Sio kawaida, namba za kushangaza Ligi Kuu Bara

WAKATI jezi za namba zilipoanza kutumika kwenye soka mwaka 1939, ilikuwa rahisi sana mchezaji kuvaa namba kutokana na nafasi anayocheza uwanjani.
Kipa atavaa Namba 1, beki wa kulia atavaa Namba 2, kushoto Namba 3. Winga wa kulia atavaa Namba 7 na winga wa kushoto atavaa Namba 11, huku Namba 9 na Namba 10 zilikuwa za washambuliaji kwenye ule mfumo wa kizamani wa 4-4-2.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, ukaanza kuibuka utamaduni maalumu wa kuwapo na umaalumu kwenye namba za jezi za wachezaji. Mawinga wa viwango bora kabisa wakaanza kupewa jezi Namba 7 au 11 na hapo ndipo walipoibukia wakali kama Cristiano Ronaldo na Mohamed Salah.
Viungo wa washambuliaji waliokuwa mahiri uwanjani wakaanza kupewa jezi Namba 10 na ikawa jezi maalumu kwa watu maalumu. Wakali kama Lionel Messi, Ronaldinho, Wayne Rooney na wengine wakaanza kuonekana ndani ya jezi zenye namba hiyo mgongoni.
Namba 9 nayo ikawa maalumu kwa washambuliaji wa kati mahiri na hapo wakali kama Ronaldo De Lima. Namba 8 ikawa maalumu kwa viungo wa kati na ilionekana kwenye jezi za mastaa kadhaa akiwamo Andres Iniesta na sasa Bruno Fernandes.
Baada ya hapo, namba kwenye jezi za wanasoka hazichapishwi tu bila ya kuwa na sababu nyuma yake. Na jambo hilo limefanya kuwapo na jezi zenye namba za ajabu ndani ya uwanja. Namba zisizozingatia uhalisia wa nafasi ya mchezaji anayocheza uwanjani.
Na soka la kisasa haishangazi kumwona mshambuliaji wa kati akiwa na jezi Namba 2 mgongoni, beki wa kati akiwa na jezi yenye Namba 9 mgongoni kama ilivyowahi kutokea kwa beki wa kati wa Togo, Vincent Bossou - aliyekuwa akivaa jezi yenye Namba 9 mgongoni alipokuwa akiitumia Yanga.
Namba za jezi sasa hivi zimekuwa na sababu zake nyuma ya pazia. Namba za jezi kwa sasa zinafanywa kama nembo kama ilivyo kwa CR7 (Kwa maana ya Cristiano Ronaldo Namba 7). Kwa sasa Namba 10 kwenye soka ni za magwiji, mchezaji wa kawaida kawaida hupewi hiyo namba.
Wakati ukiendelea kutafakari mapinduzi ya namba kwenye jezi za soka yanavyozidi kupamba moto kwenye mchezo huo wenye ushabiki mwingi duniani, hawa hapa wanasoka wanaovaa jezi za kushangaza kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
JEAN BALEKE-4
Ni mshambuliaji mpya wa Simba aliyesajiliwa dirisha dogo la usajili tayari kwa kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ambayo inaongozwa na Moses Phiri ambaye ndiye kinara wa upachikaji wa mabao akiwa ameingia kambani mara 10, ameonekana akivalia jezi yenye namba nne mgongoni.
Baleke tayari ameonyesha uchu wa kuipambania timu hiyo akicheza mechi mbili tangu amesajiliwa ameshatupia mabao mawili alianza dhidi ya Dodoma Jiji Simba ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 alifunga tena dhidi ya Singida Big Stars wakiibuka na ushindi wa mabao 3-1.
PASCAL WAWA-7
Beki kisiki na mzoefu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Pascal Wawa ambaye kwa sasa anakipiga SBS ameibuka na namba mpya akionekana anatupia jezi Namba 7 ambayo imezoeleka kuvaliwa zaidi na mawinga awali akiwa Simba alikuwa akivaa jezi Namba 6.
Wawa ambaye aliletwa nchini na matajiri wa jiji, Azam FC akitokea El Merreikh ya Sudan, msimu wa 2014/15 akiitumikia timu hiyo alikuwa anavaa jezi Namba 5, hivyo amebadili namba kila timu aliyocheza Tanzania Bara.
JAMES AKAMINKO-2
Ni kiungo mshambuliaji raia wa Ghana aliyesaini mkataba wa miaka miwili Azam FC akitokea Great Olympic alikuwa ni mmoja wa viungo wabunifu kwenye Ligi Kuu ya Ghana naye ni miongoni mwa mastaa wanaovaa jezi zenye namba ya ajabu ambayo ni tofauti na nafasi anayocheza.
Kiungo huyo nyota, aliyewahi kucheza soka la kulipwa nchini Tunisia katika timu ya US Tataouine amepita pia kwa vigogo wa Ghana, Ashanti Gold na Medeama, mbali na kucheza eneo la ushambuliaji, pia anao uwezo wa kucheza kiungo mkabaji.
ISMAEL SAWADOGO-3
Ujio wake ndani ya timu ya Simba umeonekana kuwa na madhara kwa mkongwe Jonas Mkude ambaye sasa hana nafasi ya kucheza kutokana na kushindwa kuonekana kwenye mechi za Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili tofauti na mwanzo wa msimu.
Kiungo huyo ambaye amekuwa akipata nafasi ya kucheza kikosi cha Simba tangu amesajiliwa amekuwa akivaa jezi Namba 3 mgongoni akiwa ni kiungo mkabaji akicheza sambamba na Sadio Kanoute, wengi waliamini angeweza kuvaa jezi Namba 6 au 10 na zaidi.
SHABAN MSALA-4
Huyu ni kiungo mshambuliaji ambaye anakipiga Ruvu Shooting ambaye anavaa jezi Namba 4, ambayo mara nyingi imekuwa ikitumiwa zaidi na mabeki wa kati kwenye timu mbalimbali duniani na wengi ambao wamekuwa wakicheza nafasi hii bila kuwa na namba hiyo wamekuwa wakitumia Namba 10 na kuendelea.
RAMADHAN CHOMBO-3
Kiungo wa zamani wa Simba, Azam na Geita Gold ambaye kwa sasa anakipiga Polisi Tanzania na kuvaa jezi Namba 3 tofauti na timu alizozitumikia awali akiwa Simba alikuwa anavaa jezi Namba 6 wakati Biashara alikuwa anavaa 8.
PIUS BUSWITA-3
Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Mbao ya Mwanza, Ruvu Shooting ambaye sasa anakipiga Namungo FC anavaa jezi Namba 3 mgongoni na ni namba ambayo amekuwa akiitumia tangu akiposajiliwa na Yanga akitokea Mbao.
IBRAHIM MUSSA-3
Namba 3 ni maalumu kwa mabeki wa kati lakini mshambuliaji wa Ruvu Shooting, Ibrahim Mussa anaivaa na ameamua kuitupia bila kujali akiwa anacheza nafasi ya kiungo.
RADACK CHASAMBI-5
Wakati imezoeleka washambuliaji wengi kuvaa jezi Namba 9, 10 na 11, straika wa Mtibwa Sugar, Radack Chasambi amekuja na kali ya mwaka kwa kuvaa jezi Namba 5 ambayo imekuwa ikivaliwa zaidi na mabeki wa kati.