Revina daktari wa kike kwenye soka la kiume

MBEYA. “NAPITIA mengi mazito.” Ndivyo anavyosema daktari wa timu ya Ken Gold, Revina Renatus akielezea kazi yake kwenye soka akiwa mwanamke pekee kuhudumia wachezaji wa kiume.
Revina, mzaliwa wa wilayani Bunda mkoani Mara huenda akawa ni mwanamke pekee kwenye soka hapa nchini anayefanya kazi ya udaktari kwa timu za kiume First League, Championship na Ligi Kuu.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti jijini Mbeya, Revina anasimulia visa na mikasa anayopitia ndani na nje ya uwanja kutokana na kazi yake hiyo na namna anavyopambana kulinda heshima yake.
Pia, anafunguka tukio lililomtokea kunusuru uhai wake, lakini ishu ya kunusurika kutengwa na familia yao hasa baba yake alipojikita kwenye kazi ya mpira tofauti na maelekezo ya mzazi wake.
Kuhusu kutengwa
Revina anasema haikuwa kazi nyepesi kupokewa na familia yake alipoamua kujikita kwenye michezo kwani baba yake mzazi alikuwa akiamini ni sehemu isiyo salama.
Mtaalamu huyo wa afya (medical attendant) anasema baada ya kukosa ajira alipomaliza masomo yake ya chuo alianza kujitolea katika timu ya wasichana ya TSC Queens ya jijini Mwanza 2019.
Anasema wakati akiendelea na shughuli hiyo baba yake hakutaka kusikia taarifa zake badala yake alitaka kumuona mwanaye huyo anafanya kazi kwenye hospitali, vituo vya afya au zahanati.
“Baba akawa mkali sana akaamini huko naenda kupotea. Ikawa ni vikao vya mara kwa mara akitaka niende kufanya kazi hospitali au zahanati, lakini mimi nikawa napenda mpira,” anasema Revina.
Daktari huyo anaongeza kuwa akiwa bado mtoto alipenda sana mpira kama ilivyo kwa baba yake japokuwa hakucheza soka la ushindani, lakini ni mpenzi mkubwa wa soka na shabiki wa Yanga.
“Pale TSC sikudumu sana nikawa nimehamia Alliance Girls ambapo waliniajiri kwa mkataba, lakini bado baba hakuwa anataka niendelee kuwa kwenye mpira,” anasema.
Revina anasema 2021 akiwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu kati ya Gwambina FC na Biashara United kamera zilimnasa akitoa huduma ya kwanza ambapo baba yake aliona anachofanya.
“Baada ya mchezo huo nikaona baba ananipigia simu anasema ameniona kwenye TV. Akanipongeza kwa kazi akasema nipambane nitafika mbali. Kuanzia hapo akaanza kunipa ushirikiano hadi sasa,” anasema.
Mikasa kazini
Daktari huyo mwenye umbo lake anasema kazi yake ina changamoto nyingi hasa kila mmoja kutaka kuwa naye kimahusiano, lakini anapambana kukwepa mishale ili kulinda heshima yake, familia na jamii.
Anasema tangu aanze kazi hiyo, mapema alitamani kuishia njiani, lakini kadri siku zilivyokuwa zinasogea anazidi kuzowea maisha na hadi sasa haoni kitu kipya isipokuwa anajua kuishi nao.
“Kusafiri na wachezaji wa kiume nyakati zote hata usiku siyo kazi ndogo ukizingatia wengi ni vijana damu inachemka, lakini niliweza japokuwa mwanzoni ilinipa wakati mgumu nikatamani kuacha,” anasema.
Mwanadada huyo anaeleza kuwa usumbufu upo ndani na nje ya uwanja, lakini anafikiria zaidi maisha yake na kwamba anaamua kupotezea visa vyote akilenga kesho yake zaidi.
Anusurika kifo
Mrembo huyo anasema moja ya matukio ambayo hatasahau maisha yake ni 2020 aliponusurika kifo akiwa na timu ya Alliance Girls wakati wakitokea Dar es Salaam walipopata ajali wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
Anasema tukio hilo licha ya kwamba halikuwa na madhara makubwa kwao, lakini jinsi walivyoanguka na gari kubinuka aliamini wamekufa, lakini Mungu aliwanusuru.
“Ilikuwa ni baada ya mechi yetu na Simba Queens na tulipoteza kwa mabao 4-0. Ile tumekaribia Usagara gari lilibinuka siwezi kusahau majeruhi walikuwa kama wachezaji wanne wengine tulikuwa sawa,” anasema Revina.
Ndoto yake
Revina anasema mojawapo wa malengo yake akiwa shuleni alitamani kuwa mwandishi wa habari, lakini ghafla ndoto ziliyeyuka na kuingia katika masuala ya afya.
Anasema kutokana na mapenzi yake ya mpira alikuwa akipata nafasi ya kuitwa kwenye vyombo vya habari jijini Mwanza kufanya uchambuzi kwenye soka - kazi ambayo ilimvutia.
Anabainisha kuwa baada ya kumaliza elimu ya sekondari na ufaulu wake wazazi walimpeleka Chuo cha Afya Mkula kilichopo mkoani Simiyu.
“Siwezi kusema hii kazi ni mbaya wakati ndio inaniendeshea maisha, lakini nilitamani kuwa mwandishi wa habari. Nilipenda sana kuwa kwenye taaluma hii lakini nashukuru na hapa nilipo,” anasema daktari.
Avutiwa na Fatma Omary
Mtalaamu huyo wa afya anasema licha ya changamoto zilizopo kwenye kazi yake hiyo, lakini alivutiwa na aliyekuwa kocha wa makipa wa KMC, Fatma Omary ambaye alikuwa akifanya kazi yake kwa weredi.
Anasema hata yeye huendelea kupambana akiamini itafika siku ambayo atapata sehemu kubwa ya kufanya kazi hata kama ni katika klabu za Simba na Yanga ili maisha yaendelee.
“Nikajiuliza yule Fatma anafanyaje. Nikaona lolote linawezekana kama nitapambana bila kusikia kelele za watu pembeni na nitafikia malengo hata kufanya na timu kubwa ndani na nje.”
Mafanikio
Akizungumzia mafanikio, Revina anasema kwa muda mfupi aliopo kazini anashukuru kwa miradi mbalimbali aliyonayo katika maisha yake ya baadaye na kwamba, kutokana na ushirikiano alionao kwa watu mbalimbali hafikirii kuacha soka.
Anasema kupitia kazi yake imeendelea kumpa heshima hata kwenye familia kutokana na namna anavyoshiriki kwenye uchumi wa kifamilia, na zaidi kupanua wigo kwa watu mbalimbali.
Mwanamama huyo anasema anatarajia hadi kustaafu kazi hiyo awe na shughuli zake binafsi za kumuingizia kipato, huku akisisitiza kuwa hata akistaafu kazi hiyo lakini ataendelea kuwa mdau wa michezo.