na ule mkasa wa chui ndani ya ngozi ya kondoo. Kwamba kwa nje anaonekana kondoo...mpole sana. Lakini kumbe kwa ndani ni chui...hatari sana.
Hivi ndivyo ulivyo mwaka 2025...kwa nje unaonekana kama mwaka mwingine tu wa kawaida, lakini kwa ndani uko tofauti kabisa kwa upande wa michezo.
Mwaka 2025 una matukio ya kipekee na ya kushangaza kama ilivyokuwa 2004 yaani mwaka wa maumivu kwa waliozoea furaha, na furaha kwa waliozoea maumivu.
Mwaka 2025 umekuwa wa ajabu sana katika michezo, kwani umeleta matukio mengi ya ajabu na kushangaza kwa wanyonge na kibonde kuwatoa kapa wababe na watemi.
HARRY KANE NA UKAME WA MIAKA 31
Kama kuna wachezaji ambao daraja lao lilistahili kupata taji miaka mingi iliyopita, lakini walikosa, basi kamba moja anaweza kuwa Harry Kane.
Nyota huyo mwenye uwezo wa kupata namba katika timu yoyote dunia ni, klabu au ya taifa, alikuwa hajawahi kushinda taji klabuni kwake Tottenham Hotspur.
Akahamia Bayern Munich msimu wa 2023/24, timu ambayo mataji ni rafiki yao...lakini katika msimu wake wa kwanza, akakosa.
Lakini Mungu si Athuman, mwaka huu, 2025, ameshinda taji lake la kwanza akiwa na miaka 31.
BOLOGNA NA UKAME WA MIAKA 51
Bologna ya Italia ilimaliza ukame wa miaka 51 baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya AC Milan katika fainali ya Kombe la Italia, sawa na Kombe la Shirikisho la CRDB hapa nyumbani Tanzania.
Bao la dakika ya 53 la Dan Assane Ndoye, raia wa Uswisi mwenye asili ya Senegal, lilitosha kuwafanya wainue makwapa kwa mara ya kwanza tangu 1974 walipotwaa taji hilo hilo.
NEWCASTLE UNITED NA MIAKA 70
Ushindi wa 2-1 katika fainali ya Kombe la Ligi (Carabao) dhidi ya Liverpool uliwafanya Newcastle United kumaliza ukame wa miaka 70 bila taji.
Mabao ya mapema ya Dan Burn na Alexander Isak yaliwatosha Newcastle kufanya biashara asubuhi, huku Liverpool wakifungua duka jioni wakati wenzao wanafanya mahesabu.
Hili lilikuwa taji la kwanza kwa Newcastle baada ya miaka 70. Mara ya mwisho kwao kushinda taji ilikuwa mwaka 1955 walipotwaa Kombe la FA.
GO AHEAD EAGLES NA MIAKA 92
Huko Uholanzi kuna timu inaitwa Go Ahead Eagles ambaye mwaka 2025 imemaliza ukame wa maka 92 bila taji baada ya kushinda Kombe la NVB Beker ambalo ni sawa na Kombe la Shirikisho la CRDB hapa nchini Tanzania.
Ushindi wa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 dhidi ya AZ Alkmaar, ulitengeneza historia ya ajabu kwa mashabiki wa timu hiyo.
Timu hizi zimeshinda mataji haya baada ya miaka mingi ya kuvunjika moyo ikiwemo kushuka madaraja...furaha pekee waliyokuwa wakiipata katika nyakati hizo ni kupanda daraja au kunusurika kushuka.
PALACE NA KIU CHA MIAKA 120
Crystal Palace ya England ilishinda Kombe la FA mbele ya Manchester City kwa bao 1-0 la dakika ya 16 lililofungwa na Eberechi Oluchi Eze, Mwingereza mwenye asili ya Nigeria.
Hata hivyo, ilibidi teknolojia iingilie kati kuinusuru Palace na adhabu ya kadi nyekundu kwa kipa wao Dean Henderson aliyeonekana kumfanyia madhambi ya kuzuia nafasi ya kufunga ya Erling Haaland.
Lakini VAR ikabaini kwamba haikuwa hivyo, ila ilistahili kuwa penalti...Omar Marmoush akapiga na Henderson akaiokoa.
Hili ni taji la kwanza kabisa kwa klabu hiyo yenye umri wa miaka 119, ikiwa ilianzishwa mwaka 1861.
ILIVYOKUWA MWAKA 2004
Kama ilivyo 2025, ndivyo ilivyokuwa mwaka 2004...vibonde wasiotarajiwa walifanya maajabu ambayo wengi wao kama sio wote, wameshindwa kurudia hadi sasa.
UGIRIKI NA EURO
Katika hali ya kushangaza, timu ya taifa ya Ugiriki ilishinda ubingwa wa mataifa ya Ulaya, Euro 2004, kwa kuwafunga wenyeji Ureno kwa bao 1-0.
Bao la dakika ya 57 la Angelos Charisteas aliyeunganisha kona ya Angelos Basinas, liliwapa Ugiriki taji lao la kwanza kama taifa, na pekee hadi sasa.
Kabla ya fainali hizi, Ugiriki ilikuwa imeshiriki mashindano hayo mara moja tu, mwaka 1980, na walitoka hatua ya makundi bila ushindi hata mmoja...wakiburuza mkia kwenye kundi lao.
TUNISIA NA AFCON
Wakiwa wenyeji wa mashindano, Tunisia ilishinda AFCON kwa kuifunga Morocco 2-1 katika mechi ya fainali. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Tunisia kushinda AFCON, na ndio pekee hadi sasa.
SAN MARINO NA USHINDI WA KWANZA
Aprili, 28, 2004 – timu ya taifa ya San Marino rilipata ushindi wao wa kwanza baada ya kuwafunga Liechtenstein 1–0.
Nchi hiyo ilipata uanachama wa FIFA mwaka 1990 na ndio wakacheza mechi yao ya kwanza rasmi dhidi ya Uswisi...lakini hawakuwahi kushinda hadi 2004.
Naaba ya hapo hawakushinda tena hadi 2024...miaka 20 baadaye, tena kwa kumfunga mpinzani yule yule, na kwa matokeo yale yale. Ama hakika mwaka 2025 umetukumbusha mwaka 2004.