Sarpong: Tulieni nimejipanga, narudisha ubora
Moja ya mchezaji mwenye jina kubwa aliyetarajiwa kufanya makubwa ndani ya Yanga hutaacha kumtaja mshambuliaji Michael Sarpong,ambaye Yanga waliamini anakuja kurudisha ufanisi wa safu yao ya ushambuliaji katika kufunga.
Hata hivyo matarajio hayo na kasi aliyoanza nayo bado haijaweza kukata kiu ya mashabiki wa Yanga na Mwanaspoti likaamua kumtafuta na kuzungumza naye ili kuweza kujua mambo mbalimbali.
Maisha ndani ya Yanga yakoje?
Sarpong anaanza kuelezea maisha yake yalivyo tangu afike ndani ya Yanga akisema anaishi maisha mazuri sio tu Yanga bali hapa Tanzania ambako ni kama sehemu ya pili ya nyumbani kwake
“Maisha ndani ya Yanga ni mazuri,nafurahia kuwa katika klabu hii kubwa na niseme hapa Tanzania ni kama sehemu ya pili ya nyumbani kwangu kila kitu kwangu nakiona kama nipo nyumbani kwetu Ghana,hakuna matatizo kabisa kwangu kwa kuishi hapa,”alisema Sarpong.
Hatua ya mapokezi yake ilikuaje
“Niseme ukweli mapokezi yangu wakati nafika hapa yalinishtua sana sikutegemea kupata mapokezi kama yale,lilikuwa tukio la kusisimua sana ambalo mashabiki wanaonyesha ni jinsi gani wana imani na wewe na walikuwa wanakusubiri.
“Ile hali pekee ilikuwa ni ujumbe tosha kwamba natakiwa kufanya kazi kwa nguvu hapa kwa kuwa wako watu maelfu nyuma wanatarajia makubwa kutoka kwako,mashabiki wa hapa hasa Yanga ni watu wa pekee sana hata kule kwetu Ghana walipoona walichanganyikiwa sana na wengine wakatamani hata niwapelekee jezi za klabu hii.
Nafasi gani anacheza vyema uwanjani?
“Mimi ni mshambuliaji nikisema hivi namaanisha nacheza namba tisa hapo ndio naweza kufunga,hii ndio nafasi ambayo naweza kucheza vizuri lakini pia kuna wakati naweza kucheza kama mshambuliaji wa nyuma ya mshambuliaji wa mwisho,huwa nafurahia sana nikicheza kama namba tisa hapo ndio naweza kufanya kazi yangu vyema.
Mabao 4 mechi 17 ikoje hii?
“Hali ilivyo iko nje ya mipango ambayo niliiweka wakati nafika hapa lakini sikata tamaa kuna wakati kwenye mpira kitu kama hiki kinatokea kuchelewa kuonyesha ubora wako halisi, huu ni mwaka wangu wa kwanza napambana niweze kuzoea mazingira kwa haraka ili niweze kufanya vizuri zaidi.
“Mimi ni mchezaji ambaye najiamini na naamini uwezo wangu,naamini maisha yatabadilika haraka na nitarejea katika ubora wangu wa kufunga zaidi,mashabiki wasiwe na wasiwasi na mimi watafurahia kazi yangu na uwepo wangu hapa.
“Kwasasa nimekuwa na ratiba ngumu sana ya kurudisha uwezo wangu,nafanya mazoezi zaidi ya nilichokuwa nafanya hapo kabla kuna programu nazifanya naamini wakati wowote ligi ikiendelea mtamuona Sarpong halisi akiwa Yanga.
Kipi kimemkwamisha katika ufungaji?
“Sioni hasa kipi kimenikwamisha lakini ukiniuliza swali hilo jibu langu naliona ni suala la muda tu kama nilivyosema inawezekana nimechelewa kuzoea mazingira ya hapa.
Nikweli yuko kwenye presha ya kutokufunga?
“Hapana sina presha kabisa niko sawa,kawaida huwa siruhusu maisha yangu kuingiwa na presha kabisa kama nakutana na changamoto hatua nzuri ni kujipanga na kuhakikisha mambo yanabadilika haraka ili maisha yaendelee wala sijaumizwa.
sana ingawa natamani kufanya vizuri zaidi kama binadamu mwingine mwenye malengo yote kwa yote nasema mambo yatabadilika haraka.
Tofauti ya ligi ya Rwanda vs Tanzania
Kabla ya kuja Yanga Sarpong alikuwa mchezaji wa APR ya Rwanda ambako alifanya mambo makubwa huko katika ufungaji na hapa anaeleza utofauti wa soka la nchi hizo mbili
“Kuna tofauti ipo naiona,Hapa Tanzania ligi ni ngumu sana wachezaji wanatumia sana nguvu uwanjani lakini pia wanatumia ufundi baadhi yao lakini Rwanda ni tofauti sawa wapo wanaotumia nguvu lakini sio sana kule wanapenda sana kutumia wachezaji wenye ufundi zaidi.
Jinsi anavyokabiliana na mabeki wa ligi
“Hakuna beki ambaye anapenda kumruhusu mshambuliaji afunge kirahisi,siku zote mabeki wa hapa wamekuwa wakicheza au wakinikaba kwa kutumia nguvu kubwa,kuna wakati wapo ambao wananichezea vibaya wapo wengine wanakutukana kwa matusi lakini nafahamu hizo ni mbinu ninachotakiwa ni kuwajibu kwa kufunga tu
Marefa anawaonaje?
“Kinachoniumiza kwa waamuzi wengi wamekuwa hawachukui hatua ya kuwaadhibu wanaocheza vibaya unaona kabisa mwamuzi ameona tukio husika lakini anasita kuchukua hatua,zipo penalti za wazi na hata adhabu ndogo lakini waamuzi wamekuwa wakiacha,sio kitu kizuri sana unachokitegemea kukiona kwa mwamuzi anayechezesha ligi hapa lakini ndio mpira mapambano yanaendelea hakuna kukata tamaa.
Tukio la kusakwa na Polisi Rwanda ilikuaje?
Wiki chache kabla ya kutua nchini kuja kusaini Yanga Sarpong alikumbana na mkasa wa kusakwa na jeshi la Polisi la nchini Rwanda hatua ambayo ilitishia kuchelewa kwa usajili wake hapa anaeleza tukio zima.
“(Anacheka, najiuliza umejuaje hii?)Ni hivi nakumbuka ilikuwa wakati wa maambukizi ya ugonjwa wa Covid 19 sasa pale Rwanda kila mtu alitakiwa kukaa ndani kwako na hakuna kuzurula sasa ilifika siku ya kukumbuka siku yangu ya kuzaliwa na niliwalika marafiki zangu wa karibu sana kuja kwangu na tulichukua tahadhari zote ikiwemo kutosogeleana sana pamoja na kuvaa barakoa.
“Hayakuwa ni maisha ambayo tuiliyazoea sasa kuna wakati nilivua kwa muda barakoa na kuna picha tulipiga zikasambaa,zile ndio zilileta shida na nikaonekana nimepuuza zile tahadhari sasa polisi wakawa wananitafuta kwa kutaka kuniweka ndani lakini nashukuru viongozi wa timu yangu walilimaliza haraka kabla ya mambo hayajaharibika.”
Usajili wa Simba ulikwama wapi?
Kabla ya Sarpong kutua Yanga mapema taarifa zilizagaa kwamba Simba na Azam zilikuwa zinamtafuta kwa nia ya kusajili hapa anaeleza mambo yalivyobadilika.
“Nikweli Simba walinitafuta sana na kuna wakati niliamini naweza kwenda kule pia hata Azam nao walinitafuta lakini mambo yalibadilika unajua mazungumzo yote niliamua yafanyike chini ya usimamizi wa meneja wangu,sikuwa najua Simba walikwama wapi lakini meneja wangu alinifuata na kunaimbia kwamba kuna timu ya Yanga wamekuja nao na wako haraka sana kumaliza dili na nilikubali kwa kuwa nayo ilikuwa ni timu nzuri na klabu kubwa hapa Afrika.
Mbio za ligi anazionaje?
“Ligi ni ngumu hapa kila mechi huwa na ugumu wake hakuna mechu ambayo ni rahisi hata ile mnayoshinda nayo huw na ugumu wake,Yanga tuna malengo yetu kama timu tunataka kuchukua ubingwa na hii ndio silaha kubwa ambayo imetufanya kuwa imara na kupambana kwa kila mchezo ulio mbele yetu.
Anakionaje kikosi chao?
“Tuna timu imara sana yenye wachezaji bora lakini pia tuna makocha wazuri wanaojua kutengeneza umoja,hii ni familia wachezaji tunashirikiana na kuhamasishana wakati wote,kama nilivyosema malengo yetu ni kuchukua makombe sasa tumerejea baada ya mapumziko na ndio maana tunatakja kujipanga vizuri zaidi ili ligi ikiendelea tuendelee na ubora wetu.
“Hapa presha tunayoipata ni kama timu na sio mchezaji mmoja mmoja hatujapoteza mechi na kila timu tutakayocheza nayo haitaki kuona rekodi hiyo kwahiyo tunategemea ugumu lakini kwa kikosi tulichinacho tunaweza kushinda changamoto hizi.
Yanga inaweza kuchukua makombe?
“Hilo linawezekana kabisa kama hali hii ya ushindani tutaiendeleza,wapinzani wetu Simba na Azam tnawapa heshima kwa ubora walionao lakini sisi tunahesabu zetu kama Yanga na malengo yetu kwa hamasa tuliyonayo tunaweza kufikia malengo yetu.
Viungo wachezeshaji Yanga anawaonaje?
“Hapa kuna viungo bora wanaojua kutengeneza nafasi hili haliwezi kuwa jukumu la mtu mmoja pekee,angalia wachezaji kama Fei Toto(Feisal Salum), Saido (Said Ntibazonkiza),Tuisila (Kisinda),Farid (Mussa),Kaseke (Deuse) na hata Yacouba (Sogne) unapowaona uwanjani wakati wowote wanaweza kutengeneza kitu bora.
Nikweli alitaka kuondoka?
“Huwezi kuzuia uvumi kila sehemu kuna uvumi lakini jambo zuri ni kujikita katika kile kinachotokea na kuonekana kimetokea,mimi bado nipo hapa Yanga na nina mkataba wa miaka miwili na hii klabu kubwa,hayo mengine siyapi nafasi kwangu.”
Maisha na mashabiki wa Yanga mitaani
“Huwa nafurahia ninapotembea au kuonekana katika maeneo mbalimbali,unaona jinsi mtu anavyofurahi kukuona,kuna kitu cha kujifunza hapa kuwa mashabiki wa hapa ni watu wenye upendo sana na wachezaji sio rahisi kuona unafanyiwa kitu kibaya unapokutana na mtu.
Jamaa anataa kufungua taasisi yake
“Akiwa kwao Ghana katika mapumziko ya hivi karibuni Sarpong alionekana akitoa misaada katika kituo cha watoto wenye uhitaji na hapa anaelezea hatua hiyo.
“Nitafungua taasisi yangu muda sio mrefu sana kule nyumbani Ghana,unajua katika maisha unachokipata kuja wakati lazima ukumbuke kuna wengine hawajapewa na unatakiwa pia uwape kama ambavyo Mungu amekujalia wewe kupata nina ndoto hizo za kuendelea kusaidia zaidi wale wanaohitaji msaada hatujui kesho yetu.
Humwambii kitu kwa Farid Mussa
Kila mtu anapenda kuwa rafiki yake katika maisha yake na Sarpong anamuibua rafiki yake kuwa ni Farid Mussa;”Rafiki yangu mkubwa hapa Yanga ni Farid (Mussa),tumejikuta tunakuwa karibu na kushibana huwa ndio mtu ambaye napenda kukaa nayer muda mrefu ukiniuliza kipi kilitokea mpaka ikawa hivyo hata sijui lakini napenda ushirikiano wake kwangu.