Prime
SIKU 197 ZA BARKER: Alivyotafuna mfupa mgumu Simba uliowashinda makocha saba
Muktasari:
- Lakini sasa, Kocha raia wa Afrika Kusini, Steve Barker ameanza kuandika ukurasa mzuri Msimbazi kwa kufanya kile ambacho makocha saba waliomtangulia walishindwa kukifanya.
KWA takribani misimu mitano, benchi la ufundi la Simba limekuwa kama kiti cha moto. Makocha walikuja na kuondoka mmoja baada ya mwingine wakiahidi kuirejesha timu katika kilele cha mafanikio, lakini wote walishindwa kuvunja utawala wa Yanga kwenye mashindano ya ndani.
Lakini sasa, Kocha raia wa Afrika Kusini, Steve Barker ameanza kuandika ukurasa mzuri Msimbazi kwa kufanya kile ambacho makocha saba waliomtangulia walishindwa kukifanya.
Baada ya kutua Simba Desemba 19, 2025, Barker amemaliza msimu wake wa kwanza siku chache zilizopita kwa kuipa Simba Kombe la Shirikisho la CRDB, baada ya kuifunga Azam mabao 1-0 kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa Gombani, Pemba, Julai 4, 2026. Hicho ni kipindi cha siku 197 tangu kuteuliwa hadi kushinda kombe.
Mafanikio hayo yamemfanya kuwa kocha wa kwanza tangu Mfaransa, Didier Gomes Da Rosa mwaka 2021 kuipa Simba taji la mashindano hayo huku pia Barker akishinda Kombe la Muungano ambalo alitwaa Aprili 2026 baada ya kuichapa Yanga bao 1-0, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, ikiwa ni sehemu ya kukisuka upya kikosi hicho.
Ushindi huo una maana ni ishara Simba imeanza kurejesha utambulisho wake wa ushindani baada ya kupitia kipindi kigumu ambacho Yanga imetawala soka la Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitano mfululizo.
Gomes ndiye aliyekuwa kocha wa mwisho kuipa Simba Kombe la FA (sasa CRDB Federation Cup) Julai 25, 2021, timu hiyo ilipoifunga Yanga bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, bao pekee likifungwa na kiungo Taddeo Lwanga.
Msimu huo Gomes pia aliiongoza Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mafanikio yaliyomfanya kuwa mmoja wa makocha bora kuwahi kuinoa klabu hiyo.
Baada ya Gomes kuondoka Oktoba 2021, Simba iliingia kwenye mzunguko wa kubadilisha makocha bila kupata mafanikio yaliyotarajiwa.
Aliyekuja kwanza alikuwa Pablo Franco raia wa Hispania, ambaye alikaa siku 204, akaondoka bila kombe. Nafasi yake ikachukuliwa na Zoran Manojlovic ambaye alidumu siku 67 pekee kabla ya kuondoka mikono mitupu.
Kisha akafuata Mbrazili, Roberto Oliveira 'Robertinho', aliyedumu siku 310, alishinda Ngao ya Jamii mwaka 2023, akaondoka baadaye.
Alikuja Mualgeria, Abdelhak Benchikha, naye akakaa siku 149 kabla ya kuachia ngazi akishinda Kombe la Muungano pekee, ndipo Mhispania Dani Cadena akawa kocha wa mpito kwa siku 28.
Msimu wa 2024-2025 Simba ilimkabidhi timu kocha raia wa Afrika Kusini, Fadlu Davids, ambaye alikaa siku 443. Ingawa aliifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huo, hakufanikiwa kuiangusha Yanga katika harakati za kushinda mataji ya ndani.
Baada ya kuondoka kwa Fadlu, Simba ilimteua Dimitar Pantev raia wa Bulgaria aliyedumu kwa muda mfupi wa siku 73.
Hapo ndipo Barker alipopewa jukumu la kuanza upya safari ya kuijenga Simba huku akiingia katikati ya msimu.
Alikabidhiwa timu iliyokuwa imepoteza imani ya mashabiki kutokana na miaka minne mfululizo bila ubingwa wa Ligi Kuu na bila kufika hata fainali ya Kombe la FA tangu 2021.
Hiyo ndiyo sababu viongozi wa Simba walimuona Barker kama mtu sahihi kutokana na kazi kubwa aliyofanya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini kabla ya kuhamia Tanzania.
Tofauti na waliomtangulia, Barker hakuhitaji muda mrefu kuonyesha mabadiliko.
Aliijenga Simba yenye nidhamu ya ulinzi, uwezo mkubwa wa kudhibiti mchezo na ari ya kupambana hadi dakika ya mwisho.
Matokeo yake yakawa kuikalia Yanga kooni hadi kutangaza ubingwa siku ya mwisho ya msimu kwa tofauti ya pointi mbili huku Simba ikitwaa Kombe la CRDB na kurejesha matumaini ya mashabiki kuwa klabu hiyo inaweza tena kutawala soka la Tanzania.
Ubingwa huo pia unamfanya Barker kuwa kocha wa kwanza baada ya miaka mitano kuipa Simba kombe kubwa la ndani jambo ambalo linaweza kuwa mwanzo wa safari ya kurejesha enzi za mafanikio za Wekundu wa Msimbazi.
MSIKIE BARKER ANACHOSEMA
Ndani ya siku 197 alizokaa Simba tangu ateuliwe Desemba 19, 2025 hadi aliposhinda Kombe la CRDB Julai 4, 2026, Steve Barker anaamini safari ya mafanikio ya timu hiyo ndiyo kwanza imeanza.
Kocha huyo amesema kutwaa Kombe la CRDB na Muungano ni hatua ya kwanza tu katika mchakato wa kuijenga Simba yenye uwezo wa kutawala soka la Tanzania na kufanya vizuri katika mashindano ya Afrika.
Barker amesema benchi la ufundi kwa kushirikiana na uongozi wa klabu tayari limeanza kupanga maboresho ya kikosi kwa ajili ya msimu ujao ili kuongeza ushindani katika maeneo mbalimbali.
"Mwanzo wetu msimu uliopita haukuwa mzuri. Tulikubaliana kwamba tulihitaji kujijenga upya, hivyo hatukujiwekea presha kubwa kwenye mashindano ya kimataifa. Kitu muhimu kilikuwa ni kujenga timu yenye msingi imara na kulinda heshima ya Simba," amesema na kuongeza;
"Ninaamini msimu ujao watu wataiona Simba halisi. Tutakuwa na maandalizi bora zaidi, tutajiongeza katika maeneo muhimu na malengo yetu ni kupambana katika kila mashindano tutakayoshiriki."
Majukumu makubwa yanayomsubiri Barker ni kuirejeshea Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara uliotwaliwa na Yanga kwa misimu mitano mfululizo, sambamba na kuifikisha mbali timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
REKODI INAYOTISHA
Takwimu zinaonyesha Barker ameijenga Simba yenye ushindani mkubwa kwenye mashindano ya ndani.
Katika Ligi Kuu Bara ameiongoza Simba kwenye mechi 25, akishinda 18 na kutoka sare saba, hajapoteza hata mchezo mmoja. Hiyo ina maana ya asilimia 72 ya ushindi na asilimia 100 ya kutopoteza mechi yoyote katika ligi akiwa kocha.
Kwa upande wa Kombe la CRDB, Barker alionyesha kuwa ni moto wa kuotea mbali. Simba imeshinda mechi zote sita ilizocheza na kutwaa ubingwa ikiwa na rekodi ya asilimia 100 ya ushindi.
Rekodi hiyo imeongeza imani kwa mashabiki kwamba kocha huyo anaweza kuwa mtu wa kuirudisha Simba kwenye mafanikio makubwa ya ndani na kimataifa.
WADAU WAMPA SIFA
Nyota wa zamani wa Mbeya Kwanza, Boniface Nyagawa; alisema: "Kwa kazi aliyoifanya Barker ndani ya muda mfupi, naamini anastahili kuwania tuzo ya Kocha Bora wa Msimu. Ameikuta Simba ikiwa katika kipindi cha mpito, lakini ameijenga na kushindania ubingwa wa ligi na mwishowe wamechukua Kombe la CRDB."
Kwa upande wake kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, bdallah 'King' Kibadeni alisema: "Barker ameonyesha utulivu na uwezo mkubwa wa kusimamia timu. Kwa mafanikio aliyoyapata ndani ya miezi michache, anastahili kutambuliwa kama mmoja wa makocha bora wa msimu. Kama atapewa usajili anaouhitaji, msimu ujao unaweza kuwa mzuri zaidi kwa Simba."