Singida Black Stars inavyofukuzia ufalme wa Azam FC

Muktasari:
- Kutoka kwenye changamoto za msimu wa 2023/2024, ilipomaliza ligi nafasi ya saba hadi kujiweka katika nafasi nne za juu msimu huu timu hiyo imevunja vikwazo na kuonyesha umahiri.
SINGIDA Black Stars ni moja ya timu zinazovutia Ligi Kuu Bara ikionyesha kiwango cha juu msimu huu kikiwa ni kielelezo cha mabadiliko makubwa kutoka msimu uliopita na ilikuwa ikifahamika kama Ihefu.
Kutoka kwenye changamoto za msimu wa 2023/2024, ilipomaliza ligi nafasi ya saba hadi kujiweka katika nafasi nne za juu msimu huu timu hiyo imevunja vikwazo na kuonyesha umahiri.
Wachezaji wapya, usajili bora na juhudi za benchi la ufundi chini ya makocha tofauti waliopo na waliopita akiwemo Patrick Aussems ambaye aliuanza msimu kabla ya kibarua chake kuota nyasi, vimeifanya Singida Black Stars kuwa tishio.
Hiyo ni timu iliyojaa ari, matumaini na ndoto za kumaliza msimu ikiwa miongoni mwa timu tatu za juu. Ikiwa na pointi 50 baada ya michezo 26, Singida Black Stars inahitaji kujidhatiti katika mechi zilizobaki ili kutimiza malengo.

Wakati ubora wa safu ya ushambuliaji ikiongozwa na Jonathan Sowah na Elvis Rupia, kocha David Ouma anajivunia timu inayopigana hadi dakika za mwisho huku akithamini mchango wa kila mmoja ikiwemo viongozi pamoja na mashabiki ambao wamekuwa wakiwaunga mkono.
Je, Singida Black Stars itaweza kufikia kilele cha mafanikio? Hapa tunaletea undani safari ya timu hiyo hadi sasa, changamoto zilizopo na matumaini kwa mechi zilizobaki kabla ya msimu kufika tamati.
WATAWEZA KWELI
Kwa sasa Singida ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 50 katika michezo 26.
Kwa mechi zilizobaki, timu hiyo ina nafasi nzuri ya kumaliza nafasi tatu za juu ikiwa itaendelea na kiwango bora ilicho nacho.
Mechi zilizobaki ni dhidi Tabora United (Aprili 19, nyumbani), Simba (Mei 14, ugenini), Dodoma Jiji (Mei 21, ugenini), na Tanzania Prisons (Mei 25, nyumbani).

Kulingana na takwimu hizo na pointi ilizonazo, Singida ina uwezo wa kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu au hata ya pili ingawa inahitaji kufanya vizuri zaidi kuipiku Azam iliyopo nafasi ya tatu na Simba iliyo ya pili.
Msimu wa 2023/2024, wakati timu hiyo ikiitwa Ihefu SC, ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya saba na pointi 36. Ilishinda mechi tisa, sare tisa na kupoteza 12. Hii inaonyesha wazi msimu huu, kuna mabadiliko makubwa katika kiwango chake na hivyo kufanya kuwa na matokeo bora zaidi.
KIWANGO CHAO
Msimu huu, Singida imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na msimu uliopita. Hii inadhihirika kwa idadi ya pointi walizokusanya na vilevile idadi ya mabao waliyofunga.
Msimu uliopita, ilikuwa na pointi 26 kwa mechi 24, ilikuwa katika kundi la timu 10 za chini na haikuwa na uwezo mkubwa wa kutisha dhidi ya timu kubwa.

Hata hivyo, msimu huu, timu imetoka mbali na imeongeza pointi hadi 50, ikiwa na michezo minne iliyobaki.
Uwekezaji mkubwa umefanywa katika kuimarisha timu, wachezaji wenye uzoefu mkubwa wameletwa ili kuleta mabadiliko. Jonathan Sowah kutoka Ghana ni mmoja wa wachezaji waliosajiliwa dirisha dogo na ameonyesha kiwango cha juu kwa kufunga mabao tisa katika michezo 10.
Kinara wa mabao wa Singida kwa msimu uliopita alikuwa Marouf Tchakei aliyefunga mabao tisa, Ismail Mgunda na Elvis Rupia kila mmoja akiwa na mabao sita.
Aidha, wachezaji wengine kama Emmanuel Keyekeh (Ghana), Josephat Bada (Ivory Coast) na Muhamed Camara (Guinea) ambao wamebadili uraia wa nchi walizotoka na kuwa Watanzania, wameongeza ubora na nguvu katika timu.

Kufanikiwa kwa Singida kunatokana na usajili wa wachezaji wa daraja la juu ikiwemo hao ambao wameleta mabadiliko makubwa kuanzia kwenye safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji.
SOWAH, RUPIA
Mchezaji anayeonekana kuibeba zaidi Singida ni Sowah, ambaye ameonyesha uwezo wa juu kwenye safu ya ushambuliaji.
Tangu aingie kwenye kikosi hicho dirisha dogo, amefunga mabao tisa katika michezo 10 aliyocheza.
Awali timu hiyo ilikuwa ikibebwa na Rupia - mmoja wa washambuliaji walioonyesha viwango vya juu msimu huu akiwa na mabao 10 kwenye ligi na ni mmoja wa wachezaji hatari kwenye safu ya mbele ya Singida.
Kwa pamoja, Sowah na Rupia wanaunda safu ya ushambuliaji yenye nguvu ambayo imezalisha mabao 19 na kusaidia timu kupata matokeo bora dhidi ya wapinzani wao ikiwemo dhidi ya Azam siku chache zilizopita.
Kwa upande wa ulinzi, Singida imetoka kuwa na safu dhaifu msimu uliopita ambayo iliruhusu mabao 36 hadi kuwa na safu thabiti ya ulinzi msimu huu ikiruhusu 21 kwenye michezo 26 jambo ambalo linadhihirisha benchi la ufundi limefanya kazi kubwa kuboresha eneo hilo.

BENCHI LA UFUNDI
Kocha wa Singida, David Ouma amekuwa na maoni chanya kuhusu kiwango cha timu yake msimu huu.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Ouma anasema timu hiyo imekuwa na mwenendo mzuri na ni suala la kuendelea na juhudi kubwa ili kumaliza msimu kwa mafanikio.
Ouma amefurahishwa na ushirikiano mzuri kati ya wachezaji na benchi la ufundi na wachezaji wamesikia na kutekeleza mbinu zinazowekwa.
“Tunajivunia hatua tuliyofikia. Licha ya kuwa bado tunahitaji kufanya kazi zaidi, tunajua kuwa tuna nafasi nzuri ya kumaliza kwenye nafasi nzuri msimu huu. Mechi zilizobaki zitakuwa ngumu, hasa dhidi ya timu kama Simba, lakini tunahitaji kujiamini na kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kupata matokeo bora.”