Sio Luis Miquissone tu... Hata hawa kiboko ya Ahly

MASHABIKI wa Simba wanatembea vifua mbele kutokana na ushindi ilioupata timu yao dhidi ya Al Ahly jijini Dar es Salaam katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Huo ulikuwa ushindi wa tatu kwa Simba dhidi ya wababe hao wa soka Afrika, bao pekee lililowazamisha watetezi hao wa michuno hiyo ya Afrika likiwekwa kimiani na Luis Jose Miquissone katika dakika ya 31 ya mechi hiyo ya Kundi A.

Luis alifunga bao hilo lililoipa Simba pointi tatu kwa mguu wa kulia baada ya kuwazidi akili mabeki wa Ahly, lakini limekuwa ni la sita kwa Mafarao dhidi ya timu za Tanzania, kwani kabla ya hapo kuna nyota wengine watano waliowatungua.

Ebu wasome wakali hao waliowahi kuzigusa nyavu za Al Ahly katika mechi mbalimbali za kimataifa, japo timu zao zilienda kutaabika waliporudiana nao kwenye uwanja wao wa nyumbani jijini Cairo, Misri.

MEDDIE KAGERE

Mshambuliaji wa Simba ambaye msimu wa 2018-2019 aliifungia klabu yake bao pekee kwa shuti kali wakati Ahly wakipoteza mchezo wa hatua kama hii walipokutana katika Kundi D na kuipa timu yake ushindi muhimu.

Bao hilo la Kagere mbali na kumfanya Mnyarwanda huyo mwenye asili ya Uganda kuingia kwenye vitabu vya kihistoria kwa kuwatungua Al Ahly, lakini pia liliisaidia Simba kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi hilo kwa kufikisha pointi tisa zikiwamo nyingine sita dhidi ya JS Saoura ya Algeria na AS Vita ya DR Congo waliokuwa nao ndani ya kundi hilo.

Hata hivyo, Ahly ilimaliza kinara na wote wakaingia hatua ya robo fainali, kumbuka msimu huo Simba haikupoteza mechi yoyote ya nyumbani na pia haikushinda mechi yoyote ya ugenini kwani ilipigwa 5-0 na Al Ahly na As Vita na kupoteza pia 2-0 kwa JS Saoura.

CANNAVARO

Beki na nahodha huyo wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliingia kwenye historia kwa kuvunja minyororo ya unyonge wa miaka 32 kwa timu yake dhidi ya timu za Kiarabu. Beki huyo wa kati, aliifungia bao muhimu katika mechi iliyopigwa 2014 kwa kichwa kikali akipokea mpira wa kona ya Saimon Msuva dakika ya 82.

Kona hiyo ilitokana na Yanga iliyowabana vyema Ahly kufanya shambulizi kali wakati Emmanuel Okwi akiachia shuti kali na kipa wa Waarabu hao kupangua na kuwa kona iliyopigwa kiufundi na Msuva na Cannavaro akajitwisha na kuikata minyororo ya unyonge wa miaka 32 kwa Yanga dhidi ya Waarabu, lakini ukiwa ushindi wa kwanza kwa Yanga dhidi ya Al Ahly. Ikumbukwe kuwa, Yanga ikiwa ndio klabu pekee ya Tanzania iliyocheza mara nyingi zaidi na Al Ahly na mara zote ilikuwa ikichapika tangu 1982, na ilikuwa haijawahi kupata ushindi wowote mbele ya Mafarao hao, zaidi ya vipigo vya aibu ama kuambulia sare. Katika mechi 10 walizokutana tangu 1982 Yanga iliruhusu mabao 18 na yenyewe kufunga manne tu, ikipoteza mechi sita, kushinda moja iliyotokana na bao la Cannavaro na kutoka sare tatu - mechi moja ikiondoshwa kwa penalti 4-3 baada ya Wamisri kulipa kisasi cha bao la beki huyo na kwenda kwenye matuta.


MOGELLA NA MTEMI

Simba ni wababe hasa wa Waarabu na hata Al Ahly wanajua bao la juzi la Miquissone haikuwa bahati mbaya kwao, bali ni mwendelezo wa ubabe wa Simba dhidi yao na timu nyingine za Afrika Kaskazini - maarufu kama Waarabu.

Unaambiwa 1985 Simba waliwanyoosha Al Ahly katika mechi ya Kombe la Washindi ambalo 2003 liliungwanishwa na lile la Kombe la CAF na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika 2004.

Simba iliwanyoa Al Ahly kwa mabao 2-1 katika mechi hiyo ya kihistoria iliyopigwa Uwanja wa CCM - Kirumba na mabao ya Mnyama yakiwekwa kimiani na wanaume wa shoka wawili waliowahi kutamba Tanzania na anga za kimataifa, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ a.k.a Morgan ama DHL na jingine la kiungo fundi wa zamani, Mtemi Ramadhani aliyekuwa nahodha wakati huo wa Simba. Mogella alifunga bao la kwanza kabla ya kutoa pasi tamu kwa Mtemi aliyekwamisha ushindi huo ambao hata hivyo haukuwa na faida kwao Simba baada ya kwenda kupoteza ugenini kwa mabao 2-0 na kiung’olewa, japo tayari ilishaweka heshima mbele ya Mafarao hao.

OMARI HUSSEIN

Unaambiwa Yanga ndio iliyokuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kufunga bao dhidi ya Al Ahly walipokutana na wababe hao Juni 8, 1982 walipotoka sare ya bao 1-1. Bao hilo la Yanga liliwekwa kimiani na Omar Hussein ‘Keegan’ likipoza machungu ya kipigo cha mabao 5-0 ilichopewa mchezo wa kwanza uliopigwa Juni Mosi.

Tangu kufungwa kwa bao hilo, Yanga ilikuwa haijawahi kufunga tena dhidi ya Al Ahly hadi Machi Mosi, 2014 kwa bao la Cannavaro.

DONALD NGOMA

Mchezaji wa mwingine aliyeitunga Al Ahly kwa upande wa Yanga alikuwa ni Donald Ngoma aliyefungia bao la kufutia machozi katika mechi ngumu iliyoelekea kuivusha Yanga kwenye raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa 2016.

Ngoma alifunga bao hilo na kuelekeza mechi kwenye matuta kwani katika mchezo wa kwanza Yanga ililazimisha sare ya 1-1 kwa bao la kujifunga la Ahmed Hegaz aliyeshindwa kuokoa mkwaju wa Issoufou Boubacar aliyelishangilia sana, japo bao hilo alipewa beki huyo wa Al Ahly. Ngoma alifunga likiwa la kusawazisha dakika ya 67 baada ya wenyeji kutangulia kupitia kwa Hossam Ghaly na kwenye dakika za majeruhi, Abdallah Said akaivusha Al Ahly kwa bao la ushindi, ikiwa ndio mechi ya mwisho kwa Yanga kucheza dhidi ya Al Ahly mwaka huo wa 2016.