Mayay: Kisa Dabi, Wazee Yanga walituomba radhi

Muktasari:
- Nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kuwika CDA Dodoma, Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay Tembele aliyefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti amesimulia namna mechi za dabi zilivyo na mambo mengi akirejea tukio la kuwahi kuja kuombwa radhi na Wazee wa klabu ya Yanga.
ACHANA na kinachoendelea kwa sasa kuhusu Kariakoo Dabi ambao awali ilipangwa kupigwa Machi 8 kisha ikaahirishwa kitatanishi na Bodi ya Ligi Kuu Bara na kupangwa ipigwe kesho Jumapili, huku kukiwa na kila dalili za kutokuwepo kwa pambano hilo.
Nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kuwika CDA Dodoma, Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay Tembele aliyefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti amesimulia namna mechi za dabi zilivyo na mambo mengi akirejea tukio la kuwahi kuja kuombwa radhi na Wazee wa klabu ya Yanga.
Mbali na kusimulia mkasa huo, pia amefunguka mambo mengine ikiwamo vitu vinavyoweza kufanywa ili kulifanya soka la Tanzania lisonge mbele zaidi huku akiweka bayana safari yake kama mchezaji hadi kuja kuwa mmoja wa viongozi wakubwa wa michezo hapa nchini.
Mayay aliyewahi kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Michezo nchini na kugombea nafasi ya Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ameshindwa kujizuia na kumtaja beki wa pembeni wa kimataifa anayekipiga Simba, Shomary Kapombe kama mchezaji wa mfano kwa wengine. Kivipi? Endelea...!

USAJILI WA VIATU NA SH 30,000
Mayay ni mmoja ya wachezaji walioacha kucheza soka wakiwa bado na uwezo mkubwa uwanjani na mwenyewe amefichua kilichomstaafisha kwa kusema alipokuwa akicheza alishapanga mapema kwamba itakapofika mwaka 2004 atundike daruga, wakati huo alikuwa nahodha wa Yanga na Stars.
"Tulicheza soka la ridhaa sio kama kipindi hiki ambapo ni la kulipwa, mikataba yetu ilikuwa kuandika orodha ya majina katika karatasi, mfano mimi Ally Mayay Tembele najiunga na Yanga msimu wa 1998/99 ukiisha unaofuata unafanya hivyo hivyo," anasema Mayay na kuongeza;
Anasema kipindi anasajiliwa Yanga hakukuwa na dau la usajili, badala yake walikuwa wanaahidiwa viatu vya kuchezea, kupewa pesa kidogo kama Shilingi 30000 na tiketi za kusafiri na familia katika mikoa yote ya Tanzania.
"Hakukuwa na taknolojia kama ilivyo kwa sasa hata upatikanaji wa taarifa haikuwa kazi rahisi, bahati niliyoipata mimi Edibily Lunyamila, Ephraim Makoye na Abdallah Saleh 'Sabebe' mwaka 1999/2000 tulikwenda Jamhuri ya Chile, Santiago tulifanya mazoezi kwa miezi sita na timu moja ya huko, tukapata nafasi ya kwenda Argentina ila changamoto ikawa viza, maana ilitakiwa turudi hadi Afrika Kusini, tukashindwa tukarejea nyumbani."
Anasema baada kuona maisha ya wachezaji wa Jamhuri ya Chile, wanavyochukulia soka kama ajira, tofauti na Tanzania ilikuwa ni kujenga afya na kupata burudani, ikamshawishi kutafuta timu nje.
"Mwaka 2000 nilikwenda kucheza soka India ilikuwa takribani kama miezi sita, kilichonirudisha nchini, wadhamini waliyokuwa wanatulipa walijitoa, hivyo ikabidi wachezaji wote wa kigeni turudishwe makwetu, pamoja na kwamba teknolojia haikuwepo kama iliyopo sasa inayowarahisishia wachezaji kuonekana kwa haraka na timu za nje, ila nilionyesha juhudi zangu binafsi," anasema.
Anasema baada ya kustaafu mwaka 2004 alirejea kuendelea na masomo ambapo hadi sasa ana Shahada ya Pili (Masters) ya Biashara na Masoko, akisisitiza elimu ni endelevu.
SOKA LA SASA
Anachovutiwa na soka la sasa anasema wachezaji wamebadilika kimtazamo, mpira wa miguu wanauchukulia ni chanzo cha kujipatia fedha, vituo vya soka vinavyowapa muongozo wa kuziona fursa za kufika mbali hata kucheza klabu kubwa duniani.
"Ni kweli zamani kulikuwa na vipaji vikubwa ila kulikuwa na kuridhiki kwingi hasa wachezaji waliyocheza Simba na Yanga waliona ndiyo mafanikio makubwa badala ya kufikiria kwenda kucheza timu kubwa kama Manchester, Liverpool, Arsenal,Barcelona, Real Madrid," anasema na kuongeza;
"Kwa sasa naliona hilo kupitia vituo vya soka, kuna mawakala ambao wanapeleka vijana wa umri chini ya miaka 17 katika program academy za nje, zitazkazowasaidia kupata fursa ya kucheza timu kubwa na zenyewe zitanufaika kupata asilimia pindi watakapouzwa.
"Kuhusu changamoto ninayo iona ni miundo mbinu katika jamii, hapo simanishi viwanja vikubwa kama Benjamin Mkapa, Uhuru au vile vinavyotumika kwa mechi za ligi, namanisha viwanja vya wazi huko mitaani ambako kunapatikana vipaji vikubwa, hivyo vipaswa kuzingatiwa, sheria ya mipango miji iendelee kutilia mkazo hilo maana katika kila kata lazima kuwa na eneo la wazi kwa ajili ya michezo na burudani."
Kuhusu kasi wachezaji wakubwa kutoka nje, anataja moja ya sababu inayowakwamisha ni Ligi ya Tanzania kuwa kati ya ligi za Ukanda wa Afrika Mashariki zinazowalipa vizuri mastaa.
"Ingawa inaumiza kuona wageni ndiyo wanaopata pesa ndefu kuliko wazawa, ila wanapaswa kujifunza kutoka kwa wageni kipi kinachowapa thamani, kuna mchezaji mmoja kutoka Uganda katajirikia Tanzania kwao ni milionea ila siwezi kumtaja jina," anasema.

WAZAWA vs WAGENI
Anasema wachezaji wa kigeni wameongeza thamani na nidhamu ya Ligi Kuu, kiufundi wana kitu cha ziada kutokana na kupitia mafunzo sahihi ya mpira wa miguu pia wana mameneja wanaowasimamia kazi zao.
"Kama unavyowaona wasanii wa muziki kina Diamond, Ali Kiba wana mameneja wanaowasimamia katika kazi zao ambao ndiyo watalamu wa sekta hiyo, sasa kwa wachezaji wazawa asilimia kubwa wanatumia vipaji bila wasimamizi wazoefu ambao wana uwezo wa kuwatetea ili wasipoteze haki zao.
"Nimeona madai, wachezaji wa kigeni ni rahisi kupata haki zao, ila wazawa ni ngumu, kwani wanakosa mameneja wazoefu na wataalamu ni wachache sana wenye uelewa na hilo."
ZAWADI ZA MASHABIKI
"Japokuwa kila nyakati na zama zake, mimi, Lunyamila, Sekilojo Chambua tulikuwa tunaishi Sinza, hivyo tukishinda mechi kama leo, kesho tunakwenda Manzese kununua mitumba tukiwa na Sh5000 kila mmoja, ajabu tukifika huko tunarudi na suruali za jinzi nne kila mtu ambazo tumenunuliwa na mashabiki, tulikuwa tunalipiwa nauli katika daladala, kwa kifupi tulinufaika na mengi," anasema na kuongeza;
"Ndiyo maana nasema hakuna mchezaji ambaye hajanufaika na soka, utofauti wetu na wa sasa wanapewa mamilioni wanayoweza kufanya maendeleo kwa uharaka na ukubwa."
Kitu kingine alichonufaika nacho kupitia soka anasema amejiendeleza kusoma mambo ya ukocha, hivyo wanapata nafasi ya kushauri katika klabu na mashirikisho mbalimbali ya michezo ya namna wachezaji wanapaswa kuwa ili kula matunda ya vipaji vyao.

WAZEE WAOMBA RADHI
Anasema mechi iliyobakia katika kumbukumbu ya maisha yake ni ya Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba na Wazee wa Yanga waliwaomba radhi wachezaji baada ya kushtuka kuwa walizunguza.
"Kipindi hicho klabu kongwe tulikuwa tunapewa maandalizi tofauti ingawa ilikuwa ni ratiba ya ligi, ila tulipata muda wa kujiandaa kwa muda wa wiki mbili au tatu, wakati huo timu zingine zilikuwa zinacheza, ndiyo maana tulikuwa tunaweka kambi sehemu mbalimbali," anasema Mayay na kuongeza;
"Ilikuwa mwaka 1999 kama sikosei, tuliweka kambi Kigamboni ya wiki mbili kujiandaa kucheza na Simba, kipindi hicho pantoni ilikuwa mwisho saa 2:00 usiku pale Feri na huduma za usafiri huo ilikuwa inafungwa, ajabu wazee wa Yanga walikuja na pantoni saa 6:00 usiku na ikawasubiri.
"Tuliamshwa tukaenda kantini kipindi hicho kocha alikuwa Raoul Shungu, Mwenyekiti wa klabu akiwa ni Tarimba Abbas ambaye akaanza kusema kuna taarifa ya orodha ya wachezaji wamechukua pesa Simba."
Mayay akaongeza kwa kusema; "Akaanza kutaja wachezaji wote wa kikosi cha kwanza, Peter Manyika, mimi, Bakari Malima, Salvatory Edward, Lunyamila na Chambua. Nikaanza kuwaza mbona wote tunatajwa hapo lengo ni nini hadi kocha alivurugwa, tukakaa kimya na kwenda kulala.
"Asubuhi tulipoamka kocha akatuita wakati wa chai, akaanza kutaja listi ya wachezaji ya kupeleka katika kikao, kama nahodha nikasimama na kumwambia kocha asibadilishe kikosi kitacheza kilekile, maana tulipanda wiki moja kabla na mazoezi tukawa tunafanya kulingana na tutakavyocheza, baada ya kupeleka wazee wakapata taarifa hiyo wakachukia.
"Tukaenda uwanjani kama sio dakika ya pili basi ya tatu tukafungwa bao, wazee walisimama na kushangilia, kipindi cha pili tukashinda mabao 3-1 baada ya kurudi Kigamboni wale wazee wakaja kutuomba radhi."
Anasema tukio hilo liliwaamsha wazee na viongozi kuwaachia wachezaji kupanga kikosi cha mechi, ikafikia hatua hadi kupendekeza usajili na aliwahi kufanya hivyo kwa kushauri asajiliwe Fredy Mbunda na klabu ikafanikisha hilo.
"Figisu ilikuwepo, ipo na itaendelea kuwepo inategemea umejipangaje, kwa Simba na Yanga ni utamaduni, ukikosa umakini unavurugwa, watakwambia mchezaji fulani tulimuona na wa upinzani, tena kwa kipindi hiki cha teknolojia ni hatari, wanaweza wakaunganisha picha kuonekana ushahidi," anasema Mayay anayekiri hajawahi kuifunga bao Simba.
Japo hakuwahi kuwafunga Wanamsimbazi ila alikuwa anafunga mabao mengi na analolikumbuka zaidi ni la penalti ya mwisho dhidi ya Villa ya Uganda iliyoipa ubingwa Yanga wa Afrika Mashariki na Kati, iliyopigwa jijini Kampala mwaka 1999, macho ya Watanzania yalisubili kuona nini kitatokea, lakini tukarudi mashujaa."
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Yanga kubeba taji jijini Kampala, Uganda baada ya awali kufanya hiyo 1993 kwa kuifunga pia SC Villa kwa mabao 2-1.

HUZUNI YAKE
Kwa upande wa tukio la huzuni wakati anacheza ni akiwa na CDA na ilicheza dhidi ya Lipuli mechi iliyopigwa Iringa.
Anasema kuna mshambuliaji alikuwa anaitwa Mohamed Mgalike aliyetokea Nyota Nyekundu kujiunga na Lipuli, alimvamia yeye (Mayay) na kipa Rashid Omary Mahadhi, akapasuka kichwa na wakati akiwa chini mchezaji huyo aliupiga mpira nyavuni na refa akaweka mpira kati.
"Kwa namna damu zilivyokuwa zinanivuja kichwani wachezaji wenzangu waliogopa, baada ya kushonwa bila ganzi nikarejea uwanjani nikamfuata mwamuzi kumlalamikia, ajabu wenzangu wote walikuwa upande wake wakaanza kuniambia dogo cheza mpira maana nilikuwa chipukizi na nilikuwa nimepaniki, mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 hilo ni kati ya matukio mabaya niliyowahi kukutana nayo."
ISHU ZA USHIRIKINA
Anasema hiyo ni aina ya maisha kwa klabu mbalimbali, akisisitiza mambo hayo yalikuwepo na yataendelea: "Mfano Yanga na Simba mashabiki wapo tayari kufanya lolote kwa ajili ya kuhakikisha timu zao zinapata matokeo, wapo watu ambao wanaweza kuchinja mbuzi, kutoa kuku weusi, mara paka weupe kila mtu ana imani yake."
MVULIA KOFIA KAPOMBE
Anasema kuna wachezaji ambao wanafanya vizuri kama ilivyokuwa kwao zamani, kitu anachokiangalia ni muendelezo wa viwango vyao, anamtolea mfano beki wa Simba, Shomari Kapombe, kustahili kupewa maua yake na kuigwa na wengine.
"Siyo jambo la kubeza kwa Kapombe kucheza kwa kiwango kwa miaka minane, anatumiwa kama mfano wa kuigwa na kizazi hiki, inaonyesha namna anavyojitambua tofauti na wengine misimu miwili wakivuma inayofuata wanapotea kabisa," anasema Mayay anayemtaja staa wa zamani Ntenze John alikuwa anakokota mpira akimwangalia mpinzani usoni, kitu ambacho hakijatokea hadi sasa.
ALIPACHIKWA JINA LA MEJA
Anasema kutokana na misimamo yake uwanjani wachezaji wenzake walimpachika jina la Meja ambacho ni cheo cha kijeshi na alipoulizwa kama amewahi kusomea kozi hiyo anajibu: "Hapana ila waulize niliocheza nao kama Bakari Malima, Lunyamila ama Chambua watakwambia kwa nini walinipa jina hilo."
ISHU YA DABI
Kuhusu mvutano wa mechi ya Dabi ya Kariakoo inayotakiwa kuchezwa kesho Jumapili, Mayay anasema alitegemea sakata la kuahirishwa kwa dabi ya Yanga na Simba ya Machi 8, 2025 ingekuwa imetatuliwa ili kujipa nafasi na muda wa kuandaa michuano ya CHAN Tanzania ikiwa mwenyeji, lakini anaona bado linazidi kuwa kubwa.
"Agosti siyo mbali kuna maandalizi ya CHAN, hivyo ingependeza kupata muda wa kufanya maandalizi kama CAF ilivyoiamini Tanzania, kanuni zitumike, lazima mwishowe kuna upande utaumia sana na mwingine kidogo huo ndio mpira, Simba na Yanga zina ukubwa wake na serikali haiwezi kuingilia mpira kama alivyosema Waziri wa Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, kwa sababu FIFA ina kanuni zake," anasema.
SIFA ZA NAHODHA
"Nahodha wa timu lazima awe na sifa ya uongozi, ambao utasaidia kuituliza timu ikiwa na presha, kufanyika daraja baina ya wachezaji na viongozi, kutumia busara na miongoni mwao wenye sifa hizo anamtaja beki wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala'," anasema.

KAKA YAKE MACOCHA
"Nina kaka zangu wawili ambao tumepishana nao mwaka mmoja mmoja, Macocha alikuwa mchezaji mzuri kipindi hicho na CDA ilimtaka ila muda mwingi alikuwa chuo na sasa ni Balozi wa Tanzania yupo Indonesia na mwaka jana aliialika Taifa Stars, mwingine ni Hamis naye ni kiungo mzuri sana," anasema.