Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ripoti Maalumu... Simba, Yanga zinavyopigwa  mabilioni ya fedha kwa jezi feki

Jezi Pict
Jezi Pict

Muktasari:

  • Wachambuzi wanakadiria klabu hizi zinaweza kuwa zinapoteza bilioni kadhaa za shilingi kutokana na mafuriko ya bidhaa feki sokoni.

KUKAMATWA kwa kontena mbili Oktoba mwaka jana, zilizokuwa na jezi feki za zinazodaiwa kuwakilisha Yanga, Simba, Azam na Taifa Stars, kunaweza kuonyesha sehemu tu ya tatizo kubwa la ulaghai linalolikabili soka la Tanzania.

Wachambuzi wanakadiria klabu hizi zinaweza kuwa zinapoteza bilioni kadhaa za shilingi kutokana na mafuriko ya bidhaa feki sokoni.

Ingawa hakuna utafiti rasmi uliofanywa kuhusu athari kamili za bidhaa feki za michezo nchini, utafiti wa mwaka 2016 uliofanywa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) uligundua asilimia 47 ya bidhaa za walaji, ikiwemo chakula, dawa na vifaa vya ujenzi ni za ulaghai.

Ripoti hiyo, iliyotokana na data kutoka kwa mahojiano na watumiaji 250 na watengenezaji 47, inaonyesha ulaghai umekuwa tatizo kubwa katika soko la Tanzania.

FEKI 01
FEKI 01

Kesi ya jezi zilizokamatwa bado inaendelea kuchunguzwa na hakuna tamko rasmi lililotolewa.

Hata hivyo, jezi feki 45,000 ambazo zingekuwa zimeuzwa kwa bei ya sasa zingezalisha zaidi ya Sh2 bilioni kwa Yanga na Simba.

Msimu huu, jezi ya Yanga inauzwa Sh 45,000, wakati jezi ya Simba inauzwa Sh42,000.

Hata hivyo, feki zinauzwa kwa Sh10,000 tu, zikiwa na bei ya chini sana ikilinganishwa na mauzo halisi.


ATHARI KWA MAPATO

Mwaka jana, Yanga iliripoti kupoteza Sh1.1 bilioni, ikiwa na mapato ya Sh21.2 bilioni dhidi ya gharama za Sh22.3 bilioni. Ingawa si kila kitu kinaweza kuhusishwa moja kwa moja na jezi feki, aliyekuwa meneja wa mawasiliano wa klabu, Haji Manara anadhani uwezo wa klabu kuingiza mapato unaweza kuimarika kwa kiasi kikubwa kwa kudhibiti usambazaji na uuzaji wa jezi halali.

FEKI 02
FEKI 02

“Tunahitaji kubuni mfumo wa kudhibiti mauzo ya jezi. Kwa idadi ya mashabiki wetu, tunaweza kupata faida kubwa kila mwaka,” alisema Manara.

Hata hivyo, jezi feki bado ni kikwazo kikubwa, kwani zinauzwa sokoni kwa bei ya chini sana, hivyo kudhoofisha uwezo wa klabu kupata mapato.


UWEZEKANO MKUBWA

Matukio kama Wiki ya Wananchi ya Yanga na Siku ya Simba yanaonyesha uwezo mkubwa wa masoko wa klabu hizo. Sherehe hizi huwavutia maelfu ya mashabiki kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakitafuta kuonyesha uaminifu kwa timu zao. Ikiwa kila mmoja wa mashabiki 60,000 wanaoshiriki matukio haya atakunuwa jezi halali, Yanga na Simba wanaweza kupata kati ya Sh2.5 bilioni na Sh2.7 bilioni katika siku moja.

Katika kiwango zaidi, ikiwa hata asilimia tatu ya watu wa Tanzania milioni 61.7 watanunua jezi za timu, klabu hizo zinaweza pamoja kupata Sh3.9 bilioni hadi Sh4.1 bilioni. Hata hivyo, takwimu hizi bado ni za nadharia, kwani bidhaa feki zinaendelea kujaza soko.

FEKI 03
FEKI 03

TATIZO LINALOKUJA

Jezi feki, hasa zinazouzwa kupitia njia za kawaida, zinatoa changamoto kubwa kwa kutekeleza sheria.  Februari mwaka 2022, polisi katika eneo moja la Dar es Salaam walikamata watu 17 kwa tuhuma za kuuza jezi feki za Yanga 1,208. Miezi mitano baadaye, mamlaka za Mwanza zilikamata mfanyabiashara kwa kuwa na jezi feki 296 za Yanga na Simba. Kimbe anakadiria zaidi ya asilimia 90 ya jezi zinazouzwa nchini ni za ulaghai yani feki na zinawaathiri pia klabu maarufu za Ulaya kama Chelsea na Bayern Munich.

“Jezi nyingi zinazoonekana sokoni ni feki kwa sababu huenda hakuna wakala waliojiandikisha wa klabu hizi hapa,” alisema Kimbe.

Jezi halisi za klabu kama Bayern Munich na Chelsea, zinazouzwa mtandaoni kwa Sh245,000 hadi Sh300,000, zinapatikana mitaani Dar es Salaam kwa Sh10,000 tu, mara nyingi zikionyesha nembo na lebo lakini hazina ubora.

FEKI 05
FEKI 05

BIASHARA NA HAKIMILIKI

Mamlaka ya Viwango vya Tanzania (TBS) awali ilichunguza ikiwa jezi hizo ni za kiwango cha chini, wakati Brela, Shirika la Usajili wa Biashara na Leseni, limehusika kwa sababu za ukiukaji wa alama za biashara.

Kulingana na TBS, jezi feki ni ukiukaji wa hakimiliki zaidi ya suala la ubora na Brela imeeleza kuwa wamiliki wa alama ua chapaa za biashara wanapaswa kuonyesha hasara mahakamani ili kutafuta fidia.

“Mmiliki wa chapaa wanahitaji kuonyesha jinsi bidhaa feki zimeathiri mauzo yao na uaminifu wa wateja. Hii mara nyingi inahitaji ushahidi wa kina wa hasara za soko,” alisema Andrew Malesi, Ofisa wa Kisheria wa Brela.

Sheria ya Hakimiliki na Haki za Jirani ya Tanzania ya mwaka 2019 inaweka adhabu ya juu ya Sh20 milioni (Dola 7,200) au kifungo cha hadi miaka mitano kwa ukiukaji wa hakimiliki.

Hata hivyo, masuala ya chapa za biashara, kama ilivyo kwa jezi feki, mara nyingi yanakuwa katika eneo lililo na kivuli ambacho kinahitaji ushahidi maalum wa madhara ya kifedha.

Bidhaa feki zinaifanya serikali kukosa mapato ya ushuru pia. Kulingana na Richard Kayombo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ni vigumu kufuatilia mapato ya ushuru mahsusi kutoka kwa mauzo ya jezi kwa sababu biashara zinatozwa ushuru kulingana na mauzo yote bila kufafanua mauzo ya jezi.

FEKI 04
FEKI 04

HATUA ZA KISHERIA

Kutokana na ongezeko la matatizo ya bidhaa feki, Yanga hivi karibuni imetangaza nia ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wauzaji wasioruhusiwa wa bidhaa zao zenye chapa.

Mkurugenzi wa Sheria wa Klabu ya Yanga, Simon Patrick alisema wanasubiri ripoti kamili kutoka kwa polisi kuhusu jezi zilizokamatwa kabla ya kuendelea.

“Tuko tayari kuchukua hatua za kisheria mara tutakapokuwa na taarifa kamili kuhusu jezi ngapi zilihusika,” alisema Patrick.

Wawakilishi wa Simba na TFF pia walionyesha wako tayari kuchukua hatua lakini wanaendelea kuwa waangalifu wakati uchunguzi wa polisi unaendelea.


ITAKUWAJE SASA

Wakati klabu za soka la Tanzania zinapojaribu kuongeza vyanzo vya mapato kupitia bidhaa halali, kudhibiti soko la bidhaa feki ni muhimu.

Kuanzisha njia rasmi za mauzo na kuwaelimisha mashabiki kuhusu umuhimu wa kununua jezi halisi kunaweza kuboresha mapato.

Kumaliza mauzo ya bidhaa feki kunahitaji hatua za pamoja kati ya klabu, vyombo vya sheria, na mashirika kama Brela na TBS. Pamoja na idadi ya watu nchini wenye shauku ya soka, kufikia udhibiti mzuri juu ya mauzo ya jezi kunaweza kuongeza faida za klabu lakini pia kuboresha ubora wa bidhaa zinazopatikana kwa mashabiki.