Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Senzo anavyowaanzishia safari ya uhakika Yanga

ZIMEKUWA ni wiki mbili za klabu kubwa hapa Tanzania kwa kuonyesha makubwa katika medani ya soka wakifanya matukio tofauti ya kimaendeleo kila moja ikiwa na jambo lake ambalo imelifanya katika macho ya umma.

Simba walitangulia kuibuka na mashindano mafupi ya klabu tatu Afrika wakiyaita Simba Super Cup yaliyomalizika mwisho wa wiki iliyopita na kuwa na taswira nzuri ya ukuaji wa klabu hiyo kongwe.

Yanga nao wakajibu juzi walipoibua na siku ya vyombo vya habari wakialiaka vyombo vyote katika kambi yao ya Avic iliyopo Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kuwa na shughuli mbalimbali kuhusu klabu yao.

Nilikuwa mmoja wa waliohudhuria siku hii na nilivutiwa na jinsi ya mpangilio wa matukio ya shughuli ilivyoendeshwa - ilikata kiu ya kujua jinsi timu ya wanawake, Yanga Princess inavyoandaliwa, hali kadhalika timu zao za vijana tulipata nafasi ya kuzishuhudia. Tuliona maendeleo ya timu yao kubwa inayoongoza Ligi Kuu Bara.

Matukio hayo hayakuishia hapo wadhamini wao wote nao walikuwa sehemu ya shughuli hiyo wakiwa pamoja na viongozi wa klabu kila mmoja akieleza jinsi anavyoshirikiana na mwenzake, lakini kila taarifa ambayo mwanahabari aliihitaji kutoka kwa yeyote hakuna ambaye alishindwa kutoa ufafanuzi wa lolote.

Wakati flani nikiwa katikati ya matukio hayo nilianza kupata shida ya kutambua akili ya namna hii Yanga wametoka nayo wapi wakija na kitu cha tofauti, na baadaye nikagundua kwamba kuna mtu ambaye wamemuingiza ndani ameanza kuonyesha thamani ya ubongo wake, huyu ni Senzo Mazingisa na akili yangu ikapata uhakika alipotamka Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said kuwa hiyo ni akili kubwa ya raia huyu wa Afrika Kusini.

Senzo ameonyesha ameishi katika mpira na katika klabu kubwa akiwa na uzoefu wa kutosha wa kuhakikisha taasisi kama Yanga ambayo licha ya umri wake mrefu na ikiwa nyuma kimaendeleo inabadilika na kuanza kuishi kama klabu kubwa zilizopiga hatua kubwa duniani. Tukio hili limeifanya Yanga kujijengea heshima ya kujua kuitangaza klabu yao na kuipa hadhi kama klabu kubwa kwa kuhakikisha maisha wanayoishi hayawi kitu cha siri kama ambavyo tulizoea ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Senzo kupitia tukio hilo linaweza kuwavutia wawekezaji zaidi hususan wadhamini mbalimbali wakiona jinsi klabu hiyo inaweza kuwapa thamani katika kupata upana wa kutambulika katika jamii hasa wakitumia muunganiko wao mzuri na wanahabari.

Tukio kama hili pekee Yanga wanaweza kulitumia kwa faida kwa kumuonyesha mdhamini kisha kwa haraka akaingia nao mkataba akiridhika kwamba kuna viongozi wana fikra za maendeleo na kwamba wanaweza kufanya nao kazi.

Hatua ya pili inaweza kuwa sehemu ya kuwabadilisha wachezaji akili zao na kuacha tabia ya kuviona vyombo vya habari kama watu hatarishi kwao - kwa jinsi walivyotolewa woga na kuongea kwa uhuru hali ambayo imekuwa ni ngumu kwao kufanya miaka ya nyuma.

Kupitia tukio hili naanza kuona Yanga wakianza kuonja utamu wa kuwa na mtu kama Senzo katika kuongoza klabu yao na kwa matukio haya endapo watazidisha utulivu wa usikivu kwake, Yanga inaweza kubadilika kwa haraka zaidi na kujikuta wanavuna mengi kutoka akili yake.

Kinachofuata sasa ni kwamba wadau wanatamani kuona mafanikio zaidi ya kiushindani wa kutanua mfuko wa mapato kwa klabu kama hii ambayo miaka michache iliyopita ilikuwa inanuka hali mbaya ya ukapa kiasi cha wanachama na mashabiki kuamua kuichangia ili kukamilika hata kwa safari yao ya kufika kucheza mechi za ligi.

Matukio kama haya yatatanua zaidi fursa za mapato lakini pia yatasaidia kuiweka Yanga katika thamani ya kutambulika na kuheshimika kwa klabu zingine, kisha baadaye kuja kuvuna matunda zaidi ya kazi hii kupitia matukio kama haya. Tuendelee kufuatilia akili ya Senzo pale Yanga taratibu mpaka mwisho wa mkataba wake.