Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Salim: Dakika 180 za heshima Stars

Muktasari:


  • Sare isiyo ya mabao dhidi ya Ethiopia nyumbani na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Guinea ugenini imeipa heshima Stars, huku majina ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga bao la kusawazisha na Mudathir Yahya aliyetupia chuma cha ushindi ndio yanayotajwa zaidi katika matokeo hayo ya ugenini.

POINTI nne ilizopata timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mechi mbili za Kundi H la kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Afcon 2025, zimeiweka timu hiyo katika nafasi nzuri kundini nyuma ya DR Congo.

Sare isiyo ya mabao dhidi ya Ethiopia nyumbani na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Guinea ugenini imeipa heshima Stars, huku majina ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga bao la kusawazisha na Mudathir Yahya aliyetupia chuma cha ushindi ndio yanayotajwa zaidi katika matokeo hayo ya ugenini.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba licha ya nyota wote wa Stars walijitoa na kuisaidia timu kutoka na alama hizo nne katika mechi hizo, kuna mtu mmoja hatajwi katika ufanisi huo, kipa Ally Salim Katoro, aliyedaka michezo hiyo kwa dakika 90 za kila pambano na kuiweka Stars salama mbele ya wapinzani hao.

Kipa huyo namba tatu wa Simba, ndiye aliyeaminiwa na kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliyedaka mechi hizo na kuruhusu bao moja tu la Guinea, huku kwa Ethiopia alisimama imara na kutoka na clean sheet.

Kocha Morocco, anaonekana kuweka imani kwa Salim ambaye katika kikosi cha Simba, anakabiliwa na changamoto ya namba mbele ya Moussa Camara wakati  huo Ayoub Lakred akiuguza majeraha, Aishi Manula akijitafuta huku Hussein Abel naye akisota.

Si mara ya kwanza kwa Salim kuonyesha kiwango chake pindi anapopata nafasi, alifanya hivyo  katika mechi dhidi ya Zambia ya Novemba 6, 2024, Tanzania ikishinda ugenini bao 1-0 bao lililofungwa na Waziri Junior mchezo huo ulikuwa ni wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.


AFUNIKA WENZAKE

Salim amewafunika makipa wengine walioitwa ndani ya kikosi hicho, akiwamo Yona Amos wa Pamba Jiji ambaye ni kipa namba moja wa kikosi hicho kilichomsajili akitokea Tanzania Prisons. Yona ni kipa mwenye uhakika wa namba katika timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu, huku Salim (Simba), Aboutwalib Mshery (Yanga), hao wote wanakaa benchi mbele ya makipa wa kigeni Diarra Djigui na Camara.

Hata hivyo, licha ya kwamba makipa hao wengine wamekuwa na uhakika na kutumika katika klabu zao pale makipa namba moja wao wanapokosekana kama Mshery pale Diarra anapokosekana, lakini Salim ameaminiwa pamoja na kwamba hatumiki mbele ya wenzake.

Katika mechi hizo mbili, licha ya ukweli Stars ilikuwa ikilindwa na ukuta madhubuti wa mabeki na viungo wakabaji, lakini kipa Salim alionyesha uwezo wa kuokoa hatari kwa mashambulizi yaliyotengenezwa na wapinzani na kuifanya Stars iwe salama kuonyesha wazi kwanini Morocco alimuamini mbele ya wenzake.


UZOEFU KIMATAIFA

Kilichombeba Salim ni uzoefu alionao katika michuano ya kimataifa, kwani ikumbukwe msimu 2022/23 mchezo ambao alianza kudaka kipa huyo dhidi ya Ihefu, Yanga na Azam FC zilipoteza kwenye Uwanja wa Highland Estates, ila yeye alilinda vyema lango timu yake ikishinda mabao 2-0, kipindi hicho Manula aliyekuwa kipa namba moja alikuwa anasumbuliwa na majeraha.

Salim hakuishia hapo akaaminiwa kudaka dhidi ya Yanga, Simba ikishinda mabao 2-0 katika Ligi Kuu Bara na pia akadaka katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad timu yake ikitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 , baada ya timu hizo kila moja kushinda bao 1-0 kwenye uwanja wake wa nyumbani hiyo ikiwa ni mechi ya robo fainali.

Mbali na mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Salim pia alicheza mechi mbili za michuano mpya ya African Football League (AFL) dhidi ya Al Ahly ya Misri, ambapo Simba ilitoka sare ya 2-2 nyumbani kisha kwenda kupata nyingine ya 1-1 ugenini na timu hiyo kung’olewa kwa kanuni ya bao la ugenini.

Katika mechi hizo zilizochezwa Oktoba mwaka jana, Salim alionyesha uwezo wa kuokoa hatari za nyota wa Al Ahly licha ya uchanga wake, kwani kipindi hicho Aishi Manula alikuwa bado anajiuguza, lakini kipa huyo aliibeba Simba mabegani, sema kanuni ya bao la ugenini liliitoa Simba kwa matokeo ya jumla ilikuwa sare ya mabao 3-3 na kama isingekuwa kanuni hiyo timu hizo zilikuwa zikienda katika penalti.


AIREJESHA NGAO MSIMBAZI

Baada ya Yanga kubeba kwa misimu miwili Ngao ya Jamii, msimu uliopita kipa huyo akiwa langoni jijini Tanga aliiwezesha Simba kurejesha taji hilo kwa kudaka mechi mbili ngumu dhidi ya Singida FG na Yanga.

Katika fainali ya michuano hiyo, Salim alidaka penalti tatu za Yanga, huku akiruhusu moja tu na kuipa Simba taji kwa ushindi wa mikwaju 3-1, licha ya kulalamikiwa kwa kutoka katika mstari kabla ya nyota wa vijana wa Jangwani kuzipiga, lakini Simba ilibeba ubingwa iliyopoteza msimu huo.


MAONI MAKIPA

Mwenendo mzuri wa Salim, umewagusa makipa wa zamani, kuona kuna haja Simba, Yanga na Azam FC kujaribu kuwatengeneza makipa wazawa, ili kulisaidia taifa lao, katika mashindano mbalimbali.

Kipa wa zamani wa Simba na Stars, Peter Manyika alisema anakumbuka mwaka  2014 aliumia Ivo Mapunda, akaachwa kupangwa ila namba mbili Hussein Sharrif ‘Casillas’ akapangwa adake dhidi ya Yanga, mechi ikamalizika kwa suluhu, anafichua kilichomsaidia ni nidhamu ya mazoezi.

“Salim anazingatia mazoezi ndio maana anadaka katika kiwango kizuri anapoitwa timu ya Stars, vinginevyo siyo rahisi kusimama langoni bila kucheza mechi muda mrefu, kuna namna mchezaji anaweza akapoteza kujiamini,” anasema. Manyika Jr, mtoto wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Manyika Peter.

Kwa upande wa kipa wa zamani wa Simba, Yanga, Gor Mahia ya Kenya, Saint -George, African Lyon, Congo United na Azam FC, Ivo Mapunda anasema; “Kuna haja klabu ambazo zinatoa wachezaji wengi Stars, ambazo ni Simba, Yanga na Azam, zitengeneze mfumo wa kuwaamini makipa wazawa.”