Simba kimataifa shida ilianzia hapa

Simba ilipone hapa kwa USGN

KWA misimu minne mfululizo, Simba imekuwa ikiteseka na mabao yatokanayo na mipira ya juu ya krosi, kona na frii-kiki.

Katika misimu hiyo ambayo imeshiriki mashindano ya kimataifa, idadi kubwa ya mabao ambayo wamefungwa, yametokana na aina hiyo ya mipira.

Msimu wa 2018/2019 ambao ilifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba hadi inatolewa na TP Mazembe kwenye hatua hiyo, iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara 21 ambapo zaidi ya 65% ya mabao hayo yalitokana na mipira ya juu ya krosi, kona na frii-kiki.

Awamu iliyofuata Simba ilitolewa raundi ya awali na UD Songo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani kufuatia kutoka sare ya bila kufungana ugenini.

Na katika msimu uliopita ambao Simba ilifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, waliruhusu nyavu zao kutikiswa mara saba huku mabao manne yakitokana na mashambulizi yaliyotokana na mipira ya kona, frii-kiki na krosi za juu.

Msimu huu mambo yanaonekana kujirudia kwa Simba kwenye mashindano ya klabu Afrika ambapo walianzia katika Ligi ya Mabingwa Afrika na baadaye wakaangukia katika Kombe la Shirikisho Afrika ambapo hivi sasa wapo hatua ya makundi.

Kiujumla kwenye mashindano ya klabu Afrika msimu huu wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara tisa ambapo kati ya hayo, mabao saba yamezalishwa kutokana na mipira ya juu ya frii-kiki, kona na krosi.

Ni tatizo sugu ambalo linaonekana kutofanyiwa kazi kwa muda mrefu licha ya makocha na wachezaji tofauti kupita ndani ya Simba na haionekani kama italishughulikia kwa siku za hivi karibuni.

Hata hivyo, tathmini iliyofanywa na gazeti hili, imeonyesha kuwa tatizo linaloikabili Simba ni matokeo ya kile ambacho kimekuwa kikifanyika katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika Ligi Kuu Tanzania Bara imekuwa ni nadra sana kwa timu kutumia aina hiyo ya mashambulizi jambo ambalo pengine limekuwa likipelekea timu kutoona haja ya kufanyia kazi namna ya kujilinda dhidi ya aina hiyo ya mashambulizi.

Uhaba wa mabao yatokanayo na mipira ya juu ya krosi, frii-kiki na kona kwenye ligi ya ndani, Ligi Kuu Bara, pengine unasababisha makocha wasione haja ya kushughulika na kutafuta suluhisho na kujikita na mbinu nyingine hivyo athari yake huja kuonekana kwenye mashindano ya kimataifa.


Takwimu za Ligi

zinapodanganya

Kwa kutazama mechi zilizopita za Ligi Kuu msimu huu kabla ya zile zilizochezwa jana na juzi, ni wazi kwamba zinatoa majibu ya dalili kwamba makocha wanaonekana kutotoa kipaumbele katika kutafuta dawa ya kukabiliana na aina hiyo ya mashambulizi.

Kati ya mabao 243 yaliyofungwa kabla ya mechi za jana na juzi, jumla ya mabao 68 sawa na 28% yamefungwa kutokana na aina hiyo ya mipira kwa raundi 16 tu ambazo zilikuwa zimeshachezwa.

Hii inamaanisha kuwa mabao yanayofungwa kwa mipira ya juu ya kona, frii-kiki na krosi katika Ligi Kuu Tanzania Bara ni kama robo tu ya mabao yote.

Ni timu chache tu ambazo zimekuwa zikitumia aina hiyo ya mashambulizi na hata pale zinapojaribu kufanya hivyo, zimekuwa butu katika kuyageuza kuwa mabao.


FRII-KIKI tatizo zaidi

Kumekuwa na uhaba mkubwa wa mabao yatokanayo na frii-kiki zinazopigwa moja kwa moja langoni ambapo hadi sasa wakati Ligi imeingia katika raundi ya 17 ni mabao nane tu yametokana na frii-kiki za moja kwa moja zikifungwa na wachezaji nane tofauti.

Katika hali ya kushangaza hadi sasa hakuna mchezaji anayeweza angalau kupewa sifa za umahiri wa kufunga kutokana na mipira ya frii-kiki kwa hao wanane kila mmoja amefunga bao moja tu.

Nyota hao wanane ambao kila mmoja amefunga bao moja tu ni Saido Ntibazonkiza (Yanga), Richardson Ngondya (Mbeya City), Ramadhan Chombo (Biashara United), Habib Kyombo (Mbeya Kwanza), Abdulrahman Musa (Ruvu Shooting), Never Tigere (Azam), David Luhende (Kagera Sugar) na Jeremiah Juma (Tanzania Prisons).

Mabao hayo nane ya frii-kiki za moja kwa moja ni sawa na asilimia 3 tu ya mabao yote 243 yaliyofungwa kwenye Ligi Kuu kabla ya mechi za jana na juzi.

Sababu kubwa iliyotajwa kama chanzo cha uhaba wa mabao yatokanayo na frii-kiki za moja kwa moja ni wapigaji husika kutojiandaa vilivyo katika viwanja vya mazoezi.

“Mazoezi ni kitu muhimu mtu akishajulikana ana ubora huo basi anatakiwa aendelee kufanyia mazoezi upigaji huo, lakini sasa mazingira hayaruhusu kufanya hivyo kwa sababu timu nyingine hazina mazoezi ya hivyo na mtu yeyote anapiga ndio maana hazifungwi, anasema Mahadhi na kuongeza;

“Hatufanyii mazoezi, wengi wanafanya kwa mazoea hata hao wanaofunga, kikubwa inabidi tufanye sana mazoezi kwenye mipira ya adhabu ili tufunge,” anasema mchezaji wa Geita Gold, Juma Mahadhi.


Namba zaiumbua Simba

Katika kudhihirisha kuwa Simba wenyewe wamekuwa hawafanyii sana mazoezi ufungaji wa aina hiyo ya mabao jambo ambalo lingewasaidia hata katika kujilinda, imekuwa ni kati ya timu zilizofunga idadi ndogo ya mabao kutokana na mipira ya krosi za juu, frii-kiki na kona.

Timu hiyo katika mechi 15 ilizokuwa imecheza za Ligi Kuu kabla ya ile ya jana dhidi ya Biashara United, ilikuwa imepachikla mabao matano tu kwa aina hiyo ya mashambulizi huku mabao mengine 11 ikifunga kwa staili nyingine.


Azam, Ruvu

Shooting kiboko

Inawezekana Azam FC na Ruvu Shooting ndio timu ambazo zimekuwa zikifanya mazoezi ya mara kwa mara ya kushambulia kwa aina hiyo jambo ambalo linawasaidia hadi katika kuzuia kwani ni kati ya timu zilizofungwa mabao machache kutokana na mipira hiyo.

Azam FC ndio timu iliyofunga idadi kubwa ya mabao kwa staili hiyo ambapo kati ya mabao yake 20, 12 imeyapata kupitia mipira ya juu, frii-kiki, kona na krosi ikifuatiwa na Ruvu Shooting ambayo yenyewe ina mabao 10 ya aina hiyo huku manne tu ikipata kupitia njia nyingine.

Timu zilizofunga mabao machache zaidi kutokana na njia hiyo ni Biashara na Tanzania Prisons zilizopachika mabao matatu kila moja na Coastal Union iliyofunga mabao manne.


Makocha, wadau wafunguka

Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi ameeleza kuwa kufunga au kuzuia mipira ya juu kwa wachezaji wa Tanzania imekuwa ngumu kutokana na mazingira ya wachezaji wanayokulia.

“Tunashindwa kuitumia mipira hiyo kiufasaha kwakuwa mtu anafundishwa kufanya hivyo akiwa mkubwa. Pili na la muhimu ni miundombinu yetu kutokuwa rafiki kwa mipira hiyo,” alisema Mwalwisi na kuongeza;

“Wachezaji wetu wengi makuzi yao ni mtaani katika viwanja ambavyo unakuta goli lina urefu na upana tofauti pia, uwanja huo huo unakuta una njia katika, mabonde na milima hivyo inakuwa shinda tunapoenda kucheza na wenzetu ambao wachezaji wao walipata mafunzo hayo tangu wakiwa wadogo na kwenye miundombinu bora.”

Nyota wa zamani wa Kagera Sugar, Simba, Yanga na Taifa Stars, Amri Kiemba ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka anasema;

“Ni utamaduni. Kwa hapa Tanzania watu hawaandaliwi kufanya hivyo kama sehemu ya kupatia mabao bali wanatumia mipira hiyo kwa sababu imetokea, tofauti na wenzetu ambao wanaamini mipira ya kona au krosi ni nusu bao,” alisema Kiemba na kuongeza;

“Iwe kulinda au kufunga sisi tunachukulia poa tu kwakuwa kwenye ligi zetu matunda au hasara za mipira ya namna hiyo sio makubwa lakini tukitoka nje lazima tuaibike kwani wenzetu wanaithamini na kuiheshimu sana mipira hiyo.

“Kingine ni woga kwa wachezaji wetu kutokana na waamuzi wetu walivyo, mara nyingi mipira ya frii-kiki isiyo na kuotea inatafsiriwa vibaya na waamuzi hivyo washambuliaji wanaogopa kukimbia nyuma ya ukuta ili mpigaji audondoshe hapo na mfungaji afunge kwakuwa wanahofia kuwa ‘offside’.

“Lakini wakati huo huo, mabeki wetu hapo ndipo wanazoea vibaya juu ya kukaba mipira hiyo na wakienda kimataifa ambako marefa wanajua vyema sheria ya mipira hiyo, wanakaba kama wako Tanzania na mwisho wa siku wanaadhibiwa.”

Naye Mathias Lule alisema; “Huwa kuna sababu mbili kwenye suala hili, kwanza ni wachezaji kuichukulia mipira hiyo kirahisi, yaani wamekuwa hawajitoi linapokuja suala la kuokoa kwenye mipira ya aina hiyo, vilevile shida inawezekana ikawa kwa kocha wa timu husika huenda wasiwe wanafanya mazoezi ya kutosha kuona jinsi ya kuzuia aina hiyo.”

“Sioni kama kuna shida ya kimo kwa sababu, ukiangalia timu ya taifa ya Japan na China zina wachezaji wengi wafupi lakini wamekuwa hawafungwi kirahisi aina hiyo ya mipira,” aliongeza Lule, huku Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema;

“Mimi naona tatizo hili halipo Tanzania pekee ni duniani kote, kwa sasa mabao mengi yamekuwa yakifungwa kwa aina hiyo kwa sababu tumepoteza viungo wabunifu kwa kiasi kikubwa.”

Nyota huyo wa zamani wa kimataifa aliyewahi kuwika na Yanga, Pan Africans na Taifa Stars kabla ya kugeukia ukocha aliongeza; “Ni timu chache sana zinazoweza kucheza vizuri kwenye eneo la kiungo na kutengeneza mashambulizi kupitia mipira ya kawaida. Hiyo imefanya kila kocha kuona njia pekee ya kupata bao kirahisi ni kupitia mipira hiyo ya kona ama ya kutengwa.”

“Lakini nikizungumzia kile ambacho kinatutafuna sisi ni umakini wa wachezaji wetu kwenye eneo hilo, wamekuwa na umakini mdogo ambao huenda unasababishwa na aina ya utimamu wetu wa kimwili au kile ambacho wamefunzwa mazoezini.”