Singida BS Vs Simba, mechi ya lawama

Muktasari:
- Katika mechi hizo nane imevuna jumla ya mabao 17 na kufungwa mawili tu katika pambano lililomalizika kwa Mnyama kutakata kwa ushindi wa mabao 5-2. Hayo ndio mabao pekee ambayo timu hiyo y Simba imeruhusu tangu ilipofungwa na Yanga.
SIMBA imecheza mechi nane mfululizo za Ligi Kuu Bara bila kupoteza tangu ilipofungwa na Yanga bao 1-0 katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Oktoba 19 mwaka huu.
Katika mechi hizo nane imevuna jumla ya mabao 17 na kufungwa mawili tu katika pambano lililomalizika kwa Mnyama kutakata kwa ushindi wa mabao 5-2. Hayo ndio mabao pekee ambayo timu hiyo y Simba imeruhusu tangu ilipofungwa na Yanga.
Lakini leo Jumamosi timu hiyo itakuwa ugenini kuvana na Singida Black Stars katika mechi ya lawama. Ni mechi ambayo itatoa dira ya kile alichokuwa akikitarajia kocha Fadlu David ya kumaloiza duru la kwanza timu ikiwa kileleni mwa msimamo kwa kuvuna pointi 40.
Hii ni moja kati ya shoo mbili za Ligi Kuu Bara zinazopigwa leo Jumamosi, kwani ukiondoa mechi hiyo itakayofanyika kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida, pia kuna pambano la Dodoma Jiji dhidi ya Mashujaa, jijini Dodoma mechi zitakazofuatiliwa kwa vile kule England hakuna mechi ya EPL kwa leo.

Ligi ya England itapigwa kesho Jumapili kwa mechi sita tofauti, zitakazoenda sambamba na mechi mbili za Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Fountain Gate na ile ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union dhidi ya KMC zote zikiopigwa saa 10:00 jioni.
Bahati mbaya ni kwamba Simba inakutana na timu inayoonekana kuwa bora msimu huu, ikiundwa na wachezaji wenye uchu wa kufumaini nyavu, huku mashabiki na wapenzi watakuwa na hamu ya kutaka kuona waamuzi watalichezeshaje pambano hilo kutokana na kelele zinazoendelea mitandaoni juu ya timu hiyo na waamuzi.
Mechi iliyopita ambayo dhidi ya JKT ilionekana kama ilikuwa inaenda kuisha kwa suluhu kabla ya kupatikana kwa penalti iliyowapa ushindi Simba, huku lawama zikienda kwa waamuzi kama ilivyokuwa katika mechi nyingine kadhaa nyuma ambapo Wekundu wa Msimbazi wamekuwa wakipata penalti na kuisaidia kushinda.

Ni mechi ya lawama kwa mabeki wa timu zote ambao watakuwa na kazi ya kuwazuia washambuliaji wenye uchu na wanaofukuzana kileleni mwa orodha wafumania nyavu. Elvis Rupia wa Singida anaongoza orodha kwa sasa akiwa na mabao manane, akifuatiwa na Charles Jean Ahoua wa Simba mwenye saba zikiwamo penalti tatu.
Pia kuna wakali wengine wa timu zote, Josephat Bada, Marouf Tchakei, Ayoub Lyanga na ingizo jipya, Victorien Adebayor anayesaka bao la kwanza la Ligi kwa upande wa Singida, wakati Simba ikiwa na Leonel Ateba, Steven Mukwala na ingizo jipya, Elliem Mpanzu anayetafuta pia bao la kwanza la ligi hiyo vile vile.
MTEGO ZAIDI
Mechi hiyo ya Simba na Singida na ikle ya kesho Jumapili kati ya Yanga na Fountain Gate ni za kimtego zaidi kwa vigogo kwani kila moja inahitaji matokeo ili kuweza kumaliza duru lwa kwanza ikiwa kileleni na pointi za maana zitakazosaidia mbele ya safari katika mbio za ubingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu.

Simba ipo kileleni kwa sasa nan pointi 37, moja zaidi na ilizonazo Yanga inayoshika nafasi ya pili, ilihali Azam iliyokuwa uwanjanin usiku wa jana dhidi ya JKT pamoja na Singida zilikuwa zinalingana kwa pointi 33 zikifuata nafasi ya tatu na ya nne mtawalia.
Mechi hizo mbili zinawakutanisha wakongwe wa soka nchini ambao wanakwenda kucheza dhidi ya timu ambazo mwanzo zilikuwa pamoja kabla ya kutengana msimu huu.
Msimu uliopita, kulikuwa na timu inaitwa Singida Fountain Gate ambapo ziliunganishwa timu mbili za Singida Big Stars na Fountain Gate.
Baada ya ushirikiano huo kutamatika, msimu huu kila upande umebaki kwake. Fountain Gate wana timu yao na Singida Black Stars imechukuliwa kutoka Ihefu.
Kwa Simba na Yanga, kama kila moja itashinda basi msimamo utaendelea kama ulivyo, lakini kaa Simba itateleza ama kwa kutoka sare au kupoteza, kisha Yanga ikashinda ina maana Mnyama atang’oka kileleni na kuwapisha watetezi hao watakaokuwa wamefikisha pointi 39 kabla ya mwaka 2024 kumalizika siku tatu zijazo.

SINGIDA BS v SIMBA
Ni mchezo ambao kila mmoja anautolea macho ukizingatia kwamba timu hizo zipo katika kupambana kila mmoja kuhakikisha haitoki nafasi nne za juu wakati Simba yenyewe inautaka ubingwa.
Singida Black Stars ambayo ilianza kwa kasi kubwa, hivi sasa inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 33 huku ikitoka kuichapa KenGold mabao 2-1 nyumbani katika mchezo uliopita wakati Simba ikishinda 1-0 mbele ya JKT Tanzania.
Ushindani mkubwa katika mchezo wa leo unabebwa na mambo mengi ikiwemo rekodi nzuri ya Simba mbele ya wapinzani wao hao tangu wameanza kukutana.
Singida Black Stars ambayo awali ilikuwa ikifahamika kwa jina la Ihefu, imekutana na Simba mara saba ikiwemo mechi sita za ligi na moja Kombe la FA ambapo Simba haijawahi kupoteza zaidi ya sare moja pekee ambayo ilipatikana katika mchezo wa mwisho kukutana kwao.

Katika mechi hizo saba kwa jumla, Simba imeshinda sita na sare moja, ikifunga mabao 12 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu.
Rekodi hizo zinaonyesha Singida Black Stars ni wanyonge lakini ubora wa kikosi chao kwa msimu huu zinawapa jeuri ya kuikabili Simba kibabe.
MECHI YA KIMATAIFA
Unaweza kusema hii ni mechi ya kimataifa kutokana na aina ya wachezaji waliopo kwenye timu zote mbili na umuhimu wao mkubwa katika kuzipa matokeo mazuri.
Wachezaji wa kimataifa katika timu hizo wamekuwa na mchango mkubwa wa kufunga mabao na kutengeneza nafasi za mabao kulinganisha na wazawa.
Ndani ya Singida Black Stars yenye mabao 22, Elvis Rupia ndiye kinara wa mabao ambaye pia ni kinara wa jumla katika ligi hiyo akifunga manane na asisti moja. Nyota mwingine wa kikosi hicho ambaye anafanya vizuri pia ni Marouf Tchakei mwenye mabao manne na asisti mbili wakati Josephat Arthur Bada akifunga matatu na asisti nne.
Mwingine ni Emmanuel Keyekeh mwenye mabao mawili na asisti tatu. Kwa wazawa, Ayoub Lyanga na Kennedy Juma pekee ndiyo waliofunga mabao kila mmoja akiwa na moja.
Pale Simba timu hiyo iliyofunga mabao 30 ikiongoza kwa kucheka na nyavu, Jean Charles Ahoua ndiye mtu mwenye mchango mkubwa wa mabao akifunga saba na asisti 11 wakati Leonel Ateba akifunga matano na asisti moja.

Steven Mukwala naye ana mabao manne na asisti mbili akionekana kufanya vizuri katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar alipofunga mawili Simba ikishinda 5-2.
Ubora wa kiwango cha Fabrice Ngoma eneo la kiungo cha ukabaji, unaipa pia jeuri Simba kwani nyota huyo mbali na kuimarisha eneo lake, pia anafunga akiwa na mabao mawili.
Wazawa wa Simba wenye mabao ni Valentino Mashaka (2), Awesu Awesu (2), Edwin Balua (2) na Shomari Kapombe (2), huku pia nahodha Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akichangia mabao manne akifunga moja na asisti tatu. Kwa upande wa asisti, Ladack Chasambi naye anazo tatu.
ULINZI IMARA
Katika safu ya ulinzi, Simba ipo imara zaidi ya wapinzani wao ingawa hawajapishana kwa kiwango kikubwa sana. Simba ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache zaidi msimu huu yakiwa ni matano, kazi kubwa ikifanya na mabeki, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza na kipa wao Moussa Camara ambaye ni kinara wa clean sheet akiwa nazo 11 akicheza mechi 14.
Singida Black Stars iliyoruhusu mabao 10 katika mechi 15, kipa wao Metacha Mnata anafanya kazi nzuri kwani ana clean sheet saba akizidiwa nne na kinara.
TANO ZA MWISHO
Mechi tano za mwisho walizocheza Singida Black Stars kwenye ligi, wameshinda tatu, sare moja na kupoteza moja, huku Simba ikishinda zote jambo linalowafanya kuhitaji ushindi pia leo ili kuendeleza moto wao huo huku hesabu zikiwa ni kumaliza duru la kwanza na pointi 40.
Singida Black Stars inatarajiwa kuwa na kikosi chao kamili cha mapambano, huku Simba ikiwa na furaha baada ya kurejea kwa Kibu Denis ambaye alikosekana mechi mbili zilizopita dhidi ya Kagera Sugar na JKT Tanzania.
Kurejea kwa Kibu, kinamfanya Kocha wa Simba, Fadlu Davids kuwa na wigo mpana katika eneo la ushambuliaji ingawa Joshua Mutale hatakuwepo.
Hii inamaanisha kwamba, pale mbele ambapo Jean Charles Ahoua, Elie Mpanzu, Awesu Awesu, Ladack Chasambi na Kibu Denis ambao wanatumika zaidi kusaidia mashambulizi, wawili watalazimika kuanzia benchi.
MZIKI WA KESHO
Mechi ya kesho itakuwa ni ya tano mfululizo kwa kocha Sead Ramovic katika Ligi Kuu baada ya awali kuanza na Namungo na kushinda kwa mabao 2-0, ikaichapa Mashujaa kwa mabao 3-2, kisha kuzipiga 4-0 Tanzania Prisons na Dodoma Jiji, huku ikikutana na timu yenye ukuta unaovuja wa Fountain Gate.
Fountain Gate ndio timu ya pili kwa kuruhusu mabao mengi ikifungwa 27, mawili pungufu na iliyofungwa KenGold inayoshika mkia na kuongoza kuwa na ukuta mwepesi zaidi.
Kazi ya safu ya ushambuliaji ya Yanga katika mechi nne zilizopita, hususani kwa Clement Mzize na Prince Dube wenye mabao matano kila mmoja katika mechi 14 ilizocheza timu hiyo, zinaiweka katika lawama nzito safu ya mabeki ya Fountain Gate kuizuia Yanga kwenye Uwanja wa KMC Complex, iliyovuna mabao saba katika mechi za mwisho zilizopita na kufungwa mawili tu.
Hata hivyo, safau ya ushambuliaji ya FOG nayo sio ya kubezwa kwani katika mechi 15 ilizocheza hadi sasa imefunga 24 ikiwa ni moja ya timu tatu zenye mabao mengi katika Ligi Kuu ikiwa nyuma ya Simba yenye 30 na Yanga iliyofunga 27 hadi sasa katika mechi zao 14 ilizocheza katika ligi hiyo.
Ikimtegemea Edgar William mwenye mabao matano, nyuma ya Seleman Mwalimu aliyefunga sita lakini yupo nje ya uwanja kwa kujiuguza kwa muda sasa, mbali na kuwepo kwa Salum Kihimbwa anayejua kufunga na kuasisti ni wazi mabeki wa Yanga chini ya Dickson Job na Ibrahim Bacca wana kazi za kufanya kesho KMC.
Ni wazi haitakuwa mechi nyepesi kwa pande zote, lakini itabeba lawama kwa yeyote atakayesababisha timu moja wapo kupoteza mchezo huo na malengo la kila timu katika kukusanya pointi za kutosha za kuwabeba mbele ya safari za mbio za ubingwa kwa msimu huu wa 2024-2025 ambao hautabiriki kwa ushindani uliopo. Tusubiri!