Simba kanyaga twende robo fainali

Muktasari:
- Simba yenye pointi sita baada ya kucheza mechi tatu za Kundi A, itakuwa wageni wa Sfaxien kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi uliopo jijini Tunis, Tunisia, ambapo kama itashinda itafikisha pointi tisa ambazo zitaisogeza pazuri kutinga robo fainali kwa mara ya sita katika misimu saba ya kushiriki michuano ya CAF.
BAADA ya Yanga kumalizana na TP Mazembe ya DR Congo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa nyumbani jana, leo Jumapili ni zamu ya Simba iliyopo ugenini ambayo itavaana na CS Sfaxien ya Tunisia katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo ushindi utawaweka Wekundu njiani kwenda robo fainali.
Simba yenye pointi sita baada ya kucheza mechi tatu za Kundi A, itakuwa wageni wa Sfaxien kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi uliopo jijini Tunis, Tunisia, ambapo kama itashinda itafikisha pointi tisa ambazo zitaisogeza pazuri kutinga robo fainali kwa mara ya sita katika misimu saba ya kushiriki michuano ya CAF.
Ushindi utaisaidia Simba kabla ya kwenda ugenini kuvaana na Bravos do Maquis ya Angola kisha kuisubiri CS Constantine kutoka Morocco jijini Dar es Salaam, ambao nao wana pointi sita kama ilizonazo Simba ambazo nazo zitavaana leo kukamilisha mechi za raundi ya nne. Sfaxien ndio vibonde wa kundi kwani haina pointi yoyote licha ya kucheza michezo mitatu vilevile.

Huu ni mchezo wa pili kuzikutanisha timu hizo baada ya ule wa kwanza Simba ikiwa nyumbani kushinda mabao 2-1 tena ikitokea nyuma na kusawazisha kisha kupata bao la ushindi dakika ya 90+.
Hii ikiwa ni mara ya pili kukutana kwao, lakini kitendo cha Simba kuwa ugenini kinawaumiza vichwa kwani timu hiyo imekuwa haina matokeo mazuri.
Simba msimu huu pekee tayari imecheza mechi mbili ugenini na hakuna iliyoshinda zaidi ya kuambulia matokeo ya 0-0 nchini Libya katika hatua ya mtoano dhidi ya Al Ahli Tripoli, kisha makundi ikafungwa 2-0 na CS Constantine pale Algeria.

Katika mechi kumi zilizopita ambazo Simba imecheza ugenini michuano ya kimataifa, imepata sare tano na kupoteza michezo mitano. Haina ushindi jambo ambalo wachezaji wa timu hiyo leo wana kazi ya ziada ya kufanya kuondoa rekodi hiyo mbaya.
Kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji, wanalitambua hilo huku kiungo Mzamiru Yassin akisema: “Mechi za ugenini zinakuwa ngumu haijalishi tunacheza na timu gani. Tunatakiwa kupambana kuhakikisha tunapata pointi tatu ili mechi zinazokuja ziwe rahisi, hatutakiwi kusubiri mechi ya mwisho iamue hatma yetu.”
Ukiweka kando hilo, Simba imekuwa na matokeo mazuri katika mechi tano za mwisho michuano tofauti ikishinda zote ikiwemo moja ya Kombe la Shirikisho na zingine Ligi Kuu Bara.

Wenzao Sfaxien mechi tano za mwisho michuano tofauti, hali ni mbaya kwani imepoteza zote. Kati ya hizo, mbili Kombe la Shirikisho na tatu ligi ya kwao Tunisia.
Hata hivyo, Sfaxien imekuwa na matokeo ya wastani katika michuano ya Caf inapocheza nyumbani huku rekodi zikionesha mechi kumi zilizopita imepoteza tatu na kushinda tano, huku sare zikiwa mbiili.
Unyonge wa Sfaxien katika Kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, hauifanyi Simba kuamini moja kwa moja kwamba inaweza kushinda kirahisi leo.

Ukiangalia namna mchezo uliopita ulivyokuwa na ushindani na aina ya matokeo waliyoyapata Simba utapata jibu kwamba Sfaxien sio wanyonge kwani Simba ilisubiri hadi dakika za nyongeza kupata pointi tatu huku wageni wao hao wakianza kufunga mapema dakika ya tatu kupitia Hazem Haj Hassen kabla ya Kibu Denis kusawazisha dakika ya 7 na 90+8 kufunga la ushindi yote kwa kichwa.
Hata mechi zingine ilizopoteza, tofauti ya mabao ilikuwa ndogo sana, ilianza kufungwa nyumbani 1-0 dhidi ya CS Constantine kisha ugenini 3-2 dhidi ya Bravos, hivyo leo Simba itegemee ushindani uleule, ikizubaa imekula kwao.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids, alisema: “Naijua Sfaxien na aina ya soka inalocheza ikiwa nyumbani, tulipata alama tatu kwetu ni vivyo hivyo tunatakiwa iwe ugenini ili kukamilisha hesabu nzuri kwenye kundi hili. Wachezaji wote wako timamu na tayari nimeshawaambia kuwa jambo la muhimu ni alama tatu tu, ili kuipa heshima timu na kuwa nafasi nzuri.”

SFAXIEN PIGO, SIMBA FRESHI
Unaweza kusema kuelekea mchezo huu wenyeji Sfaxien wamepata pigo mara mbili huku Simba mambo yakiwa freshi.
Kwanza Sfaxien wamefungiwa mechi mbili za nyumbani kucheza bila ya mashabiki kutokana na vurugu walizozifanya mchezo wa kwanza dhidi ya Constantine.
Jambo lingine ni kwamba hawatakuwa na kocha yule ambaye alikuwepo benchi mara ya kwanza wakati wanapoteza mbele ya Simba, Alexandre Miguel Crispim Santos kwani kibarua chake kilisitishwa Desemba 23, 2024 kutokana na mfululizo mbaya wa matokeo.
Kikosi hicho kikakabidhiwa kwa kocha wa timu ya vijana, Oliviya Beran ambaye ameongoza mechi mbili za ligi na zote wakipoteza dhidi ya Stade Tunisien (2-1) na Esperance (1-0). Hata hivyo katika mchezo wa leo timu hiyo itakuwa na kocha mpya, Saad Al Daredi aliyepewa timu hiyo jumla na ataanza na Simba.
Simba kwao freshi kutokana na kwamba hawatakuwa na presha ya mashabiki, lakini pia kuongezwa kwa winga Elie Mpanzu ambaye anaruhusiwa kucheza baada ya usajili kukamilika dirisha dogo, ni faida kubwa kwao.
Mpanzu ambaye tayari amecheza mechi tatu za ligi akiwa na Simba, licha ya kwamba hana mchango wowote wa bao, lakini uchezaji wake umeongeza kitu eneo la ushambuliaji na uwepo wake utampa machaguo mengi kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids.

Endapo Sfaxien itashinda, zitakuwa ni pointi zao tatu za kwanza lakini itaendelea kukaa mkiani, huku ikipiga hesabu ifanye vizuri michezo miwili itakayofuatia ugenini dhidi ya CS Constantine na ule wa nyumbani mbele ya Bravos ishinde yote kwani lolote linaweza kutokea.
Simba nayo hesabu zao leo ikishinda, itafikisha pointi tisa ambazo zitawaweka karibu zaidi na kufuzu robo fainali ikiwa ni kuifukuzia rekodi yao ya kutinga hatua hiyo kwa mara ya sita ndani ya kipindi cha misimu saba.
Wakati huohuo, mchezo mwingine wa kundi hilo utakaochezwa leo, wenyeji Constantine wanapiga hesabu za kuichapa Bravos ambapo timu zote zina pointi sita hivyo kuufanya mchezo huo kuwa kama fainali, atakayeshinda atakaa juu ya mwenzake kwa tofauti ya pointi tatu zikibaki mechi mbili kumaliza hatua ya makundi.
MAREFA WASENEGALI
Pambano hilo litachezeshwa na waamuzi kutoka Senegal, mpuliza filimbi atakuwa ni Daouda Gueye wakati mwamuzi msaidizi namba ni Amadoua Ngom, huku Mamadoua Ba atakuwa msaidizi wa pili na mezani atakuwepo Alloume Sandugui.
Refa Daouda aliyeanza kazi 2011 na aliyekuwa miongoni mwa waliochezesha fainali za Chan 2023, aliwahi kukumbwa na kashfa za rushwa 2018 na kusimamishwa kwa muda huku mwamuzi msaidizi kutoka Ghana, David Laryea alifungiwa maisha na maofisa wengine saba pia wa Ghana walifungiwa kwa miaka 10 kila mmoja.