Prime
Simba hawakujiandaa kibingwa CAFCC

Muktasari:
- Simba, ambayo imekuwa timu ya pili kufika fainali ya mashindano hayo baada ya Yanga miaka miwili iliyopita ilitakiwa kugeuza matokeo ya kipigo cha mabao 2-0 ilichopata Morocco wiki moja iliyopita kwa kupata ushindi mnono wa kuanzia mabao 3-0, lakini ndoto zilizimwa na mchezo wa maarifa, ufundi, jitihada na malengo ulioonyeshwa na RS Berkane.
KWA mara nyingine Watanzania wanajifariji kwamba wamejitahidi baada ya Simba kushindwa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani walipolazimishwa sare ya bao 1-1 na Renaissance de Berkane ya Morocco, matokeo ambayo yalimaanisha wawakilishi hao wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho wamelala kwa jumla ya mabao 3-1.
Simba, ambayo imekuwa timu ya pili kufika fainali ya mashindano hayo baada ya Yanga miaka miwili iliyopita ilitakiwa kugeuza matokeo ya kipigo cha mabao 2-0 ilichopata Morocco wiki moja iliyopita kwa kupata ushindi mnono wa kuanzia mabao 3-0, lakini ndoto zilizimwa na mchezo wa maarifa, ufundi, jitihada na malengo ulioonyeshwa na RS Berkane.
Miaka miwili iliyopita, Yanga ilishindwa kutwaa ubingwa huo mbele ya USM Alger ya Algeria baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 nyumbani na baadaye kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini ambao haukutosha kubadili matokeo.
Lakini, hapa nyumbani tulishukuru kwa matokeo hayo kwa kuwa kwanza Yanga ilifika fainali, pili ilipoteza mbele ya timu kutoka mataifa ya Kaskazini ambayo yako mbele kisoka na tatu timu ilijitahidi kwa angalau kushinda ugenini; kwamba ilichokosa ni bao la pili tu ambalo lingeipa ubingwa, lakini bahati haikuwa yake.

Shukrani hizo kwa Mwenyezi Mungu tumezitoa tena msimu huu baada ya Simba kushindwa kutwaa ubingwa huo. Kwamba timu ilicheza vizuri mechi ya marudiano iliyofanyika Uwanja wa Amaan jijini Unguja, kwamba bao ambalo lingeongeza morali kwa wachezaji lilikataliwa na mwamuzi, kwamba isingekuwa kadi nyekundu kwa Yusuf Kagoma timu ingeweza kutwaa ubingwa na kwamba refa aliipendelea RS Berkane kwa kuwa mmiliki wake ni makamu wa rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Na wote tunaungana kujifariji kwamba refa aliyekataa bao la Yanga katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, Dahane Beida, ndiye aliyechezesha mechi ya Simba na Berkane na kuwa chanzo cha kukosa ubingwa.
Ni sahihi kujifariji kwa hayo yote? Kwangu mimi siyo sahihi. Kufika fainali ni hatua kubwa, lakini hatuwezi kujifariji kwamba tulikosa ubingwa kwa kuwa ni mara ya kwanza, la hasha! Timu ikifika fainali ina nafasi sawa ya kutwaa ubingwa hata kama fainali hiyo ni dhidi ya Barcelona.

Lakini tunashindwa nini? Labda tuangalie fainali ya wiki iliyopita baina ya Simba na RS Berkane. Sitaki kuzungumzia sana uwanjani, bali mienendo ya viongozi, mashabiki na watendaji wakati wa kuelekea mechi hiyo.
Inaonekana RS Berkane walikuwa wanaiwaza zaidi mechi hiyo kimaandalizi kuliko Simba. Inaonekana walishatuma watu wao Tanzania hata kabla ya mechi ya kwanza. Walikuwa hapa kusubiri uthibitisho wa uwanja ambao ungetumika. Baada tu ya kutaarifiwa Mei 14 kuwa itafanyika Zanzibar, mara moja wakapanga hoteli ambayo timu ingefikia.
Wakati Brazil wanaelekea kutwaa ubingwa mwaka 1994, kocha Carlos Alberto Pereira ndiye aliyekuwa na falsafa hiyo. Kwamba hapendi kuona wachezaji wake wakizubaa sehemu ya mapokezi wanapofika hotelini. Alituma watu mapema kuandaa hoteli na vyumba, kiasi kwamba timu inapowasili kutoka mji mmoja, wachezaji wanatumia dakika chache sana mapokezi na kupata muda mwingi wa kupumzika vyumbani.

Kwa hiyo suala la malazi kwake ni kubwa ingawa linaonekana kama dogo. Huku Simba walikuwa wanahangaika kuujaza uwanja wa Benjamin Mkapa bila ya hata kuwasiliana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), CAF na serikali kujua hatima ya uwanja huo baada ya kufungiwa kutokana na kujaa maji nyakati za mvua.
Na kibaya zaidi ni kwamba uamuzi wa kuufungia ulitokana na hali iliyoonekana wakati Simba yenyewe ikicheza na Al Masry mchezo wa robo fainali, wakati wafanyakazi wa uwanja walipolazimika kufagia maji yatoke eneo la kuchbezea, lakini bila ya ufanisi.
Kitendo cha kuigeuzi kibao CAF kuwa imeifanyia hujumu kwa kupeleka mchezo Uwanja wa Amaan mjini Unguja, kilitakiwa kitanguliwe na utafiti kujua ukweli halisi kabla ya kuanza kutafuta huruma kwa mashabiki.
Wakati wanatakiwa kufanya maandalizi, viongozi walijikita zaidi katika suala la uwanja, hadi kwenda kutembelea na kupiga picha kuonyesha nyasi ziko katika hali nzuri, wakati tatizo lilikuwa ni miundombinu ya kutoa maji uwanjani kwa haraka iwapo mechi inachezwa nyakati za mvua. Kwa hiyo akili ya viongozi iliondoka relini na tatizo hilo likahamishiwa kwa mashabiki n ahata wachezaji.

Kitendo cha kuituhumu CAF kuwa iliwasiliana na RS Berkane kwanza kabla ya Simba, nacho kilitakiwa kitanguliwe na utafiti kujua ukweli halisi, Na hata ilipogundulika kuwa shutuma hazikuwa sahihi, ilikuwa busara kurudi hadharani na kuomba radhi na kueleza tatizo lilikuwa wapi. Viongozi walizidi kuwatoa mchezoni mashabiki na wachezaji.
Wakati wote huo RS Berkane walijitenga na malumbanio yoyoye yale. Akili yao ilikuwa kwenye mechi mbili za fainali.
Tuhuma na shutuma dhidi ya CAF ziliendelea hadi siku ya mchezo, kuonyesha kuwa RS Berkane ingependelewa kwa kuwa inamilikiwa na mtu ambaye ni makamu wa rais wa CAF. Siku zote hisia za uwezekano wa upendeleo zinaweza kupandisha morali kwa wachezaji (kwamba wapambane dhidi ya timu inayobebwa) au kushusha morali, kwamba hata wafanyeje, hawataweza kufanikiwa.

Viongozi na watendaji walijikita kuonyesha kwamba kuna uwezekano wa wageni kupendelewa. RS Berkane walikaa kimya.
Uwanjani, Simba iliyocheza mjini Berkane ndiyo ileile iliyocheza Amaan, pamoja na kuwepo kwa mabadiliko ya wachezaji wachache kutokana na majeraha na uamuzi wa kocha.
Lakini kimbinu, haikuwa tofauti. Yaani haikuficha makali yake ilipocheza Berkane na hivyo ilimaliza kila kitu. Ungetegemea timu itumie wachezaji wengi wenye uwezo wa kuzuia katika mechi ya kwanza ili kuzuia wenyeji kutengeneza ushindi nyumbani kwao, lakini ilienda na timu isiyo ya kimkakati.
Ufundi wao wote uliishia Morocco na hivyo RS Berkane ilikuja Amaan ikiijua vizuri Simba wakati inashambulia na inapojilinda. Huku ni kukosa uzoefu wa mechi za mtoano. Ilifanya hivyo katika mechi za mechi za Shirikisho dhidi ya Orlando Pirates ilipotolewa robo fainali. Ilicheza kwa kushambulia nchini Afrika Kusini, ikaishia kuchapwa mabao 4-0 na ushindi wa mabao 3-0 nyumbani haukutosha kubadili matokeo.
Kwa timu ambayo inapambana kubadili matokeo ya kipigo cha mabao 2-0, nidhamu binafsi ya mchezo kwa wachezaji ni kitu muhimu kuliko vyote. Ungetegemea timu inayojilinda ndio ipoteze mchezaji kwa kadi nyekundu, lakini Simba ndio wakampoteza Kagoma wakati wakihitaji ushindi kwa udi na uvumba.
Tena baada ya refa kumuonya Kagoma kwamba akirudia kucheza rafu, angepata kadi ya pili ya njano na hivyo kutolewa. Hakukuwa na sababu ya kulala ili audokoe mpira kutoka kwa mchezaji wa RS Berkane ambaye ndio kwanza alikuwa duara la katikati. Na mchezaji alimuona Kagoma kuwa angelala na hivyo akatanguliza mguu wa kushoto ili auguse na kuwa faulo ambayo ilimtoa nje.
Wakati Vinicius anazozana na refa katika mechi za michuano ya Amerika Kusini, Raphinha alimfuata kumkemea kuwa kitendo chake kinaweza kusababisha aonyeshwe kadi na hivyo kuikosa mechi dhidi ya Argentina. Nahodha wa Simba hakuona kuwa mchezo wa matumizi ya nguvu wa Kagoma ungeiathiri Simba?
Kitendo cha Simba kupiga shuti moja lililolenga lango katika mechi ya marudiano, kinaonyesha ama wachezaji hawakutekeleza kile walichofundishwa na kocha wao, ama Fadlu Davids hakujikita katika kunoa makali ya ushambuliaji kwa ajili ya mechi ya marudiano. Ndiyo maana nimesema hapo awali kuwa Simba iliyocheza Morocco ndiyo iliyocheza Zanzibar.
Kocha Moine Chaaban wa RS Berkane aliajiriwa tangu Februari 12, 2024 kuchukua nafasi ya Amine El Karma, hivyo kuna uwezekano mkubwa kuwa alishauri viongozi wachezaji ambao angetaka waongezwe au ambao asingetaka waruhusiwe kuondoka.
Ameiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Morocco na kutwaa Kombe la Shirikisho.
Fadlu Davids aliajiriwa Julai mwaka jana kipindi ambacho viongozi walikuwa wakisaka wachezaji. Kwa hiyo ameajiriwa sambamba na wachezaji wengi wa Simba. Alihitaji muda kuijua vizuri timu, utamaduni wake na mpira wa Tanzania.
Si ajabu kwa kocha wa Simba au Yanga kuiongoza timu kuwa katika nafasi mbili za juu hata awe mbovu. Hata kufika fainali ya Shirikisho mwaka huu hakuwezi kushawishi wengi kuwa kumetokana na uwezo wake, hasa ikizingatiwa kuwa ugumu wa mashindano umepungua baada ya timu zilizokuwa zinaingia hatua za mwisho za mashindano hayo kutoka Ligi ya Mabingwa, kuondolewa.
Si nia yangu kusema kuwa Davids si kocha mzuri, bali kuonyesha kuwa tabia za kibingwa za klabu huonekana hata katika kuajiri makocha. Kuajiri makocha sambamba na usajili ni kutozingatia utaalamu wake.
Leo Real Madrid wameshamtambulisha Alonso kama kocha mpya, lakini walishaingia naye makubaliano mapema na akawadokeza wachezaji ambao angewataka na wale ambao asingependa waondoke.
Kwa kulinganisha uundwaji wa benchi la ufundi la RS Berkane na Simba unaona kabisa kuwa Wamorocco walijiandaa kibingwa zaidi ya wenyeji.
Yako mambo mengi ya kuangalia, lakini hakuna sababu ya kuendelea kulalamikia mamlaka kutokana na kutotwaa ubingwa. Kwa sasa tunaweza kusajili wachezaji wa viwango vya juu Afrika na hata makocha bora, lakini tunashindwa kupata mafanikio. Kwa hiyo ni muhimu sasa kuanza kujiangalia tunafanya nini katika maandalizi yetu. Je tunajiandaa kibingwa?