Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu kifo cha bondia Zimbambwe

no

WIKI iliyopita Jumatatu habari kubwa katika ulimwengu wa michezo ilikuwa ni kifo cha mwanamasumbwi kijana toka nchini Zimbabwe, Taurai Zimunya (24) aliyefariki dunia baada ya kupigwa kwa knock out (KO).

Mwanamasumbwi huyo alikutana na mauti katika raundi ya tatu ya pambano lisilo la ubingwa lililopigwa eneo la Borrowadale jijini Harare mara baada ya kupigwa ngumi nyingi kichwani bila majibu.

Katika video za pambano hilo la raundi sita lililochezwa Jumamosi Zimunya alionekana akipigwa ngumi nyingi zilizotua kichwani na kumfanya kwenda chini na kuzimia. Bondia huyo anayepigana uzito wa Super Bantam alikimbizwa katika hospitali ya Parirenyatwa na kulazwa kwa siku mbili kisha alifariki dunia Jumatatu Novemba Mosi.

Tukio hilo limeupa simanzi ulimwengu wa michezo kiasi cha kuwaibua wanaharakati nchini Zimbabwe kulaumu mamlaka zinazosimamia mchezo wa ngumi. Wamezinyoshea kidole mamlaka hizo kuwa zimeshindwa kuwalinda mabondia kwa kuwekea taratibu rafiki kuwalinda wanapokuwa katika mchezo huo.

Katika jicho la kitabibu ni dhahiri kuwa kifo hicho kimetokana na ngumi nyingi kutua kichwani na kusababisha majeraha ya ndani kwa ndani ya ubongo. Kitendo cha mchezaji wa ndondi kupoteza fahamu kwa muda mrefu akiwa amelazwa hospitali ni dhahiri kuwa alipata majeraha mabaya ya kichwa ndani ya ubongo.

Itakumbukwa mwezi wa uliopita katika pambano la uzito wa juu duniani katika ya Tyson Fury na Deontay Wilder nilizungumzia madhara ambayo anaweza kuyapata bondia. Katika pambano hili Wilder alipigwa vibaya kiasi cha kupoteza fahamu kwa sekunde kadhaa. Tuliona madhara mbalimbali ikiwamo kupata majeraha mabaya ya kichwa ambayo yanaweza kumsababishia kupata majeraha mabaya ya ubongo na kufariki dunia.

Katika video ile Taurai alionekana kupigwa makonde mazito kichwani ambayo tayari yalishamyumbusha na kuanza kupoteza mwelekeo, huku mpinzani wake alionekana akiendelea kumshindilia makonde mfululizo. Ubongo ndiyo kituo kikuu cha kudhibiti mambo yote ya mwili ikiwamo kupumua, kudhibiti kasi ya mapigo ya moyo na shinikizo la damu.

Kupatwa na majeraha katika tishu za ubongo kunaweza kusababisha hali ya kuchanika au kuraruka au kujeruhiwa na kuvimba kwa ubongo au kuvujia kwa damu hatimaye tishu za ubongo kukosa damu. Hali kama hii inapotokea ndiyo chanzo cha kupoteza maisha.

Kifo hiki kimezungumzwa kila mahala duniani na kuwahuzunisha wengi. Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti tukio hilo ikiwamo magazeti makubwa duniani kama The Sun na The Mirror. Mpaka sasa mamlaka zinazohusika nchini Zimbabwe hazijaweka wazi taarifa za kina za uchunguzi wa kifo hicho.

Mmoja wa viongozi wa bodi ya masumbwi na mieleka Zimbabwe, Lawrence Zimbudzana anasema kwa sasa hawana la kusema mpaka baada ya taratibu za maziko kwisha. Anaeleza kuwa watakaa na kufanya uchunguzi wa tukio hilo la kusikitisha lililokatisha uhai wa bondia mchanga mwenye kipaji, huku akisisitiza kuwa taratibu zote za kitabibu zilizingatiwa wakati wa kuhudumiwa kwa Zimunya.


MAJERAHA YA UBONGO

Majeraha ya ubongo yanaweza kuainishwa katika aina tatu, lakini kwa tukio hili yanaangukia katika jeraha la kati mpaka la makubwa. Kuna majeraha ya mtikisiko wa ubongo yanayojulikana kama concussion, kuchubuka kwa ubongo kitabibu ni brain contusion na kuchanika au kuraruka kwa ubongo kitabibu ni brain laceration.

Aina ya pili na ya tatu ndiyo huwa na matokeo au madhara mabaya kwa mwathirika na mara nyingi husababisha kifo au ulemavu wa kudumu ikiwamo kuwa katika koma au kupooza kwa viungo.

Katika mchezo wa masumbwi hali ya kupata majeraha ya kati mpaka makubwa ya ubongo inaweza kutokea kutokana na kupigwa na kitu kizito ambacho huwa ni ngumi zilizomo ndani ya glovu.

Kasi ya makonde na uzito wake ni moja ya mambo yanayochangia kutokea kwa majeraha ya aina hii. Ukitazama namna bondia yule alivyopigwa ni kwamba, ngumi nzito zenye kasi na uzito zilitua kichwani katika eneo la mbele la kichwa na pembeni mwa eneo hilo.

Vilevile hata ngumi hizo zilipomdondosha akiwa katika hali ya kuzimia, upo uwezekano wa kupigiza kichwa katika sakafu ya jukwaa na kuongeza ukubwa wa tatizo. Inaweza ikatokea kupigwa na kitu kizito mara moja ikasababisha jeraha la kawaida, lakini baadaye sehemu hiyo ikapigw tena na kitu kizito na kuongeza ukubwa wa jeraha.


DALILI

Dalili za kupata aina hii ya majeraha ni pamoja na kupoteza fahamu kwa zaidi ya saa mpaka siku kadhaa, maumivu makali ya kichwa, kutapika kunakojirudia, kupata degedege, kutanuka kwa mboni ya jicho au yote mawili, majimaji kutoka puani na masikioni.

Vilevile kushindwa kuamka na kupata fahamu au kutojitambua, kudhoofika au kupooza kwa viungo vya mwili na inaweza kuambatana na hali ya ganzi katika maeneo ya miguuni na mwili kukosa uratibu.

Matukio kama hili la bondia kupoteza maisha kutokana na mchezo huo sio mengi, lakini ipo haja ya kuchunguza tukio na majibu kupatikana ili kuchukua hatua mathubuti kuepukana nayo.


IMEANDIKWA NA DK. SHITA SAMWEL