Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RIPOTI MAALUMU: Ukata, unyanyasaji katika soka la wanawake Bongo

WAKATI ikianzishwa Ligi Kuu England kwa Wanawake miaka 13 iliyopita, kulikuwa na changamoto nyingi ambazo Chama cha Soka nchini humo (FA), ilikabiliwa nazo na walizikubali na kuzifanyia kazi kabla ya kuwa moja ya Ligi Bora zaidi duniani huku ikiliingiza pato taifa hilo.

Kama ilivyo kwa England na mataifa mengine makubwa Ulaya, inawezekana pia kwa Tanzania kupiga hatua upande huo na kuwa na moja ya ligi bora zaidi ya wanawake ambayo zitakuwa tishio kwa mataifa kama vile Morocco, Afrika Kusini na Nigeria.

Kwa kiasi kikubwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), serikali na wadau mbalimbali  wamekuwa wakipambana kuhakikisha Tanzania inapiga hatua upande huo ambao unaonekana unaweza kuiletea nchi heshima.

Mfano mzuri tuliona mwaka jana (2022), vile ambavyo timu ya taifa ya wanawake U17 ya Serengeti Girls ilivyotutoa kimasomaso kwenye Fainali za Kombe la Dunia la Vijana nchini India.

Bendera ya Tanzania ilipeperushwa vyema kwenye fainali hizo kwa Serengeti Girls kufika hadi hatua ya robo fainali, pia ndani ya mwaka huo, tulishuhudia Simba Queens ikitinga hadi hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kama haitoshi mwaka huu, timu ya wasichana ya Fountain Gate ilitwaa ubingwa wa michuano ya Shule za Sekondari inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kuifunga Ecole Omar IBN Khatab kutoka nchini Morocco kwa mabao 3-0.

Kuonyesha ubora wa soka la wanawake nchini, hata nyota wa kigeni wamekuwa wakimiminika Tanzania.

Hata hivyo, licha ya kuanza kuonekana kwa dalili njema za nchi kuelekea katika mafanikio makubwa na kuwa moja ya taifa tishio katika soka la wanawake, yapo mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi ili soka la wanawake lipige hatua zaidi kama ilivyokuwa kwa England na mataifa mengine yaliyoendelea kimichezo barani Ulaya na hata Afrika kwa ujumla.


TUHUMA ZA USAGAJI

Lipo kundi la wachezaji wa kike ambao wamebadili mitindo ya maisha ambayo ni kinyume na utamaduni wa kiafrika kwa kutaka wafanane na Wanaume na wanapokuwa wanaishi kambini hutoka kimapenzi na wanawake wenzao.

Kumekuwa na baadhi ya kesi katika timu, mchezaji hachezi kama mpenzi wake (wa kike ambaye ni mchezaji mwenzake) hapangwi. Ama baadhi ya wachezaji wanaposajiliwa wanaweka masharti ya kusajiliwa na huyo mwenzake (mchezaji wanayejihusisha naye).

Tabia hii imeanza kuonekana ya kawaida katika timu za Ligi Kuu kwani inaelezwa kuwa baadhi wanapoenda kwenye mechi mikoani hoteli wanalala vitanda kama mke na mme, na kwenye siti za magari ya timu wanakaa kulingana na mahusiano yao (mtu na mpenziwe)

Mmoja wa waliokuwa makocha wa timu fulani ya Mwanza, Godfrey Chapa, anasema tabia hiyo ya usagaji ni moja ya sababu kubwa iliyoisambaratisha timu hiyo na kupotea kwenye ramani ya soka.

"Hilo suala (usagaji) limetusumbua sana Marsh, ulikuwa ukivamia ghafla kambini unawakuta wanafanya hivyo vitendo ama wamelala wanabembelezana kama mke na mme, Kuna ambao ulikuwa ukiacha kumpanga mtu wake naye anagoma kucheza," anasema na kuongeza;

"Kwahiyo tulijitahidi lakini hawa watoto hawasikii wengine walisajiliwa timu nyingine na ukitazama wamekwenda kuendeleza hivyo vitendo huko, hili jambo livaliwe njuga sana watoto wanaharibiwa na wazazi wataogopa kuruhusu wasichana kucheza soka."

Huyu hapa nyota wa miongoni mwa timu kutoka Kanda ya Kati mwa Tanzania anaeleza namna ambavyo aliingia kwenye vitendo hivyo kiasi cha kuathiriwa na tabia hizo hivyo kila ambapo amekuwa akijaribua kuachana nazo imekuwa mtiani.

"Sikuwa na tabia za namna hiyo wakati nikianza kucheza soka, nimekutana na wachezaji kutoka sehemu tofauti kila mmoja amekuwa na malezi yake, kwetu sisi ni watu wa dini sana, ilianza kama utani kambini kwetu huwa tunalala wachezaji wawili kitanda kimoja, nilishangaa mwenzangu siku moja usiku akinipapasa," anasema na kuongeza;

"Nilijua ilikuwa bahati mbaya au yupo kwenye ndoto kwa sababu wapo watu wengine wakiota wamekuwa wakifanya na vitendo, hivyo sikufanya lolote nilikausha lakini kadiri ambavyo alikuwa akifanya nilijikuta nikipandwa na hisia."

Anaendelea kusimulia kwa kusema,"Nilimstua baadae na kugundua kwamba hakuwa usingizini wala nini, alikuwa akijua nini anafanya, nilikuwa mkali lakini huo haukuwa mwisho, nilishangaa alikuwa akionyesha upendo sana kwangu kwa kunipa vitu vidogovidogo,"

"Sikuwa na mawazo mabaya lakini nikajikuta mbeleni na mimi nimenogewa na kale kamchezo, nikajikuta nakata mawasiliano kabisa na mwanaume ambaye nilikuwa kwenye mahusiano naye, nimekuwa nikijaribua kuachana na hizi tabia lakini najikuta nashindwa kutokana na mazingira," anasema.


RUSHWA YA NGONO

Zipo timu ambazo zimesimama kidete kukabiliana na rushwa ya ngono lakini hili ni janga kubwa kwenye soka la Wanawake, wapo ambao wamekuwa wakipenda kuajiri makocha wa kike au viongozi wa jinsia hiyo ili kuondokana nalo.

Mmoja wa wachezaji kati ya timu ambazo zimemaliza kwenye nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi ya Wanawake, ni mrembo kimuonekana jina lake tunalo anasimulia vile ambavyo amekabiliana na changamoto hiyo.

"Wanawake tunakumbana na changamoto nyingi sana, shida ni kwamba bado hakuna muamko wa kuwepo kwa makocha wengi ambao ni jinsia yetu hivyo inabidi tuwe chini ya makocha wa kiume ambao husababisha matatizo kwenye timu japo sio wote wapo ambao ni makini na wamekuwa wakizingatia maadili yao," anasema na kuongeza;

"Sasa kibaya ni kwamba kama timu ikiwa na kocha wa kiume mzuri ambaye hana mambo ya hovyo unakuta kiongozi anakuwa msumbufu, unaweza kukuta mchezaji fulani ni mzuri lakini akawa anasugua benchi bila ya sababu zozote za msingi, nimekutana na mazingira ya namna hiyo hivyo naeleza kitu ambacho nakijua."

Anaendelea kueleza,"Nimekutana na changamoto hiyo nikiwa na timu mbili tofauti, unaweza kuwa na roho ngumu lakini sio rahisi kushinda changamoto zote, sisi nao ni binadamu kuna muda tunachoka na kwakua mpira ni maisha yetu tunajikuta kwenye hiyo mitego, mbaya ni kwamba leo akiwa na wewe kesho anakuwa na yule."

Kwa mujibu wa wachezaji wa timu mbalimbali za Ligi Kuu ya Wanawake, wamekuwa wakinasa kwenye mitego hiyo kwa kununuliwa viatu, simu za mkononi na vingivevyo ambavyo kikawaida imekuwa changamoto upatikanaji wake kwao kutokana na kucheleweshewa kwa mishara yao na vile vile kutokidhi mahitaji.

"Siwezi kusema ni mchezaji gani ila nimewahi kutembea naye wa timu yetu kubwa (Wanaume) ili kupata chochote," anasema mchezaji mwingine wa timu hiyo.


MISHAHARA DUNI

Kutokuwepo kwa bajeti kubwa ya soka la wanawake kuanzia katika timu za taifa hadi klabu, kunazaa malipo kiduchu kwa wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi katika timu za wanawake kulinganisha na upande wa wanaume.

Kwa upande wa klabu wapo wachezaji wengi wanaolipwa mshahara usiozidi Sh 100,000 ambao nao wamekuwa hawaupati kwa wakati na wamekuwa wakilipwa kiasi kidogo cha fedha katika nyakati za usajili.

Kipindi fulani aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba Queens, Matty Mseti alithibitisha alipofanya mahojiano na kituo kimoja cha redio kiasi cha kibarua chake kuota nyasi.

Kocha huyo ambaye kwa sasa yupo zake Falme za Kiarabu analinukuriwa akisema,"Nalipwa Sh500,000 lakini wapo wachezaji katika Ligi Kuu ya Wanawake ambao wanalipwa Sh50,000 tu na wapo wengine ambao hata kulipwa hawalipwi."

Ni mwaka sasa umepita tangu sakata hilo litokea, Mwanaspoti iliamua kuchimbua ili kubaini kama kuna mabadiliko yoyote lakini imebaini kuwa bado hali ni tete kwani hata wale nyota ambao wamekuwa wakifanya vizuri wamekuwa akimbulia laki tatu huku wengine wakivuta  laki nne kwa timu kubwa.

Upande wa timu za daraja la kati na chini huko wapo ambao wamekuwa wakilipwa laki moja na wengine elfu hamsini, huyu hapa mmoja wa wachezaji ambaye timu yake imeshuka daraja anaeleza vile ambavyo mambo yalikuwa upande wao.

"Ni ngumu kusema tumekuwa tukilipwa zaidi tumekuwa tukipata posho tu. Ukiniuliza mara ya mwisho lini nimepokea mshahara nitakuwa nakudanganya kaka yangu (Eliya) tumekuwa tukiishi kwa kutegemea posho tu kwa sababu hata kusafiri kwenyewe kwetu imekuwa mtiani, tunacheza soka kwa sababu ni mchezo ambao tunaupenda pia tunaimani kuwa mbeleni pengine mambo yatakaa sawa," anasema.


KAMBI ZAO

Siku chache kabla ya msimu huu kumalizika ambao JKT Queens ilitwaa ubingwa, Mwanaspoti ilitembelea kambi za timu mbalimbali kwenye ligi hiyo na kubaini nusu ya timu ambazo zinashiriki ligi hiyo mazingira yake sio rafiki.

Ukiziondoa timu tano ambazo sipo nafasi za juu JKT Queens, Simba Queens, Fountain Gate Princess, Yanga Princess na Alliance zilizosalia hali zao sio nzuri mfano Mkwawa Queens na Amani Queens ambazo zimeshuka daraja.

Kwa siku moja ambayo nilikuwa Iringa nilibaini kuwa ni kama Mkwawa Queens imetelekezwa, ilikuwa ni ngumu kwao kushindana na miamba ya ligi hiyo ambayo wachezaji wake wamekuwa wakikaa kwenye mazingira mazuri.

Zipo timu ambazo zimekuwa zikitumia maji ya kunywa kwenye madumu huku ratiba ya chakula ikibadilika mara kwa mara,"Malengo yao (wachezaji) ni kuonyesha vipaji vyao ili kupata nafasi ya kuonekana timu kubwa, hizi timu za chini ukata umekuwa ukiwatafuna hivyo ni ngumu kuwa sawa kiushindani na timu kubwa," anasema Shomary ambaye aliwahi kuwa mmoja wa watumishi wa Mkwawa.

Anaendelea kueleza,"Unaweza kudhani kuwa ni gesti, sijui maisha ya timu yatakuwaje mbele tukishuka daraja, kuna haja ya watu wa Iringa kuamua kusimama na timu zetu, ni ngumu kuwa na timu shindani kwa staili hii."


UKATA WA TIMU

Licha ya Ligi Kuu ya Wanawake kuwa na mdhamini ambaye ni Kampuni ya Bia ya Serengeti, bado maisha yameendelea kuwa magumu kwa wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayozikabili timu za wanawake.

Hiyo imesababisha wachezaji kutopata huduma stahiki kwa wakati lakini pia kuzifanya timu zipate ugumu katika uendeshaji jambo ambalo limekuwa likichangia kudumaza ligi ya wanawake na kupunguza ushindani na mvuto wake.

Mwanaspoti kwa uthibitisho kutoka kwa viongozi mbalimbali wa timu za wanawake, limebaini kuwa kumekuwa na ucheleweshwaji wa fedha za udhamini na hata pale zinapotolewa, zinakuwa ni za mafungu jambo ambalo limekuwa likisababisha viongozi na wadau kutumia fedha zao ili kusaidia timu.

“Mara nyingi tumekuwa tukitumia fedha zetu ili tu timu iweze kusafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine na iweze kucheza kwani tumekuwa hatupati kwa wakati fedha za udhamini na hata zinapotolewa huwa ni kidogo kulingana na mahitaji ya wakati husika,” anasema mmoja wa viongozi.


SAFARI ZAO

Mbali na timu nyingi kwenye ligi ya wanawake kusafiri kwa kuungaunga tofauti na upande wa wanaume ambapo karibu timu zote zimekuwa zikimudu gharama za usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa hata kupanda ndege, changamoto ambayo wanakumbana nayo wanawake ni kusafiri umbali mrefu wakiwa wamekunja miguu.

Maumbile ya wanawake ni tofauti na wanaume hivyo imekuwa ikiwawia vigumu kwao kusafiri kwa zaidi ya saa 10 wakiwa katika magari ya viwango vya kawaida hivyo inaweza kuathiri utendaji wao wa kazi wakiwa uwanjani.

Miongoni mwa wanasoka wa kike,Zuwena Aziz anaeleza vile ambavyo inaweza kuwa changamoto kwenye safari ya umbali mrefu kwa mchezaji ambaye anakuwa eda huku akitoa wito kwa wadau kuwekeza upande huo.

"Hata hivyo tumepiga hatua, mazingira ya kusafiri ni magumu ni vile tu wengi wetu tumezoea mazingira ya namna hiyo lakini huwa ni changamoto sana kwa mtu ambaye yupo period, inabidi upambane tu kwa sababu ya mapenzi ambayo upo nayo na mpira," anasema na kuongeza;

"Natamani kuona wadau wakijitokeza kutushika mkono, itapendeza siku moja na sisi tukiwa tunapanda ndege kama ilivyo kwa wanaume kutoka sehemu moja kwenda nyingine kucheza michezo ya ligi, kusafiri kwa Coastal sio mchezo kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine."


HALI ILIVYO

Edna Lema ambaye alicheza soka hilo kwenye kiwango cha juu ngazi ya klabu na timu ya taifa kwa mafanikio kabla ya kugeukia ukocha ambapo napo amefanya makubwa anasema,"Hatuwezi kuwa na majibu ya moja kwa moja kuhusu rushwa ya ngono lakini hizo habari nimekuwa nikizisikia,"

"Lakini hakuna uthibisho hata kwa upande wa mapenzi ya jinsia moja hili ni janga ambalo halisemwi tu kwenye mpira wa wanawake hata kwa wanaume au wasanii," anasema kocha huyo wa zamani wa Yanga Princess

Anaendelea kueleza kwa kusema; "Tunapaswa kukemea kwa sababu hili ni suala la nchi na sio kwenye mpira tu, muhimu ni kila mtu kumlinda mwenzake kwa kukemea na kuelimisha jamii kwamba si jambo zuri, wenye vipaji waachwe watimize ndoto zao na kuelimisha kuacha vitu ambavyo vitakwamisha ndoto zao."

"Kwangu mimi mpaka nimefikia hapa na nina watu walioko nyuma yangu wananishauri na kunisaidia kuhakikisha natimiza ndoto zangu na kuyaacha yaliyo mabaya..Suala la maslahi pia siwezi kusema moja kwa moja ni madogo kwa sababu soka lenyewe halina muda mrefu tangu limeanza kuwa la ushindani," anasema Edna na kuongeza;

"Tumepiga hatua na tunaendelea vyema hatuwezi kuwa kwenye kiwango sawa na wanaume na hatupaswi kuwa na haraka hiyo tunapaswa kupambana na kujenga ubora utaotupa hiyo thamani...," anasema kocha huyo."


MDAU NORWAY AFUNGUKA

Allen Mlagulwa ambaye ni mmiliki wa timu ya daraja la kwanza Allan Queens Foundation anaeleza ukuaji wa soka la Wanawake Tanzania na changamoto ambazo wanakumbana nazo huku akieleza vile ambavyo wenzetu Norway alipo kwa sasa walivyoweza kupiga hatua, "Soka la wanawake linakuja vizuri tu Tanzania kulinganisha na nchi nyingi za Afrika, kikubwa ni kuhamasisha uwekezaji, klabu za kiume huko mtaani nazo ziwe na timu za wanawake mfano Abajalo Girls na Sinza Star,"

"Norway kuna uwekezaji mkubwa mno kwenye michezo  yote. Lengo Lao sio kushindana ila kuweka jamii pamoja kufurahia michezo, kupiga vita madawa, Ulevi, ngono zembe nk. kwa vijana baada ya shule wanakwenda kwenye michezo, wazee nao wanapiga tizi kuimarisha Afya,"

"Ligi ya Wanawake Norway ni moja kati ya ligi kubwa sana hapa Ulaya nadhani ipo kwenye tano bora, ni nchi tajiri sana, natamani kuona wachezaji wa Kitanzania wakipiga hatua na kuja kucheza huku najua hata hali zao za kimaisha zitainuka,"anasema mdau huyo.


MSIKIE MWANASAIKOLOJIA

Kulingana na mapito ambayo wachezaji wengi wa kike wamekuwa wakipitia wakati wa utafutaji wao wa mafanikio kwenye soka, mwanasaikolojia, John Ambrose anaeleza vile ambavyo inaweza kusababisha tatizo la afya ya akili.

"Tutambue kwamba  namna ambavyo tunawaza na kufanya maamuzi inatokana namna ya maumbile ya mawazo yetu yalivyo. Tunavyozungumza maamuzi kuna pattern ambazo ndizo zinatutegenezea sisi aina ya maamuzi ambayo tunayafanya na hiyo ndio changamoto ya kisaikolojia na wakati mwingine ndio shida ya afya ya akili, tukilichukulia hili suala la mtoto wa kike kwenye mpira, tayari ni changamoto ya afya ya akili ambayo huwa tunaichukulia ni mwepesi kulubuniwa kwenye rushwa ya ngono," anasema na kuongeza;

"Ule mtizamo tuliona unaotokana na mazingira tunavyoishi ndio changamoto ya afya ya akili, ambayo inakupelekea wepesi wa kufikilia hivyo kutokana na mtazamo wa mtu aliona kwa kusema hivyo ni wazi inaweza kuwaletea athari kubwa msichana au mwanamke ambaye yupo katika mazingira ya kucheza mpira naye akawa ameathirika kisailokojia kwa aina hiyo kwamba hii ni fursa niitumie."

Anaendelea kufafanya kwa kusema,"Pia wanaweza kuathirika wale watoa mafunzo kwa kuona hii ni fursa, katika ile hali ambayo fursa inaonekana ambayo sio halisi ni ugonjwa, ni maradhi ya kisaikolojia ambapo sasa akikueleza atatoa ushahidi anakuwa hana majibu toshelezi kwanini anafanya hivyo kwa kuona anaweza kupata fedha au kitu,"

"Mazingira yaliyopo kwa mwanaume huwa sawa na hata kwa mwanamke lakini huathiriwa kisaikolojia kutokana na mtazamo wa jinsia katika mazingira ya kazi, hii huathiri hata katika mtazamo wa kimaumbile na ndio maana wapo ambao hupata wanaume umri ukiwa umeenda baada ya kumaliza kucheza maana anaweza kuona kuwa na familia kwa sasa inaweza kuwa changamoto ya kufikia malengo yake."