Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Richard Mtangi: Mbabe ko aliyeanza kusaka taji la dunia

NGUMI Pict

Muktasari:

  • Bondia huyo mwenye urefu wa futi tano kwenda juu anacheza kwenye uzani wa middle katika ngumi za kulipwa ambao umekuwa ukitajwa ni mmoja kati uzani wenye pesa ndefu kwenye soko la mchezo huo ulimwenguni kutokana ushindani na ubora wa mabondia wake.

RICHARD Mtangi ni mmoja kati ya mabondia wenye uwezo mkubwa wa kushinda mapambano yao kwa ushindi wa uhakika wa knockout katika ngumi za kulipwa.

Bondia huyo mwenye urefu wa futi tano kwenda juu anacheza kwenye uzani wa middle katika ngumi za kulipwa ambao umekuwa ukitajwa ni mmoja kati uzani wenye pesa ndefu kwenye soko la mchezo huo ulimwenguni kutokana ushindani na ubora wa mabondia wake.

Mtangi mwenye rekodi ya kucheza mapambano 11 mpaka sasa akiwa ameshinda tisa kati ya hayo nane akishinda kwa knockout, amepigwa mara moja na ametoka sare pambano moja.

Bondia huyo ambaye pia amekuwa akitambulika kwa jina la utani kama King Duma anapewa uwezo wa asilimia 87.5 wa ushindi wa knockout huku akiwa bondia wa 106 kati ya mabondia 2013 wakati nchini anakamata nafasi ya pili mbele ya namba moja Hassan Mwakinyo katika mabondia 52 wa uzani wake.

Mtangi kwa sasa amefikisha hadhi ya nyota mbili na nusu kutokana na ubora wake ndani ya ulingoni lakini amekuwa bondia wa 14 katika mabondia bora kutoka kwenye kilo zote.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na bondia huyo mzaliwa wa Tanga mjini ambapo amefichua mambo mengi katika safari yake kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa huku akisisitiza kuwa kama siyo ngumi alitamani zaidi kuwa mwanamitindo licha ya familia kumtupa kwenye ufundi magari ‘gereji’ kutokana na utukutu wake.

“Safari yangu haikuwa rahisi pengine katika mchezo huu kwa sababu awali familia yangu ilinipeleka gereji nijifunze mambo ya ufundi wa kutengeneza magari ambayo hadi leo bado nina uwezo wa kufanya,” anasema.

“Lakini ndoto yangu ilikuwa kwenye mambo ya mitindo ndiyo maana kwangu jambo la kunikuta nimependeza ni kawaida japokuwa upande wa michezo nilipenda sana ngumi.”

NGUM 01

Kitu gani kilikuvutia kuingia sasa kwenye ngumi?

“Unajua kiukweli mchezo nilikuwa naupenda sana, lakini kuwaona mabondia kama Hassan Mwakinyo ambaye alikuwa akifanya vizuri ndiye aliyenishawishi kuweza kuwa bondia.

“Nilianza kujifunza kwanza maana nakumbuka wakati nipo Dar nilienda kwa mzee Habibu Kinyogoli ‘Master’ kuomba kujifunza lakini kwa bahati mbaya sikuweza kupata nafasi.

“Lakini wakati huo kutokana na shughuli za mambo ya ufundi wa magari kwa maana ya gereji nikawa nimerudi Tanga ambapo huko nilikutana na rafiki wa baba yangu ambaye ni mdau mkubwa kwenye huu mchezo.

“Unajua alishangaa kunikuta gereji, akaniuliza kwa nini siendelei na harakati za ngumi ikiwa anajua nina uwezo na kipaji, nilimueleza changamoto ambayo ilikuwa mbele yangu wakati huo.

“Yeye akachukua jukumu la kuniambia kwamba atanipeleka kwenye gym ya Hassan Mwakinyo ambayo wakati huo ilikuwa inasimamiwa kaka yake Hamis Mwakinyo.

     

NGUM 04

  “Sasa nakumbuka siku ambayo tulikubaliana kwenda kwa kuanza mazoezi kwa kina Mwakinyo nilipata ajali ya kukatika kidole cha shahada (pete), hiyo gereji sasa, nikapelekwa hospitali maana nililazwa.

“Ukweli nikahisi ndoto zangu zikawa zimeishia hapo na jamaa alikuja kuniona hospitali aliangalia mkono wangu akaniambia bado nina uwezo wa kucheza ngumi licha ya kidole kuwa kimekatwa kidogo.

“Nakumbuka akasisitiza atanipeleka kwa Mwakinyo na atanikabidhi kwake pamoja na kaka yake Hamis ndiyo wataweza kunifundisha ngumi. Kweli nilienda nikafundishwa baada ya kupona kwa kuwa chini yao.

“Siku ya kwanza kocha Hamis Mwakinyo aliniuliza kama nataka kuwa bondia au najifunza kwa ajili ya kujilinda ila nilimueleza ndoto ni kuwa bondia, nilifundishwa na baada ya miezi mitano ndiyo nilikutana Hassan Mwakinyo.

“Baada ya kufanya mazoezi muda mrefu na kuona nimeanza kuiva niliomba kwenda Dar kutafuta mapambano kwa sababu wakati huo Tanga hakukuwa na mapambabo ya kutosha, kocha akaridhia bila shida.

“Nilivyokuja Dar nikafikia Gongo la Mboto kwenye nyumba ya familia ambayo nilipewa chumba kitupu yaani hakina kitu chochote nikawa nalala chini kwa kutandika maboksi huku nafanya shughuli za ngumi na kazi za gereji.

“Nidhamu na kujituma mazoezini ndiyo vilinifanya nijulikane kwa pale Gongo la Mboto, nikawa napata mapambano hadi kwenda Songea katika pambano ka Selemani Kidunda na Tshimanga Katompa, nilicheza na Joseph Maigwisa nikampiga ila nilidhulumiwa ushindi.”

NGUM 02

Ikawaje ukaingia Mafia?

“Nakumbuka watu walikuwa wakipata sifa zangu akiwemo Ibrahim Mafia sasa alivyokuwa na pambano yeye aliambiwa na watu kuwa mimi ni bondia wa Tanga, akaomba nikampe ‘sparing’ kwa kuwa alikuwa na pambano lake na hapo ndiyo safari yangu ikawa ipo kwenye mikono salama ya Mafia Boxing Promotion kama menejimenti yangu.”


Kitu gani huwezi kusahau tangu ulivyoingia kwenye ngumi?

“Nakumbuka niliuza laptop yangu ambayo nilinunuliwa na marehemu bibi yangu kwa Sh100,000 ili ninunue glovu za kupigania kwa Sh35,000.

Lakini kitu kingine familia yangu haikuwa inaamini kwenye uwezo wangu kutokana na kupitia changamoto nyingi za familia nilikuwa naonekana mtukutu, sina malengo na wala sitaki kazi.

“Pia kuna ndugu yangu anaitwa (anamtaja jina) alijitoa kwa ajili yangu ilifika wakati akauza hadi simu ili nipate nauli za pesa ya kula njiani kwa ajili ya mimi nifike Dar.”

NGUM 03

Pesa yako ya kwanza nyingi kupata kwenye ngumi ilikuwa kiasi gani?

“Nakumbuka nilipata Sh450,000 ambayo nililipwa kwenye pambano nikaenda kununua godoro  kubwa ili nisiendele kulala chini.”


Chakula una kula kuanzia kilo ngapi?

“Napenda sana wali na mara nyingi nakula nusu na robo halafu napenda kunywa maziwa sana.”


Umewahi kupata dili gani kubwa kwenye ngumi?

“Nakumbuka niliwahi kupata pambano la Dola 25,000 nchini  Uingereza ila sikuweza kwenda  kutokana na kupata majeraha.


Una mipango gani kwa sasa?

“Nadhani ipo mingi lakini nisifiche kwamba bila ya Mafia Boxing Promotion ambao wananisimamia nisingekuwa hapa kwa sasa maana naweza kwenda kuweka kambi nchi yoyote. Naushukuru uongozi kwa juhudi zake.

“Lakini nataka siku moja nitimize ndoto ya kuleta Tanzania mkanda mkubwa wa ubingwa wa dunia, siyo kwa kushinda nikiwa ndani ya nchi nataka nishinde kutoka nje ya nchi hilo ndiyo jambo kubwa ndani akili yangu.”