Simba miaka 7 bila namba 9

Muktasari:
- Zamorano alilazimika kutumia jezi namba 18, lakini akaweka alama ya 'jumlisha' kati ya tarakimu hizo mbili ili kupata hesabu ya namba 9 aliyokuwa akiipenda kuivaa, ila alilazimika kumuachia Mbrazili huyo.
WAKATI Ronaldo De Lima 'R9' alipojiunga Inter Milan mwaka 1997 katika uhamisho ulioweka rekodi kipindi hicho akitokea FC Barcelona ya Hispania, alisisitiza apewe jezi namba 9 kwa mmiliki wa awali wa jezi hiyo, Ivan Zamorano aliyelazimika kufikiria mbinu mbadala. Unajua alifanya nini?
Zamorano alilazimika kutumia jezi namba 18, lakini akaweka alama ya 'jumlisha' kati ya tarakimu hizo mbili ili kupata hesabu ya namba 9 aliyokuwa akiipenda kuivaa, ila alilazimika kumuachia Mbrazili huyo.
Hii inaonyesha jinsi gani jezi namba 9 inavyothaminiwa duniani kote, hasa kwa washambuliaji wa kati, lakini cha ajabu kwa miaka saba sasa, hali imekuwa tofauti kwa Wekundu wa Msimbazi, Simba.
Ni kama vile jezi hiyo imeachwa au imestaafishwa, ikionekana kuwa na gundu.

Mara ya mwisho jezi hiyo ilivaliwa msimu wa 2016/17 na Mrundi Laudit Mavugo, ambaye hakuwa na msimu wa mafanikio. Tangu wakati huo, imeachwa wazi, na kila mshambuliaji aliyekuwa akijiunga na miamba hiyo ya soka la Tanzania ameisusa. Hali hiyo inawafanya wengine kuamua kutumia mbinu kama ile ya Zamorano kwa kuchanganya namba tofauti.
Mfano mzuri wa hilo ni Freddy Michael Kouablan, ambaye badala ya kuvaa jezi namba 9, aliamua kuchukua jezi namba 18. Je, kuna nini nyuma ya jezi hii wakati kihistoria inatajwa kuwa chaguo la washambuliaji wengi hatari na hata Simba walikuwa na mastaa waliotamba wakiwa wameivaa?
GUNDU AU IMANI?
Hili ndilo swali linalowatatiza wadau wa soka la Tanzania. Kwa mujibu wa chanzo ndani ya Simba, imani kuwa jezi namba 9 ina gundu imeenea sana. Hata baadhi ya washambuliaji waliotaka kuvaa jezi hiyo walikatazwa kwa sababu ya historia yake ya karibuni. Mfano mzuri ni Pa Omar Jobe.
"Pa (Omar Jobe) alitaka kuvaa jezi namba 9, lakini alielezwa historia yake ya karibuni. Uchaguzi wa mwisho ukabaki kwake, na akaamua kuchukua jezi namba 2," chanzo hicho kilisema.
Hali hiyo imejirudia kwa mshambuliaji mpya wa Simba, Leonel Ateba, ambaye alijitokeza kuwa mkombozi kwenye mechi dhidi ya Al Ahly Tripoli katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Kama ilivyokuwa kwa Jobe, Leonel naye alielezwa kuhusu imani mbaya iliyoambatanishwa na jezi namba 9 na kuamua kuvaa namba 13.

ISHU IPO HAPA
Rekodi zinaonyesha wachezaji kadhaa wa miaka ya karibuni waliowahi kuivaa jezi namba 9 ndani ya Simba walishindwa kutoboa.
Gervas Kago aliwahi kuivaa jezi hiyo msimu wa 2011 lakini mambo yamlichachia na kushindwa kufanya maajabu licha ya kusajiliwa kwa matumaini makubwa ya kuibeba timu.
Mwingine aliyechemsha na jezi hiyo ni Wilker Da Silva aliyetua Msimbazi mwaka 2019 kutoka Brazili ambaye hakuwa na maajabu yoyote akiumia mapema na kushindwa kuitumikia timu hiyo hadi anaondoka.
Pia kuna Betram Mwombeki aliwahi kuitumia namba hiyo msimu wa 2013, lakini alipoona yanampalia alihamia namba 23, sawa na ilivyokuwa kwa Fredrick Blagnon aliyekuwa akivaa jezi hiyo kabla ya kumuachia Mavugo mwaka 2016 na kuchagua namba 27, ikiwa na hesabu zilezile za namba tisa (2+7=9), lakini bado mambo yaliwaendea wote wawili kwani Mavugo alichukua namna 11 baadae.

Kwa wasiojua Mavugo alipopokelewa na kutambulishwa Sima 2016 alipewa jezi namna 45 (4+5=9), kisha kuachiwa jezi namba 9 na Blagnon, lakini akachemsha na kukimbilia 11 hadi anatimkia Zambia akiwa hajafikia kiwango alichotoka nacho Vital'O ya Burundi alipofunga mabao zaidi ya 60 katika misimu miwili ya ligi.
WALIOTAMBA NAYO
Licha ya imani hii, kuna wachezaji waliotamba sana na jezi namba 9 ndani ya Simba. Mmoja wao ni Mogella, mshambuliaji hatari aliyecheza kwa mafanikio makubwa ndani ya klabu hiyo. Mogella anasema, “Imani tu zinawaharibu wachezaji. Mimi nilivaa jezi namba 9 Simba na nilikuwa nafunga sana.”
Nyota mwingine aliyeitamba nayo ni Edward Chumila, ambaye alikabidhiwa jezi hiyo baada ya Mogella kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Chumila aligeuka kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba baada ya kufunga mabao muhimu, hususan dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.
SHINDIKA ALIIKATAA
Mwaka 2013, nahodha wa zamani wa Simba, Henry Joseph, alikataa kuvaa jezi namba 9 baada ya kurejea kutoka Norway. Joseph aliwaambia viongozi wa Simba kuwa namba hiyo haimvutii.
"Kwanza niliwaambia wakati naondoka Simba nilikuwa navaa jezi namba 6 na hiyo ndiyo chaguo langu," anasema Joseph. Alipendekeza apewe jezi namba 12 au 14 badala ya 9, ambayo aliona haimfai.

ITAWEZEKANA?
Kwa miaka saba sasa, hakuna mchezaji wa Simba aliyevaa jezi namba 9. Hii ni tofauti na hali ilivyo kwa klabu nyingi kubwa duniani ambapo jezi hiyo ni ishara ya mshambuliaji hatari. Simba wanakabiliwa na changamoto ya kushawishi washambuliaji wao wapya, jezi hiyo haina gundu, kama inavyoaminika na baadhi ya mashabiki na wachezaji.
Klabu inaweza kuamua kuacha kuzingatia imani na badala yake kuhamasisha washambuliaji kuchukua jezi namba 9 kwa kujenga utamaduni mpya wa ufanisi na ushindi. Kwa sasa, jezi hiyo inabaki kuwa kama mzigo wa kihistoria, ambao wengi wanaukwepa.
Kwani hata kule Yanga, jezi hiyo iliogopwa na washambuliaji waliowahi kuichezea timu hiyo, lakini Fiston Mayele aliamua kujivisha mabonu na kuinyakua na katika misimu miwili aliyoitumikia klabu hiyo alifanya makubwa na kuacha alama ambazo bado zinaishi Jangwani, ikiwamo kufunga mabao 33 katika Ligi Kuu Bara na kuifikisha timu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika akiibuka Mfungaji Bora na mabao saba.

Simba ya msimu wa 2024-2025
1- Ally Salim
2- Karaboue Chamou
3- David Kameta 'Duchu'
4- Hussein Kazi
5-
6- Fabrice Ngoma
7- Joshua Mutale
8- Omary Omary
9-
10-Charles Ahoua
11-Steven Mukwala
12-Shomary Kampombe
13-Lionel Ateba
14-Abdulrazak Hamza
15-Mohammed Hussein 'Tshabalala'
16-Saleh Kalabaka
17-Debora Mavambo
18-
19-Mzamiru Yassin
20-Fondoh Che Malone
21-Yusuf Kagoma
23- Awesu Awesu
24-Kelvin Kijili
25-Augustine Okajepha
26-Moussa Camara
27-Valentino Mashaka
28-Aishi Manula
29-Valentin Nouma
30-Hussein Abel
36-Ladack Chasambi
37-Edwin Balua
38-Kibu Denis
40-Ayoub Lakred