Rekodi tamu, chugu Bara

MAISHA hayafanani. Huu ndio ukweli mchungu kuhusu muda wetu hapa duniani. Yaani unaambiwa wakati Yanga inaongoza kwa mabao mengi kwenye Ligi Kuu Bara kufikia sasa msimu huu, Kagera Sugar wanaburuza mkia wakiwa wamefunga mabao matano tu sawa na aliyofunga straika wa Yanga, Fiston Mayele.
Wababe wa Jangwani ndio winara wa ligi baada ya kucheza michezo 11 wakifunga mabao 20, huku ndani ya mabao hayo mshambuliaji Mayele ndiye kinara wa kufumania nyavu akitupia kambani mara tano sawa na mabao ya Kagera Sugar waliyofunga kwenye michezo 10.
Kagera licha ya kuwa nyuma mchezo mmoja dhidi ya vinara hao wa Ligi Kuu baada ya kucheza michezo 10 imepoteza mechi tano, imetoka sare tatu na kushinda mbili na kuambulia pointi tisa.
Mwanaspoti linakuletea rekodi kwa namba hadi sasa kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kusimama kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi yaliyoanza Januari 2, mwaka huu Visiwani Zanzibar.
86
Ni michezo iliyochezwa hadi sasa ambayo ni sawa na dakika 7,740 kwa timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.
166
Ni mabao yaliyofungwa kwenye michezo 86 iliyochezwa, huku vigogo wa ligi Simba, Yanga na Azam FC wakiwa wamefunga mabao 47 wakati timu nyingine 13 zikiwa zimefunga 119.
230
Ni pointi zilizopatikana kwenye michezo iliyochezwa, huku Yanga ikiwa ni vinara wa kukusanya pointi nyingi zaidi baada ya kucheza michezo 11 na kufanikiwa kukusanya 29 wakati watani zao wamevuna pointi 24.
18
Ni mabao waliyofungwa Ruvu Shooting baada ya kucheza michezo 11, wakifungwa michezo saba, wametoka sare mchezo mmoja na kushinda mechi tatu. Hii ndiyo timu yenye ukuta dhaifu ulioruhusu idadi kubwa zaidi ya mabao kufikia sasa Ligi Kuu. Wanaowafuatia ni KMC walioruhusu mabao 14, huku waliofungwa mabao machache zaidi ni Simba na Yanga (manne kila moja).
11
Ni idadi ya timu zinazolingana kwa pointi - Kagera Sugar na Biashara United (zinalingana kwa kuwa na pointi tisa), Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting (pointi 10), Mbeya Kwanza, Tanzania Prisons na KMC (pointi 11), Mbeya City na Dodoma (pointi 16) ilhali Polisi Tanzania na Coastal Union kila moja ina pointi 17.
5
Ni idadi ya vinara wa mabao wakiongozwa na nyota wazawa wanne na mgeni mmoja. Wazawa ni Jeremiah Juma, Vitalis Mayanga, George Mpole, Reliants Lusajo huku Mayele ndiye mgeni - raia wa DR Congo.
WASIKIE WADAU
Akizungumza mwenenendo wa Ligi Kuu Bara, kocha wa zamani wa Yanga, Kenedy Mwaisabula alisema kila timu imevuna ilichopata na sasa ni wakati sahihi kwa makocha kuhakikisha wanaboresha upungufu waliyouona kwenye vikosi.
“Ligi imesimama kuna timu zimepata nafasi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi na nyingine zimekosa nafasi. Sio muda wa kutumia vibaya, muda uliopo wanatakiwa kusajili na kupata michezo (ya kirafiki) ili kujiweka fiti kabla ya mzunguko mwingine haujaanza,” alisema.
Aliyekuwa kocha wa Namungo, Hemed Suleiman ‘Morroco’ alisema ni muda sahihi kwa timu kufanyia kazi upungufu ulioonekana kabla ya mchakamchaka mwingine kuanza.
“Kuna timu zimeanza vibaya ili kujikwamua na janga la kushuka daraja kipindi hiki ligi imesimama na usajili unaendelea wanatakiwa kuongeza nguvu na kupata timu kwa ajili ya michezo ya kirafiki ili kuendelea kuwaweka fiti wachezaji wao,” alisema.