Sababu za Real Madrid kumrudisha mtaalam huyu

Muktasari:

KATIKA mechi ya mwisho ya kumalizia Ligi Kuu Hispania maarufu kama La Liga, ilishuhudiwa Barcelona ikicheza Jumamosi dhidi ya Eibar bila kuwepo kwa mchezaji wake tegemeo, Lionel Messi.

KATIKA mechi ya mwisho ya kumalizia Ligi Kuu Hispania maarufu kama La Liga, ilishuhudiwa Barcelona ikicheza Jumamosi dhidi ya Eibar bila kuwepo kwa mchezaji wake tegemeo, Lionel Messi.

Mshambuliaji huyo, mbabe mara sita wa tuzo ya mchezaji bora duniani ‘Ballon d’Or’ mwenye umri wa miaka 33, hata Ijumaa katika mazoezi ya timu kujiandaa na pambano hilo hakuwepo.

Hali hiyo ilisababisha maswali mengi kutoka kwa mashabiki ambao walirusha maneno katika kuta za mitandao ya kijamii ya klabu hiyo, wengi wakitaka kujua kulikoni.

Wapo waliodai hizo ni dalili za mshambuliaji huyo kuachana na klabu hiyo ambayo mpaka sasa msimu wa kiangazi wa usajili barani Ulaya ukikaribia kuanza, hajasaini mkataba mpya.

Kocha wa Barcelona, Ronald Koeman alisema kuwa mechi ya mwisho kwao haikuwa na uzito wowote, kwani pointi walizokuwa nazo zilikuwa zinawaweka pembeni katika kinyang’anyiro cha ubingwa wa ligi hiyo. Hivyo alitoa kibali cha mapumziko kwa nyota huyo ambaye ameisaidia klabu hiyo msimu huu kubeba Kombe la Copa del Rey.

Vilevile Eibar waliyocheza nayo tayari imeishashuka daraja, hivyo aliamua kukubaliana na uamuzi wa kumpumzisha mshambuliaji huyo ambaye msimu huu ametupia mabao 38 katika mashindano yote.

Mapumziko hayo yanampa nafasi ya kupumzika kwani msimu wa kiangazi ana jukumu la kuisadia nchi yake ya Argentina katika mashindano ya Copa America yanayoanza mwezi ujao.

Itakumbukwa kuwa, mchezaji huyo bado hajaipa nchi yake taji lolote na kupumzishwa katika mchezo huo kuna maana kubwa kwake katika utimamu wa afya ya mwili.

Katika klabu hiyo ya Cataluna, Messi ni nguzo na mafaniko mengi ya timu yanamtegemea ndiyo maana alipangwa mechi zote za msimu na ni nadra kuona akitolewa kipindi cha pili au kuingia akitokea benchi. Kutegemewa sana na klabu hiyo ndiko kunamfanya achezeshwe michezo mingi bila kupumzishwa.

Kama inavyojulikana mchezo wa soka una hekaheka nyingi zinazoweza kuchangia mwili kufanya kazi kupita kiasi au kupata majeraha mara baada ya kufanyiwa faulo ama kujijeruhi mwenyewe.

Pamoja na kwamba ni kweli mechi hiyo ilikosa mvuto kutokana na watu kutaka kumuona mshambuliaji huyo, ila mapumziko hayo yalikuwa ni muhimu kwake.

Kwa mchezaji kama Messi ambaye anatumika sana mapumziko yanampa nafasi ya kupona vijeraha vidogovidogo vya ndani

kwa ndani katika misuli. Sio tu Messi anayehitaji mapumziko mara baada ya mechi au mazoezi magumu, bali ni kwa mwanamichezo yeyote kupumzika hakuepukiki.


FAIDA ZA KUPUMZIKA

Mwili umeuumbwa kwa ufanisi wa hali ya juu katika kutenda mambo mbalimbali ikiwamo kukimbia, kutembea, kuruka, kufikiri na kuongea. Kufanya mazoezi mfululizo au kucheza michezo mingi huambatana na vijeraha vya ndani kwa ndani ambavyo ni vigumu kuhisi au kuvigundua kutokana na udogo wake.

Endapo mchezaji ataendelea kucheza bila kupumzika, vijeraha hivyo huongezeka ukubwa na kuwa kikwazo katika uchezaji au ushiriki wa michezo. Misuli imeumbwa kwa bunda la nyuzi zenye uwezo wa kunepa au kuvutika kama mpira, hivyo pale tunapofanya mazoezi huvutika mara nyingi na pengine kupitiliza kiwango chake.

Jambo hilo ndilo linalosababisha mpaka kufikia misuli kuchanika na kusababisha majeraha makubwa.

Ili kulinda afya ya mwili kwa mfanya mazoezi yapo mambo yanayohitajika na mwili ili kuweza kusahihisha na kujikarabati kwa ajili ya kuponyesha majeraha ikiwamo kupumzika na kulala.

Kwa wachezaji kama Messi wana majumba ya kifahari ambayo yana mazingira mazuri pamoja na vitu vingine vya kuupa mwili utulivu ikiwamo mabwawa ya kuogelea na mabafu maalumu.

Kipindi kama hiki alichopata mapumziko hujituliza katika majumba yao ya kifahari na hatimaye mwili hupona vijeraha vya ndani kwa ndani.

Tunapofanya mazoezi au shughuli misuli hufanya kazi huku ikitumia sukari ya mwilini katika kuwezesha misuli kujikunja na kukunjuka kufanya mambo mbalimbali ikiwamo kutembea, kukimbia na kuruka.

Kipindi hiki hutokea mabadiliko mengi ikiwamo tishu za misuli kuvunjika vunjika, kupungua kwa sukari iliyohifadhiwa katika misuli (muscle gycogen) na mwili kupoteza maji.

Wakati wa kupumzika ndipo mwili unapopata nafasi ya kusahihisha upungufu wa maji na sukari pamoja na kukarabati tishu za misuli zilizopata madhara au kujeruhiwa. Hivyo bila mwili kupata mapumziko ya kutosha ina maana utandelea kupata athari katika tishu za misuli.

Zipo dalili zinazoashiria mwili kuchoshwa na mazoezi makali yasiyo na mapumziko ikiwamo uchovu wa mwili mzima, sonona (depression), kushuka kiwango cha uchezaji na kupata majeraha kirahisi. Unapopumzika siku 1-2 (mapumziko marefu) kwa wiki ndicho kipindi ambacho majeraha yaliyotokana na mechi au mazoezi magumu yanapopona, hivyo kumfanya mtu kujisikia mpya asiyehisi uchovu.

Vilevile mapumziko mafupi ya saa baada ya mazoezi magumu nayo hutoa nafasi kwa mwili kujiponya na majeraha yaliyotokana na mazoezi.

Hivyo basi, ndiyo maana Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) limeweka utaratibu wa mapumziko kati ya hatua moja kwenda nyingine ili kutoa nafasi kwa wachezaji kuimarika kimwili kwa ajili ya kucheza vyema hatua nyingine.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza watu wanaofanya mazoezi kwa ajili ya kuboresha afya kuyafanya kwa saa 150 kwa wiki ambazo ni sawa na nusu kwa siku kwa siku tano za wiki. Hivyo siku mbili za wiki zinatakiwa kuwa za mapumziko na vilevile kitabibu inashauriwa mwanamichezo kulala saa 6 - 8 kwa usiku mmoja.

Hapa tunaona kwa Messi kupata mapumziko yupo ndani ya ushauri wa wataalamu wa afya. Tusubiri kuona mshambuliaji huyo anayetamaniwa na Manchester City na PSG atafanya nini kuisadia nchi yake katika mashindano hayo maarufu kwa nchi za Amerika Kusini.

Imeandikwa na Dk Shita Samwel