Sabilo: Nilipakwa pilipili uwanjani

KUNA wakati wachezaji wanapitia changamoto ndani ya uwanja ambazo ni ngumu kuzungumzia hadi wakusimulie jinsi wanavyokumbana na vitu vya ajabu kwenye kazi yao.

Ukitaka kuamini hilo, huu ni ushuhuda wa Sixtus Sabilo ambaye kuna siku alijikuta haoni ghafla na kushindwa kuendelea na mechi, baada ya kupakwa pilipili machoni na mchezaji wa timu pinzani anayemfahamu.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, anafunguka namna ambavyo mchezaji anaweza akafanya vitu vya ajabu na mashabiki wakamshambulia bila kujua ameona nini ndani ya uwanja ama kafanyiwa kitu gani.

"Kiukweli kazi yetu licha ya kutakiwa kufanya mazoezi, nidhamu na bidii ila inamhitaji zaidi Mungu, maana uwanjani kuna vitu vingi vya kutisha, kuna wakati unaweza ukarudia kuangalia video ya mechi unajishangaa pale nilifanya kitu gani," anasema staa huyo wa Mbeya City.

Nusu apofoke macho
Anasimulia ilikuwa mechi ya Ligi ya Mkoa, akiwa na Town Stars ambayo kwa sasa ni Stand United 'Chama la Wana' ilipocheza dhidi ya Baruti FC mwaka 2014, zilipokutana katika nusu fainali.

"Nilikuwa mchezaji tegemeo ndani ya kikosi changu, sasa wapinzani walikuja na mbinu mpya, kuna jamaa ninafahamiana naye kabisa, mikono yake aliipaka pilipili, wakati tupo uwanjani akaja akanishika usoni, nikawa sioni ghafla.

"Sikuweza kurudi tena uwanjani kuendelea na mechi, tukafungwa bao 1-0, kiukweli sitakaa niisahau katika maisha yangu, maana ule ni unyama ama ukatili mbaya, maana soka ni burudani na siyo vita, yule jamaa sijui angejisikiaje kama mpaka leo ningekuwa sioni kabisa."

Anajina mbali
Sabilo anasema kukata tamaa kwake ni mwiko, ana ndoto kubwa hivyo anapambana kuhakikisha anaibadili inakuwa kwenye vitendo.

"Najipa misimu michache, huyo Sabilo wa leo atakuwa mwingine kama ilivyo kwa mastaa wengine ambao wanatamba kila kona."
Anasema ili kufikia hatua hiyo anahitajika kuwa na heshima, juhudi ili kuongeza uwezo binafsi na pia kumtegemea Mungu kwenye kila jambo.

Ligi ngumu
Msimu huu 2022/23, unaoendelea kutimua vumbi, kwake anakiri kuwa mgumu kutokana na kila timu kupambana katika kila mchezo ili kupata matokeo mazuri.

Anasema ushindani ni jambo linalomfanya kujituma wakati wote ili kuisaidia timu yake kumaliza ndani ya nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi.

"Naamini malengo hayo yatatimia na mimi pia natamani kufunga mabao 15 msimu huu, yasipungue hapo hata yakizidi sawa, lakini lengo kubwa ni hili kwa kushirikiana na wenzangu, najua nitatimiza ndoto hii," anasema.

Simba, Yanga
Hakutaka kupepesa macho kuzizungumzia Simba, Yanga na Azam FC kutokana na miundombinu yao, inawafanya wachezaji kutamani siku moja kuvaa jezi zao kwa kuzitumikia.

"Kiukweli ni ndoto ya kila mchezaji wa Bongo kuzitumikia timu hizo kutokana na kipato chao, pia ni rahisi sana kupitia timu hizo mchezaji kujitangaza nje ya nchi na kupata timu," anasema.

Sabilo anasema, wachezaji wengi wakipata nafasi kwenye hizo timu hata maisha yao yanabadilika tofauti na sehemu ambazo wametoka.

Mastaa wa kigeni wamkosha
Uwepo wa wachezaji wa kigeni katika ligi anasema unawapa ushindani na kuamka kiakili kupigania namba kikosi cha kwanza, kwani presha ya maisha humfanya mchezaji akili izinduke kama imelala.
"Uwepo wao unatufanya tusijisahau, unasaidia kutumia vyema nafasi tunazoaminiwa kucheza na makocha wetu maana bila ya kupambana hauwezi kupata namba," anasema.

Wazawa kukwama nje
Sabilo anasema wazawa wanakwama kukaa nje kwa muda mrefu kama ilivyo kwa maproo kuja kwa wingi nchini kwa kuwa wanajisahau na kufikiria nyumbani zaidi.

"Tanzania ni tofauti na nchi nyingine ambazo hawawashobokei wachezaji wa kigeni, wanachoangalia zaidi ni uwezo wao, mfano mzuri ni Mbwana Samatta wakati yupo kwenye kilele alizungumzwa kila kona," anasema.

Chama/Dube noma
Kwa wachezaji wa kigeni anaowakubali Sabilo, anawataja Clatous Chama wa Simba kwamba anatumia akili kubwa kufanya kazi yake, jambo ambalo mabeki wanashindwa kumsoma namna ya kumkaba na mwingine ni Prince Dube wa Azam FC.

"Chama siyo mchezaji wa kawaida, anajua nini anakifanya na kwa wakati sahihi, hata sisi tunajifunza vingi kupitia yeye, hata wengine wa kigeni ni wazuri," anasema.

Matokeo yalimuumiza
"Hakuna kitu kinachoniuma katika msimu huu kama kufungwa mabao 6-1 na Azam FC, ni mengi sana, natamani itokee siku na sisi tuje tuipige timu moja bao nyingi kabla ya kumaliza msimu huu," anasema.

Anasema hakuamini matokeo yaliyotokea siku hiyo kwani ilikuwa ngumu kwake na kila akiikumbuka anakosa majibu ya kilichotokea.

Changamoto
Anasema changamoto zipo nyingi lakini hatasahau msimu wake wa kwanza anasajiliwa Stand United kwani aliingia kwenye timu akacheza mechi chache na kupata majeraha yaliyomfanya akae nje ya msimu nusu mwaka na kujiona kama mtu mwenye mkosi.

"Niliona ndio nimetoboa baada ya kupambana muda mrefu kupata timu ya Ligi Kuu na kwa bahati mbaya ndio hivyo tena nikaumia, mpaka dirisha dogo linafika nilikuwa sijacheza mechi hata moja, nilimshukuru Mungu nilipona lakini nilikata tamaa sana," anasema.

Miundombinu
Miundombinu ni moja ya nyenzo kwa mchezaji, lakini ikitokea viwanja vikawa vibovu inapelekea mchezaji kushindwa kuonyesha kiwango chake kizuri.

"Ubovu wa viwanja ni changamoto kubwa ila sasa hivi kuna unafuu zaidi ndio maana wanavifungia zaidi ili wahusika wavirekebishe kutupunguzia majeraha," anasema Sabilo.

Alikopita
Timu ya kwanza kuichezea kwenye Ligi Kuu ilikuwa ni Stand United kisha KMC, Polisi Tanzania, Namungo FC na Mbeya City.

"Kumbukumbu ambayo sitaisahau wakati nipo Namungo ni fursa ya kucheza michuano ya CAF, maana kukutana na De Agosto, Raja Casablanca siyo mchezo," anasema.