Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mazoea yamelifikisha sakata la dabi hapa

ZENGWE Pict

Muktasari:

  • Tangu Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, maarufu kama Kamati ya Masaa 72 ilipoahirisha mchezo kati ya Yanga na Simba uliopangwa kufanyika Machi 8, sijaona kama mamlaka yaani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) zikichukulia sakata hilo kwa umakini na uzito wake kulishughulikia na kutafuta suluhisho na kuahidi kuboresha zaidi mfumo wa ufanyaji maamuzi, hasa katika mazingira magumu.

KILA wakati nimekuwa nikiandika kuwa tatizo lolote linapotokea ni fursa ya kujisahihisha na kubuni mbinu za kuzuia lisijirudie au kutengeneza mfumo mpya ambao utaboresha utatuaji wa matatizo kila yanapojitokeza.

Tangu Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, maarufu kama Kamati ya Masaa 72 ilipoahirisha mchezo kati ya Yanga na Simba uliopangwa kufanyika Machi 8, sijaona kama mamlaka yaani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) zikichukulia sakata hilo kwa umakini na uzito wake kulishughulikia na kutafuta suluhisho na kuahidi kuboresha zaidi mfumo wa ufanyaji maamuzi, hasa katika mazingira magumu.

Nimekuwa nikiona kama mamlaka zinachukulia suala hilo lingeisha kimazoea kama yalivyotokea mengine huko, ukirejea kubadili muda wa mechi ya Simba na Yanga ya misimu miwili iliyopita ndani ya saa 24 wakati Yanga walipopeleka timu na kuahidi kutocheza, lakini baadaye wakakubali.

Hali kama hiyo ilijitokeza msimu uliopita katika mechi kati ya Kagera Sugar na Simba wakati vigogo hao wa Kariakoo waliposema hawangepeleka timu uwanjani kutokana na wachezaji wao kuugua mafua. Bila ya kuwasilishiwa vielelezo vyovyote Kamati ya Masaa 72 ikaahirisha mechi saa chache kabla ya muda wa mchezo kuanza. Mechi hiyo ilipangiwa tarehe nyingine na ikachezwa.

Kwa mwenendo huo, unaona dhahiri kuwa Bodi ya Ligi na TFF walitegemea suala hilo lingeisha kama hayo mengine mawili na mengine mengi ya uahirishwaji wa mechi kiholela.

Haikuwa sahihi kwa Kamati ya Saa 72 kuahirisha mechi saa chache kabla ya muda wa kuanza mchezo kwa kusalimu amri kwa tishio lililotolewa na Simba kuwa isingepeleka timu uwanjani hadi waliohusika kuizuia kutumia haki yake ya kikanuni kufanya mazoezi siku moja kabla, wachukuliwe hatua.

Mpira una utamaduni wake wa kuhakikisha mashindano yanaendelea huku wanaokiuka kanuni wakishughulikiwa kadiri ipasavyo. Kwa hiyo uamuzi wa kuahirisha mchezo haukuwa na baraka za kikanuni na ndio maana kamati ikatumia kanuni tata inayoipa mamlaka ya kufanya uamuzi huo “kwa kadri itakavyoona inafaa”. Kanuni hiyo ni lazima iwe na wajibu wa kuhakikisha kuna sababu na ushahidi wa kutosha kuahirisha mechi kuzuia wajumbe kufanya uamuzi kwa maslahi yao binafsi na sio ya mpira wa miguu.

Hilo lilikuwa kosa la kwanza kwa TPLB. Na Yanga ilijua hilo ikapeleka timu uwanjani na baadaye kuanza kudai ipewe ushindi, huku ikisema haikuwa na imani na viongozi wa bodi.

Matamko ya viongozi wakuu wa TFF na TPLB ndio yakachochea moto zaidi. Rais Wallace Karia wakati fulani akayazungumzia madai hayo kuwa ni sinema huku akihoji ubora wa viongozi waliotoa shinikizo dhidi ya viongozi wa TPLB. Mwenyekiti wa Bodi, Steven Mguto akatoa matamshi ambayo yaliashiria kuwa walifanya uamuzi kuepusha timu kushuka daraja na baadaye akagusia rufaa ya Yanga kurejeshwa nchini.

Hivi sasa madai ya Yanga yamepanuka zaidi. Sasa wanataka Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao ajiuzulu wakidai ameshindwa kuchukua hatua dhidi ya uamuzi mbovu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB Almasi Kasongo ajiuzulu na Kamati ya Saa 72 ivunjwe ili waweze kucheza mechi hiyo ya Juni 15 na nyingine zilizobaki, huku wakigomea hata fainali ya Kombe la FA hadi watakapopewa fedha zao za ubingwa kwa kutwaa kombe hilo msimu uliopita.

Mbaya zaidi wanasema yasipotekelezwa hayo, hawatashiriki hata ligi msimu ujao, kitu kinachoonyesha ni kwa kiasi gani wanataka haki itolewe. Maana yake wanatuma salamu si tu kwa TFF na TPLB, bali kwa wadau wote na hasa wawekezaji kwenye mpira wetu ambao ni pamoja na Azam Media, NBC wanaodhamini Ligi Kuu, CRDB wanaodhamini mashindano ya Kombe la Shirikisho, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) walio na haki za matangazo ya redio na wengine wanaodhamini ligi na klabu.

Wanajua uhondo uliondolewa kwa sababu za nje ya uwanja, hauwezi kuendelea kuwepo bila moja ya timu hizo mbili, Yanga na Simba kuwepo na wanajua suala hilo litakuwa tiketi ya kuwaondoa wawekezaji kwenye mpira wa miguu ambao nguvu yake imetokana na unazi mkubwa uliopo kwa Yanga na Simba kutokana na historia ya nchi hii.

Kwa mujibu wa msemaji wa Yanga, Ali Kamwe uchunguzi wa tukio hilo umeshafanyika lakini ripoti imekuwa siri kutokana na yaliyomo, likiwemo suala la kigogo wa serikali kuagiza Simba wasifunguliwe geti kuingia Uwanja wa Benjamin Mkapa kufanya mazoezi siku moja kabla. Iwe ni kweli au la, ripoti ya uchunguzi wa sakata hilo ni lazima iwekwe hadharani kwa kuwa inaweza kuwa ndio afya ya baadaye ya mpira wetu.

Pamoja na Kasongo kusema kuwa matakwa ya Yanga yanahitaji vyombo vya juu vya mpira, bado kuna masuala binafsi ya kufanyia maamuzi. Kama shinikizo ni kwa watendaji kujiuzulu, huwezi kuhitaji mamlaka zikutane, bali ni waliotuhumiwa kuchukua uamuzi wa kujiuzulu kusubiri vyombo vya juu kama vitakubaliana na maombi yao ya kuachia ngazi.

Hayo ni maamuzi ya kujitenga na tuhuma dhidi ya mtu binafsi na mara nyingi huwajenga wale wanaojiuzulu iwapo tuhuma hazitathibitika.

Lakini ni kwa jinsi gani chombo cha utendaji cha TFF kimechukulia suala hili kwa uzito? Tangu Machi 8 hadi Juni 8, takriban miezi mitatu sijasikia Kamati ya Utendaji ya TFF ikiitishwa kwa dharura kujadili mwenendo wa sakata hilo. Hiki ndicho chombo ambacho kingeweza kujadili sakata hilo kwa mapana yake na kuja na uamuzi.

Rais wa TFF ndiye msimamizi wa sekretarieti ya shirikisho wakati katibu mkuu ndiye kiongozi wa shirikisho. Kamati ya Utendaji hutaka ripoti kutoka kwa mwenyekiti ambaye ndiye anasimamia sekretarieti.

Kwa kifupi Kamati ya Utendaji ingeweza kumsimamisha katibu mkuu wa TFF kupisha uchunguzi, lakini kwa mujibu wa katiba rais ndiye anayependekeza jina la katibu mkuu na hivyo ni lazima awe mtu wake. Tatizo hilo. Ni tofauti na katibu anayepatikana kwa mchakato wa ajira.

Kwa upande mwingine wa TPLB, niliona Kamati ya Uongozi wa bodi ikikutana muda mfupi baada ya sakata hilo kuibuka. Lakini haikutoa maazimio yoyote. Tatizo jingine ni kwamba mwenyekiti wa bodi, ndiye mwenyekiti wa kamati ya uongozi na hivyo hawezi kujiwajibisha kwa kuhusika katika kuahirisha mechi kiholela akiwa mwenyekiti wa Kamati ya Saa 72. Kwa vyeo hivyo vitatu akiwa ndiye mwenyekiti, hakuna kanuni za utawala bora zinazoweza kufanya kazi.

Lakini hii ndiyo kamati ambayo ingeweza kumsimamisha ofisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi kupisha uchunguzi, hasa katika mazingira haya ambayo hayakuwa ya haraka awali hadi sasa yamekuwa ya dharura.

Kama hatua zingechukuliwa mapema kusingekuwa na madai ya kutaka Kamati ya Saa 72 ivunjwe. Lakini majibizano yaliyotokana na kutaka kuonyeshana nani ana mamlaka badala ya kushughulikia tatizo ndiyo yamesababisha hali imefikia hapa tulipo.

Na kwa hali ya kufikia hapa tulipo, msimamo wa Yanga ilishajionyesha kuwa matakwa yao yasipotekelezwa, msimu utakuwa umevurugika na kampuni zilizowekeza katika mpira wa miguu zitakuwa hazijapata thamani ya fedha. Hili ni fundisho kwa viongozi wa mpira wa miguu kwamba mpira ni zaidi ya zile dakika 90 za uwanjani na mamlaka ni kuwajibika kwa umma na si kutoa uamuzi pekee na ni somo kwamba wenye mpira si chombo kilichosajiliwa kisheria, bali wale wanaoucheza wakitumia mabilioni ya fedha kusajili, kulipa mishahara, kulipa posho, kusafirisha timu, kulipia malazi, kushawishi watu waende viwanjani kudhamini klabu. Hao wanapaswa kuheshimiwa kuliko kitu kingine chochote.

Yanga pia wamewasilisha hoja ya kutaka Bodi ya Ligi itengenezewe muundo mpya na iwe chombo huru kama mpango wa muda mrefu. Pengine kama kuna watu wamekuwa wakiikurubia hoja hii, basi naweza kuwa kileleni mwa orodha hiyo.

Tulipoianzisha Bodi ya Ligi, ikiwa kama Kamati ya Mashindano tuliipa mamlaka kamili. Iliajiri watendaji wake wachache wakati huo bila hata TFF kuingilia. Rais wa sasa, Karia ndiye alikuwa mwenyekiti wa kwanza.

Hiki ni chombo ambacho kwa mpira wa Tanzania kina siasa kubwa na ndicho chenye mapato mengi kuliko hata shirikisho. Binafsi nilikuwa mgumu kukubaliana na wazo la kuipa Bodi ya Ligi uhuru kamili, lakini ghasia za malipo ya waamuzi, makamisaa na wengine zilipoondoka ofisi ya katibu mkuu nilipata ahueni na kuona umuhimu wa uhuru wa chombo hiki.

Lakini tukaambiwa baadaye kuwa hakikuwa kimekomaa kiasi cha kusimama chenyewe. Fikiria, miaka zaidi ya 14 tangu kuzaliwa hakijawa imara? Kwanza muundo wake ni mbovu. Haiwezekani mwenyekiti wa bodi akawa ndiye mwenyekiti wa kamati ya uongozi wa TPLB na huyohuyo akawa ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi.

Haiwezekani mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ndio akawa mtendaji mkuu kivuli wa shughuli za TFF halafu asiwe anawasilisha kikaoni maagizo au maslahi ya shirikisho katika uamuzi.

Tulianza kwa mfumo wa uongozi unaohusisha wenyeviti wa klabu katika nafasi za uongozi, kitu kinachomuondoa Mguto kwenye uenyekiti wa Bodi ya Ligi baada ya Coastal Union kumchagua mwenyekiti mwingine. Hata hivyo, hata walioanza na mfumo huo barani Ulaya sasa wameshauacha kwa sababu bodi za ligi zimekuwa ni sawa na mashirika ya kibiashara na hivyo ni lazima yajali maslahi ya kibiashara ya kila mdau.

Leo hii Ligi Kuu England inaongozwa na bodi inayoundwa na watu watano yaani mwenyekiti na ofisa mtendaji mkuu (CEO) wanaoajiriwa kwa sifa za kuongoza mashirika makubwa (corporate organisations), na wakurugenzi watatu wasioshiriki katika menejimenti (ex-officials).

Muundo huu huwezesha kuwepo na uwajibikaji na usimamizi wenye ufanisi. Bodi ya Ligi Kuu England huwajibika kwa mkutano mkuu wa wanahisa ambao ni klabu 20 zenye hisa moja kila moja. Mkutano huo ndio wenye mamlaka ya mwisho kwa kila kitu kuanzia mikataba ya udhamini, haki za matangazo hadi mapendekezo ya kanuni.

Hiki ndicho chombo kitakachoondoa uamuzi wa hivyo kwenye mpira wetu badala ya huu wa ridhaa tulionao unaoweza kutofasirika kwamba hauangalii zaidi mahitaji ya wakati ya kimchezo na kiuchumi. Kama haya yangekuwa yanaangaliwa mapema na kwa uzito unaostahili, hasa kwa sakata hili lililojadiliwa kwa takriban miezi mitatu baadhi ya uamuzi ungekuwa umeshachukuliwa na hali kurekebishwa mapema kuzuia mpira wetu kufikia hatua hii.

Tunahitaji chombo huru cha kuendesha ligi, muundo huru wa uamuzi, uwajibikaji na utamaduni mpya wa kufanya uamuzi utakaoondoa maslahi binafsi. Sakata la mchezo wa Yanga na Simba linapaswa kuchukuliwa kama fursa ya kurekebisha hayo na kujenga misingi imara ya haki, uwajibikaji, uhuru wa kufanya mazoezi na kuondoa utamaduni wa kufanya mambo kwa mazoea.