Nyuma ya pazia jeraha, upasuaji wa Musiala

Muktasari:
- Musiala alilazimika kutolewa nje ya uwanja kwa machela na kupelekwa haraka katika huduma za juu za tiba baada ya uchunguzi uwanjani kubaini ana viashiria vya mvunjiko wa mguu na kuteguka kifundo. Tukio hilo lilitokea wakati kipa wa PSG alipopiga mbizi na kugongana na Musiala huku kifundo cha mguu cha mchezaji huyo kikijipinda vibaya katika uelekeo hasi kimwili.
JUMAMOSI iliyopita katika robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu ilikuwa mbaya kwa mshambuliaji wa Bayern Munich, Jamal Musiala baada ya kupata majeraha mabaya ya mguu. Aliumia mwishoni mwa kipindi cha kwanza wakati alipokumbana na kipa Gianluigi Donnarumma wa PSG katika Uwanja wa Mercedes-Benz mjini Atlanta nchini Marekani.
Musiala alilazimika kutolewa nje ya uwanja kwa machela na kupelekwa haraka katika huduma za juu za tiba baada ya uchunguzi uwanjani kubaini ana viashiria vya mvunjiko wa mguu na kuteguka kifundo. Tukio hilo lilitokea wakati kipa wa PSG alipopiga mbizi na kugongana na Musiala huku kifundo cha mguu cha mchezaji huyo kikijipinda vibaya katika uelekeo hasi kimwili.
Baadaye Jumapili katika uchunguzi wa juu ilidokezwa kuwa amevunjika mfupa saidizi wa mguu ujulikanao kitabibu kama Fibula. Kampeni ya Bayern Munich katika Kombe la Dunia la Klabu ilimalizika vibaya kwani walifungwa mabao 2-0 na PSG wakiwa wamepoteza wachezaji wawili kwa kadi nyekundu.
Jeraha alilopata liliwastua watazamaji na wachezaji wengi uwanjani ambao walionekana wakishika vichwa kama ishara ya kuona hali aliyokuwa nayo Musiala. Inatajwa kuwa ni moja ya ajali mbaya ya kandanda iliyosabisha jeraha kubwa kwa staa wa timu ya taifa ya Ujerumani ambaye ana umri wa miaka 22. Huwa ni kawaida wachezaji kunyoosheana vidole hasa wale wa upande wa timu uliofungwa.
Kipa wa Buyern Munich, Manuel Neuer anaamini upigaji mbizi wa Gianluigi Donnarumma ulikuwa 'hatari' na ndio ulisababisha jeraha baya kwa Musiala. Anasema mpira ulikuwa karibu zaidi kwa Musiala, hivyo kipa huyo angeweza kuepusha tukio hilo.
Donnarumma alionekana kuwa na huzuni wakati timu zikitoka uwanjani muda wa mapumziko, lakini Neuer anaamini Muitaliano huyo lazima akubali kuwajibika kwa tukio hilo.
Baada ya mchezo huo kocha wa Bayern Minich, Vincent Kompany hakuweza kutoa taarifa za kina, lakini ripoti ya Jumapili na Jumatatu zilithibitisha kwamba alikuwa amevunjika mfupa na kuteguka kifundo na atakuwa nje ya uwanja kwa miezi kati ya miinne au mitano.
UPASUAJI ALIOFANYIWA
Vipimo vilibaini kuwa Musiala alivunjika mfupa saidizi wa mguu yaani Fibula ambao ni mojawapo ya mifupa miwili kwenye mguu wa chini, ulio nje ya mguu kati ya goti na kifundo cha mguu. Vilevile kulikuwa na kuteguka kwa kifundo cha mguu maana yake mmoja wa mfupa wa ungio la kifundo ulihama kutoka eneo lake.
Mvunjiko unaweza kuanzia mivunjiko midogo, ya wastani na mikubwa, na mara nyingi husababishwa na kugongwa moja kwa moja, utumiaji kupita kiasi miguu, udhaifu eneo husika, kujipinda uelekeo hasi na kuwa na jeraha linaloendelea. Musiala alipata jeraha baya la kuvunjika mfupa hivyo ni moja ya kiashiria cha kuhitaji upasuaji mkubwa.
Habari nzuri ni kuwa amefanyiwa upasuaji wa kisasa wenye mafanikio Jumatatu nchini Ujerumani.
Taarifa hiyo ilitolewa Jumatatu jioni na Bayern Munich ilithibitisha kwamba mchezaji huyo kijana tegemeo kwa klabu na taifa alikuwa "amefaulu upasuaji" na sasa ataanza mpango maalumu wa uuguzi wa jeraha Jumanne ili kuwezesha kupona kwa wakati.
Upasuaji huo uliofanywa na mabingwa wabobezi wa mifupa ulichukua takribani saa tatu ukihusisha upasuaji wa wazi kwa kutumia vifaa vya kisasa na usaidizi wa picha za mionzi. Kitabibu hii inaleta ufanisi ikiwamo kuona kwa usahihi tishu zilizojeruhiwa, kuunganisha mifupa hiyo kwa vyuma maalumu na kukarabati tishu zilizojeruhiwa.
Upasuaji ulikuwa muhimu ili kurekebisha mifupa na kuimarisha mifupa kwa kutumia vyuma kama vile sahani, boriti na vipande bapa. Itakumbukwa kabla ya jeraha alikuwa ametoka kwenye majeraha. Alijiunga na timu katika michuano hiyo nchini Marekani na alikuwa akianza kwa mara ya kwanza katika mchezo huo. Aliumia katika ungio la kifundo eneo ambalo ana historia nalo kuumia mara kwa mara. Eneo hilo liligongwa na shinikizo la mwili wa kipa mwenye uzito wa kilo 90.
DALILI, VIASHIRIA MVUNJIKO WA MFUPA
Zipo dalili na viashiria kwamba mchezaji amepatwa na mvunjiko wa mfupa ikiwamo kupata maumivu makali yasiyovumilika, uvimbe upande wa nje wa mguu wa chini, kushindwa kuhimili uzito wa mwili wakati wa kutembea na mguu uliojeruhiwa, michubuko au kubadilika rangi eneo lilipo jeraha, hisia ya ganzi au baridi kwenye mguu.
Utambuzi wa jeraha huwa ni uchunguzi wa kimwili ikiwa ni pamoja na kuangalia hali ya maumivu, uvimbe na aina mbalimbali za utendaji kazi kwa kutathimini majaribio ya mwendo katika ungio, huku vipimo muhimu ikiwa ni pamoja na picha za X-ray ili kubaini mvunjiko na pia kutofautisha majeraha mengine.
Katika baadhi ya majeraha CT scan au MRI zinaweza kuhitajika ili kutathmini uharibifu wa tishu laini au mivunjiko na mkazo wa misuli.
MATIBABU, UDHIBITI WA MIGUU
Baada ya upasuaji matibabu huwa ni uzuiaji jeraha lisijeruhiwe zaidi kwa kuwekewa kiatu cha muda, P.O.P au kiatu maalumu cha kutembelea ili kuleta uimara na kuzuia kujijeruhi hatimaye kuruhusu uponaji. Dawa za kupunguza maumivu hutolewa kwa tahadhari ili kutoingilia uponaji. Barafu inaweza kusaidia kupunguza maumivu na uvimbe wakati wa huduma ya kwanza na kabla ya matibabu ya juu ya hospitali.
Tiba ya kimwili baada ya maumivu kuisha huwa ni kurudisha utendaji kazi wa misuli na uingio eneo hilo. Baadaye huhitajika kufanyishwa mazoezi ya kurejesha nguvu, kunyumbulika na aina mbalimbali za mwendo. Urejeshaji utimamu wa mwili, muda wa uponaji hutofautiana kulingana na ukali wa mvunjiko, lakini inaweza kuchukua wiki kadhaa hadi miezi.
Tiba ya kimwili ni muhimu kwa kurejesha utendaji kazi kamili na kuzuia matatizo ya muda mrefu ikiwamo maumivu sugu, ganzi, kifundo kutokuwa na utulivu, baridi yabisi na uharibifu wa neva. Uuguzi huzingatia aina ya lishe, mapumziko na kulala na tiba ya kisaikolojia ikiwamo elimu ya afya jinsi ya kuishi na jeraha hilo.
NINI HATIMA YA MUSIALA?
Musiala atakuwa nje kwa miezi kati ya minne na mitano hivyo atakosa mechi zote za maandalizi ya ligi na zile za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga).
Ni kawaida aina hii ya majeraha kuwa tishio kwa hatima ya mchezaji kwani yanaweza kuunga vibaya na kuleta ulemavu wa kudumu. Vilevile tishu za kifundo cha mguu huchukua muda mrefu kupona kwani ungio hilo ndilo linabeba shinikizo la mwili mzima, lina tishu nyingi ikiwamo mishipa ya damu na fahamu.