Wameanza vyema VPL, wakazingua
BAADA ya kusimama kwa kipindi kirefu, Ligi Kuu Bara (VPL) itaendelea Februari 4 kwa uwepo wa mechi mbili za viporo zitakazokutanisha timu za Dodoma Jiji dhidi ya Simba na Namungo dhidi ya KMC.
Hadi wakati inasimama, mzunguko wa pili ulikuwa umeanza na kila timu ilicheza mechi moja ya raundi ya pili kati ya 17 ambazo kila moja itacheza katika mzunguko huo.
Katika mzunguko wa kwanza, wapo wachezaji ambao walianza vyema kwa kuonyesha viwango bora, lakini ghafla viwango vyao vikatetereka hadi kujikuta wakishindwa kile walichokianza mwanzoni na baadhi yao wakapoteza nafasi katika vikosi vya kwanza vya timu yao.
Bila shaka wachezaji hao watakuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kurudisha imani ya makocha kwao kama ilivyokuwa mwanzoni kwa kucheza vyema.
Makala hii inakuletea orodha ya wachezaji ambao walianza vyema msimu huu, lakini ndani ya muda mfupi wamejikuta wakishindwa kuonyesha kile ambacho walianza nacho.
Michael Sarpong - Yanga
Katika mchezo wa kwanza tu wa Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Michael Sarpong wa Yanga aliyesajiliwa kutokea Rayon Sports aliifungia timu hiyo bao katika sare ya bao 1-1.
Baada ya hapo aliendelea kuanza kikosi cha kwanza cha Yanga ingawa alikuja kupoteza imani ya makocha wake kutokana na udhaifu wake wa kukosa idadi kubwa ya mabao pindi akiwa ndani ya eneo la hatari la adui.
Kwa sasa hana uhakika wa kucheza katika kikosi cha kwanza cha Yanga na ilikuwa nusura atupiwe virago na timu hiyo katika dirisha dogo la usajili ingawa ameifungia mabao manne.
Hassan Dilunga - Simba
Alikuwa kipenzi cha kocha Sven Vandenbroeck ambaye mwanzoni mwa msimu huu alimpatia nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na uhodari wa kiungo huyo mshambuliaji wa kuchezesha timu, kupiga pasi za mwisho na hata kufunga mabao.
Katika mechi za hivi karibuni, nafasi ya Dilunga kwenye kikosi cha kwanza cha Simba imekuwa finyu akishindwa kucheza mbele ya Clatous Chama na Luis Miquissone.
Kennedy Wilson - Simba
Aliumaliza vyema msimu uliopita kwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara na pia mechi za mwanzoni mwa msimu huu, alikuwa akianza katika nafasi ya beki wa kati, akichezeshwa sambamba na Joash Onyango.
Ghafla mambo yamemuendea kombo na amejikuta akisotea benchi ama kutazama idadi kubwa ya mechi akiwa jukwaani huku nafasi yake wakicheza kina Onyango, Pascal Wawa, Erasto Nyoni na Ibrahim Ame.
Ditram Nchimbi - Yanga
Juhudi na nidhamu yake ya kutimiza vyema majukumu anayopewa na benchi la ufundi vilimfanya Nchimbi awe na nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha Yanga.
Hata hivyo, mambo yamekwenda tofauti katika siku za hivi karibuni ambapo mshambuliaji huyo amekuwa hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara akionekana kushindwa kuhimili ushindani wa namba dhidi ya wachezaji kama Saido Ntibazonkiza, Farid Musa, Songne Yacouba na Deus Kaseke.
David Kissu - Azam FC
Alianza vizuri ndani ya kikosi cha Azam baada ya kusajiliwa akitokea Gor Mahia ambapo aliweka rekodi ya kucheza mechi nne mfululizo za mwanzo za Ligi Kuu bila kuruhusu bao jambo ambalo lilichangia pia kumpatia fursa ya kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars.
Lakini upepo umeonekana kumbadilikia ghafla kipa huyo wa zamani wa timu za Simba, Njombe Mji na Singida United ambapo amejikuta akipoteza nafasi mbele ya makipa Wilbol Maseke na Mathias Kigonya na ilikuwa chupuchupu atemwe katika usajili wa dirisha dogo.
Anuary Jabir - Dodoma Jiji
Katika Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita, Anwar Jabir ndiye alikuwa mshambuliaji tegemeo wa Dodoma Jiji FC na alitoa mchango mkubwa katika kuipandisha daraja timu hiyo.
Msimu huu ulianza kwa benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Mbwana Makatta kuendelea kumpa nafasi lakini baadaye mambo yakamuendea kombo na kiwango chake kikayumba, jambo lililopelekea apoteze nafasi ya kuduma katika kikosi cha kwanza.
Abdulhalim Humud - Namungo
Usajili wake ulionekana kama ungekuwa msaada kwa Namungo FC katika mashindano ya kimataifa kutokana na uzoefu alionao na ndio maana haikuwa ajabu kwa benchi la ufundi la timu hiyo kumpa nafasi mara kwa mara katika mechi za mwanzoni mwa msimu huu.
Hata hivyo makosa ya mara kwa mara ambayo alikuwa akiyafanya uwanjani, yalimgharimu na kujikuta akipoteza naafsi mbele ya Khamis Khalifa na Fred Tangalu ambao wamekuwa wakifanya vyema katika moyo wa kiungo wa Namungo FC.